▪️Wachimbaji Madini wapongeza upatikanaji wa Leseni na mazingira rafiki ya biashara
▪️Waziri Mavunde aainisha mafanikio 16 ya Rais Samia kwenye sekta ya Madini
▪️Aagiza uanzishwaji wa Soko la Dhahabu Katoro
▪️RC Shigela aja na mikakati mizito ya kupaisha sekta ya madini Geita
*Katoro,Geita*
Wachimbaji na Wafanyabiashara wa Madini wa Mkoa wa Geita wamempongeza Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia sekta ya madini katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.
Hayo yamesemwa jana kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na wachimbaji hao katika eneo la mnada wa zamani Katoro,Geita kwa lengo la kumpongeza Rais Samia kwa mafanikio yaliyopatikana kupitia sekta ya madini.
Akitoa maelezo ya awali,Mwenyekiti wa Chama cha Wachimba Madini Mkoa wa Geita(GEREMA) Ndg. Titus Kabuo amesema dhumuni kubwa la kusanyiko hilo ni kumpongeza Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kuiboresha sekta ya madini na kuweka mazingira rafiki ya uchimbaji na ufanyaji biashara hali inayopelekea kukua kwa shughuli za uchimbaji na kuathiri chanya maendeleo ya wachimbaji na uchumi wa nchi.
Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimba Madini Tanzania(FEMATA) Ndg. John Bina amesema katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia sekta ya madini imeshuhudia mabadilko makubwa hasa katika upatikanaji wa Leseni kwa wachimbaji na hatua iliyoanzwa na serikali ya kufanya utafiti wa kina ili kuwaongoza vyema wachimbaji madini nchini.
Akiwasilisha hotuba yake,Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde ameyataja mafanikio 16 ya Rais Samia S. Hassan katika kuipaisha sekta ya madini kubwa ikiwa ni kuongezeka kwa mchango wa sekta ya madini kwenye pato la Taifa kufikia 10.1%,ununuzi wa Dhahabu kupitia Benki Kuu,Kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuli kuelekea lengo la kukusanya Shilingi Trilioni moja na upatikanaji wa mitambo ya kuchoronga 15 kwa ajili yaa wachimbaji wadogo.
Aidha, Waziri Mavunde ametumia fursa hiyo kukipandisha hadhi kituo cha ununuzi wa dhahabu cha Katoro na kuwa soko kamili la Dhahabu la Katoro.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wabunge Joseph Msukuma na Tumaini Magesa wamempongeza Rais Samia kwa kuweka mazingira rafiki ya biashara ambayo yamesaidia kupatikana kwa maendeleo makubwa na kukuza uchumi wa watu wa Geita.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mh. Martin R. Shigela amesema Mkoa wa Geita umejipanga kuchochea shughuli za madini kwa kuboresha mazingira ya uchimbaji ili kukuza uchumi wa wananchi wa mkoa wa Geita kupitia upatikanaji wa Leseni zaidi ya 5308 na mitambo ya Uchorongaji ambayo Mh. Rais ameitoa kwa kwa wachimbaji wadogo.
0 comments:
Post a Comment