JSON Variables

Monday, April 14, 2025

TUTAENDELEA KUDHIBITI UHALIFU WA KIFEDHA-MAJALIWA

................ 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania itaendelea kushiriki na kutimiza matakwa ya kimataifa katika kupambana na kudhibiti uhalifu wa kifedha.
 
Amesema kuwa Tanzania inatambua changamato za uhalifu wa kifedha na imejidhatiti katika kudhibiti hali hiyo kwa viwango vya kimataifa vilivyopo.
 
Amesema hayo leo Jumatatu (Aprili 14, 2025) wakati Ufunguzi wa Mkutano kati ya Ujumbe wa Tanzania na Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Kudhibiti Fedha Haramu, kwenye ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.
 
Amesema kuwa kufuatia tathmini zilizofanywa na taasisi za Kuthibiti Uhalifu wa Kifedha Kusini Mashariki mwa Afrika mwaka 2021 na Kikosi cha Kimataifa cha Ushirikiano na Tathmini ya mwaka 2022, Tanzania imeimarisha mifumo ya kupambana na fedha haramu ikiwemo kujengea uwezo wa rasilimali watu na vifaa taasisi zinazohusika katika mapambano hayo.
 
Waziri Mkuu ameyataja maeneo yaliyofanyiwa kazi kuwa ni mabadiliko ya sheria na sera, matumizi ya takwimu na teknolojia, kuimarisha sekta nyumba na ardhi, kuwajengea uwezo wadau na kuimarisha usimamizi wa Taasisi za za kifedha.
 
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Tanzania baada ya kupokea mpango kazi kutoka Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Kupambana na Fedha Haramu ilifanya maamuzi ya ngazi ya juu ya kuimarisha usimamizi uhalifu wa kifedha nchini hali ambayo imeonesha mafanikio makubwa

 

TPDC, ZPDC ZAENDELEA KUSHIRIKIANA UENDELEZAJI SEKTA YA GESI NCHINI

.................

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) mwezi Februari, 2022 liliingia makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Maendeleo ya Petroli Zanzibar (ZPDC) ambapo kupitia ushirikiano huo masuala mbalimbali yamekuwa yakifanyika kuiendeleza Sekta  ikiwemo kubadilishana ujuzi na utaalam.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Aprili 14, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Kwahani, Mhe. Khamis Yussuf Mussa Mkenge aliyeuliza ni lini Serikali  itainufaisha Zanzibar katika matumizi ya Nishati ya Gesi ili iweze kutumika katika magari.

"Mheshimiwa Spika katika ushirikiano huu suala la kupeleka gesi Zanzibar ni mojawapo ya agenda kuu. Pande zote mbili bado zinaangalia namna bora ya kufikisha gesi asilia Zanzibar ili iweze kupatikana kwa bei nafuu kwa watumiaji.". Amesema Mhe. Kapinga 

Saturday, April 12, 2025

BALOZI NCHIMBI ASAINI KANUNI ZA MAADILI YA UCHAGUZI MKUU 2025

******

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ameshiriki katika utiaji saini wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025. Shughuli hiyo imefanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ikitanguliwa na mjadala wa Makatibu Wakuu wa Vyama vya Siasa vyote vyenye usajili wa kudumu, waliohudhuria na kuridhia kanuni hizo, leo Jumamosi, tarehe 12 Aprili 2025.







 

Watumishi Watakiwa Kuzingatia Taratibu za Ununuzi Ili Kuepusha Mianya ya Rushwa

 


Na Mwandishi Wetu

TABORA


Watumishi kutoka Taasisi mbalimbali wametakiwa kuzingatia taratibu za manunuzi ili kuepusha mianya ya Rushwa na  kuendelea kujenga uchumi wa nchi imara kwa manufaa ya taifa.


Hayo yanesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Paul Matiko Chacha wakati akifunga mafunzo ya kujengea uwezo watumishi kutoka taasisi mbalimbali kuhusu matumizi ya Mfumo wa NeST     ambayo yamefanyika kuanzia Aprili 07 hadi 11, 2025 katika ukumbi wa Mwanakiyungi Mkoani Tabora.

Mhe. Paul amesema mafunzo hayo yamekuwa ya kipekee kwa sababu yamejikita katika moduli mpya na muhimu kwa maboresho ya michakato ya ununuzi wa umma nchini ambapo Mfumo wa NeST unaendelea kuboresha uwazi, uwajibikaji, na ufanisi katika matumizi ya fedha za umma.


“Sasa ndugu zangu mara nyingi tunasikia mfumo unachelewesha lakini mimi nasema mifumo haicheleweshi, mifumo hii imekuja kwaajili ya kurahisisha kazi zetu sasa ninyi wataalamu wetu mpo hivyo muikotroo na kwa bahati nzuri  mifumo hii inaindeshwa na wewe hivyo tujitahidi kuwa waadilifu ili tuache kusingizia mfumo”alisema Mkuu wa Mkoa.

Aidha, kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhandisi Deusdetith Katwale amesema mafunzo hayo  ni muuendelezo wa jitihada za serikali katika kuhakikisha changamoto za ununuzi ndani ya taifa ziwe zinashughulikiwa kimifumo ili kuendana na teknolojia inayozidi kushika kasi nchini.


“Sasa hivi serikali inashika kasi kwenye mambo ya kidijitali ambapo zamani tulikuwa tunasema serikali inawasiliana kwa makaratasi tu lakini sasa hivi serikali tunawasiliana kidijitali kwa hiyo ni mwendelezo wa kuhakikisha inakuwa na mifumo imara ya mawasiliano hivyo ni imani yangu kwamba mafunzo yaliyofanyika hapa yataendelea kuleta chachu na kupunguza mianya ya rushwa katika Serikali yetu” aliongeza Mkuu wa Wilaya.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Kujenga Uwezo na Huduma za Ushauri kutoka PPRA Makao Makuu, Bi. Winfrida Samba amesema, lengo kuu la mafunzo hayo ni kupata elimu kuhusu Mfumo wa  NeST na katika mfumo huo kuna moduli mbalimbali na nyingine ni moduli ni mpya ambazo  zilizopelekea kufanya mafunzo hayo. 


“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa katika Mfumo wetu wa NeST tuna moduli mbalimbali ikiwemo usajili  ambayo inahusika na wazabuni pamoja na taasisi nunuzi, moduli nyingine ni “Etendering” ambayo inahusika na uchakataji wa zabuni  pia tuna moduli ya “E-contract Management” ambayo nayo inahusika na usimamizi na utekelezaji  wa Mikataba, tuna “Epayment”ambayo inahusika na masuala ya malipo lakini pia tuna moduli ndogo ambazo hizi ndizo washiriki wamejifunza zaidi” alisema Mkurugenzi Samba.

Mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa serikali  kuhusu Mfumo wa NeST yameanza tarehe 7 hadi 11 Aprili, 2025 katika ukumbi wa Mwanakiyungi Mkoani Tabora.

Friday, April 11, 2025

KAPINGA ASEMA KIPAUMBELE CHA SERIKALI NI KUFIKISHA UMEME KWENYE TAASISI ZOTE


.............................

πŸ“Œ Taasisi 1,272 zaunganishwa na umeme  Lindi

πŸ“Œ  Maeneo ya pembezoni mwa miji kuendelea kuguswa na miradi ya umeme

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha Taasisi zote zinazotoa huduma za kijamii, kiuchumi na kidini zinafikiwa na nishati ya umeme wakati wa utekelezaji wa miradi ya umeme Vijijini.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Aprili 11, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Maimuna Pathan aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itakamilisha kupeleka umeme kwenye Shule na Taasisi zote zikiwepo za dini katika Mkoa wa Lindi.

"Hadi kufikia mwezi Machi 2025, jumla ya Taasisi  1,272 zimeunganishiwa umeme katika Mkoa wa Lindi zikijumuisha: Zahanati 259; Vituo vya Afya 42; Hospitali 9; Shule za Msingi 554; Shule za Sekondari 151; na Taasisi za Dini 257 (Misikiti 142 na Makanisa 115). ". Amesema Mhe. Kapinga

Ameeleza kuwa, kupitia miradi inayoendelea kutekelezwa na kusimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Taasisi 27 zinatarajiwa kupatiwa umeme mkoani humo.. 

Akijibu swali la Mbunge wa Mbogwe, Mhe. Nicodemas Maganga aliyeuliza kuhusu Makanisa na Misikiti Mbogwe kutokuwa na umeme na mpango gani Serikali inao kuzipelekea Taasisi hizo umeme, Mhe. Kapinga amesema Taasisi hizo zitafikiwa na huduma ya umeme kupitia miradi ya Vitongoji inayoendelea katika Jimbo la Mbogwe, 

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Dkt. Christina Mzava kwa niaba ya Mbunge wa Kishapu, Mhe. Boniphace Butondo aliyetaka kujua ni ipi kauli ya Serikali juu ya Kata ambazo hazijaunganishiwa umeme Kahama na Shinyanga, Mhe. Kapinga amesema Serikali ina mikakati ya kuweka miradi ya umeme pembezoni mwa miji ili wananchi waunganishiwe umeme kwa bei rahisi.

Awali, akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kishapu, Mhe. Boniphace Butondo juu ya lini vijiji 42 vilivyobaki vya Wilaya ya Kishapu vitapatiwa umeme, Mhe. Kapinga amesema Jimbo la Kishapu lina jumla ya vijiji 117 ambapo hadi kufikia tarehe 30 Machi, 2025 vijiji vyote 117 sawa na asilimia 100 vilikuwa vimekwisha unganishwa na huduma ya umeme kupitia miradi mbalimbali iliyotekelezwa na Serikali.

Akijibu swali la Mbunge wa Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Waitara aliyetaka kufahamu wananchi wa Nywamwaga, Sirari na Nyamongo ni lini wataanza kuunganisha umeme kwa bei ya shilingi elfu 27, Mhe. Kapinga amesema maeneo ya Vijijini yanaunganishwa na umeme kwa shilingi elfu 27 na kwa yale ya pembezoni ipo miradi mingine ya pembezoni mwa mji.

 

SERIKALI INAENDELEA NA UKARABATI WA MIUNDOMBINU YA UMEME – KAPINGA


...........


πŸ“Œ Lengo ni kuondokana na changamoto ya kukatika kwa umeme

πŸ“Œ Ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Kilindi, Tanga waffikia asilimia 35.

πŸ“ŒBilioni 2.63 kulipa fidia wanaopisha njia ya kusafirisha umeme Mkata- Handeni-Kilindi

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inaendelea na ukarabati wa miundombinu ya kusambaza umeme ili kuondokana na changamoto ya kukatika kwa umeme nchini.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Aprili 10, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Handeni Mjini, Mhe. Reuben Kwagilwa aliyeuliza ni lini Serikali itaondoa changamoto ya kukatika kwa umeme wilayani Handeni.

"Changamoto ya kukatika umeme Wilayani Handeni inatokana na uchakavu na urefu wa miundombinu ya kusambaza umeme. Katika kukabiliana na changamoto hii Serikali kupitia TANESCO inaendelea na ukarabati wa miundombinu ya umeme ikiwa ni pamoja na kubadilisha nguzo za miti na kuweka za zege". Amesema Kapinga

Ameeleza kuwa, Serikali kupitia mradi wa gridi imara inaendelea na ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Mkata, Handeni ambacho kipo kwenye hatua za awali za ujenzi.

Ameongeza kuwa,  ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Kilindi, Tanga umefikia asilimia 35 na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132 kutoka Mkata kupitia Handeni hadi Kilindi umeffikia asilimia 30.

Akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Mhe. Rashid Shangazi aliyeuliza kuhusu Serikali kuona umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa vituo vya umeme vya Mkata, Lushoto na Kilindi kutokana na umuhimu wa vituo hivyo kuimarisha upatikanaji wa umeme Mkoa wa Tanga, Mhe. Kapinga amesema tayari Wizara ya fedha imeihakikishia Wizara ya Nishati kuwalipa wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kwa wakati ili waikamilishe.

Na kuhusu kusuasua kwa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Mkata hadi Kilindi kutokana na ulipwaji wa fidia, Mhe. Kapinga amesema fidia ya wananchi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Mkata, handeni hadi Kilindi ni takribani shilingi bilioni 2.63 ambayo Wizara ya fedha wameihakikishia Wizara ya Nishati kuilipa fidia hiyo.

Mhe. Kapinga ameongeza kuwa, fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Mkata, Handeni tayari wameshalipwa fidia.

Akijibu swali la Mbunge wa Hanang’, Mhe. Mhandisi Samwel Xaday aliyeuliza ni lini Serikali itatatua changamoto ya kukatika kwa umeme Wilaya ya Hanang’, Mhe. Kapinga amesema Wilaya ya Hanang’ ipo katika mradi wa ujenzi wa gridi imara awamu ya pili ambapo kitajengwa kituo cha kupokea na kupoza umeme ambapo kwa sasa Serikali inaendelea na awamu ya kwanza ya mradi wa gridi imara.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Mhe. Grace Tendega kuhusu kukatika kwa umeme mkoani humo hasa Jimbo la Kalenga, Mhe. Kapinga amesema Serikali inayo mikakati ya kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Iringa ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya umeme kwa kubadilisha nguzo na nyaya chakavu.

Aidha, Mhe. Kapinga amesisitiza kuwa kutokea Mkoa wa Iringa, Tunduma hadi Katavi Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa kusafilisha umeme wa TAZA ambao unahusisha ujenzi wa vituo vya kupoza umeme ambavyo vitaboresha upatikanaji wa umeme maeneo yote ya ukanda huo na kuongeza kuwa mradi huo utaunganisha gridi za Taanzania na Zambia.




 

Thursday, April 10, 2025

NCC YAFUNZA MBINU KUPUNGUZA GHARAMA ZA UJENZI


  

..........................

Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limeendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu wa sekta ya ujenzi nchini kwa kutoa mafunzo yatakayowawezesha kutekeleza miradi kwa ufanisi, kupunguza gharama zisizotarajiwa, na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vilivyokusudiwa.

Kupitia mafunzo hayo, NCC imelenga kuwajengea uwezo waajiri, wakandarasi na washauri elekezi kusimamia mabadiliko ya kazi, madai na migogoro kwa njia inayozuia upotevu wa muda, fedha, na rasilimali nyingine hali inayopunguza gharama kwenye miradi ya ujenzi.

Kwa mujibu wa wataalamu wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), miradi ya ujenzi huathiriwa na mabadiliko ya kazi, ucheleweshaji wa kushughulikia madai, na migogoro, ambavyo kwa pamoja husababisha ongezeko la gharama, muda wa mradi na hata kushusha viwango vya ubora.

Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Arusha, Mhandisi Tumaini Lemunge kutoka NCC amesema, lengo lao ni kuona miradi ya ujenzi inatekelezwa kwa gharama zilizopangwa na kwa ubora unaokubalika.

“Kupitia mafunzo haya, washiriki wamepata mbinu za kupunguza mabadiliko yasiyo ya lazima, kushughulikia madai mapema, na kutatua migogoro kwa mujibu wa mikataba” amesema Mhandisi Tumaini

Aidha Wadau mbalimbali wa sekta ya ujenzi waliopata nafasi ya kushiriki wameeleza namna mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mhandisi Lyda Osena kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) amesema “Mafunzo haya yameniongezea uwezo wa kutambua, kuepusha na kusimamia migogoro na madai kwa njia ya kisheria, vilevile yatanisaidia kutekeleza miradi kwa ufanisi zaidi, ndani ya muda, bajeti na ubora uliokusudiwa.”

Mkadiriaji Majenzi kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi amesema kuwa amepata  uelewa mpya kuhusu umuhimu wa mabadiliko katika mikataba ya ujenzi hivyo anafahamu kuwa mabadiliko hayawezi kuepukwa lakini yanahitaji usimamizi makini ili kuepusha gharama zisizokuwa za lazima.

Kwa upande wake, Mwanasheria Elizabeth Kimako kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) amesema, Mwanasheria anaposhiriki katika mchakato wa ujenzi anatakiwa kuelewa kwa kina masuala ya kimkataba.

Amesema kuwa mafunzo hayo yamempa uelewa wa kusaidia taasisi yake kuendesha miradi mbalimbali kwa kwa ufanisi mzuri.

Wednesday, April 9, 2025

MNRT SPORTS CLUB YATINGA KAMBINI KWA KISHINDO.

..,............

Na Sixmund Begashe - Dodoma

Club ya michezo ya Wizara ya Maliasili na Utalii ijulikanayo kama "MNRT SPORTS CLUB" imeanza kwa kishindo mazoezi ya kujifua tayari kwa kukabiliana na timu yeyote itakayo kutana nayo kwenye michezo ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Dunia (MEI MOSI) inayotarajiwa kurindima Mkoani Singida hivi karibu.

Akizungumzia uwepo wa Kambi hiyo Jijini Dodoma, Mwenyekiti Msaidizi wa Club hiyo yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa Bi ,Sharifa Dunia Salum amesema mwaka huu wamejipanga vyema katika kuhakikisha wanaibuka na ushindi mnono katika kila mchezo.

"Wachezaji wetu wote wako imara na wanahari kubwa ya kuhakikisha Wizara yetu ya Maliasili na Utalii inaibuka kidedea katika michezo yote, hatutakuwa na huruma na timu yeyote itakayokuja mbeleyetu tutaiadhibu vikali" Alisema Bi. Salum

Aidha Bi. Salum ameushukuru Uongozi wa Wizara chini ya Waziri Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, kwa kuiwezesha Club hiyo kuingia kambini na kwenda kushiriki mashinda hayo muhimu kwa ustawi wa Wafanyakazi na Taifa kwa ujumla.

"Tunaushukuru sana uongozi wa Wizara yetu, umetupa heshma kubwa na sisi tunaahudi tutailinda heshma hii kwa kutoka na ushindi wa kishindo katika michezo yote na kurejea na Makombe" Alisisitiza Bi. Salum

Club hiyo maarufu ya michezo, imekuwa ikifanya vyema kila mwaka katika michezo yake mbalimbali dhidi ya wapizao wao ambao ni timu za Wizara mbalimbali hapa nchini, na sasa inakwenda tena kuzitunishia misuli timu hizo kwenye michezo ya Mei Mosi 2025.