JSON Variables

Friday, April 18, 2025

IMF YAKUNWA NA UTEKELEZAJI MIPANGO YA TANZANIA YA KUKUZA UCHUMI NA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiongoza kikao cha kuhitimisha vikao vya majadiliano kati ya Serikali na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuhusu tathimini ya awamu ya tano ya utekelezaji wa program ya Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha ufadhili wa dola za Marekani bilioni 1.832, kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii pamoja na awamu ya pili ya utekelezaji wa program ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la Resilient and Sustainable Fund (RSF) yenye jumla ya ufadhili wa dola za Marekani bilioni 1.832, kutoka Shirika hilo,  tukio liliofanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha, Dar es Salaam)
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
 
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amelihakikishia Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwamba, Serikali itaendelea kufanya maboresho ya sera na mipango yake kwa kuhakikisha sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii pamoja na kuimarisha sekta binafsi zinapewa kipaumbele.
 
Dkt. Nchemba amesema hayo wakati akifunga vikao vya majadiliano kati ya Serikali na Timu ya Wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), baada ya kukamilisha tathimini ya awamu ya tano ya utekelezaji wa program ya Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii pamoja na awamu ya pili ya utekelezaji wa program ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la Resilient and Sustainable Fund (RSF) kutoka Shirika hilo.
 
Akifunga vikao hivyo katika Kikao cha majumuisho kilichofanyika Benki Kuu  ya Tanzania (BoT), Jijini Dar es Salaam, Dkt. Nchemba, alieleza kufurahishwa kwake na taarifa iliyowasilishwa na Kiongozi wa Timu hiyo Bw. Nicolas Blancher, inayoonesha kuwa Tanzania imetekeleza ipasavyo vigezo vilivyowekwa na Shirika hilo katika mipango hiyo ya ECF na RSF.
 
Aliahidi kuwa Serikali itaendelea kusimamia ipasavyo utekelezaji wa programu hizo mbili zenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 1.832, ambapo kiasi cha dola bilioni 1.1 ni kwa ajili ya Mpango wa kuimarisha Uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na kiasi cha dola milioni 786 ni kwa ajili ya Mpango wa nchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambapo program hizo mbili zinatekelezwa katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2022/2023 hadi 2025/2026.
 
Kwa upande wake, Kiongozi wa Timu ya Wataalam kutoka IMF waliofanya tathimini hiyo, Bw. Nicolas Blancher, alisema kuwa tathimini yao ya awamu ya tano imeonesha kuwa Tanzania imetekeleza vizuri mpango wa ECF na RSF na kushauri hatua kadhaa zinazotakiwa kuendelea kuchukuliwa ikiwemo kuimarisha zaidi huduma za jamii na kuendelea kuimarisha mazingira bora ya kufanyabiashara na uwekezaji. 
 
“Matarajio ya uchumi wa Tanzania ni mazuri kwakuwa utaendelea kukua kwa kasi, huku mfumuko wa bei ukiendelea kuwa chini, nakisi ya mauzo na manunuzi ya bidhaa na huduma nje ya nchi ikipungua, na upatikanaji wa fedha za kigeni ukiongezeka” alisema Bw. Blancher.
 
Aliongeza kuwa hatua za kuwianisha vizuri mapato na matumizi ya serikali katika mwaka wa fedha wa 2025/26, zitasaidia kuhifadhi uhimilivu wa deni la serikali, huku zikilinda matumizi yenye kipaumbele katika huduma za kijamii. 
 
Bw. Blancher alisema kuwa kuendelea kutekeleza sera za kukabiliana na athari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, zinazoungwa mkono na mpango wa RSF, kutasaidia kujenga ustahimilivu katika kushughulikia madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
 
Alisema kuwa mapendekezo ya tathimini hiyo yatapelekwa mbele ya Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na kwamba uamuzi utakaotolewa na Bodi utaiwezesha Tanzania kupokea ufadhili wa dola za Marekani milioni 441.
 
Tanzania imefanyiwa Tathimini ya Awamu ya Tano ili iweze kupata fedha kutoka IMF kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ambapo hadi sasa Program ya ECF imepokea kiasi cha dola za Marekani milioni 754.3 kati ya dola za Marekani bilioni 1.1 na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 55 zimepokelewa  kupitia dirisha la RSF, mradi wenye thamani ya dola za Marekani milioni 786.
 
Kikao hichi kilihudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, na Manaibu Gavana, pamoja na Maafisa Waandamizi wa Serikali na wajumbe wa Timu ya Tathimini kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF.

BUGUMBA ATOA UJUMBE MAADHIMISHO SIKU YA MALIKALE

Mhifadhi Mkuu Mambo ya Kale na Mkuu wa Kanda ya Magharibi Makumbusho na Malikale anayesimamia uhifadhi na uendelezaji maeneo ya kusini mwa Tanzania Lindi na Mtwara Revocatus Bugumba akizungumzia  siku ya Kimataifa ya Malikale ambayo hufanyika tar 18 April ya kila mwaka.

Mhifadhi Mkuu Mambo ya Kale na Mkuu wa Kanda ya Magharibi Makumbusho na Malikale anayesimamia uhifadhi na uendelezaji maeneo ya kusini mwa Tanzania Lindi na Mtwara Revocatus Bugumba akionyesha jengo la Makumbusho ya awali ambalo sasa linabaki kama malikale.

.....................

NA MUSSA KHALID

Watanzania wametakiwa kushiriki kutembelea maeneo ya Malikale zilizopo nchini ikiwemo kuzuia uharibifu wake ili waweze kujifunza historia ya nchi yao.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mhifadhi Mkuu Mambo ya Kale na Mkuu wa Kanda ya Magharibi Makumbusho na Malikale anayesimamia uhifadhi na uendelezaji maeneo ya kusini mwa Tanzania Lindi na Mtwara Revocatu Bugumba wakati akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi katika kuadhimisha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Malikale ambayo hufanyika tar 18 April ya kila mwaka.

Bugumba  amesema kuwa Malikale zinajumuisha maeneo na kumbukumbu za kihistoria ambayo yanahifadhiwa ikiwemo majengo ,bustani,maeneo ya kumbukumbu za kivita.

Akitolea mfano wa mji wa Dar es salaam kumesheheni maeneo ya majengo ya kale kama makanisa,mahekalu ya wahindi,majengo ya kiserikali ,maeneo ya mnazi mmoja,majengo kuanzia Ikulu na hata bustani za kale.

‘Kiujumla maeneo mengi ya Malikale huwa yanaathiriwa kwa changamoto za kiasili ambazo ni kama mabadiliko ya Tabia ya nchi,mvua kali ukame na kutokea kwa matukio makubwa yakiwemo vita” amesema Bugumba

Amesema msingi wa dhima ya Malikale imesisitiza kufanya ukusanyaji wa kumbukumbu ikiwemo kufanya tathmini ya maeneo ya malikale na kuyaweka kwenye orodha jambo ambalo litazuia uharibu.

Bungua amesema mpango mwingine ni kusisitiza jamii ishirikishwe kwa namna mbalimbali lakini pia usimamizi kuhakikisha inatumiwa mbinu za asili za uhifadhi za Malikale ili kuepukana na mtindo wa kuondoa thamani ya maeneo hayo na kuweka vitu vya kisasa.

Pia ametumia fursa hiyo kuisistiza jamii kutoa taarifa kuhusu Malikale zilizopo kwenye maeneo yao ambazo zinataka kuharibiwa  ili ziweze kuhifadhiwa kwa muda mrefu.

Katika hatua nyingine ,Bugumba ametoa rai kwa Mamlaka za serikali za mitaa kuendeleza maeneo ya Malikale zilizopo kwenye miji yao ili kutopoteza uhalisia na historia ya maeneo hayo.

Mwaka huu 2025 maadhimisho hayo yanakwenda na kauli mbiu ya kuangazia madhara ya majanga na migogoro katika maeneo ya Malikale lakini pia kutafakari miaka sitini ya utekelezaji wa baraza la kimataifa la Malikale katika kutatua migogoro ya malikale na kushughulikia majanga yanayoathiri malikale hizo.

Zoezi la Uhakiki Malipo ya Mbolea za Ruzuku kwa Wakulima wa Tumbaku Tabora larizisha

............
 
Tabora, 

Katika kuhakikisha wakulima wa tumbaku wanapata ruzuku za mbolea Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw. Joel Laurent, amefanya ziara ya kikazi katika vituo viwili vinavyo hakiki taarifa hizo mkoani Tabora kujionea maendeleo ya zoezi hilo na kuhakikisha linakamilika kwa wakati.

Baada ya kutembelea vituo hivyo katika ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika Mirambo na ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU), Bw. Laurent amesema kuwa, zoezi hilo limefikia hatua nzuri itakayowezesha kuanza kwa taratibu za malipo kwa wakulima wa Tumbaku nchini. 

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Laurent ameeleza kuwa, lengo la uhakiki ni kuhakikisha wakulima wote waliozalisha Tumbaku katika msimu wa mwaka 2023/2024 wanalipwa na fedha hizo zinamfikia mkulima anayestahili moja kwa moja kupitia akaunti yake.

Ameeleza kuwa, zoezi hili linafanyika kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Kilimo, TFRA, TCDC na vyama vikuu vya ushirika vilivyo chini ya shirikisho la TCJE.

Akizungumza na Mkurugenzi Laurent, Ndg. Innocent Nsena Katibu Tawala wa Wilaya ya Urambo alieleza kuwa, suala la ruzuku limekuwa kilio cha muda mrefu kutoka kwa wakulima na kwamba utekelezaji wa mpango huu utapunguza gharama za uzalishaji kwa mkulima.

“Ninamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia ombi la kutoa ruzuku kwa wakulima wa tumbaku, kwa kuwa zao hili awali halikuwa miongoni mwa mazao yanayopata ruzuku” alisema Ndg. Nsena.

Kwa upande mwingine, akitoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi la uhakiki katika ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika WETCU, kiongozi wa timu hiyo, Ndg. Byaga Nzohumpa, alieleza kuwa, zoezi hilo limekamilika kwa asilimia 100 baada ya kuhakiki taarifa za vyama vya msingi 248 walivyokabidhiwa.

Naye Ndg. Godwin Mwalongo, kiongozi wa timu ya uhakiki katika ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika Mirambo, amesema kuwa, kazi ya uhakiki imefikia hatua nzuri na inatarajiwa kukamilika kwa wakati.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TCJE, Ndg. Seleman Abasi Maona, alieleza kuwa, miongoni mwa changamoto kubwa zilizokabili zoezi hilo ni uandaaji hafifu wa takwimu za wakulima wa tumbaku kwa msimu wa kilimo wa 2023/2024, hasa kutokana na taarifa zisizo sahihi kutoka kwa wakulima.

Alisisitiza kuwa kama kungekuwepo mfumo madhubuti wa ukusanyaji taarifa kuanzia ngazi ya chini, changamoto hizo zingeweza kuepukwa na kuahidi kuboresha kwa ajili ya manufaa ya baadaye kwa wakulima







Thursday, April 17, 2025

KUELEKEA MAADHIMISHO MALIKALE,MAKUMBUSHO YABAINISHA MAFANIKIO YAKE

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga wakati akizungumza ofisini kwake jijini Dar es salaam akielezea katika kuelekea maadhimisho ya siku ya Siku ya Kimataifa ya Malikale ambayo hufanyika tar 18 April ya kila mwaka.

........................

NA MUSSA KHALID

Taasisi ya Makumbusho ya Taifa la Tanzania imeisisitiza jamii kuendelea kushiriki kikamilifu katika kuhifadhi malikale zilizopo nchini ili kuepukana na madhara yanayosababishwa na majanga na migogoro katika sekta hiyo.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga wakati akizungumzia kuhusu  kuelekeza maadhimisho ya siku ya Siku ya Kimataifa ya Malikale ambayo hufanyika tar 18 April ya kila mwaka.

Dkt Lwoga amesema kuwa lengo la kufanyika maadhimisho hayo ni kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa malikale katika maisha yao sambamba na kushiriki katika uhifadhi wa malikale kwa faida ya jamii hiyo.

‘Kwa mwaka huu 2025 maadhimisho haya kauli mbiu kubwa ni kuangazia madhara ya majanga na migogoro katika maeneo ya Malikale lakini pia kutafakari miaka sitini ya utekelezaji wa baraza la kimataifa la Malikale katika kutatua migogoro ya malikale na kushughulikia majanga yanayoathiri malikale hizo”

Aidha Dkt Lwoga amesema mambo yanayoathiri Malikale ni pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo maeneo ya bahari yakiongezeka kina na kuleta madhara kwenye malikalie pia kuna madhara ya nayosabishwa na majanga ya asili kama vile mafuriko.

Vilevile kwa shughuli za binadamu pia zimekua zikiathiri Malikale kwa watu kuvamia baadhi ya maeneo na kubomoa jambo linalosababisha kukosa uwepo wa ushahidi wa eneo hilo la kihistoria.

Dkt Lwoga amewasisitiza watanzania kutambua na kuhifadhi vitu vya kale ili kusaidia vizazi vya sasa na vya baadae huku akihamasisha jamii kuanzisha makumbusho binafsi.

Kuhusu Mafanikio ya Makumbusho amesema kwa sasa  wageni zaidi laki mbili wanazitembelea Makumbusho ya Taifa pamoja na maeneo ya Malikale ili kujifunza na kuelewa historia ya nchi yao.

 

WALICHOKIFANYA BODABODA MWANZA KWA MKUU WA WILAYA NYAMAGANA

 


Boda boda na samia mkoa wa mwanza wamefanya maandamano ya kushtukiza kuelekea kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya nyamagana kwa ajili ya kwenda kumuelezea nia yao kwa nchi ya Tanzania na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt samia Suluhu Hassan kwa namna anavyotekeleza miradi ya kimkakati .

Akizungumza mara baada yakufika kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya nyamagana mwenyekiti wa boda boda na samia Ramadhan Musabi ameeleza niya yao ya kile kilichopelekea kufanya kufanya maandamano hayo ya kwenda kwa mkuu wa wilaya ya nyamagana. 

Nae mkuu wa wilaya ya nyamagana Amina makilagi baada ya kuwapokea boda boda boda hao ameeleza furaha yake na kuwashukuru kwa nia yao ya dhati huku akiwaahidi kuungananao katika harakati zao zote za kuzunguukia miradi mikubwa yote iliyopo hapa mkoani mwanza.

Mbeto: Haki ya wananchi kushiriki uchaguzi isiporwe na Vyama vya Siasa


 

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar


Chama cha Mapinduzi (CCM)  kimesifu kupevuka kwa  maono ya  kisiasa  yalioonyeshwa na Kiongozi wa ACT  Wazalendo, Dorothy  Semu ,aliyeitangazia dunia  chama chake kitashiriki uchaguzi  Mkuu oktoba  mwaka huu bila  longolongo.


Pia CCM  kimebaini kuwepo  tofauti  ya uelewa, upeo, busara  na ufahamu  kati ya Kiongozi wa ACT  na Mwenyekiti  wake  Othman  Masoud Othman .


Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati  Maalum  ya NEC Zanzibar,  Idara  ya itikadi , Uenezi na Mafunzo ,Khamis  Mbeto  Khamis,  aliyesema kwa chama makini  ni aibu kukimbia  uchaguzi wa kidemokrasia.  


Mbeto  alisema haki ya kushiriki  uchaguzi inawahusu  zaidi  wananchi kupitia  vyama vyao  lakini  si halali kwa viongozi wa Vyama vya siasa  kuwazuia wananchi wasitumie  haki na wajibu wa kuchagua au kuchaguliwa.


Alisema si hivyo  tu ,bali kiongozi  wa ACT Wazalendo amezungumza mambo ua msingi  akitumia lugha  komavu ,maneno  yenye hekima na busara,  tofauti na matamshi holela yanayokuwa yakitolewa mara kwa mara na Mwenyekiti  wake.


"Viongozi wa Vyama vya Siasa wasipore madaraka na  haki za wananchi  Waache  kuwazuia ili wasishiriki chaguzi  za kidemokrasia. Haki za vyama zisikwapue matakwa ya  kisheria na kikatiba ya wananchi  na kugeuza  miliki ya viongozi wa vyama " Alisema Mbeto 


Aidha  Katibu  huyo Mwenezi  alisema  maelezo  alioyatoa kiongozi wa ACT Wazalendo,  hayakuambatana kabisa na maneno ya   vitisho au yenye   kujenga hofu na taharuki katika  jamii .


"Kiongozi wa ACT amejenga hoja  zake  bila kutumia  lugha  ya ubabe tofauti na Mwenyekiti wake .Hii ni tofauti iliopo kati ya Mwenyekiti na kiongozi  wa chama. Ama kweli maarifa ya  kinamama huwazidi baadhi ya kinababa ' Alieleza


Hata hivyo,  katika maelezo yake, Mbeto  akimtaka Semu afute  ndoto za ACT kukishikda CCM kwakuwa hakijapata  uwezo huo  na wananchi hawajawa tayari  kukiamini  ACT ili kuiongoza Zanzibar.


Pia  Mbeto  alisema chini ya usimamizi wa  Tume ya Uchaguzi  Zanzibar  na Tume huru ya Uchaguzi  Tanzania, vyama vya  upinzani  vimekuwa vikishinda na kupata viti vingi ikiwemo  kura za urais .


"Ni masikitiko kwa ACT  Wazalendo  kumsimamisha  Othman kuwania nafasi ya urais ili ashindane na mgombea wa CCM Rais Dk Huseein  Ali  Mwinyi. Tunakwenda kushinda mapema asubuhi kweupe" Alisema Mbeto 


Katibu   huyo Mwenezi  alisema  kulingana na kazi kubwa ilofanywa na Serikali  ya awamu ya nane, CCM kina kazi nyepesi mno ifikapo oktoba  mwaka huu.

SERIKALI KUTUMIA TRILIONI 1.18 UJENZI WA MIUNDOMBINU YA BARABARA ZA WILAYA



Dodoma


Katika mwaka wa fedha 2025/26, Ofisi ya Rais - TAMISEMI kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA imepanga kutumia shilingi trilioni 1.18 kwa ajili ya ujenzi, matengenezo, ukarabati wa miundombinu ya barabara na usafiri na usafirishaji wa vijijini na mijini. 


Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 257.03 ni za Mfuko wa Barabara, shilingi bilioni 127.50 Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali, shilingi bilioni 325.77 ni za tozo ya mafuta ya petroli na dizeli ya shilingi 100 kwa lita na shilingi bilioni 423.79 ni fedha za nje.


Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, OR-TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa  Mwaka wa Fedha 2025/2026 jijini Dodoma.


Amesema kupitia Mfuko wa Barabara, fedha hizo zitaenda kutekeleza matengenezo na ukarabati wa barabara za wilaya zenye urefu wa  kilomita 23,105.78, box kalavati 23, mistari ya kalavati 1,647, Drift 2, na mifereji ya maji ya mvua mita 73,405, barabara za lami kilometa 17, barabara za changarawe kilometa 108.8 na madaraja 2.


Aidha, ujenzi wa kilometa 91.97 kwa kiwango cha lami, kilometa 2,621.40 za changarawe, madaraja 85, box kalavati 91, mitaro ya maji ya mvua mita 10,989 drifti tano (5), mistari ya kalavati 666 na taa za barabarani 345 zitatekelezwa kupitia Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.


Ameongeza kuwa kupitia tozo ya mafuta ya petroli na dizeli ya shilingi 100 kwa lita, fedha hizo zitatekeleza ujenzi wa km 252.42 kwa kiwango cha lami, kilomita 6,939.41 za changarawe, madaraja 51, box kalavati 336, mistari ya kalavati 1,719, Drift 2, na mifereji ya maji ya mvua mita 63,836.


Mhe. Mchengerwa amesema ujenzi wa barabara za lami Km 147.50, ujenzi wa mifereji ya maji ya 

mvua mita 24,600, ujenzi wa masoko 9, ujenzi wa stendi kuu 4

za mabasi na stendi ndogo 2 pamoja na ujenzi wa maghala 2 

ya kuhifadhia mazao kwenye miji 12 ya Fungu la Kwanza la Mradi wa TACTIC unaendelea.


Pia kuanza kwa ujenzi kwenye Halmashauri za Miji 15 za Fungu la Pili la Mradi wa TACTIC pamoja na kukamilisha mchakato wa maandalizi ya 

Mradi wa TACTIC Fungu la Tatu katika 

Halmashauri za Miji 18.


Amesema ujenzi wa barabara Km 33 kwa kiwango cha lami katika halmashauri za Wilaya za Iringa (Wenda-

Mgama kilomita 19) na Mufindi (Mtili-Ifwagi

kilomita 14) unaendelea, pmoja na kuanza kwa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Km 33 katika halmashauri za Wilaya za Handeni, Ruangwa na Mbogwe kupitia mradi wa RISE.


Vilevile, uboreshaji wa Bonde la Msimbazi lenye Hekta 5.7, ujenzi wa karakana ya mabasi 

ya mwendo kasi katika eneo la Ubungo 

Maziwa, ujenzi wa tuta kilomita 6.7 katika eneo la Bonde la Mto Msimbazi, ujenzi wa Bohari Mpya ya BRT eneo la Ubungo Maziwa, ujenzi wa miundombinu ya barabara awamu ya kwanza zenye jumla ya 

kilomita 132 katika Manispaa za Kinondoni,

Ubungo, Temeke, Ilala na Kigamboni.


Pia, ujenzi wa miundombinu ya 

barabara awamu ya pili ya Mradi wa DMDP 

zenye urefu wa kilomita 118 kiwango cha 

lami katika Manispaa za Kinondoni, Ubungo,

Temeke, Ilala na Kigamboni.

RAIS MWINYI:TUTANGAZE FURSA ZA UWEKEZAJI NA KUZINGATIA DIPLOMASIA YA UCHUMI.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi amewasisitiza Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika Nchi mbalimbali kuzingatia Diplomasia ya Uchumi na Kuzitangaza fursa za Uwekezaji ziliopo.


Rais Dkt, Mwinyi ameyasema hayo   alipozungumza  na Mabalozi wa  Tanzania wa Nchi za Rwanda,Zimbabwe ,Sweden na Msumbiji Waliofika Ikulu kumuaga  kabla ya kwenda katika Vituo vyao vya Kazi Baada ya kuteuliwa hivi karibuni.


Amewahimiza Mabalozi  hao kufanya Juhudi Maalum za kuitangaza Sera ya Uchumi wa Buluu na Utalii katika Mataifa hayo Ili kuvutia Wawekezaji Zaidi kuwekeza  Nchini.


Amesema Zanzibar bado inahitaji Wawekezaji wengi Hususan katika Sekta hizo Kuu za kipaumbele kutokana na kuwepo kwa fursa nyingi ikiwemo Uvuvi,Utalii na Mafuta na Gesi.


Halikadhalika Rais Dkt, Mwinyi ameeleza kuwa  Suala la Mahusiano ya Kimataifa hivi sasa limeelekezwa zaidi katika Uchumi hivyo wanapaswa kuzingatia zaidi Kuimarisha Uhusiano wa Kiuchumi.


Ameyataja Maeneo ambayo Yana fursa za kutosha kuwa ni Uwekezaji katika Sekta ya Bandari ikiwemo Bandari za Makontena ,Usafirishaji wa Mzigo, na Mafuta na Gesi.


Akizungumzia Sekta ya Biashara  amewaagiza Mabalozi hao kuzitafutia Masoko Bidhaa za Tanzania ikiwemo Bidhaa za Viungo zinazozalishwa kwa Wingi hapa Zanzibar pamoja na Utalii wa huduma na  Vivutio vya Utalii ili kuwavutia Watalii wa Mataifa hayo kutembelea Zanzibar.


Nao Mabalozi hao  wameahidi kuyatumia Maelekezo ya Rais Dkt, Mwinyi kuwa ni nyenzo na dira ya kufanya Kazi zao kwa Ufanisi pamoja na kuyazingatia Maeneo Muhimu ya Kiuchumi  kwa kuwashawishi Wawekezaji  kuwekeza.


Mabalozi walioaga ni Balozi Dkt, Habibu Kambanga- Rwanda, Balozi CP Suzane Kaganda- Zimbabwe, Balozi Mobhare Matinyi - Sweden na Balozi CP Hamad Hamad - Msumbiji.