JSON Variables

Tuesday, April 22, 2025

MAJALIWA AMWAKILISHA RAIS DKT. SAMIA KIKAO KAZI CHA MAAFISA UTAMADUNI NA MICHEZO

******

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Aprili 22, 2025 anamwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa kikao kazi cha 15 cha Maafisa Utamaduni na Maafisa Maendeleo ya Michezo Tanzania.

Kikao hicho cha Mafundo na Mazingativu kinalenga kujadili maendeleo ya sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Pia kikao hicho kinatoa nafasi kwa washiriki kujadili fursa za sekta, kubaini changamoto zinazoikabili sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo na kupendekeza njia za utatuzi wa changamoto hizo.






 

ULEGA ATOA SIKU 30 KWA MKANDARASI BARABARA YA NSALAGA - IFISI KUWEKWA LAMI


Waziri wa Ujenzi,  Abdallah Ulega ametoa siku 30 na kumtaka Mkandarasi Kampuni ya CHICO anayetekeleza ujenzi wa upanuzi wa barabara ya Nsalaga - Ifisi (km 29) kwa njia nne, jijini Mbeya kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo ili uweze kukamilika na kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo.


Aidha, Waziri Ulega amemuagiza Mkandarasi huyo kufanya kazi usiku na mchana, kuongeza vifaa pamoja wafanyakazi ili kufanikisha mradi huo ukamilike haraka iwezekanavyo.


Ulega ametoa maelekezo hayo jijini Mbeya wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya mradi huo na kutoridhishwa na hatua za utekelezaji wake ambao hadi sasa umefikia asilimia 25.

Ulega ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari imeshatoa malipo ya Shilingi Bilioni 35 kwa Mkandarasi huyo na matarajio yake ni kuona kupitia fedha hizo angalau kilometa kadhaa za lami zimekamilishwa kujengwa katika barabara hiyo.


“Serikali imeshatoa Bilioni 35 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kutoka Nsalaga hadi Ifisi, na fedha hizi Mkandarasi hajazifanyia kazi ipasavyo, Sasa basi Nimemuagiza Mkandarasi afanye kazi usiku na mchana na kuona mabadiliko ya haraka katika mradi huu”, amesisitiza Ulega.


Pia,  ametoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mbeya kumsimamia Mkandarasi kwa ukaribu ili hadi kufikia mwanzoni mwa Mwezi Juni mwaka huu Mkandarasi awe amekamilisha  kilometa 10 za lami katika barabara hiyo na kuahidi kurudi tena kwa ajili ya kukagua maendeleo hayo.

Ulega amemuelekeza Meneja huyo wa TANROADS kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unaenda sambamba na ufungaji wa taa za barabarani ili kuupendezesha mji wa Mbeya na kuimarisha masuala ya ulinzi na usalama wa wananchi wanaotumia barabara hiyo katika shughuli zao za kiuchumi za kila siku.


Vilevile, Ulega amepokea Ombi la Mbunge wa Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson la ujenzi wa kilometa tano za lami zinazoingia katika mitaa ya iiji la Mbeya na kuahidi kulifanyia kazi.


Kadhalika, Ulega amemuagiza Meneja wa TANROADS mkoa wa Mbeya kumsimamia Mkandarasi katika kuhakikisha kazi ndogondogo   zinazofanywa na Mkandarasi zinatolewa kwa vijana wa Mkoa wa Mbeya ili kutoa fursa za ajira  na vijana hao waweze kunufaika na matunda ya mradi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge  la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ameeleza kuwa wananchi wa Mbeya wamekuwa wakisubiri kwa hamu upanuzi wa barabara hiyo kukamilika ili kutatua changamoto za msongamano wa magari jijini humo.


Dkt. Tulia ameiomba Wizara ya Ujenzi kufanyia kazi mapendekezo yaliyoombwa katika barabara hiyo ya kuongezwa kwa barabara kilometa 3.5 kuanzia Ifisi hadi Songwe Airport na kilometa 5 kuanzia Nsalaga kuelekea Mlima Nyoka katika Bajeti mpya ya mwaka 2025/26 ili wananchi wa Mbeya kuendelea kunufaika na ujenzi wa mtandao wa barabara jijini humo.

Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Eng. Matari Masige ameeleza kuwa Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa matabaka ya udongo G3, G7 na  G15, ujenzi wa makalvati madogo na makubwa pamoja na ujenzi wa daraja la Nzovwe katika barabara hiyo.

Sunday, April 20, 2025

MALIASILI SC YAIBURUZA TAMISEMI 2-1

.......

Na Sixmund Begashe

Timu ya Wanawake ya mchezo wa kuvuta kamba ya MNRT Sports Club ya Wizara ya Maliasili na Utalii, imeiburuza vikali 2-1 timu ya TAMISEMI wanawake katika mchezo wa marudiano uliofanyika leo Mkoani Singida kwenye mashindano ya Maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi Duniani (MEI MOSI 2025).

Wakizungumzia michezo hiyo inayoshika kasi Mjini Singida, mashabiki mbalimbali wamesikika wakisema kuwa mashindano ya mwaka huu yamekuwa na mvuto mkubwa kutokana na timu za Wizara hiyo inayojishighulisha na Uhifadhi na Utalii nchini kuwa moto mkali kwa timu zingine pinzani.

"Hawa wachezaji wa Maliasili, sijui mwaka huu wamekula nini, wamekuwa na nguvu zaajabu mithili ya tembo wa Tarangire, hii inatupatia rahaa sana, wameleta changamoto kubwa kwa timu pinzani" alisema Bw. Ally Ramadhan, mkazi wa Gidasi Manyara.

Katika mchezo uliochezwa jana jioni timu ya Mpira wa Miguu wanaume iliwalegezea nguvu wapinzani wao timu ya Ardhi na kuwapa heshma ya sare (0-0), huku Mwenyekiti wa Club hiyo Bw. Gervas Mwashimaha, amesema bahati ya zawadi ya Sikukuu ya Pasaka waliyoipata timu ya Ardhi isitegemewe kwa timu nyingine yeyote kwenye michezo hiyo itakayofikia kilele chake siku moja kabla ya sherehe za Mei Mosi 2025 Mkoani Singida.

 

MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI IBADA YA SIKUKUU YA PASAKA


..................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa wazazi hususani wakinamama kuwaongoza watoto wao hasa vijana kuacha tabia ya kushabikia vurugu wakati wa kampeni na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu.

Makamu wa Rais ametoa rai hiyo mara baada ya kushiriki Ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege Dodoma. Amewasihi Watanzania kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu kwa kuwa vurugu sio sehemu ya jadi ya Watanzania.

Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa wote watakaopata dhamana ya kusimamia uchaguzi kuhakikisha wanazingatia sheria na miongozo watakayopewa pamoja na kutenda haki kwa wote watakaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.

Halikadhalika, Makamu wa Rais amewasihi watumiaji wa vyombo vya moto kuwa na busara na umakini katika matumizi ya vyombo hivyo ili kuepusha kupoteza Maisha ya watu barabarani.

Makamu wa Rais amewatakia heri na baraka watanzania wote katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka na kuwasihi kusherehekea kwa amani na furaha.

Ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na Mwenza wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango imeongozwa na Padre Dionis Paskal Safari. 

Saturday, April 19, 2025

MALIASILI SC YAIHUKUMU MAHAKAMA 28–18

**********

Na Sixmund Begashe

Timu ya Mpira wa Pete ya Wanawake ya Wizara ya Maliasili na Utalii imeifunga vikali Timu ya Wanawake ya Mahakama kwa mabao 28 kwa 18 katika mchezo uliochezwa leo kwenye uwanja wa michezo wa VETA, mkoani Singida.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo uliovutia mashabiki wengi, Bi. Getrude Kassara, Mratibu wa Michezo wa Wizara ya Maliasili na Utalii, amesema ushindi huo ni zawadi mahsusi kwa Viongozi na Watumishi wa wizara hiyo, ambayo inaongoza kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni.

"Tumejiandaa vizuri sana, hatuna sababu ya kutofanya vizuri. Hiki kichapo tulichokipa timu ya Mahakama, ndicho kitakachozikumba na timu nyingine," alijigamba Bi. Kassara.

Timu zinazoshiriki mashindano ya mwaka huu ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (MEI MOSI), mkoani Singida, zinaendelea kuingiwa na hofu zaidi zinapobaini kuwa zinakutana na timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kutokana na uimara wa wachezaji wa Maliasili Sports Club.

Friday, April 18, 2025

IMF YAKUNWA NA UTEKELEZAJI MIPANGO YA TANZANIA YA KUKUZA UCHUMI NA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiongoza kikao cha kuhitimisha vikao vya majadiliano kati ya Serikali na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuhusu tathimini ya awamu ya tano ya utekelezaji wa program ya Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha ufadhili wa dola za Marekani bilioni 1.832, kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii pamoja na awamu ya pili ya utekelezaji wa program ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la Resilient and Sustainable Fund (RSF) yenye jumla ya ufadhili wa dola za Marekani bilioni 1.832, kutoka Shirika hilo,  tukio liliofanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha, Dar es Salaam)
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
 
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amelihakikishia Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwamba, Serikali itaendelea kufanya maboresho ya sera na mipango yake kwa kuhakikisha sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii pamoja na kuimarisha sekta binafsi zinapewa kipaumbele.
 
Dkt. Nchemba amesema hayo wakati akifunga vikao vya majadiliano kati ya Serikali na Timu ya Wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), baada ya kukamilisha tathimini ya awamu ya tano ya utekelezaji wa program ya Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii pamoja na awamu ya pili ya utekelezaji wa program ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la Resilient and Sustainable Fund (RSF) kutoka Shirika hilo.
 
Akifunga vikao hivyo katika Kikao cha majumuisho kilichofanyika Benki Kuu  ya Tanzania (BoT), Jijini Dar es Salaam, Dkt. Nchemba, alieleza kufurahishwa kwake na taarifa iliyowasilishwa na Kiongozi wa Timu hiyo Bw. Nicolas Blancher, inayoonesha kuwa Tanzania imetekeleza ipasavyo vigezo vilivyowekwa na Shirika hilo katika mipango hiyo ya ECF na RSF.
 
Aliahidi kuwa Serikali itaendelea kusimamia ipasavyo utekelezaji wa programu hizo mbili zenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 1.832, ambapo kiasi cha dola bilioni 1.1 ni kwa ajili ya Mpango wa kuimarisha Uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na kiasi cha dola milioni 786 ni kwa ajili ya Mpango wa nchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambapo program hizo mbili zinatekelezwa katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2022/2023 hadi 2025/2026.
 
Kwa upande wake, Kiongozi wa Timu ya Wataalam kutoka IMF waliofanya tathimini hiyo, Bw. Nicolas Blancher, alisema kuwa tathimini yao ya awamu ya tano imeonesha kuwa Tanzania imetekeleza vizuri mpango wa ECF na RSF na kushauri hatua kadhaa zinazotakiwa kuendelea kuchukuliwa ikiwemo kuimarisha zaidi huduma za jamii na kuendelea kuimarisha mazingira bora ya kufanyabiashara na uwekezaji. 
 
“Matarajio ya uchumi wa Tanzania ni mazuri kwakuwa utaendelea kukua kwa kasi, huku mfumuko wa bei ukiendelea kuwa chini, nakisi ya mauzo na manunuzi ya bidhaa na huduma nje ya nchi ikipungua, na upatikanaji wa fedha za kigeni ukiongezeka” alisema Bw. Blancher.
 
Aliongeza kuwa hatua za kuwianisha vizuri mapato na matumizi ya serikali katika mwaka wa fedha wa 2025/26, zitasaidia kuhifadhi uhimilivu wa deni la serikali, huku zikilinda matumizi yenye kipaumbele katika huduma za kijamii. 
 
Bw. Blancher alisema kuwa kuendelea kutekeleza sera za kukabiliana na athari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, zinazoungwa mkono na mpango wa RSF, kutasaidia kujenga ustahimilivu katika kushughulikia madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
 
Alisema kuwa mapendekezo ya tathimini hiyo yatapelekwa mbele ya Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na kwamba uamuzi utakaotolewa na Bodi utaiwezesha Tanzania kupokea ufadhili wa dola za Marekani milioni 441.
 
Tanzania imefanyiwa Tathimini ya Awamu ya Tano ili iweze kupata fedha kutoka IMF kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ambapo hadi sasa Program ya ECF imepokea kiasi cha dola za Marekani milioni 754.3 kati ya dola za Marekani bilioni 1.1 na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 55 zimepokelewa  kupitia dirisha la RSF, mradi wenye thamani ya dola za Marekani milioni 786.
 
Kikao hichi kilihudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, na Manaibu Gavana, pamoja na Maafisa Waandamizi wa Serikali na wajumbe wa Timu ya Tathimini kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF.

BUGUMBA ATOA UJUMBE MAADHIMISHO SIKU YA MALIKALE

Mhifadhi Mkuu Mambo ya Kale na Mkuu wa Kanda ya Magharibi Makumbusho na Malikale anayesimamia uhifadhi na uendelezaji maeneo ya kusini mwa Tanzania Lindi na Mtwara Revocatus Bugumba akizungumzia  siku ya Kimataifa ya Malikale ambayo hufanyika tar 18 April ya kila mwaka.

Mhifadhi Mkuu Mambo ya Kale na Mkuu wa Kanda ya Magharibi Makumbusho na Malikale anayesimamia uhifadhi na uendelezaji maeneo ya kusini mwa Tanzania Lindi na Mtwara Revocatus Bugumba akionyesha jengo la Makumbusho ya awali ambalo sasa linabaki kama malikale.

.....................

NA MUSSA KHALID

Watanzania wametakiwa kushiriki kutembelea maeneo ya Malikale zilizopo nchini ikiwemo kuzuia uharibifu wake ili waweze kujifunza historia ya nchi yao.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mhifadhi Mkuu Mambo ya Kale na Mkuu wa Kanda ya Magharibi Makumbusho na Malikale anayesimamia uhifadhi na uendelezaji maeneo ya kusini mwa Tanzania Lindi na Mtwara Revocatu Bugumba wakati akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi katika kuadhimisha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Malikale ambayo hufanyika tar 18 April ya kila mwaka.

Bugumba  amesema kuwa Malikale zinajumuisha maeneo na kumbukumbu za kihistoria ambayo yanahifadhiwa ikiwemo majengo ,bustani,maeneo ya kumbukumbu za kivita.

Akitolea mfano wa mji wa Dar es salaam kumesheheni maeneo ya majengo ya kale kama makanisa,mahekalu ya wahindi,majengo ya kiserikali ,maeneo ya mnazi mmoja,majengo kuanzia Ikulu na hata bustani za kale.

‘Kiujumla maeneo mengi ya Malikale huwa yanaathiriwa kwa changamoto za kiasili ambazo ni kama mabadiliko ya Tabia ya nchi,mvua kali ukame na kutokea kwa matukio makubwa yakiwemo vita” amesema Bugumba

Amesema msingi wa dhima ya Malikale imesisitiza kufanya ukusanyaji wa kumbukumbu ikiwemo kufanya tathmini ya maeneo ya malikale na kuyaweka kwenye orodha jambo ambalo litazuia uharibu.

Bungua amesema mpango mwingine ni kusisitiza jamii ishirikishwe kwa namna mbalimbali lakini pia usimamizi kuhakikisha inatumiwa mbinu za asili za uhifadhi za Malikale ili kuepukana na mtindo wa kuondoa thamani ya maeneo hayo na kuweka vitu vya kisasa.

Pia ametumia fursa hiyo kuisistiza jamii kutoa taarifa kuhusu Malikale zilizopo kwenye maeneo yao ambazo zinataka kuharibiwa  ili ziweze kuhifadhiwa kwa muda mrefu.

Katika hatua nyingine ,Bugumba ametoa rai kwa Mamlaka za serikali za mitaa kuendeleza maeneo ya Malikale zilizopo kwenye miji yao ili kutopoteza uhalisia na historia ya maeneo hayo.

Mwaka huu 2025 maadhimisho hayo yanakwenda na kauli mbiu ya kuangazia madhara ya majanga na migogoro katika maeneo ya Malikale lakini pia kutafakari miaka sitini ya utekelezaji wa baraza la kimataifa la Malikale katika kutatua migogoro ya malikale na kushughulikia majanga yanayoathiri malikale hizo.

Zoezi la Uhakiki Malipo ya Mbolea za Ruzuku kwa Wakulima wa Tumbaku Tabora larizisha

............
 
Tabora, 

Katika kuhakikisha wakulima wa tumbaku wanapata ruzuku za mbolea Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw. Joel Laurent, amefanya ziara ya kikazi katika vituo viwili vinavyo hakiki taarifa hizo mkoani Tabora kujionea maendeleo ya zoezi hilo na kuhakikisha linakamilika kwa wakati.

Baada ya kutembelea vituo hivyo katika ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika Mirambo na ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU), Bw. Laurent amesema kuwa, zoezi hilo limefikia hatua nzuri itakayowezesha kuanza kwa taratibu za malipo kwa wakulima wa Tumbaku nchini. 

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Laurent ameeleza kuwa, lengo la uhakiki ni kuhakikisha wakulima wote waliozalisha Tumbaku katika msimu wa mwaka 2023/2024 wanalipwa na fedha hizo zinamfikia mkulima anayestahili moja kwa moja kupitia akaunti yake.

Ameeleza kuwa, zoezi hili linafanyika kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Kilimo, TFRA, TCDC na vyama vikuu vya ushirika vilivyo chini ya shirikisho la TCJE.

Akizungumza na Mkurugenzi Laurent, Ndg. Innocent Nsena Katibu Tawala wa Wilaya ya Urambo alieleza kuwa, suala la ruzuku limekuwa kilio cha muda mrefu kutoka kwa wakulima na kwamba utekelezaji wa mpango huu utapunguza gharama za uzalishaji kwa mkulima.

“Ninamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia ombi la kutoa ruzuku kwa wakulima wa tumbaku, kwa kuwa zao hili awali halikuwa miongoni mwa mazao yanayopata ruzuku” alisema Ndg. Nsena.

Kwa upande mwingine, akitoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi la uhakiki katika ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika WETCU, kiongozi wa timu hiyo, Ndg. Byaga Nzohumpa, alieleza kuwa, zoezi hilo limekamilika kwa asilimia 100 baada ya kuhakiki taarifa za vyama vya msingi 248 walivyokabidhiwa.

Naye Ndg. Godwin Mwalongo, kiongozi wa timu ya uhakiki katika ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika Mirambo, amesema kuwa, kazi ya uhakiki imefikia hatua nzuri na inatarajiwa kukamilika kwa wakati.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TCJE, Ndg. Seleman Abasi Maona, alieleza kuwa, miongoni mwa changamoto kubwa zilizokabili zoezi hilo ni uandaaji hafifu wa takwimu za wakulima wa tumbaku kwa msimu wa kilimo wa 2023/2024, hasa kutokana na taarifa zisizo sahihi kutoka kwa wakulima.

Alisisitiza kuwa kama kungekuwepo mfumo madhubuti wa ukusanyaji taarifa kuanzia ngazi ya chini, changamoto hizo zingeweza kuepukwa na kuahidi kuboresha kwa ajili ya manufaa ya baadaye kwa wakulima