JSON Variables

Tuesday, April 22, 2025

VITONGOJI 82 TARIME VIJIJINI KUPELEKEWA UMEME NA MRADI WA HEP IIB-KAPINGA

..............................

📌Taasisi 3000 zaunganishiwa umeme na fedha za Covid 19

Vitongoji 82 ambavyo bado havijafikiwa na umeme katika Wilaya ya Tarime mkoni Mara vitapelekewa umeme kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili B  (HEP IIB) ambapo tayari zabuni ya kuwapata wakandarasi wa mradi huo imeshatangazwa na inatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, tarehe 22 Aprili, 2025 Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara aliyetaka kufahamu lini Vitongoji vyote vya Tarime, vitapata Umeme.

Amefafanua kuwa  Jimbo la Tarime Vijijini lina jumla ya Vitongoji 500 ambapo vitongoji 225 tayari vina umeme, vitongoji 52 Wakandarasi wapo wanaendelea na kazi, na vitongoji 82 zabuni ya kuwapata Wakandarasi imetangazwa kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili B  (HEP IIB) na vitongoji 141 vilivyosalia vitaendelea kupelekewa umeme kupitia miradi ijayo.

Kuhusu mpango wa Serikali wa kuunganisha Umeme katika taasisi mbalimbali kupitia fedha za mradi wa Covid 19, Kapinga amesema tayari Serikali ilishaanza kutekeleza mpango huo ambapo mpaka sasa zaidi ya taasisi 3000 zimeshaunganishwa na umeme zikiwemo taasisi za Elimu, Afya, Dini, Migodi pamoja na visima vya maji.

Vilevile amesema kuwa Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imeendelea kuwapatia umeme wananchi kupitia miradi mbalimbali ya umeme.

JUKWAA LA KIMATAIFA LA UTALII WA VYAKULA KUKUTANISHA WABOBEZI WA UTALII ZAIDI YA 300

..............

Arusha

Jukwaa la Pili la Kimataifa la Utalii Wa Vyakula la Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) Kanda ya Afrika lililoanza leo Aprili 22, 2025 jijini Arusha linatarajia kukutanisha washiriki takribani 300 wakijumuisha viongozi waandamizi katika sekta ya utalii na ukarimu, watumishi wa serikali, pamoja na wataalamu wa masuala ya upishi kutoka ndani na nje ya Afrika.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameyasema hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Hoteli ya Gran Melia jijini Arusha.

“Tukio hili linalenga kuangazia uhusiano muhimu kati ya utamaduni wa upishi na utalii, pamoja na kufanya tathmini ya mchango wa utalii wa vyakula katika kukuza maendeleo ya kiuchumi, kuhifadhi urithi wa kiutamaduni, na kuboresha maisha ya jamii linaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism), pamoja na Basque Culinary Center” amesema Mhe. Chana.

Amefafanua kuwa  hafla ya ufunguzi wa Jukwaa hilo itafanyika tarehe 23 Aprili, 2025, ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango.

Mhe. Chana ameongeza kuwa kupitia jukwaa hilo la kihistoria Tanzania itapata fursa ya kuonesha utajiri wa vyakula vya asili vinavyotokana na makabila zaidi ya 120 nchini Tanzania.

“Jukwaa hili litakuwa ni sehemu mahsusi ya kukuza utalii wa chakula, na hivyo kuongeza wigo wa mazao ya utalii nchini, kuwezesha wageni kukaa muda mrefu zaidi nchini na kuchochea mchango wa utalii katika uchumi wa taifa letu” amesisitiza Mhe. Chana.

Waziri Chana ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wadau wote wa sekta ya utalii na mapishi, pamoja na wananchi wote, kushiriki kikamilifu katika kuunga mkono na kuendeleza dhana hiyo muhimu ya utalii wa vyakula, kwa mustakabali wa maendeleo ya sekta ya utalii na utambulisho wa Taifa letu kimataifa.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Shirika la Utalii Duniani, Elcia Grandcourt, amesema jukwaa la kimataifa la utalii wa vyakula litasaidia kukuza utalii hasa vijijini na kuhifadhi utamaduni wa asili.

"Hii ni nafasi yetu ya kuonyesha tunachoweza kutoa sio tu kutoka Tanzania bali katika Bara lenyewe la Afrika" amesema Bi. Grandcourt.

Jukwaa hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wa kimataifa wakiwemo Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii Duniani, Bw. Zurab Pololikashvili, pamoja na Mke wa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Dkt. Auxillia C. Mnangagwa.


RAIS MWINYI ASHIRIKI SALA YA MAZISHI YA MAREHEMU SANYA

,
..............................

Rais wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt,Hussein Ali Mwinyi amejumuika na Wananchi katika Mazishi ya Marehemu Muhammad Ibrahim Sanya yaliofanyika Leo .

Rais Dkt,Mwinyi aliwaongoza  Waumini wa Dini ya Kiislamu katika Sala ya Maiti  katika Msikiti Jibril Mkunazini , Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 22 Aprili 2025.

Marehemu Ibrahim Sanya amefariki Jana  wakati akitibiwa  katika Hospitali ya  Rufaa ya Mkoa Wa Mjini Magharibi Lumumba .

Wakati wa Uhai wake Marehemu Ibrahim  Sanya aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Jimbo la Mkunazini  kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF).

Marehemu Sanya amezikwa eneo la Makaburi ya Kijitoupele,Wilaya ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi.

MAJALIWA AMWAKILISHA RAIS DKT. SAMIA KIKAO KAZI CHA MAAFISA UTAMADUNI NA MICHEZO

******

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Aprili 22, 2025 anamwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa kikao kazi cha 15 cha Maafisa Utamaduni na Maafisa Maendeleo ya Michezo Tanzania.

Kikao hicho cha Mafundo na Mazingativu kinalenga kujadili maendeleo ya sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Pia kikao hicho kinatoa nafasi kwa washiriki kujadili fursa za sekta, kubaini changamoto zinazoikabili sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo na kupendekeza njia za utatuzi wa changamoto hizo.






 

ULEGA ATOA SIKU 30 KWA MKANDARASI BARABARA YA NSALAGA - IFISI KUWEKWA LAMI


Waziri wa Ujenzi,  Abdallah Ulega ametoa siku 30 na kumtaka Mkandarasi Kampuni ya CHICO anayetekeleza ujenzi wa upanuzi wa barabara ya Nsalaga - Ifisi (km 29) kwa njia nne, jijini Mbeya kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo ili uweze kukamilika na kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo.


Aidha, Waziri Ulega amemuagiza Mkandarasi huyo kufanya kazi usiku na mchana, kuongeza vifaa pamoja wafanyakazi ili kufanikisha mradi huo ukamilike haraka iwezekanavyo.


Ulega ametoa maelekezo hayo jijini Mbeya wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya mradi huo na kutoridhishwa na hatua za utekelezaji wake ambao hadi sasa umefikia asilimia 25.

Ulega ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari imeshatoa malipo ya Shilingi Bilioni 35 kwa Mkandarasi huyo na matarajio yake ni kuona kupitia fedha hizo angalau kilometa kadhaa za lami zimekamilishwa kujengwa katika barabara hiyo.


“Serikali imeshatoa Bilioni 35 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kutoka Nsalaga hadi Ifisi, na fedha hizi Mkandarasi hajazifanyia kazi ipasavyo, Sasa basi Nimemuagiza Mkandarasi afanye kazi usiku na mchana na kuona mabadiliko ya haraka katika mradi huu”, amesisitiza Ulega.


Pia,  ametoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mbeya kumsimamia Mkandarasi kwa ukaribu ili hadi kufikia mwanzoni mwa Mwezi Juni mwaka huu Mkandarasi awe amekamilisha  kilometa 10 za lami katika barabara hiyo na kuahidi kurudi tena kwa ajili ya kukagua maendeleo hayo.

Ulega amemuelekeza Meneja huyo wa TANROADS kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unaenda sambamba na ufungaji wa taa za barabarani ili kuupendezesha mji wa Mbeya na kuimarisha masuala ya ulinzi na usalama wa wananchi wanaotumia barabara hiyo katika shughuli zao za kiuchumi za kila siku.


Vilevile, Ulega amepokea Ombi la Mbunge wa Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson la ujenzi wa kilometa tano za lami zinazoingia katika mitaa ya iiji la Mbeya na kuahidi kulifanyia kazi.


Kadhalika, Ulega amemuagiza Meneja wa TANROADS mkoa wa Mbeya kumsimamia Mkandarasi katika kuhakikisha kazi ndogondogo   zinazofanywa na Mkandarasi zinatolewa kwa vijana wa Mkoa wa Mbeya ili kutoa fursa za ajira  na vijana hao waweze kunufaika na matunda ya mradi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge  la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ameeleza kuwa wananchi wa Mbeya wamekuwa wakisubiri kwa hamu upanuzi wa barabara hiyo kukamilika ili kutatua changamoto za msongamano wa magari jijini humo.


Dkt. Tulia ameiomba Wizara ya Ujenzi kufanyia kazi mapendekezo yaliyoombwa katika barabara hiyo ya kuongezwa kwa barabara kilometa 3.5 kuanzia Ifisi hadi Songwe Airport na kilometa 5 kuanzia Nsalaga kuelekea Mlima Nyoka katika Bajeti mpya ya mwaka 2025/26 ili wananchi wa Mbeya kuendelea kunufaika na ujenzi wa mtandao wa barabara jijini humo.

Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Eng. Matari Masige ameeleza kuwa Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa matabaka ya udongo G3, G7 na  G15, ujenzi wa makalvati madogo na makubwa pamoja na ujenzi wa daraja la Nzovwe katika barabara hiyo.

Sunday, April 20, 2025

MALIASILI SC YAIBURUZA TAMISEMI 2-1

.......

Na Sixmund Begashe

Timu ya Wanawake ya mchezo wa kuvuta kamba ya MNRT Sports Club ya Wizara ya Maliasili na Utalii, imeiburuza vikali 2-1 timu ya TAMISEMI wanawake katika mchezo wa marudiano uliofanyika leo Mkoani Singida kwenye mashindano ya Maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi Duniani (MEI MOSI 2025).

Wakizungumzia michezo hiyo inayoshika kasi Mjini Singida, mashabiki mbalimbali wamesikika wakisema kuwa mashindano ya mwaka huu yamekuwa na mvuto mkubwa kutokana na timu za Wizara hiyo inayojishighulisha na Uhifadhi na Utalii nchini kuwa moto mkali kwa timu zingine pinzani.

"Hawa wachezaji wa Maliasili, sijui mwaka huu wamekula nini, wamekuwa na nguvu zaajabu mithili ya tembo wa Tarangire, hii inatupatia rahaa sana, wameleta changamoto kubwa kwa timu pinzani" alisema Bw. Ally Ramadhan, mkazi wa Gidasi Manyara.

Katika mchezo uliochezwa jana jioni timu ya Mpira wa Miguu wanaume iliwalegezea nguvu wapinzani wao timu ya Ardhi na kuwapa heshma ya sare (0-0), huku Mwenyekiti wa Club hiyo Bw. Gervas Mwashimaha, amesema bahati ya zawadi ya Sikukuu ya Pasaka waliyoipata timu ya Ardhi isitegemewe kwa timu nyingine yeyote kwenye michezo hiyo itakayofikia kilele chake siku moja kabla ya sherehe za Mei Mosi 2025 Mkoani Singida.

 

MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI IBADA YA SIKUKUU YA PASAKA


..................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa wazazi hususani wakinamama kuwaongoza watoto wao hasa vijana kuacha tabia ya kushabikia vurugu wakati wa kampeni na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu.

Makamu wa Rais ametoa rai hiyo mara baada ya kushiriki Ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege Dodoma. Amewasihi Watanzania kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu kwa kuwa vurugu sio sehemu ya jadi ya Watanzania.

Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa wote watakaopata dhamana ya kusimamia uchaguzi kuhakikisha wanazingatia sheria na miongozo watakayopewa pamoja na kutenda haki kwa wote watakaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.

Halikadhalika, Makamu wa Rais amewasihi watumiaji wa vyombo vya moto kuwa na busara na umakini katika matumizi ya vyombo hivyo ili kuepusha kupoteza Maisha ya watu barabarani.

Makamu wa Rais amewatakia heri na baraka watanzania wote katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka na kuwasihi kusherehekea kwa amani na furaha.

Ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na Mwenza wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango imeongozwa na Padre Dionis Paskal Safari. 

Saturday, April 19, 2025

MALIASILI SC YAIHUKUMU MAHAKAMA 28–18

**********

Na Sixmund Begashe

Timu ya Mpira wa Pete ya Wanawake ya Wizara ya Maliasili na Utalii imeifunga vikali Timu ya Wanawake ya Mahakama kwa mabao 28 kwa 18 katika mchezo uliochezwa leo kwenye uwanja wa michezo wa VETA, mkoani Singida.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo uliovutia mashabiki wengi, Bi. Getrude Kassara, Mratibu wa Michezo wa Wizara ya Maliasili na Utalii, amesema ushindi huo ni zawadi mahsusi kwa Viongozi na Watumishi wa wizara hiyo, ambayo inaongoza kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni.

"Tumejiandaa vizuri sana, hatuna sababu ya kutofanya vizuri. Hiki kichapo tulichokipa timu ya Mahakama, ndicho kitakachozikumba na timu nyingine," alijigamba Bi. Kassara.

Timu zinazoshiriki mashindano ya mwaka huu ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (MEI MOSI), mkoani Singida, zinaendelea kuingiwa na hofu zaidi zinapobaini kuwa zinakutana na timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kutokana na uimara wa wachezaji wa Maliasili Sports Club.