JSON Variables

Wednesday, April 23, 2025

KAMPUNI ZISIZO JIORODHESHA DSE KUTOFAHAMU THAMANI HALISI YA UWEKEZAJ


Serikali imesema kuwa Kampuni ambazo hazijaorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) hukutana na changamoto za kutofahamu thamani halisi ya uwekezaji kutokana na kukosekana kwa ukwasi wa hisa zao.


Hayo yalisemwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Geita Mjini, Mhe. Constantine John Kanyasu, aliyetaka kujua hasara na faida kwa kampuni kutotekeleza Sheria ya kujiorodhesha kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam.


Mhe. Chande alisema kuwa Kampuni ambazo hazijajiorodhesha katika Soko la Hisa hutawaliwa na kukosekana kwa uwazi na hivyo Serikali na wanahisa kushindwa kupata taarifa stahiki za mwenendo wa biashara na fedha.


“Kwa mujibu wa Sheria, ni Kampuni ya simu pekee ndio hulazimika kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa katika soko la hisa  isipokuwa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa kwa asilimia 25 au zaidi  na Kampuni ambazo zinatoa huduma ya minara ya simu”, alisema Mhe. Chande.


Aidha alizitaja faida za Kampuni kujiorodhesha kwenye Soko la Hisa kuwa ni pamoja na kuongeza mtaji, kuongeza ufanisi na tija, kuiwezesha Serikali kupata mapato stahiki na  kutambua thamani halisi ya hisa zake ambapo wanahisa wanapata thamani ya hisa zao wanapotaka kuuza kwa kufuata mwenendo wa soko (demand and supply).


Alisema faida nyingine ni pamoja na kuwapa wananchi fursa ya kununua hisa na hivyo kuwezeshwa kushiriki katika uchumi wa nchi na kutoa fursa kwa wawekezaji wanaotaka kuuza uwekezaji wao wakati wanapohitaji fedha.

MH. S. S. H, AMPONGEZA ALPHONCE BAADA YA KUSHIKA NAFASI YA PILI KWENYE MBIO ZA BOSTON

 

Pongezi za dhati kwa Alphonce Simbu kwa kushika nafasi ya pili katika Mashindano ya Kimataifa ya Mbio ya Boston (Boston Marathon). Umefanya kazi nzuri.


Ushindi wako ni matokeo ya kujituma kwa bidii, maandalizi mazuri, nidhamu yako kuanzia jeshini, kwenye mazoezi hadi kwenye mashindano, ukilibeba kwa heshima ya hali ya juu jina la nchi yetu. 


Endelea kuipeperusha vyema bendera ya Taifa letu.

DKT. MWAMBA ASHIRIKI MKUTANO WA AU KUJADILI AJENDA KWENDA G20

 

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, ameshiriki Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu za Afrika, uliojadili maeneo ya kipaumbele ambayo nchi za Afrika zinahitaji kuyasukuma kama agenda mahususi katika mikutano ya Kundi la nchi 20 Tajiri Duniani (G20) kwa mwaka 2025 ambapo Nchi ya Afrika Kusini ni mwenyekiti wa G20, Mkutano uliofanyika katika Ofisi za Kamisheni ya Umoja wa Afrika, kando ya mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Jijini Washington D.C, Marekani.

Aidha, majadiliano katika mkutano huo pamoja na mambo mengine, yaliangazia kuhusu Afrika kuwa na sauti moja katika kuzishawishi nchi za G20 kufanya mabadiliko yatakayosaidia upatikanaji wa fedha na mikopo nafuu kwa nchi zinazoendelea, namna ya kukabiliana na madeni, suala ambalo ni tatizo kwa nchi nyingi za Afrika kufuatia mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi, kijiografia na kisiasa.  

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, Naibu Gavana wa BoT, Dkt. Yamungu Kayandabila, Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, na Maafisa wengine waandamizi wa Serikali.

MHE. KATAMBI ASISITIZA UMUHIMU WA MICHEZO KWA WAFANYAKAZI

 

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi ametoa wito kwa Waajiri na Vyama vya Wafanyakazi kuweka msukumo kwa wafanyakazi kushiriki katika michezo ili kuimarisha afya zao.


Mhe. Katambi ameyasema jana Aprili 22, 2025 katika viwanja vya CCM Liti mkoani Singida wakati wa akifungua michezo ya Mei Mosi Taifa 2025 yenye kauli “Michezo kwa Afya, Ajira, Furaha, na Kazi Inaendelea. Wafanyakazi Tushiriki vyema Uchaguzi wa 2025 Tupate Viongozi Bora. Mshikamano Daima” 

"Michezo ni Afya na njia nzuri ya kujenga umoja na mahusiano mema mahali pa kazi, hivyo kuwa na afya bora kutawawezesha kutoa huduma nzuri kwa wananchi” amesema 


Aidha Mhe. Katambi amempongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwa chachu ya mafanikio makubwa katika sekta ya michezo ikiwemo kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo katika maeneo mbalimbali nchini.


“Jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeleta mafanikio katika michezo nchini tumeshuhudia hali ilivyo katika mchezo wa mpira wa miguu kupitia Goli la Mama namna lilivyowajenga wachezaji kuwa na hamasa” amesema.

Kadhalika, Naibu Waziri Katambi ametoa rai kwa waajiri kuhakikisha wanatenga muda kwa watumishi kufanya mazoezi na hivyo kujiepusha na magonjwa yanayoweza kuepukika.

HIZI HAPA HABARI KUBWA ZILIZO PEWA NAFASI KUBWA KATIKA KURASA ZA MBELE YA MAGAZETI LEO 23.04.2025

 Ikumbatie Mkisi Digital kwa Habari Moto Moto kutoka kote ulimwenguni, tunaangazia kwenye nyanja zote,  Karibu kupitia habari kubwa zilizo pewa nafasi kubwa katika kurasa za mbele ya magazeti ya leo tarehe 23.04.2025.






























Tuesday, April 22, 2025

TULINDE, TUENZI UTAMADUNI KWA MANUFAA YA VIZAZI VYETU- MAJALIWA

 

▪️Amesema tusikumbatie tamaduni zinazokwenda kinyume na maadili na ustaarabu


▪️Prof. Kabudi asema sarakasi ni mchezo unaongoza kuliingizia Taifa fedha za kigeni

 


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Watanzania wana wajibu wa pamoja wa kuhakikisha urithi wa utamaduni wa Taifa unalindwa, unaenziwa na kuendelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

 

Amesema hatuwezi kuwa na Taifa bila kuwa na utamaduni unaolitambulisha na kututofautisha na mataifa mengine. “Utamaduni ni utambulisho wetu halisi kama Taifa. Utamaduni wa Taifa letu ndiyo unatufanya tutambuliwe kuwa sisi ni Watanzania bila kujadili tofauti za makabila, jamii au sehemu tunazotoka.”

 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 22, 2025) alipofungua Kikao Kazi cha 15 cha Maafisa Utamaduni na Maendeleo ya Michezo kilichofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

 

“Kamwe tusikubali kukumbatia tamaduni zinazokwenda kinyume na maadili na ustaarabu wetu. Tusikubali kuwa watumwa wa tamaduni za kigeni ambazo zinadhalilisha utu wetu. Pamoja na umuhimu wa kujifunza mambo mazuri ya tamaduni nyingine ni lazima kuchuja nini cha kuchukua na nini cha kuacha.”

 


Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia Watanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inathamini sekta za utamaduni, sanaa na michezo kutokana na umuhimu wake kwa ustawi wa Taifa, hivyo wananchi washirikiane kuwarithisha watoto na vijana misingi ya utamaduni.

 

Aidha, Waziri Mkuu amesema pamoja na utambulisho wa jamii, kupitia sekta za  utamaduni, sanaa na michezo, pia jamii inapata manufaa makubwa ikiwemo kuzalisha ajira kwa mamilioni ya Watanzania na kukuza uchumi wa Taifa.


Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa sekta hizo pamoja na kutumika kusukuma agenda mbalimbali za Kitaifa pia ni chanzo cha furaha, burudani, kuelimisha, kuonya na kuhamasisha umma katika nyanja mbalimbali.

Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzipa kipaumbele sekta za utamaduni, Sanaa na michezo na hivyo kuziwesha kuwa na mafanikio makubwa. “Michezo ina nguvu na ushawishi mkubwa katika kuleta maendeleo na miongoni mwa michezo inayoongoza kuliletea Taifa fedha nyingi za kigeni ni riadha.”


Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Mchezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Tabia Maulid Mwita amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na mageuzi makubwa aliyoyafanya katika sekta.

 

Awali, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Hamisi Mwinjuma amesema kuwa ili kuendelea kuvutia mageuzi ya kidijitall, Wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI, imefanikisha uunganishaji wa Mfumo wa Wadau wa Sanaa (AMIS) na Mfumo wa TAUSI. Ametolea mfano mapato ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) yameongezeka kwa asilimia 200 kutokana na kuunganishwa kwa mifumo hiyo ya makusanyo.

 

Amesema kuwa hatua hiyo si tu imeimarisha usimamizi wa sekta ya sanaa, bali pia imefungua ukurasa mpya wa uwazi, urahisi wa upatikanaji wa huduma, na uboreshaji wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali. “Kuanzia tarehe 26 Februari 2025, mifumo hii miwili inafanya kazi kwa pamoja, na sasa wadau katika maeneo 15 ya biashara - ikijumuisha studio za muziki, picha, video, huduma za burudani na ubunifu - wanaweza kupata vibali kwa njia moja ya haraka na ya wazi zaidi.”

 

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema kuwa Kikao kazi hicho ni cha kimkakati katika kuleta mabadiliko makubwa kwa sekta za utamaduni, sanaa na michezo ikiwa ni pamoja na kurahisisha utekelezaji wa maazimio ya vikao vilivyopita.

 

Amesema kuwa kupitia vikao kazi vilivyopita, Wizara imewezesha kuanzishwa kwa Kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa,Kujengewa uwezo kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa usajili wa vyama na vilabu vya michezo nchini

 

“Kupitia vikao hivi, tumeweza kuongeza idadi ya wataalamu wa utamaduni kutoka 43 mwaka 2021 mpaka 123 mwaka 2025 na Maafisa Maendeleo ya Michezo kutoka 48 mwaka 2021 hadi Maafisa Maendeleo ya Michezo 139 mwaka 2025”

WATAALAMU KUTOKA OFISI ZA UMOJA WA AFRIKA (AUC) WATEMBELEA TMA.


Dar es Salaam.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imepokea timu ya wataalamu kutoka Ofisi za Umoja wa Afrika (AUC) wanaoratibu utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma za hali ya hewa wa “Intra-ACP Climate Services and related Applications Programme (ClimSA)”.

Ziara hiyo ilifanyika tarehe 17 Aprili, 2025 ikioongozwa na mmoja wa Wasimamizi wa mradi wa ClimSA kutoka AUC Bw. Freddy Falanga (ambaye ni rai wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), ambapo timu hiyo ya wataalamu walitembelea Ofisi Kuu ya Utabiri wa Hali ya Hewa, iliyopo Ubungo Plaza, Dar es salaam kwa lengo la kukagua utendaji kazi wa mitambo ya ufuatiliaji wa mifumo ya hali ya hewa na utabiri wa hali ya hewa, inayoitwa "PUMA STATION.", iliyotolewa kwa TMA kupitia mradi ClimSA.

Mradi wa ClimSA unatekelezwa katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AUC), ikiwemo Tanzania kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (European Union). Mradi huu unalenga kuimarisha zaidi uwezo wa nchi wanachama wa AU katika kufuatilia mifumo ya hali ya hewa kupitia teknolojia ya satelaiti ili kuboresha zaidi utabiri wa hali ya hewa na huduma za hali ya hewa kwa ujumla.

Huduma hizi ni muhimu kwa jamii na sekta za kiuchumi katika kupanga shughuli za maendeleo na kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

FIRST LADY MNANGAGWA AWASILI JIJINI ARUSHA


  Mke wa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Dkt. Auxillia C. Mnangagwa amewasili jijini Arusha na kupokelewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb), Naibu Waziri, Mhe. Dunstan Kitandula, baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Sekretarieti ya Shirika la Utalii Duniani.

Mhe.Mnangagwa anatarajiwa kushiriki Jukwaa la Pili la Kimataifa la Utalii Wa Vyakula la Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) Kanda ya Afrika kesho Aprili 23, 2025 jijini humo.