JSON Variables

Thursday, April 24, 2025

WASIRA: VIONGOZI WA DINI WAMETUTIA NGUVU KUENDELEA NA UCHAGUZI MKUU*

 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewashukuru na kuwapongeza viongozi wa dini kwa ushauri kuhakikisha Nchi inaendelea kuwa na amani hususan kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na kubariki uchaguzi huo uendelee huku, ikisisitiza kuwa haidharau maoni yanayotolewa.


CCM imesisitiza kuwa haipuuzi ushauri mbalimbali unaotolewa kuelekea uchaguzi huo, lakini imesisitiza hautaahirishwa kwa kuwa mageuzi na mabadiliko ni jambo endelevu na haiwezi kuwa hoja ya kuahirisha uchaguzi.

Hayo yalielezwa leo Chamwino mkoani Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara,  Stephen Wasira alipokuwa akipokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo.


"Uchaguzi utaendelea sio kwamba tunapuuza mawazo, tutaendelea kuzungumza mambo ambayo yanaendelea, na tunashukuru sana nchi imetulia. Viongozi wetu wa kiroho wametuongoza wametupa ushauri mzuri sana na mimi nashukuru sana kwa kututia moyo na kutuambia uchaguzi uendelee lakini kwa amani," alisema.

Wasira alisema CCM ni Chama kinachozungumza na kuhimiza amani ndio maana taifa limekuwa na utulivu kwa miaka 60, alisisitiza kwamba hilo linafanya Chama kijivunie kwa kuwa ni ushahidi kwamba kinaweza kusimamia amani.


Alisisitiza haki iko ndani ya amani na kwamba ukiondoa amani utavunja haki za watu wengi hususan wanyonge, "ukiondoa amani watakaoumia hasa ni wanawake, watoto na walemavu."


"Amani ni lazima sasa kuna wanaosema haki, na sisi tunasema ndani ya amani kuna haki, na haki hiyo inalindwa na amani kwa sababu ukiiondoa watu wengi wataathirika wala sio mtu mmoja ni wengi sana na ushahidi wake upo, sisi tumepokea wakimbizi maelfu kutokana na kuvunjia kwa amani kwa majirani zetu," alisisitiza.



HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO TAREHE 24.04.2025

 Good morning, Habari gani popote ulipo mdau wetu na msomaji wetu wa mkisi digital, Nikukaribishe kwa bashasha kubwa sana kupitia vichwa vya habari vilivyo pata nafasi katika kurasa za mbele ya magazeti ya leo tarehe 24.04.2025









Wednesday, April 23, 2025

DKT. NCHEMBA ATETA NA MKURUGENZI MTENDAJI WA UENDESHAJI WA BENKI YA DUNIA, JIJINI WASHINGTON

 

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Mb), amekutana na kufanya Mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Masuala ya Utawala na Uendeshaji wa Benki ya Dunia, Bi. Anna Bjerde, kando ya Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya IMF na Benki ya Dunia, inayofanyika Jijini Washington D.C, nchini Marekani, ambapo pamoja na mambo mengine, Dkt. Nchemba aliishukuru Benki hiyo kwa mchango mkubwa wa maendeleo ya Tanzania kupitia miradi mbalimbali inayopata fedha kutoka Taasisi hiyo pamoja na kuonesha nia ya kusaidia ujenzi wa Mradi wa Reli ya kisasa (SGR)


Aidha, katika kikao hicho, alitambulishwa Makamu wa Rais Mpya wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Bw. Ndiamé Diop, ambaye ameteuliwa hivi karibuni baada ya Bi. Victoria Kwakwa kumaliza muda wake.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Dkt. Elsie Kanza, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa, Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, Kamishna Msaidizi kutoka Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Robert Mtengule, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Bw. Nathan Belete na viongozi wengine waandamizi wa Serikali na Benki ya Dunia.


NJE SPORTS YATINGA ROBO FAINALI KWA KISHINDO, YAILAZA TPDC 36-23

 

Timu ya netiboli ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (NJE Sports) imeendelea kung’ara katika michezo ya Mei Mosi kwa kuibuka na ushindi wa mabao 36-23 dhidi ya TPDC, katika mchezo uliopigwa kwenye viwanja vya Mwenge, mkoani Singida.


Mchezo huo ulianza kwa kasi, huku NJE Sports wakionyesha ubora wa hali ya juu na kumaliza kipindi cha kwanza wakiongoza kwa mabao 19-13. Kipindi cha pili walizidi kuimarika, wakiboresha safu ya ulinzi na kushambulia kwa ufanisi zaidi.


Akizungumza baada ya mchezo, Kocha wa NJE Sports, Bw. Mathew Kambona, amewapongeza wachezaji wake kwa kujituma na kufuata maelekezo. “Tunajipanga upya kwa hatua inayofuata, tukilenga kuongeza kasi na nidhamu ya ushindi,” alisema.


Kwa matokeo hayo, NJE Sports imefuzu rasmi hatua ya robo fainali katika mashindano hayo ya kitaifa yanayoshirikisha timu kutoka wizara na taasisi mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani.

DKT. MPANGO AFUNGUA RASMI JUKWAA LA KIMATAIFA LA UTALII WA VYAKULA YAKULA




Wakulima Nchini Kunufaika na Utalii wa Vyakula


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Isdory Philip Mpango amefungua rasmi Jukwaa la Pili la Kimataifa la Utalii wa Vyakula la Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) Kanda ya Afrika leo Aprili 23,2025 jijini Arusha huku akisisitiza kuwa Serikali itashirikiana na wazalishaji wa ndani wa kilimo kutekeleza mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuwekeza katika mifumo ya kidijitali inayowezesha uhusiano kati ya watalii na wazalishaji halisi wa chakula


Amesema mpango huo utaambatana kwa karibu na mafunzo ya wapishi wa ndani katika uanzishwaji wa vituo vya upishi vinavyoendeshwa na jamii na uwekaji wa utalii wa gastronomy kama toleo la kimkakati la utalii. 


Amefafanua kuwa utalii wa Gastronomy ni sehemu muhimu ya sekta ya utalii, yenye uwezo mkubwa wa kukuza  maendeleo ya kiuchumi, maingiliano ya kitamaduni, na uwezeshaji wa jamii. 


“ Gastronomy inaanzisha uhusiano kati ya wageni wetu na ladha halisi, mila, na simulizi za watu wetu. Nchini Tanzania, tuna bahati ya kumiliki urithi wa upishi wa aina mbalimbali na wa kusisimua unaojumuisha historia yetu tajiri, wingi wa kitamaduni, na rasilimali nyingi za ardhi na maji yetu” amesema Dkt. Mpango.


Aidha, amesema kuwa Serikali inakusudia kuendelea kuongeza mazao mapya ya utalii ili kuvutia wigo mpana wa wageni kwa kutangaza uwekezaji katika utalii wa fukwe, mikutano, motisha, makongamano na maonyesho (MICE), utalii wa meli za kitalii, utalii wa kitamaduni, na utalii wa michezo, uanzishwaji wa migahawa yenye mikahawa ambayo hutoa vyakula halisi vya Kiafrika na vyakula vya kawaida vinavyopikwa nyumbani, na hivyo kuboresha hali ya jumla ya wageni.


Katika hatua nyingine, Dkt. Mpango amesema Tanzania imepata ongezeko kubwa la idadi ya waliofika kimataifa, kutoka 1,527,230 mwaka 2019 hadi 2,141,895 mwaka 2024, sawa na ongezeko la 40.25%. 

“Mafanikio hayo yanachochewa na mipango ya kimkakati ya utangazaji kama vile programu za Tanzania The Royal Tour, ambazo zinaangazia uzuri wa asili wa taifa, utamaduni, na matoleo mbalimbali ya utalii. Mwezi Mei mwaka uliotangulia, tulizindua programu ya Amazing Tanzania nchini China kwa lengo la kupanua soko letu la utalii kwa kuzingatia nchi za Asia” amesema Mhe. Mpango

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa Uutalii wa Gastronomy una uwezo mkubwa wa kuvutia watalii  Barani  Afrika hivyo ni wakati muafaka wa kutafiti namna bora ya kutumia vyakula vya Kiafrika ili kuvutia wageni zaidi.


Amesema katika kusherehekea umuhimu wa gastronomia katika nyanja ya utalii, inahusisha kuwawezesha wakulima wa ndani, wapishi, na wajasiriamali wa chakula kuchukua jukumu kuu katika mpango wa utalii wa vyakula, kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa chakula wa ndani na kuimarisha usalama wa chakula na viwango vya ubora ili kuweka imani katika bidhaa zetu za upishi.


Pia amesema ni vyema kuwezesha ubia miongoni mwa wadau wa utalii ili kuendeleza tajriba bainifu ya hali ya hewa inayovutia wageni wa kimataifa na wa ndani.

Naye Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii Duniani, Bw. Zurab Pololikashvili, amesema kuwa Jukwaa hilo ni fursa ya kuitangaza Afrika kwenye ramani ya dunia, kuendeleza maendeleo endelevu ya utalii Barani Afrika na kwingineko, kutafiti njia za uwekezaji, kuchangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Bara na uendelevu wa mifumo yake ya chakula.

Jukwaa hilo limekutanisha washiriki takribani 300 wakijumuisha viongozi waandamizi katika sekta ya utalii na ukarimu, watumishi wa serikali, pamoja na wataalamu wa masuala ya upishi kutoka ndani na nje ya Afrika.

KAMPUNI ZISIZO JIORODHESHA DSE KUTOFAHAMU THAMANI HALISI YA UWEKEZAJ


Serikali imesema kuwa Kampuni ambazo hazijaorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) hukutana na changamoto za kutofahamu thamani halisi ya uwekezaji kutokana na kukosekana kwa ukwasi wa hisa zao.


Hayo yalisemwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Geita Mjini, Mhe. Constantine John Kanyasu, aliyetaka kujua hasara na faida kwa kampuni kutotekeleza Sheria ya kujiorodhesha kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam.


Mhe. Chande alisema kuwa Kampuni ambazo hazijajiorodhesha katika Soko la Hisa hutawaliwa na kukosekana kwa uwazi na hivyo Serikali na wanahisa kushindwa kupata taarifa stahiki za mwenendo wa biashara na fedha.


“Kwa mujibu wa Sheria, ni Kampuni ya simu pekee ndio hulazimika kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa katika soko la hisa  isipokuwa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa kwa asilimia 25 au zaidi  na Kampuni ambazo zinatoa huduma ya minara ya simu”, alisema Mhe. Chande.


Aidha alizitaja faida za Kampuni kujiorodhesha kwenye Soko la Hisa kuwa ni pamoja na kuongeza mtaji, kuongeza ufanisi na tija, kuiwezesha Serikali kupata mapato stahiki na  kutambua thamani halisi ya hisa zake ambapo wanahisa wanapata thamani ya hisa zao wanapotaka kuuza kwa kufuata mwenendo wa soko (demand and supply).


Alisema faida nyingine ni pamoja na kuwapa wananchi fursa ya kununua hisa na hivyo kuwezeshwa kushiriki katika uchumi wa nchi na kutoa fursa kwa wawekezaji wanaotaka kuuza uwekezaji wao wakati wanapohitaji fedha.

MH. S. S. H, AMPONGEZA ALPHONCE BAADA YA KUSHIKA NAFASI YA PILI KWENYE MBIO ZA BOSTON

 

Pongezi za dhati kwa Alphonce Simbu kwa kushika nafasi ya pili katika Mashindano ya Kimataifa ya Mbio ya Boston (Boston Marathon). Umefanya kazi nzuri.


Ushindi wako ni matokeo ya kujituma kwa bidii, maandalizi mazuri, nidhamu yako kuanzia jeshini, kwenye mazoezi hadi kwenye mashindano, ukilibeba kwa heshima ya hali ya juu jina la nchi yetu. 


Endelea kuipeperusha vyema bendera ya Taifa letu.

DKT. MWAMBA ASHIRIKI MKUTANO WA AU KUJADILI AJENDA KWENDA G20

 

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, ameshiriki Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu za Afrika, uliojadili maeneo ya kipaumbele ambayo nchi za Afrika zinahitaji kuyasukuma kama agenda mahususi katika mikutano ya Kundi la nchi 20 Tajiri Duniani (G20) kwa mwaka 2025 ambapo Nchi ya Afrika Kusini ni mwenyekiti wa G20, Mkutano uliofanyika katika Ofisi za Kamisheni ya Umoja wa Afrika, kando ya mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Jijini Washington D.C, Marekani.

Aidha, majadiliano katika mkutano huo pamoja na mambo mengine, yaliangazia kuhusu Afrika kuwa na sauti moja katika kuzishawishi nchi za G20 kufanya mabadiliko yatakayosaidia upatikanaji wa fedha na mikopo nafuu kwa nchi zinazoendelea, namna ya kukabiliana na madeni, suala ambalo ni tatizo kwa nchi nyingi za Afrika kufuatia mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi, kijiografia na kisiasa.  

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, Naibu Gavana wa BoT, Dkt. Yamungu Kayandabila, Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, na Maafisa wengine waandamizi wa Serikali.