JSON Variables

Friday, April 25, 2025

SERIKALI YATOA UPENDELEO KWA MAKUNDI MAALUM KATIKA SHERIA YA UNUNUZI WA UMMA

 


Na Mwandishi wetu

PWANI.


Serikali inatambua umuhimu wa kuwawezesha watu wenye mahitaji Maalum kushiriki katika shughuli za kiuchumi , hivyo kuna upendeleo maalum katika Ununuzi wa Umma kwa ajili yao.


Hayo yamesemwa leo tarehe 25 Aprili, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma Bw. Dennis Simba wakati akifungua mafunzo kwa watu wenye mahitaji maalum  katika Ununuzi wa Umma. 

Amesema mafunzo haya yamekusudia kuelimisha na kuhamasisha makundi maalum juu ya haki zao na fursa wanazoweza kuzitumia katika mchakato wa Ununuzi wa Umma hivyo tunataka kuona makundi haya yanapata fursa za kibiashara ili kuchangia ukuaji wa uchumi wa Nchi. 

"mpaka sasa kuna jumla ya vikundi maalum 280 vilivyokamilisha usajili na uhuishaji wa taarifa zao katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma (NeST) ambapo vikundi hivyo vimepata tuzo za mikataba zilizotolewa kwa makundi maalum ambazo jumla ni tuzo Mia Nne Arobaini zenye thamani ya Shilingi Bilioni 15 ambapo Vijana ni vikundi 163 sawa na 58% wanawake ni vikundi 96 sawa na 34% na wenye Mahitaji maalum (Walemavu) ni Vikundi 4 sawa na 2% na wazee Vikundi 17 sawa na 6% sasa kama unavyoona usajili ni mdogo na mahitaji ni kwamba kila kikundi kiwe na kati ya watu watono hadi 20 hivyo bado kunamuamko mdogo kwenye vikundi vya watu wenye mahitaji maalum na ndio maana PPRA tumeona kuna haja ya kukutana na viongozi wa TAB na TLB , Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili tuweze kuimarisha jambo hili. Alisema Mkurugenzi Mkuu PPRA 

Aidha  Bw.  Simba amesema, Mamlaka ya Ununuzi wa Umma inajukukumu la kuhakikisha kuwa Mifumo ya Ununuzi inazingatia usawa, haki na uwazi na kutoa mafunzo kwa watu mbalimbali na kuanzisha programu za uhamasishaji na kushirikiana na wadau muhimu ili kuhakikisha kuwa makundi haya maalum yanaelewa haki zao katika michakato ya Ununuzi wa Umma. 

"Nataka kusisitiza kwamba kila mmoja wetu anajukumu la kuhakikisha kuwa anafaidika na fursa zinazotolewa kwa Makundi Maalum katika sekta ya ununuzi wa umma, Mafunzo haya ni mwanzo mzuri wa safari ya kuelewa na kutumia haki hizi katika kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza tija katika Uchumi wa nchi, hivyo nitumie fursa hii kuwashukuru kwa kujitolea na kujiunga na mafunzo haya na nimatumaini yangu kuwa mtachukua maarifa haya na kuyatumia katika shughuli zenu za kila siku" Alisistiza Mkurugenzi Dennis Simba

kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania Bw. Omary Itambu Amasi amewashukuru PPRA kwa kuwaletea mafunzo ambayo yatawasaidia katika kupata tenda mbalimbali ambazo wengine wasio na mahitaji maalum wanazipata.


" Hapo mwanzo tulishindwa kupata fursa za tenda kutokana na kukosa Elimu hii kwa hiyo leo PPRA mmekuja kutupa mkate au ufunguo ambao utafungua kila kitasa kwenye masuala ya ununuzi katika sekta za Umma hivyo niwapongeze sana lakini sana niwaombe huu sasa ni mzizi mliousimika na mzizi ukianza litakuja shina hatimae matawi maana yangu ni kwamba hiki kilichoanzishwa sasa ni jambo ambalo linahitajika katika maeneo yote 26 Tanzania Bara na niwaombe bajeti zenu zitukumbuke. Alisema Mwenyekiti Huyo. 

Uendeshaji wa mafunzo hayo ni mwendelezo wa Mamlaka wa utoaji mafunzo kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma na Mfumo wa NeST ili kuwajengea uwezo wadau wote wa sekta hii nyeti nchini.

SERIKALI KUENDELEA KUWEKEZA KATIKA SEKTA YA AFYA - DKT. BITEKO

 

.....................

Dkt. Biteko atambelea Hospitali ya Wilaya ya Meru

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Serikali imeahidi kuendelea kuboresha huduma za Afya nchini katika ngazi zote ili kuboresha huduma za Afya kwa Watanzania.

Hayo yamesemwa Aprili, 25, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiwa ziarani Mkoani Arusha ambapo amesema kuwa lengo la uwekezaji katika sekta ya afya ni kusigeza huduma za afya kwa wananchi."

Serikali inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea na uwekezaji mkubwa unaofanya kwa kujenga hospitali, vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza baada kutembelea Hospitali ya Wilaya ya Meru, iliyopo Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha, Mhe. Dkt. Biteko amesema lengo la uwekezaji katika sekta ya afya ni kuboresha afya za Watanzania.

“ Kama mnavyofahamu afya ndio mtaji wa wananchi na Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya kwa kujenga hospitali mpya na kufanyia ukarabati zilizopo,” amesema Dkt. Biteko.

Amesistiza “ Watu wote nilioongea nao hapa hospitalini wamesema hali ya utoaji huduma imeimarika na ni nzuri, nataka niwaambie Rais Samia katika uongozi wake ameapa kuboresha hali za maisha ya Watanzania. Hapo awali ilimlazimu mgonjwa kutoa makozi siku tatu mfululizo ili kumfanyia kipimo cha ugonjwa wa kifua kikuu, leo tuna mashine ya kisasa inayotumia saa mbili kupata majibu ya mgonjwa,”

Ameendelea kusema ujenzi na maboresho yaliyofanyika hospitalini hapo imetumia raslimali za ndani (force account) na kazi imefanyika kwa ubora na kuzingatia thamani ya fedha.

Ameongeza kuwa katika kuelekea miaka 61 ya Muungano uwepo wa hospitali hiyo ni kiashiria cha kuwa nchi inapiga hatua kimaendeleo. Hivyo, wananchi hawana budi kuuenzi na kuutunza Muungano.

Aidha, amewataka wagonjwa kuwa wavumilivu wanapoenda kupata matibabu huku wakizingatia kuwa wahudumu wa afya wanafanya jitihada kubwa kuwapa huduma bora.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda amesema kuwa wananchi wa eneo hilo wanafurahia huduma nzuri zinazotolewa na sasa idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa ni 12,000 kutoka 3,000 ya awali.

Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Meru, Daktari Elisante Fabiani amesema kuwa uboreshaji wa majengo katika hospitali hiyo umesaidia utoaji huduma na kuongeza idadi ya vipimo vya maabara kutoka 18 hadi 32.

“ Tuna mashine ya kisasa ya kupimia vimelea vya kifua kikuu na ndani ya saa mbili pekee mgonjwa anapata majibu ya kifua kikuu na kuanza matibabu na ina uwezo wa kugundua dawa ya kutumia,” ameeleza Daktari Fabian.

Aidha, Dkt. Biteko ameendelea na ziara yake siku tano mkoani humo ambapo ametembelea Wilaya za Longido na Monduli ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.  

DKT. MWINYI: BARABARA YA KIBADA - KIMBIJI KUWA NGUZO YA MAENDELEO KIGAMBONI

Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ally Mwinyi, ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji yenye urefu wa kilometa 41, hatua muhimu inayolenga kukuza uchumi na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Aprili 25, 2025, katika Wilaya ya Kigamboni, Dkt. Mwinyi alisisitiza kuwa uwepo wa amani nchini ndiyo msingi wa mafanikio ya miradi ya maendeleo kama huu, na kuagiza ujenzi huo ukamilike kwa wakati na kwa viwango vya juu. Alibainisha kuwa barabara hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kuunganisha maeneo ya pembezoni na fursa za kiuchumi.

Katika hotuba yake, Dkt. Mwinyi alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuendeleza Muungano na kutatua changamoto zilizokuwa zikikumba uhusiano kati ya pande mbili za Muungano, akisisitiza kuwa umoja huo ni nguzo ya maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, aliyemwakilisha Waziri wa Ujenzi, alisema mradi wa barabara hiyo ni jawabu kwa kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Kigamboni, na sasa utafungua fursa za uwekezaji na kuinua uchumi wa eneo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, alimhakikishia Rais Mwinyi kuwa Mkoa upo salama na utazidi kudumisha amani licha ya changamoto za kisiasa, huku akitoa pongezi kwa Rais Samia kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kama hii.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Muhammed Besta, alieleza kuwa barabara hiyo inajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 83.8 na itatekelezwa kwa awamu mbili chini ya mkandarasi kampuni ya Estim, ambapo hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 30.

Uzinduzi wa mradi huu umebeba ujumbe mzito wa kaulimbiu ya mwaka huu isemayo: “Muungano wetu, heshima na tunu ya Taifa – Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya Muungano. 

WAZIRI MASAUNI AWASILI BAJETI YA MWAKA 2025/26

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akiwasilisha hotuba ya mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2024/25 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2025/26 bungeni jijini Dodoma leo tarehe 25 Aprili 2025.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akiteta jambo na Naibu Waziri wake Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati wa Kikao cha 12 cha Mkutano wa Nane wa Bunge ambapo amewasilisha hotuba ya mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2024/25 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2025/26 bungeni jijini Dodoma leo tarehe 25 Aprili 2025.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja akiwa na viongozi waandamizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wakifuatilia Kikao cha 12 cha Mkutano wa Nane wa Bunge kuhusu uwasilishaji wa bajeti ya Ofisi hiyo bungeni jijini Dodoma leo tarehe 25 Aprili 2025.

........

Waziri wa Nchi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amelieleza Bunge kuwa katika mwaka 2024/2025 Serikali imeanzisha Mfumo wa Kielektroniki wa kuratibu masuala ya Muungano na Yasiyo ya Muungano (UNUMMiS).

Akiwasilisha hotuba ya mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2024/2025 na makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya Ofisi hiyo kwa mwaka 2025/2026, Waziri. Masauni amesema mfumo huo umelenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa na utendaji kazi

Waziri Masuani amesema mfumo huo kwa sasa upo katika hatua za majaribio ili kuona kama unakidhi matakwa ya watumiaji na pindi utakapokamilika utasaidia wananchi kufahamu kwa kina masuala muhimu yanayohusu Muungano.

Aidha Mhe. Masauni amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuratibu masuala ya ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuhakikisha Wizara/Idara na Taasisi zinafanya vikao vya ushirikiano.

Ameongeza kuwa hadi kufikia mwezi Machi 2025 jumla ya vikao vinane vya ushirikiano vilifanyika vilivyolenga katika kubadilishana uzoefu, Sera, Sheria na utaalamu katika utekelezaji wa mambo yasiyo ya Muungano.

Mhandisi Masauni amesema katika kuimarisha sekta ya hifadhi na usimamizi wa mazingira nchini, Serikali kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni imesajili jumla ya Miradi 73 ya Biashara ya Kaboni ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Ameongeza kuwa Biashara ya kaboni imeanza kuleta manufaa kiasi katika baadhi ya maeneo nchini ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 45 zimelipwa na kunufaisha wananchi katika Halmashauri 10 nchini kama gawio la mauzo ya viwango vya kaboni.

“Ofisi iliratibu vikao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kikao cha kuwajengea uwezo Makatibu Wakuu 21 kuhusu biashara ya kaboni, Wawakilishi wa Makampuni 27 yanayojihusisha na biashara ya Kaboni, Vikao vya kimkakati vya kuimarisha usimamizi wa biashara ya Kaboni baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara za kisekta” amesema Waziri Masauni.

Kuhusu uchumi wa Buluu, Waziri Masauni amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuratibu utekelezaji wa sera ya taifa ya uchumi wa buluu ikiwemo kuandaa Mpango wa Matumizi wa Maeneo ya Maji pamoja na kuwezesha uwepo wa utafiti na ujuzi katika matumizi ya rasilimali za Uchumi wa Buluu nchini.

Kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Mazingira Sura 191, Mhandisi Masuani amesema hadi kufikia machi 2025, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilipokea na kushughulikia malalamiko 247 yaliyohusu kelele, utupaji taka ovyo, utiririshaji ovyo wa majitaka, ujenzi holela, uchimbaji usio rasmi wa mchanga na uchafuzi wa hewa.

Ofisi ya Makamu wa Rais imeliomba Bunge kuidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 81,864,190,000 kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya Ofisi hiyo kwa mwaka 2025/2026.

NAIBU WAZIRI MKUU DKT. BITEKO AKEMEA MIGOGORO ARUSHA 

....................

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka viongozi kote nchini kuweka maslahi ya wananchi mbele na kuacha migogoro inayotokana na ubinafsi wao.

"Hawa Watanzania hawataki migogoro yetu sisi viongozi na wakati mwingine migogoro tuliyonayo ni migogoro ya maslahi binafsi. Tumeacha kuwahudumia wananchi tunashughulikiana, tunataka huyu akwame, huyu afanikiwe kwa sababu tuna cartel (makundi)," amesema Dkt. Biteko 

Akizungumza Aprili 24, 2025 Mundarara, Wilayani Longido, Dkt. Biteko amesema kuwa amani ndiyo msingi wa utoaji huduma bora "Tunataka watu waungane, wafanye kazi ya pamoja. Hakuna kitu kinachotia aibu kama unakuta kiongozi umepewa nafasi mahali fulani ama wewe una cheo mahali fulani badala ya kuzungumza shida za watu unawazungumza watu, Huyu kwako mbaya, yule mbaya, huyu mbaya, Wewe ukiulizwa uzuri wako huna cha kuonesha." 

Amesisitiza kuwa viongozi waliopata nafasi wanapaswa kumtumia mwananchi kama mteja wao wa kwanza, wa pili, na wa tatu "Viongozi tuliopata nafasi mteja wetu wa kwanza awe mwananchi, mteja wetu wa pili awe mwananchi, mteja wetu wa tatu awe mwananchi. Hawa wananchi ndiyo wanatupa uhalali wa sisi kuitwa viongozi, tukumbuke ni kwa kodi zao tupo hapa, Tusihubiri chuki. ”amesisitiza Dkt. Biteko.  

TANZANIA HAIWEZI KUWEPO BILA YA MUUNGANO, TUULINDE KWA WIVU- DKT. TULIA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesema kuwa ni wajibu wa kila mtanzania kuhakikisha anailinda kwa wivu wote tunu ya Muungano iliyoanzishwa na waasisi wa taifa hilo.

Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 25 Aprili 2025 wakati akizungumza na wananchi wa wa Mkoa wa Pwani wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika stendi ya Kibaha ikiwa ni sehemu ya shughuli za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara baada ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanyika katika mkoa huo.

Kiupekee, Dkt. Tulia amemshukuru na kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha anasimamia maendeleo katika nyanda zote za bara na visiwani.

“Tanzania haiwezi kuwepo bila Muungano, Muungano huu umejengwa katika misingi imara umedumu na utaendelea kudumu. Kila mmoja wetu anapaswa kutafakari matendo na maneno yake yawe chachu ya kudumisha Muungano wetu, niwahakikishie kwamba Bunge litaendelea kuwa daraja katika pande zote mbili ili kuhakikisha Muungano unazidi kuwa madhubuti, unadumu na kuwa imara zaidi” Amesisitiza Dkt. Tulia 

HIZI HAPA HABARI KUBWA ZILIZO PEWA NAFASI KWENYE KURASA ZA MBELE YA MAGAZETI LEO TAREHE 25.04.2025

 Good morning, Habari gani popote ulipo mdau wetu kupitia Mkisi Digital, Natumia fursa hii kuku karibisha kupitia vichwa vya habari magazetini leo ijumaa tarehe 25.04.2025

Unamaoni gani kwenye habari ambayo imekubamba kupitia vichwa hivi/ habari hizi zilizo pewa nafasi kubwa sana kwenye kurasa za mbele ya magazeti.