Takriban Wapalestina 22 waliuawa na wengine 100 kujeruhiwa katika shambulizi la siku ya Jumapili kwenye shule inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa katikati mwa Gaza inayotumiwa kama makazi ya watu waliokimbia makazi yao, wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas inasema.
Jeshi la Israel limesema lililenga "magaidi" kadhaa wa Hamas wanaoendesha shughuli zao kutoka shule ya Abu Oraiban katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat iliyoko mjini.
Walioshuhudia waliambia idhaa ya BBC Arabic hakukuwa na wapiganaji waliojihami na kwamba watoto walikuwepo ni miongoni mwa waliouawa.
Lilikuwa ni shambulio la tano katika au karibu na shule katika muda wa siku nane.
Wakaazi walisema kulikuwa na mashambulizi ya anga na mizinga katikati mwa Gaza siku ya Jumatatu, huku watu watano wakiripotiwa kuuawa wakati nyumba moja katika kambi ya wakimbizi ya Maghazi iliposhambuliwa.
Jeshi la Israel lilisema ndege yake ilishambulia makumi ya maeneo ya "ugaidi yaliyolengwa" katika eneo lote katika siku iliyopita.
Wakati huo huo, Hamas ilisema mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja juu ya makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka na Israel "yanaendelea" wakati kunatokea shambulio la anga katika eneo la kusini mwa al-Mawasi Jumamosi ambalo wizara ya afya ilisema liliua zaidi ya watu 90.
Jeshi la Israel lilisema lililenga eneo ambalo mkuu wa tawi la wapiganaji la Hamas, Mohammed Deif, alikuwa amejificha pamoja na kamanda wa Brigedi ya Khan Younis, Rafa Salama.
Jeshi limetangaza kwamba Salama aliuawa, lakini walisema ni mapema mno kuhitimisha kama Deif pia alifariki. Upande mwingine, Hamas wamesema Deif yu bukheri wa afya.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema Antony Blinken alionyesha wasiwasi mkubwa kuhusu raia waliojeruhiwa hivi majuzi wakati wa mkutano na maafisa wawili wakuu wa Israel siku ya Jumatatu.
Israel ilianzisha kampeni ya kijeshi huko Gaza ili kuiangamiza Hamas kujibu shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.
Zaidi ya watu 38,660 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo, ambayo takwimu hazitofautishi kati ya raia na wapiganaji.
0 Comments