Walioingia kwenye kinyang'anyiro wawekwa hadharani.
NA MWANDISHI WETU
TUZO za Muziki wa Injili Tanzania (Tanzania Gospel Music Awards (TGMA)) zinatarajia kufikia kilele Mei 23, 2025 kwa utoaji wa Tuzo na fedha kwa washindi katia hafla itakayofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa jana Aprili 25, 2025 na Msemaji wa Kamati ya Maandalizi ya Tuzo hizo Mchungaji Haris Kapiga akizungumza na waandishi wa habari wakati akibainisha watu walioingia kwenye kinyang'anyiro cha tuzo hizo zenye vipemgele 20.
Mchungaji Kapiga amesema kuwa mchakato wa Tuzo hizo ulianza tangu Novemba Mwaka jana kwa kufungua dirisha la kila Msanii wa Muziki wa Injili kuwasilisha kwa hiari yake nyimbo zake anazotaka ziingie kwenye kinyang'anyiro hicho huku sharti likiwa ni lazima nyimbo hizo ziwe ni za Mwaka Jana.
"Tuliwaomba watu wawasilishe kazi zao wenyewe kwa vipemgele wanavyoona vinawafaa wao, kazi ya TGMA ni kuwatia moyo watu wenye vipawa ambavyo Mungu amewapatia," amesema Mchungaji Kapiga.
Mchungaji Kapiga ameeleza kuwa jumla ya kazi 529 zilipokelewa ambapo wahusika walipigiwa kura na kupatikana watu watano kwa kila kipemgele na kwamba hatua inayofuata wataendelea kupigiwa kura na kubakia watu watatu kwa kila kipengelea ambapo washindi watapatikana siku ya kilele cha tuzo hizo.
Ametaja vipemgele vya tuzo hizo kuwa ni pamoja na wimbo Bora wa kuabudu wa Mwanamuziki wa Injili wa Mwaka, wimbo Bora wa Muziki wa Sifa, Wimbo Bora wa Muziki wa Injili wa Mwaka na Wimbo Bora wa Injili wa Mwaka kwa wanamuziki wa nje ya Nchi.
Vipengele vingine ni Msanii Bora wa Muziki wa Injili wa Mwaka, Msanii Chipukizi wa Muziki wa Injili, Mwimbaji Bora wa kiume wa Muziki wa Injili wa Mwaka, na Mwimbaji Bora wa Kike wa Muziki wa Injili wa Mwaka.
Akiendelea kutaja vipengele vingine Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Tuzo hizo Nina Mbura, amesema ni Kwaya/bendi bora ya Muziki wa Injili ya Mwaka, Video Bora ya Muziki wa Injili, Mtayarishaji Bora wa Video ya Muziki wa Injili wa Nota na mtunzi Bora wa Muziki wa Injili wa Mwaka.
Vingine ni Mwandaaji Bora wa Muziki wa Injili wa Mwaka, Mtayarishaji wa bora wa Muziki wa Injili wa Mwaka, Kiongozi wa Miziki wa Injila wa Mwaka, ushirikiano wa bora wa Muziki wa Mwaka na tuzo ya heshima Kwa mtu mwenye mchango mkubwa kwenye ukuaji wa Tasnia ya Muziki wa Injili nchini.
Baadhi ya wasanii wanaowania tuzo hizo ni Paul Clement, Water Chilambo, Japheth Zabron wa Zabron Singers, Joel Lwaga, Rehema Simfukwe, Zabron Singers na kadhalika.
Hata hivyo Mchungaji Kapiga amebainisha kuwa hadi sasa maandalizi ya hafla hiyo yamefikia asilimia 80.