Arusha, Aprili 2025 – Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendeleza juhudi zake za kukuza utalii wa kiikolojia kupitia vyakula asilia vinavyotokana na misitu ya Tanzania, katika mkutano wa UN Tourism on Gastronomy for Africa unaoendelea jijini Arusha.
Katika mkutano huo, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, na Mwenyekiti wa Bodi ya TFS, Meja Jenerali Dkt.Mbaraka Naziad Mkeremy, walifanya mazungumzo ya kimkakati na wadau mbalimbali kuhusu mchango wa misitu katika kutoa ladha halisi ya utamaduni wa wenyeji kwa watalii.
Prof. Silayo alisema kuwa misitu ya Tanzania siyo tu chanzo cha rasilimali za kiuchumi, bali pia hazina ya vyakula asilia na mimea ya dawa vinavyoweza kuendelezwa kama vivutio muhimu vya utalii wa chakula (gastronomy tourism).
“Tunatambua kuwa mapishi ya jadi, uyoga wa misitu, mimea ya dawa, na mazao mengine ya asili vinatoa fursa ya kipekee kwa watalii wanaotafuta uzoefu wa kiutamaduni na ikolojia,” alisema Prof. Silayo.
Kupitia ushirikiano na jamii zinazozunguka misitu, TFS inalenga kuhakikisha kuwa utalii wa chakula unachangia moja kwa moja katika uhifadhi wa mazingira, kuongeza kipato cha wananchi, na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii endelevu nchini.
Meja Jenerali Dkt.Mbaraka Naziad Mkeremy alisisitiza kuwa mafanikio ya kukuza utalii wa gastronomy yanategemea matumizi endelevu ya rasilimali za misitu na mafunzo kwa jamii kuhusu thamani ya vyakula vya asili.
Mkutano huo wa UN Tourism umewakutanisha wadau kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika, ukilenga kuibua mbinu bora za kuendeleza utalii wa chakula kama njia ya kuongeza thamani ya utalii na kuinua uchumi wa jamii zinazohifadhi mazingira..