Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi kimesema kwa miaka yote kimepokea , kusikiliza na kutekeleza Ushauri wa Wazee, watu mbalimbali , Viongozi wa Dini na Kijamii bila kukiuka matakwa ya Katiba na Sheria.
CCM na serilali zake huendesha utawala bila kuingilia mipaka ya Sheria huku kikiheshimu madaraka ya Serikali, Bunge na Mahakama.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis , ameeleza hayo alipotakiwa kutoa maoni yake kufuatia ushauri uliotolewa na Waziri Mkuu Mstaafu Joseph Warioba.
Mbeto alisema Serikali haziwezi kuzuia Uhuru wa mawazo ya watu na ushauri wa Wazee, lakini akawataka wanaoshauri , watambue kuna mahali unapoishia ushauri wao.
Alisema kupokea ushauri si kosa ila kosa huweza kuwa makosa zaidi aidha katika utekelezaji wa Ushauri huo usiokiuka na kuvunja Sheria, Katiba au kuingilia madaraka ya mihimili mingine.
'Ushauri wa Wazee utabaki kuwa sehemu ya utamaduni wa Serikali za CCM. Kama Taifa tumefika mahali tulipo kwa kuthamini michango na ushauri wa Wazee . Kila jambo lina kipimo na mipaka ya utekelezaji wake " Alisema Mbeto .
Katibu huyo Mwenezi aliongeza kusema , kupokea ushauri wowote , lazima anaeshauri na anayeshauriwa wote walitazame suala husika kama lipo kisheria , lina ugumu na wepesi upi , kwakuwa kila hatua, inahitaji kutekelezwa kwa umakini na tahadhari.
"Mwalimu Julius Nyerere alitoa msamaha kwa Wafungwa wa Kesi ya uhaini baada ya Mahakama kuhukumu kisheria. Rais hakuingilia kesi wakati ikiwa Mahakamani. Alifanya hivyo kwa kuheshimu dhana ya mgawanyo wa Madaraka "Alieleza
Mbeto alisema katika Kesi ya kina Michael Kamaliza na wenzake , alikuwemo Mpigania Uhuru Mstari wa mbele wa TANU , Titi Mohamed lakini Rais kwanza aliheshimu Sheria na Mhimili wa Mahakama.
Aliongeza kusema ikiwa leo Viongozi aidha wa CCM, ACT , Chadema , Chauma na vingine, ikitokea kuvunja sheria, kisha yaanze mazungumzo ya usuluhishi, itakuwa kila anayevunja sheria lazima iwepo meza ya mazungumzo , huko si katika kuheshimu dhana ya Utawala wa Sheria.
"Meli, Jahazi au Ngarawa zinapita majini .Ukiona vyombo hivyo vinasafiri Nchi Kavu au Angani huo ni uchuro. Sheria lazima ifuate mkondo wake. Iwe kwa Wazee , Wanasiasa au Viongozi wote tutumie hekima kila tunaposhauri" Alieleza.
Kadhalika Mbeto alisema katika Awamu ya Tano ya Utawala kulikuwa na baadhi ya mambo kadhaa yalioonekana kuwa magumu lakini hawakutokea
Wazee waliokuwa na ujasiri na kushauri lolote .
0 comments:
Post a Comment