JSON Variables

Saturday, May 10, 2025

RAIS MWINYI AZINDUA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amezindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia na kuiagiza Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais – Katiba, Sheria na Utawala Bora kutenga fedha maalum kwa ajili ya utekelezaji endelevu wa kampeni hiyo.


Amesema ili kufanikisha kampeni hiyo, ni muhimu kuandaa mkakati madhubuti wa kutafuta rasilimali fedha, nyenzo, na utaalamu, ili kufikia lengo la kuwafikishia wananchi wengi huduma za msaada wa kisheria kote nchini.


Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika Uwanja wa Donda, Mtende, Mkoa wa Kusini Unguja.


Aidha, amezitaka wizara zote mbili zinazoshughulikia masuala ya sheria kuongeza ushirikiano, kufanya kazi kwa ukaribu, na kubadilishana uzoefu ili kufanikisha kampeni hiyo.


Ameeleza kuwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ni nguzo muhimu ya kuimarisha utawala bora, upatikanaji wa haki na kichocheo cha amani, utatuzi wa migogoro, utulivu, na ustawi wa jamii.


Rais Dkt. Mwinyi pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake ya mbali, huruma, na upendo kwa Watanzania, kwa kuanzisha kampeni hiyo inayolenga kutoa huduma za sheria kwa wananchi wasio na uwezo wa kupata huduma hizo kwa njia ya kawaida, ameahidi kuziunga mkono kikamilifu juhudi hizo.


Amesisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuimarisha utawala wa sheria kupitia ujenzi wa mahakama saba za mikoa na mbili za wilaya, ambapo tano ni za mikoa na mbili ni za wilaya.


Vilevile, kupitia Mradi wa Maboresho ya Mahakama, Serikali inalenga kuongeza ufanisi katika utendaji wa mahakama na kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kikamilifu katika mchakato wa upatikanaji wa haki, sambamba na kuongeza rasilimali watu.


Mwisho, Rais Mwinyi ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo, hususan kwa wale wenye malalamiko yanayohusu udhalilishaji wa kijinsia, mirathi, na masuala ya wanawake na watoto.


Kampeni hii ya msaada wa kisheria ni mpango wa miaka mitatu unaolenga kuwafikia wananchi katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

0 comments:

Post a Comment