◾️ Kampuni ya kuendeleza mgodi kupatikana mwezi wa 5 mwishoni
◾️ Wananchi wamshukuru Rais Samia kwa kusimamia kuanza tena kwa shughuli za Mgodi Magambazi
▪️Wilaya ya Handeni kuongeza mapato zaidi
▪️Waziri Mavunde asisitiza ajira kwa wananchi wanaouzunguka Mgodi
📍Handeni, Tanga
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ameeleza kuwa Mgodi wa Kati wa Dhahabu wa Magambazi uliopo Wilayani Handeni Mkoani Tanga utaanza kufanya kazi rasmi ifikapo Julai 2025 na unatarajiwa kuleta tija kwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Kijiji cha Nyasa na Wilaya ya Handeni kwa ujumla.
Waziri Mavunde ameeleza hayo leo Mei 10, 2025, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Nyasa, Kata ya Kang’ata, Wilaya ya Handeni, ambapo amekuja kuleta mrejesho wa ahadi aliyotoa Aprili 6, 2025 kuhusu hatma ya uendelezaji wa mgodi huo uliosubiriwa kwa muda mrefu.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake kuhakikisha Mgodi huu wa Magambazi unaanza kufanya kazi na kuwainua wananchi wa hapa na mnyororo mzima wa shughuli za maendeleo.
Baada ya kuchukua hatua ya kupata muafaka wa kuhakikisha mgodi huo unaanza kufanya kazi, Kampuni nyingine ya tatu itateuliwa ndani ya siku 14 kuanzia Mei 12 hadi Mei 26, ambayo itaungana na Kampuni za PMM na East African Metals/CANACO ili kuendesha mgodi huo.
Kipekee nawashukuru sana wananchi wa Nyasa kwa uvumilivu wenu, hili jambo lilikuwa la muda mrefu tangu tumeanza kulifanyia kazi, mlikubali kukaa hapa na kunyeshewa na mvua, na leo mmekuja tena na kukubali kukaa nami kwenye mvua ili kuwapa mrejesho wenu.
Kampuni zinazoendesha mgodi huo kuhakikisha zinatoa kipaumbele kwa wakazi wa Nyasa katika ajira ili wananchi wa Nyasa wanufaike moja kwa moja na uwepo wa mgodi huo katika Kijiji chao.
Faida zitakazopatikana ikiwa ni pamoja na kuinua mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, uboreshaji wa miundombinu ya afya, elimu, barabara na mengine kupitia Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) pamoja na ushiriki wa Watanzania katika mgodi huo kwa kutoa huduma na kuuza bidhaa (Local Content)”amesema Mavunde
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Handeni, Mhe. Amiri Changogo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Japhari Kubecha, na Mbunge wa Handeni Vijijini, Mhe. John Sallu, wamemshukuru Waziri Mavunde kwa kufanyia kazi suala hilo na hatimaye kuondoa kiu ya muda mrefu ya wananchi wa Nyasa na Handeni kwa ujumla.
Naye, Wakili Albert Msando (aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Handeni, hivi sasa ni Mkuu wa Wilaya Ubungo) ameeleza hisia zake za kufurahishwa na hatua hiyo kwani alikuwa akilisimamia kwa ukaribu kipindi akiwa Mkuu wa Wilaya hiyo na kwamba hana deni na wananchi wa Kata ya Kang’ata na Kijiji cha Nyasa baada ya kutatuliwa kwa changamoto hiyo iliyokuwa inawakabili kwa muda mrefu.
0 comments:
Post a Comment