JSON Variables

Friday, May 9, 2025

RAIS MWINYI:ZANZIBAR ITAENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA MSUMBIJI


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt, Hussein Ali Mwinyi amesema  Zanzibar itaendelea   kuimarisha Ushirikiano  wa kiuchumi na Diplomasia na Msumbiji kwa manufaa ya Nchi hizo mbili.


Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipokuwa na Mazungumzo na Rais wa Msumbiji Daniel Francisco Chapo  ambaye yupo nchini kwa ziara maalum yaliofanyika Ikulu, Zanzibar tarehe 9 Mei 2025.


Aidha Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa uamuzi wa kufanya ziara ya Kwanza Tanzania ikiwemo Zanzibar  baada ya kuchaguliwa kunaonesha kuthamini Ushirikiano huo ulioasisiwa na Viongozi  Waasisi wa Mataifa hayo.


Halikadhalika Rais Dkt, Mwinyi amebainisha Maeneo Matano ya kiuchumi ambayo nchi hizo zinaweza kushirikiana kuwa ni Uchumi wa Buluu, Mafuta na Gesi, Uvuvi wa Bahari Kuu, Utalii na Uwekezaji .


Ameeleza kuwa Uzoefu wa Msumbiji katika  sekta ya Mafuta na Gesi ni eneo muhimu la Kiuchumi ambalo Zanzibar inaweza kujifunza kupitia Uzoefu huo wa takribani miaka 20 wa Msumbiji katika sekta hiyo .


Vilevile Rais Dkt,Mwinyi ameeleza kuwa Mafanikio ya  Zanzibar katika Sekta ya Uchumi wa Buluu nayo ni Sekta Muhimu ambayo Msumbiji inaweza   kujifunza kutokana na Mafanikio ya sekta hiyo hapa nchini.

Akizungumzia Lugha ya Kiswahili  Dkt, Mwinyi amesema ni fursa nyengine muhimu ya Ushirikiano  itakayowezesha nchi hizo kubadilishana Walimu kwa Zanzibar kutoa Walimu wa Kiswahili na Msumbiji kutoa Walimu wa Lugha ya Kireno kujifunza hatua ikayochangia kuchochea Utalii kwa nchi hizo .


Kwa upande mwingine Rais Dkt,Mwinyi ameihakikishia Msumbiji kuwa  Serikali itaendelea kutoa Ushirikiano wa kutosha kwa Wananchi wenye asili ya Msumbiji Waliopo Zanzibar wanaofikia 3000 ambao tayari wengine wameshapewa Uraia wa Tanzania.

Naye Rais Daniel Fransisco Chapo amesema Msumbiji ina dhamira ya dhati ya Kuimarisha Ushirikiano na Zanzibar na ziara yake imelenga kukamilisha azma. hiyo.


Rais Chapo ameeleza kuwa ziara hiyo itafungua milango na fursa za Kiuchumi baina ya nchi hizo pamoja Uhusiamo wa kidiplomasia wa muda mrefu.


Ameipongeza Zanzibar kwa mafanikio inayoyapata kupitia Sekta ya Utalii na Uchumi wa Buluu na kwamba Msumbiji ina kila sababu ya Kujifunza.


Alizungumzia Sekta ya Mafuta na Gesi amesema  Msumbiji imepiga hatua kubwa katika Maendeleo ya Sekta hiyo na  kuihakikishia Zanzibar  kuwa Nchi yake ipo tayari  kubadilishana uzoefu katika sekta hiyo kwa Kuwa na mazungumzo na timu za Watendaji wa pande zote mbili.

0 comments:

Post a Comment