JSON Variables

Wednesday, March 12, 2025

RAIS MWINYI AFUTURISHA WANANCHI WA MKOA WA MJINI MAGHARIBI



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt, Hussein Ali Mwinyi amejumuika na Wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi katika  kula futari ya pamoja aliyowaandalia.


Hafla hiyo imefanyika Ukumbi wa Idrissa Abdulwakil Kikwajuni ,Wilaya ya Mjini , Mkoa wa Mjini  Magharibi.


Akizungumza katika Futari Hiyo  Rais Dkt, Mwinyi  amewahimiza Waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi Kuendelea kuiombea Nchi Amani pamoja na Viongozi Wakuu Ili waendelee kuiongoza Nchi kwa Amani na  waendelee kutekeleza Mambo ya Maendeleo.


Hafla hiyo pia imehudhuriwa  na Mke wa  Rais wa Zanzibar,Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation  Mama  Mariam Mwinyi.


Rais Dkt, Mwinyi amekuwa na Utaratibu huo kila Mwaka  unaofanyika  katika Mikoa yote ya Zanzibar .

PIC YATAKA WAKANDARASI KUMALIZA KWA WAKATI UJENZI KIWANJA CHA NDEGE MSALATO


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeuelekeza Wakala wa Barabara  Tanzania (TANROADS) kuhakikisha wanawasimamia Wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.


Maelekezo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo leo tarehe 12 Machi, 2025 jijini Dodoma na Mheshimiwa Augustine Vuma, mara baada ya Kamati hiyo kukagua na kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati ambapo Kamati imeshuhudia kazi kubwa iliyofanyika.


“Tunaipongeza Serikali kwa kuendeleza mradi huu, tumeona utekelezaji wake na kuridhika nao, upande wa jengo tunaona limefika asilimia 51  na linagharimu zaidi ya shilingi Bilioni  190 na barabara ya kuruka na kutua ndege imefika asilimia 85 ambayo inagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 160, rai yetu ni kuwa mradi huu utakamilika kwa wakati kama ulivyopangwa”, amesema Mheshimiwa Vuma.


Mheshimiwa Vuma ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutachochea fursa za kiuchumi na kijamii katika mkoa wa Dodoma na nchi kwa ujumla kutokana na kuwepo kwa fursa nyingi za kibiashara na kiuwekezaji.


Aidha, Mhe. Vuma ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na kuzingatia thamani ya fedha ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa ubora na kwa wakati.


Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi, Mohammed Besta  ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo na ameahidi kuendelea kusimamia mradi huo ili kukamilika kwa muda uliopangwa.


Ameongeza kuwa mradi huo umetoa ajira nyingi kwa wazawa  kwani Wataalamu wengi walioshiriki katika ujenzi wa kiwanja hiki ni Watanzania, licha ya kuwa kampuni za ujenzi ni za Kichina.


Utekelezaji wa mradi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato unajumuisha ujenzi wa Jengo la Abiria, Jengo la kuongozea ndege, barabara ya kuruka na kutua ndege, eneo la maegesho ya ndege ambapo ujenzi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Julai, 2025 kwa mujibu wa mkataba.

WAZIRI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJI MAKOREMO-MGONGORO


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Machi 12, 2025 ameweka jiwe la msingi la Mradi wa Upanuzi wa Mtandao wa Majisafi ya Ziwa Victoria kutoka Makomero - Mgongoro, uliopo kijiji cha Mwamayoka, Igunga mkoani Tabora ambao umegharimu shilingi milioni 840.8


Akizungumza baada ya kuzindua mradi huo, ambao unatarajia kuhudumia wananchi 5,402, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali 

Inaendelea kusimamia utoaji wa huduma za maji safi na salama nchini ili kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji inawafikia wananchi kwa asilimia 100


“Ndugu zangu wananchi, mradi huu ni matokeo ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, kuweni na uhakika kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi   anayewajali, anawapenda na anasikiliza changamoto zenu, endeleeni kutekeleza majukumu yenu ipasavyo kwasababu tunaye kiongozi madhubiti”


Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza RUWASA kuongeza na kusogeza vituo vya kuchotea maji karibu na wananchi “RUWASA hakikisheni miradi hii inatoa maji wakati wote”


Mradi huo ambao umefikia asilimia 80 ya ujenzi unahusisha ujenzi wa vituo sita vya kuchotea maji, Ukarabati wa vituo sita vya kuchotea Maji, Ukarabati wa Manywesheo mawili ya Mifugo, kuchimba mitaro ya kulaza bomba na kufukia mitaro mita 25,000


Mheshimiwa Majaliwa yupo mkoani Tabora kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

KAMPUNI ZA KITANZANIA ZAHIMIZWA KUCHANGAMKIA ZABUNI COMORO

 

Kampuni za Kitanzania zimetakiwa kuomba kandarasi za ujenzi wa miradi inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa visiwani Comoro

Hayo yameelezwa wakati wa mazunguzo kati ya Balozi wa Tanzania, Comoro, Mhe. Saidi Yakubu na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa, Comoro, Bi Rejane Hugouneno De Vreyer yaliyofanyika Moroni Machi 12, 2025.

Bi. De Vreyer alimweleza Balozi Yakubu kuwa Shirika lake linafadhili miradi na programu zenye thamani takriban Euro Milioni 113 kwa mwaka katika sekta za Afya, Ujenzi, Tehama na pia kutoa ushauri katika maeneo ya mifumo ya kodi, bajeti na maboresho ya sera. 

Alisema kuwa miradi yote hiyo hutolewa kwa kandarasi za kimataifa na kutoa mwaliko kwa kampuni za Kitanzania kuchangamkia fursa hizo.

Kwa upande wake, Balozi Yakubu alimweleza Bi De Vreyer kuwa Tanzania ina ushirikiano mkubwa na Comoro katika maeneo yote aliyoyazungumzia na kwa hivi sasa wamekwishaanza kualika kampuni za Kitanzania kuchangamkia fursa za zabuni zinazotangazwa visiwani Comoro.  

Tanzania na Urusi kushirikiana kuimarisha Uhifadhi wa Misitu kwa Teknolojia za Kisasa

 

Na Mwandishi Wetu-Dodoma


Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na Urusi katika sekta ya misitu kwa lengo la kuboresha uhifadhi wa rasilimali zake kupitia teknolojia na mbinu za kisasa.  


Hayo yamejiri katika kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Pindi  Chana (Mb) na wataalamu wa misitu kutoka Urusi waliotembelea Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dodoma leo Machi 12,2025 ambapo majadiliano yao yalilenga kuboresha sekta ya misitu kupitia tafiti na ushirikiano wa kiteknolojia.  


Katika kikao hicho, kilichoshirikisha pia maofisa wa taasisi za sekta ya misitu wakiongozwa na Kamishna wa Uhifadhi, Waziri Chana alieleza kuwa Tanzania ina eneo la misitu lenye takriban hekta milioni 48.1, sawa na asilimia 55 ya ardhi ya taifa na kwamba misitu hiyo ina mchango mkubwa katika mazingira, jamii, na uchumi wa nchi.  


Hata hivyo, Mhe. Chana alionyesha wasiwasi wake kuhusu changamoto zinazoikumba misitu nchini, ikiwemo ongezeko la mahitaji ya mazao ya misitu, upanuzi wa shughuli za kilimo, na ongezeko la makazi ya watu na kusisitiza kuwa ushirikiano na Urusi utasaidia kukabiliana na changamoto hizo kwa kutumia teknolojia za kisasa kama uchunguzi wa mbali, mifumo ya taarifa za kijiografia (GIS), na mbinu bunifu za uhifadhi.


Alifafanua kuwa hatua hiyo ni sehemu ya uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Urusi, ambao ulianza tangu mwaka 1960 na pia alitaja mchango wa taasisi za ndani kama Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), na vyuo maalumu vya mafunzo ya misitu kama Chuo cha Mafunzo ya Misitu (FTI) na Chuo cha Mafunzo ya Viwanda vya Misitu (FITI).  


Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ufundi wa Misitu cha Jimbo la Saint Petersburg, Profesa Alexander Dobrovolsky, alisema kuwa Tanzania ina bioanuwai tajiri inayofaa kwa tafiti za ikolojia na mafunzo ya wanafunzi wa Urusi.  


Aliongeza kuwa Urusi itashirikiana na Tanzania kwa kutumia teknolojia za kisasa kama droni kwa ufuatiliaji wa misitu, kuzuia moto wa misitu, na kudhibiti wadudu waharibifu. Pia alitangaza kuwa chuo hicho kitatoa droni, mafunzo, na programu za kusaidia sekta ya misitu ya Tanzania.  


Kwa kuhitimisha, Waziri Chana alieleza kuwa ziara hiyo ni hatua muhimu katika juhudi za Tanzania kuboresha uhifadhi wa misitu na kuhakikisha rasilimali hizi zinanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo kwa njia endelevu.

Chief wa Kilulu, kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali aina ya fisi akiwa hai na akiishi naye nyumbani kwake.

 

Mahakama ya Wilaya Bariadi mkoani Simiyu imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela pamoja na kuchapwa viboko 12 Emmanuel John (31), maarufu kama Chief wa Kilulu, kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali aina ya fisi akiwa hai na akiishi naye nyumbani kwake.


Mshtakiwa huyo, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kilulu kilichopo kata ya Bunhamala, wilayani Bariadi, na mganga wa kienyeji, alipewa adhabu hiyo katika kesi namba 2458/2025 iliyokuwa ikimkabili kwenye mahakama hiyo.


Hukumu hiyo imetolewa jana na hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Caroline Kiliwa, mara baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.


Awali, akisoma kosa la mshtakiwa, Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mashtaka Mkoa, Lupiana Mahenge, alieleza mahakama kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa na nyara ya serikali, fisi akiwa hai, akimfuga nyumbani kwake kinyume cha sheria.


Alisema kuwa mnamo Januari 1, 2025, katika eneo la kijiji cha Kilulu, mtuhumiwa alikamatwa kufuatia Jeshi la Polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema, ambao waliripoti kuhusu mtuhumiwa kuishi na fisi hai ndani ya nyumba yake.


Alieleza kuwa mtuhumiwa aliishi na fisi huyo kama mnyama wa kufuga kinyume na kifungu cha 86 (1) na kifungu kidogo cha (2)(C)(III) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori sura ya 283, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.


Alisema kuwa kifungu hicho kinasomeka pamoja na kifungu cha 14, jedwali la kwanza na kifungu cha 57 (1), na kifungu cha 60 (2) cha Sheria ya Kupambana na Uhujumu Uchumi sura ya 200, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.


Upande wa mashtaka, katika kuthibitisha kosa hilo, ulipeleka mashahidi sita ambao waliithibitishia mahakama pasipo kuacha shaka.


Mtuhumiwa alipopewa nafasi ya kujitetea aliomba mahakama imsamehe kwa kuwa anategemewa na familia ya watoto wanne, wakiwemo mapacha, ndipo hakimu akatoa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela na viboko 12 ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine.

TAASISI ZA FEDHA ZAKARIBISHWA KUTOA ELIMU MUSOMA

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Bi. Ainess Anderson, akizungumza wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha kwa Watumishi wa Manispaa hiyo, yaliyotolewa na Wataalamu wa Wizara ya Fedha, ikiwa imeambatana  na wataalamu wengine kutoka Taasisi za Serikali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS na NSSF pamoja na Taasisi za Kibenki ikiwemo TCB, CRDB, NMB, NBC.Benki Kuu,  yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya  Manispaa ya Musoma, mkoani Mara.

Afisa Msimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bi. Elizabeth Mzava, akielezea umuhimu wa kujiwekea akiba na kufanya uwekezaji  kabla ya kustaafu kwa watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma ambapo walijitokeza kupata elimu ya fedha iliyotolewa na Wataalamu wa Wizara ya Fedha, pamoja  na wataalamu wengine kutoka Taasisi za Serikali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS na NSSF pamoja na Taasisi za Kibenki ikiwemo TCB, CRDB, NMB, NBC.Benki Kuu, yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, mkoani Mara.

Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Udhibiti Taka Halmashauri ya Manispaa ya Musoma Bw. Mwizarubi Nyaindi, akiuliza swali kuhusu utaratibu wa kujiunga na Hazina Saccos wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wataalamu wa Wizara ya Fedha, ikiwa imeambatana  na wataalamu wengine kutoka Taasisi za Serikali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS na NSSF pamoja na Taasisi za Kibenki ikiwemo TCB, CRDB, NMB, na NBC,  yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya  Manispaa ya Musoma, mkoani Mara.

Meneja Maendeleo ya Biashara wa Benki ya CRDB-Musoma, Bw. Denis Ndagara, akitoa elimu ya umuhimu wa kukopa katika Taasisi rasmi zinazotambuliwa na Serikali kwa watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma ambapo walijitokeza kupata elimu ya fedha iliyotolewa na Wataalamu wa Wizara ya Fedha, pamoja  na wataalamu wengine kutoka Taasisi za Serikali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS na NSSF pamoja na Taasisi za Kibenki ikiwemo TCB, CRDB, NMB na NBC.Benki, yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, mkoani Mara.

Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, wakifuatilia mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wataalamu wa Wizara ya Fedha, ikiwa imeambatana  na wataalamu wengine kutoka Taasisi za Serikali ikiwemo Benki Kuu (BoT), Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS na NSSF pamoja na Taasisi za Kibenki ikiwemo TCB, CRDB, NMB na NBC, yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya  Manispaa ya Musoma, mkoani Mara.

Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, wakiangalia filamu iliyokuwa na mada mbalimbali ikiwemo masuala ya mikopo, akiba, uwekezaji, kujiandaa kustaafu wakati wa  mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wataalamu wa Wizara ya Fedha, ikiwa imeambatana  na wataalamu wengine kutoka Taasisi za Serikali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS na NSSF pamoja na Taasisi za Kibenki ikiwemo TCB, CRDB, NMB na NBC, yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya  Manispaa ya Musoma, mkoani Mara.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano WF, Mara)

...........................

Na. Josephine Majura WF, Mara

 

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Bi. Ainess Anderson, amezikaribisha Taasisi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya fedha kwenda kutoa elimu ya fedha ikiwemo uwekezaji na matumizi sahihi ya mikopo kwa wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.

 

Alitoa wito huo wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha, Taasisi za Serikali na Binafsi kwa Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma ili waweze kujikwamua kiuchumi.

 

“Tunawakaribisha muda wowote kuja kutoa elimu hii muhimu kwa watumishi na wakazi wa Halmashauri yetu ili waweze kuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha”, alisema Bi. Ainess.


Aliongeza kuwa Taasisi za Fedha zinatakiwa kuchangamka kutafuta wateja maeneo yote nchini hivyo wasikae ofisini hadi wakisikia Wizara ya Fedha inaenda kutoa elimu ndipo nao watoke ofisini waambatane nao.


“Wametoa mada nzuri ikiwemo aina za mikopo inayotolewa, vigezo vya kutambua Taasisi rasmi za kukopa, uwekaji wa akiba, kwakweli mada za leo zimetujengea  uelewa mpana wa masuala ya fedha, hivyo niwaombe na niwasisitize mrudi tena kwa wananchi wetu ili elimu hii nzuri kila mwananchi aipate iweze kumsaidia katika shughuli za kila siku za kiuchumi”, alisisitiza Bi. Ainess.


Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambae ni Mtumishi wa Halmashauri ya  Manispaa ya Musoma, Bw. Juma Njwayo, ,alisema kuwa amepata elimu ya masuala ya fedha katika maeneo mbalimbali ikiwemo namna ya kuweka akiba, mikopo, Taasisi rasmi za kuchukulia mikopo na namna bora ya kujiandaa kabla ya kustaafu.


Kwa upande wake Afisa Msimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth Mzava, alisema kuwa katika mkoa wa Mara wamepata mwitikio mkubwa wa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya fedha.


“Tunaendelea kuwaomba wananchi tunapoendelea na zoezi la kutoa elimu ya fedha waendelee kujitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo  ili wawe na uelewa mpana wa masuala ya fedha”, alisema Bi. Elizabeth.


Katika zoezi la kutoa elimu kwa wananchi Timu ya Wataalamu wa Wizara ya Fedha imeambata na Wataalamu kutoka Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS na NSSF pamoja na Taasisi za Kibenki ikiwemo TCB, CRDB, NMB na NBC.

WAZIRI WA BIASHARA NA MAENDELEO YA VIWANDA ZANZIBAR AWASILI ZIMBABWE KUSHIRIKI MKUTANO WA MAWAZIRI WA SADC


Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar,  Mhe. Omar Said Shaaban amewasili jijini Harare, Zimbabwe kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika jijini hapa kuanzia tarehe 12 hadi 14 Machi 2025. 



Mara baada ya kuwasili, Mhe. Waziri Shaaban amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Inspekta Jenerali wa Polisi Mstaafu, Mhe. Simon Sirro aliyekuwa ameongoza na na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaibu Mussa. 



Waziri Shaaban anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri ambao ulitanguliwa na vikao vya Kamati ya Makatibu Wakuu bna Wataalam tarehe 3 hadi 5 Machi, 2025; Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu, tarehe 6 na 7 Machi, 2025; na Kamati ya Fedha, tarehe 9 na 10 Machi, 2025.



Viongozi wengine waliopo kwenye ujumbe wa Tanzania ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi Amina Khamis Shaaban, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Suleiman Hassan Serera, Mratibu waTanzania masuala ya SADC ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri  na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.