JSON Variables

Saturday, April 26, 2025

RECAP : WASIRA AMTAHADHARISHA MARTHA KARUA WA KENYA KUJIPIMA UBAVU NA CCM

 

Amesema kama anajiona anaweza kutatua migogoro aende nchi nyingine za Afrika


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amemjia juu Mwanasheria maarufu na mwanasiasa wa nchini Kenya Martha Karua,  ambaye amekuja nchini kumtetea Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu,  anayekabiliwa na tuhuma za uhaini na kuchapisha picha za uongo mtandaoni.

Wasira amemtaka mwanasheria huyo kuacha kujipima uzito na Chama Cha Mapinduzi huku akimwambia pia kuwa Chama kinaheshimu mamlaka ya Mahakama na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).

Amesisitiza kama Karua anajiona anaweza kushughulika na migoro basi atatue matatizo yaliyoko nchini kwake au mgogoro unaoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Congo (DRC). 

Akizungumza mbele ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma Leo Aprili 25, 2025 , akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuelezea faida za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Wasira alitumia nafasi hiyo kumjibu Karua hatua kwa hatua na kumtaka aache kuingilia mambo asiyoyajua vizuri.

“Tanzania hatuvurugi amani ya Afrika Mashariki isipokuwa tunaendesha mambo yetu kwa amani na salamu ninazompatia Mwanasheria Martha Karua ni kwamba aache kujipima na CCM, CCM ni chama kikubwa Afrika kinachoanza na nyumba kumi," alisema.

Aliongeza kuwa "CCM haina hofu na chama chochote lakini hatuwezi kuingilia kazi ya Mahakama na hatuwezi kuingilia shughuli za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuwa ni vyombo vyenye mamlaka, lakini kama ni mjuzi ashughulike na mambo ya Kenya."


"Akishindwa arudi nyumbani akaendeshe chama chake ambacho sera zake hazijulikani. Atuache Tanzania tuchaguane kwa utaratibu wetu hata mwenyewe na zungumza hapa nilichaguliwa kwa kishindo katika nafasi hii ndani ya Chama, naamini dozi hii inamtosha," amesema 

Wakati Wasira anamjibu mwanasheria huyo wa Kenya alisema Chama kinamheshimu kwa kuwa ni mtu wa Afrika Mashariki, pia kinaheshimu taaluma yake ya sheria.

Martha ni Mwenyekiti  wa Chama cha People’s Liberation Party (PLP) cha Kenya.

“Anahaki kama mwanasheria kama ameitwa na watu wanaoshtakiwa, sasa pale kuna 'katatizo' tuna Polisi, Mahakama na Tundu Lissu. Sasa Polisi wakikukuta umekosea hawaendi kwa Wasira kusema kwamba umekosea wao wamesomeshwa kujua kama umekosea, wakikuchukua hawaruhusiwi kukaa na wewe muda mrefu.

TFS LINDI YAGAWA MICHE 300 YA MATUNDA NA MBAO KUCHOCHEA MAPINDUZI YA LISHE BORA NA UHIFADHI MAZINGIRA

 

TFS Lindi Yagawa Miche 300 ya Matunda na Mbao, Yachochea Mapinduzi ya Lishe Bora na Uhifadhi Mazingira


Lindi – Katika kuadhimisha Miaka 61 ya Muungano wa Tanzania, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Ofisi ya Mkoa wa Lindi, imeshiriki kikamilifu katika sherehe hizo kwa kugawa miche 300 ya miti ya mbao, matunda na kivuli kwa wananchi.

Shughuli hiyo imefanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Nyengedi, iliyopo katika Halmashauri ya Mtama, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mheshimiwa Victoria Mwanziva, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi.


Akizungumza wakati wa hafla hiyo mapema leo, Mheshimiwa Mwanziva aliipongeza TFS kwa juhudi kubwa katika kuhifadhi mazingira kupitia upandaji wa miti, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu muhimu ya kutunza rasilimali za taifa na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tuna kila sababu ya kuunga mkono juhudi hizi, kwani miti inabeba uhai wa Taifa letu. Tuipokee na kuitunza miche hii ili iwe urithi wa kizazi kijacho. Zoezi hili pia linaunga mkono kaulimbiu ya kitaifa kuhusu lishe bora kupitia upandaji wa miche ya matunda, hivyo kusaidia kuboresha afya za wananchi wetu,” alisema Mwanziva.


Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Rondo, PCO John Olomi, aliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na TFS katika juhudi za kulinda mazingira, huku akieleza utaratibu wa upatikanaji wa miche kutoka kwa Wakala huo.

“TFS itaendelea kutoa elimu ya mazingira na kuhamasisha upandaji wa miti kwa maendeleo endelevu. Wananchi wote wanakaribishwa kutembelea bustani zetu za miche na kujipatia miche bure kwa ajili ya kupanda kwenye maeneo yao binafsi, mashamba madogo, shule na taasisi mbalimbali,” alisema Olomi.


Aidha, alifafanua kuwa, “Kwa wakulima na wananchi wa kawaida, miche ya miti hutolewa bila malipo. Hata hivyo, kwa wale wanaohitaji miche kwa ajili ya mashamba ya miti ya kibiashara, mche mmoja huuza kwa bei ya serikali ya Shilingi 500 hadi 600.”

Akibainisha zaidi utaratibu wa maombi, Mhifadhi Olomi alisema kuwa, “Mahitaji ya miche kwa mwananchi mmoja mmoja hutumwa kwa kupitia uongozi wa vijiji vyao, ambao hufanya majumuisho ya maombi yote na kuyawasilisha kwa Meneja wa Wilaya au Meneja wa Shamba husika. Utaratibu huu umewekwa mahsusi kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji sahihi wa taarifa na ufuatiliaji wa matumizi ya miche inayotolewa.”


“Tunawakaribisha wote kutumia fursa hii kuanzisha mashamba au bustani za miti, kwa ajili ya kuhifadhi mazingira na kuongeza kipato kupitia kilimo cha miti na mazao ya matunda,” alisisitiza Mhifadhi Olomi.


Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ilikuwa:

“Muungano Wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa – Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025,” ikisisitiza mshikamano, amani na umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia.


TFS inaendelea kuhamasisha wananchi kuwa sehemu ya juhudi za kitaifa za kulinda na kuhifadhi misitu na mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

BODI YA WAKURUGENZI TASAC YATAKA UFANISI WENYE TIJA YA UWEKEZAJI WA BANDARI

 


NA MWANDISHI WETU, BUKOBA

BODI ya Wakurugenzi  wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi ya ujenzi wa Bandari za Kemondo na Bukoba hivyo fedha hizo zinatakiwa kuleta tija na zirudi kutokana huduma zitazotolewa na Bandari hizo.


Akizungumza na waandishi wa habari wakati ziara Bodi katika Bandari hizo Mwenyekiti wa Bodi hiyo Nah.Mussa Mandia amesema kuwa baada ya maboresho ya miundombinu ya ujenzi wa bandari watahudumia mizigo na abiria kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na ilivyokuwa awali.


Amessema kuwa fedha ya Bandari ya Kemondo bilioni 20 na ujenzi wake umekamilika ambapo huduma zake zimeongezeka hadi kufikia tani 150000 kwa mwezi na mapato yake yameongezeka mara tatu huku Bandari ya Bukoba ujenzi wake ukiwa katika hatua za mwisho unaogharimu zaidi ya sh.Bilioni 19.


Amesema  kuwa kama wadhibiti ni kuhakikisha Bandari hizo zinaendelea kutoa huduma bora na tija kwa serikali huku akitaka wasimamizi wa bandari kusimamia kwa  weledi.


Amesema Serikali ya awamu ya Sita ya Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweza kutimiza ndoto katika upanuzi wa bandari za Kemondo na Bukoba ambayo miundombinu yake ilikuwa ya zamani ambapo haiendani na mahitaji ya sasa.


Hata hivyo amesema kazi bodi itaendelea kushauri katika taasisi wanayoidhibiti ambapo matokeo yake yanaonekana kwa miradi mbalimbali kwenye bandari nchi nzima


Mkuu wa  Bandari ya Bukoba wa TPA Malick Ismail amesema kuwa Bandari hiyo maboresho ya ujenzi bandari hiyo baada ya kukamilika watahudumia meli nne kwa wakati mmoja tofauti na ilivyokuwa awali ambapo walikuwa wakihudumia meli moja. 


WATUMISHI WA UMMA NI TASWIRA YA SERIKALI

 

Watumishi wa umma ni taswira au sura ya Serikali hivyo tunatakiwa tuangalie na kuzingatia namna tunavyofanya kazi na tunapotekeleza majukumu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa niaba ya Serikali. Kila mmoja ana wajibu kwa kutunza taswira ya Serikali tunayoitumikia chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Hayo yamesemwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo wakati anafunga mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani kwa muda wa siku tano.

Bi. Mtulo amewaeleza watumishi hao kuwa Serikali ina sheria, taratibu na kanuni zinawapa mwongozo wa namna ya kufanya kazi kama mtumishi wa umma ambapo katika hayo maadili ya utumishi wa umma, yanatuasa kuhusiana na rushwa. 


“Sisi ni Mawakili wa Serikali, tunaendesha mashauri yenye maslahi mapana ya Serikali ambapo mashauri hayo yana kiwango kikubwa cha fedha na yanahusisha watu mbalimbali ndani na nje ya nchi, hivyo Mawakili wa Serikali tujiepushe na rushwa. Aidha, inapotokea unakutana na mazingira ya rushwa, kimbia ili kulinda taswira ya taasisi na Serikali; heshima, utu na haiba yako kwa jamii na watu wanaokutegemea,” amesisitiza Bi. Mtulo.


Bi. Alice Mtulo amewataka Mawakili hao kutunza siri za Serikali kwa kuwa majukumu wanayotekeleza yanawapa nafasi ya kufahamu taarifa mbali mbali. “Jinsi unavyotunza siri zako, una wajibu wa kutunza siri za Serikali, tuwe waangalifu katika hili.Ukikutwa umevujisha taarifa za Serikali utachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” amefafanua Bi. Mtulo.

Aidha, amewaasa Mawakili hao kuzingatia mawasiliano na uhusiano baina yao na viongozi, watumishi wengine na wadau wanaofanya nao kazi. Alisisitiza kuwa na mipaka kwa kuzingatia taratibu za Ofisi ikiwemo kuwa makini kwa yale wanayoandika na kuongea ikiwa ni pamoja na kufuata sheria, kutumia hekima na busara, kuwa waaminifu na wasikivu kwa Serikali tunayoitumikia.

“Sipo tayari kumvumilia mtu yeyote asiyekuwa na nidhamu kwake yeye mwenyewe, wenzake na kwa kiongozi wake.


Vile vile, ametoa rai kwa Mawakili hao kuzingatia na kutumia mifumo ya TEHAMA kwa kuwa Serikali imejikita kwenye matumizi ya mifumo ya TEHAMA. Ofisi ina mifumo mbalimbali ya TEHAMA ambapo kila mtumishi atapimwa utendaji kazi wake kupitia mifumo hiyo. Alisisitiza kila mmoja anapaswa kujaza taarifa za utekelezaji wa majukumu kupitia mifumo hiyo. “Ukitoka Mahakamani jaza taarifa kwenye mifumo husika ili Ofisi ipate takwimu sahihi na kwa wakati.” Aidha alisisitiza kuhusiana na dhumuni na wajibu wa kila mmoja kwa Ofisi, wajibu kwa wafanyakazi wenzako na wajibu kwako wewe binafsi. “Kumbuka na tafakari kuwa ulikuja  Ofisini peke yako, usifuate mikumbo na usiwe mwanaharakati. Zingatia sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma, endapo una mahitaji ya msingi wasilisha kwa mamlaka husika kwa utaratibu uliowekwa na  yatafanyiwa kazi,” amefafanua Bi. Mtulo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Ofisi hiyo, Bi. Asha Hayeshi amewaeleza Mawakili hao kuwa ni muhimu kwa Wakili wa Serikali kutekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na watumishi wenzake ili kurahisisha mgawanyo wa majukumu na matumizi bora ya ujuzi kwa kila mmoja wakati wa kuandaa majibu ya mashauri ya Serikali, kuchambua ushahidi kwa kina na kuhakikisha mashauri yanaendeshwa kwa ufanisi mkubwa kwa maslahi mapana ya Serikali.

Friday, April 25, 2025

TAIFA LIMEPATA MAFANIKIO MAKUBWA MIAKA 61 YA MUUNGANO-MAJALIWA

 

WAZIRI MKUU,  Kassim Majaliwa amesema Tanzania ni Taifa lililopata mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali za maendeleo katika kipindi cha miaka 61 ya Muungano.


Amesema hayo leo (Ijumaa, Aprili 25, 2025) wakati akizungumza na maelfu ya wakazi wa Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Getrude Mongela. 


Mheshimiwa Majaliwa amefanya ziara ya siku moja katika Wilaya ya Ukerewe ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano.

Amesema kuwa Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar umewezesha kujenga Taifa imara na lisiloyumba “Muungano huu umewezesha kuwa na  Taifa ambalo limepata mafanikio katika miradi mbalimbali ya maendeleo Bara na Visiwani, Muungano huu ni tunu ambayo kila mmoja anapaswa kuilinda, kuienzi na kuisemea popote.”


“Kwenu hapa Ukerewe Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mabilioni mengi ya fedha yameletwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta elimu, afya, maji, mawasiliano na maeneo mengine muhimu. Serikali hii imefanya mabadiliko mengi.”


Kadhalika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa hospitali ya rufaa ya kibingwa yenye hadhi ya mkoa inayojengwa katika Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza.

Akizungumza baada ya kukagua hospitali hiyo Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa hospitali hiyo itawawezesha wakazi wa Wilaya hiyo kutotembea umbali mrefu ikiwemo kwenda  Mwanza kufuata huduma za kibingwa za afya.


Hospitali hiyo inajengwa na Mkandarasi M/S Dimetoclasa Realhope Limited JV Mponela Construction & Co. Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 25.03 na inategemewa kukamilika ifikapo Julai 8, 2026.


Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza ambalo ujenzi wake utagharimu shilingi bilioni 3.7.


Akizungumzia kuhusu sekta ya maji, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Watanzania kuendelea kuwa na imani na Serikali na amewahakikishia kuwa miradi ya maji itatekelezwa kutokana na umuhimu mkubwa wa huduma hiyo kwa jamii.

Akizungumza kuhusu maboresho ya vivuko katika Wilaya ya Ukerewe Meneja Vivuko Kanda ya Ziwa , Vitalis Bilauri amesema Serikali inakamilisha ujenzi wa vivuko vitano ambavyo vitatoa huduma katika Wilaya ya Ukerewe na visiwa vyake.


Naye Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhusiano kwa Umma Anselim Namala amesema kuwa Meli ya MV Clarius ipo katika hatua ya ukaguzi ili ukarabati uanze kufanyika.


Pia, ameongeza kuwa ukarabati wa meli ya Mv Butiama umekamilka na sasa upo katika hatua ya mwisho ya ukaguzi na kupata vibali kabla ya kuanza kutoa huduma kwa wananchi hivi karibuni.

Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema Ujenzi wa Hospitali Teule ya Rufaa ya Kibingwa yenye hadhi ya Mkoa Wilayani Ukerewe ni hatua kubwa katika utoaji wa huduma za afya katika Wilaya ya Ukelewe na Visiwa Vyake.


"Hospitali hii itakapo kamilika itakuwa ni miongoni mwa hospitali zenye hadhi kubwa za utoaji huduma nchini, Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya makubwa katika sekta ya Afya na Ujenzi wa Hospitali hii ni uthibitisho wa mafanikio hayo."

MAAJABU YA RAIS WA BUKINAFASO KUNUNUA GRADERS 1,000.

 

BREAKING: Rais wa Burkina Faso Kapteni Ibrahim Traoré amenunua Graders zaidi ya 1,000 na magari mbalimbali ili kusaidia juhudi za ujenzi wa barabara kote Nchini Burkina Faso.

Jana, alikabidhi rasmi mitambo hiyo kwa timu zinazohusika na maendeleo na matengenezo ya miundombinu ya barabara nchini humo 

Katika hotuba yake, Captain Traoré alisisitiza umuhimu wa kuwa na barabara bora kutoka mashambani hadi sokoni, akieleza kuwa barabara nzuri zitawawezesha wakulima kusafirisha mazao yao kwenda mijini kwa ufanisi zaidi na bila kuharibika.

Uwekezaji huu mkubwa katika maendeleo ya kitaifa unafanyika licha ya shutuma za awali kutoka kwa Jenerali Langley, ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Marekani Kamandi ya Afrika ambaye alidai kuwa Traoré anatumia vibaya akiba ya dhahabu ya nchi ya Burkina Faso kwa manufaa yake binafsi.

MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA, ARUMERU YAPOKEA SHILINGI BILIONI 100.6 ZA MAENDELEO

 

 Dkt. Biteko asisitiza Watanzania wasijaribu kuchezea amani

Dkt. Biteko awataka Watanzania kuenzi, kudumisha Muungano 

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema wananchi wa wilayani Arumeru, mkoani Arusha na Watanzania kwa ujumla wana kila sababu ya kumshukuru na kumuombea Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.


Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 25, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Tengeru Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha ambapo amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia wilaya ya Arumeru imepokea zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Arusha DC imepata fedha kiasi cha shilingi bilioni 49.6 na Wilaya ya  Arumeru imepokea zaidi ya shilingi  bilioni 51  kwa ajili ya shughuli na miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema Dkt. Biteko.


Akiwa Wilayani humo amekagua mradi wa kuboresha miundombinu ya Hospitali ya wilaya Arumeru na mradi wa ujenzi wa jengo la utawala la Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru ambapo ameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa miradi hiyo.

 

Ametoa mfano wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kuwa ni miradi ya umeme na Tanzania ni kati ya nchi chache barani Afrika ambazo zimefanikiwa kuzalisha umeme kwa asilimia 100.


Miradi mingine iliyotekelezwa ni ujenzi wa shule, maabara, hospitali, vituo vya afya, miradi ya kilimo pamoja na barabara.

Licha ya mafanikio hayo Dkt. Biteko ameeleza kuwa Serikali ni sikivu na itaendelea kutatua changamoto za barabara, maji na madaraja zilizopo mkoani Arusha pamoja na maeneo mengine nchini.


Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amewahimiza Watanzania kudumisha amani na mshikamano kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo yaliyopatikana.


 “ Tusijaribu kuichezea amani, amani inapaswa kulindwa kwa gharama yoyote. Rais Samia ameapa kuilinda amani hii kwa gharama yeyote. Nitumie nafasi hii kumkumbusha kila Mtanzania kuwa tunu ya amani ndiyo inayofanya tuendelee kuwa salama na bila amani hatuwezi kuwa na chochote,” amesisitiza  Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano, Watanzania waendelee kudumisha amani, umoja na kuwa na mshikamano usioangalia dini, kabila wala itikadi za siasa. Aidha, Muungano ulipo wa Tanganyika na Zanzibar ni  wa kipekee na wenye faida nyingi, huku akitaja kauli mbiu yake kuwa  “Muungano wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa; Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”


Vilevile, amewahimiza wananchi kushiriki katika Uchanguzi Mkuu na kumchagua Rais, wabunge na madiwani mwezi Oktoba mwaka huu. 

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda amesema kuwa katika mchoro wa mkoa uliopo kutakuwa na barabara ya  itakayojengwa eneo la Usa River pamoja na arabara kuelekea Uwanja wa Ndege Kisongo ili kupunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa Arusha.

Ameendelea kusema kuwa barabara ni ajenda kubwa katika Mkoa huo na kuwapongeza  wananchi kwa kuelewa kuwa maendeleo ni mchakato na kuwa madiwani na wabunge wamekubaliana kipaumbele chao kwa mwaka 2025/26 ni barabara.


Ametoa pongezi kufuatia miradi ya umeme mkoani humo “Tunakushukuru  Naibu Waziri  Mkuu kwa kutuletea mradi wa umeme wa REA na wananchi wanaunganishiwa umeme kwa shilingi 27,000.  Mradi utakaokamilisha umeme katika vijiji na vitongoji vyote kupata umeme katika mkoa wa wetu,” 

Awali akizungumza, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu amesema kuwa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ni taasisi ya kipekee inayotoa huduma za maendeleo ya jamii nchini ambayo ilianzishwa mwaka 1963.


Ameeendelea kusema kuwa Taasisi hiyo ni tegemeo la kuzalisha wataalamu wa maendeleo ya jamii na inaendelea na ujenzi wa jengo la utawala litakalo gharimu shilingi bilioni 5.6 na hadi sasa wametumia shilingi bilioni 2.7.


“Tuna kila sababu ya kumshukuru Rais Samia kwa kutupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu ambao ukikamilika utatatua changamoto ya uhaba wa ofisi kwa kuwa na ofisi 44 zitakazo hudumia watu 94,” amesema Dkt. Jingu.


Aidha, Dkt. Biteko ameendelea na ziara yake siku tano mkoani humo ambapo tayari ametembelea Wilaya za Monduli, Longido na Aumeru ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

USHIRIKIANO WA ZANZIBAR NA OMAN KUENDELEZA KUIMARIKA KATIKA NYANJA MBALI MBALI

 

Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano na Serikali ya Oman katika nyanja mbali mbali ili kuziletea nchi hizo maendeleo.


Ameyasema hayo Ofisini kwake Mazizini Wilaya ya magharibi B wakati alipokuwa akizungumza na mjumbe kutoka Serikali ya Oman Sheikh Abdullwahab Suleiman alipomtambulisha kuwepo Zanzibar kwa ajili ya kufundisha elimu ya mwezi, nyota na sayari nyengine.


Amesema ni muhimu kwa maulamaa kufahamu elimu hiyo katika kuwasaidia kuzitambua vyema sayari na mwenendo wake ambapo elimu hiyo ina manufaa wakati wa muandamo wa mwezi.


Aidha, Mufti huyo aliwataka Maulamaa hao kuzingatia kwa umakini na kuifahamu elimu hiyo, kwani itawaletea Wazanzibari manufaa kujua masuala ya sayari.


Nae Mtaalam wa maswala ya nyota kutoka Oman Sheikh Abdullwahabi Suleiman amesema ujio wake huo Zanzibar una lengo la kutoa elimu kwa Maulamaa pamoja na Mashekh kutoka Ofisi ya Mufti ili kuweza kufahamu elimu hiyo.


Pia ameishukuru Ofisi ya Mufti mkuu wa Zanzibar kwa mapokezi mazuri ambayo yataleta mshikamano baina ya Serikali hizo kwani Zanzibar na Oman wanaudugu wa muda mrefu.


Mtaalam wa maswala ya nyota na sayari Sheikh Abdulwahabi yupo Zanzibar kwa muda wa wiki moja kwa lengo la kutoa elimu hiyo.