JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Jumatatu, 19 Mei 2025

BIASHARA YA MAZAO YA MISITU NA NYUKI YAPAA – MAUZO NJE YA NCHI YAONGEZEKA KWA ASILIMIA 333%


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Serikali imebainisha mafanikio makubwa katika biashara ya mazao ya misitu na nyuki nchini, ikiwemo ongezeko la uzalishaji, viwanda na mauzo nje ya nchi, ikiwa ni matokeo ya uwekezaji wa kimkakati unaofanywa kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Akizungumza leo Mei 19, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati wa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alisema kuwa ndani ya miaka mitano, sekta hizo mbili zimeonyesha ushahidi wa wazi wa kuimarika kwa msingi wa uchumi wa kijani nchini.

Aliongeza kuwa, katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2024/2025, uzalishaji wa mbao kutoka mashamba ya miti ya Serikali unaolimwa kibiashara umeongezeka kutoka mita za ujazo 1,108,791 hadi 1,264,535, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya 155,000 m³.

Aidha, viwanda vya kati na vikubwa vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ya misitu vimeongezeka kutoka 636 mwaka 2020 hadi 1,671 mwaka 2025, huku viwanda vidogo vidogo kama vya useremala vikifikia zaidi ya 7,000 kote nchini.

Waziri Chana alisema kuwa thamani ya mauzo ya mazao ya misitu nje ya nchi nayo imepanda kwa kasi, kufikia Shilingi 458.47 bilioni mwaka 2024/2025, kutoka Shilingi 105.68 bilioni mwaka 2020/2021. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 333.8, jambo alilolieleza kuwa ni matokeo ya kuimarika kwa viwango vya usimamizi na ubora wa bidhaa zinazozalishwa.

Katika upande wa nyuki, Serikali imewezesha ujenzi wa viwanda nane (8) vya kati na vikubwa vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ya nyuki, kutoka kiwanda kimoja (1) mwaka 2020. Viwanda hivyo vimejengwa katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Singida, Iringa, Katavi na Geita.

Mpaka kufikia Aprili 2025, Tanzania imeuza nje ya nchi jumla ya tani 1,321.35 za asali zenye thamani ya Shilingi 15.86 bilioni, ikilinganishwa na tani 430.61 za mwaka 2020/2021 zenye thamani ya Shilingi 5.17 bilioni — ikiwa ni ongezeko la asilimia 206.9.

Kutokana na mafanikio haya, Shirika la Wafugaji Nyuki Duniani limeiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Dunia wa Wafugaji Nyuki (APIMONDIA) utakaofanyika mwaka 2027 na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 4,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani.

“Kuongezeka kwa uzalishaji na thamani ya mauzo ya mazao ya misitu na nyuki ni ushahidi wa mafanikio ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Tunajenga msingi wa uchumi wa kijani unaozingatia uhifadhi, maendeleo ya viwanda na ajira kwa vijana wetu,” alisisitiza Waziri Chana.

Katika hatua nyingine, Waziri Chana amewakaribisha wabunge wote na wadau wengine wa sekta ya maliasili kushiriki maonesho ya Siku ya Nyuki Duniani ambayo yanaendelea jijini Dodoma, na kufikia kilele chake kesho Mei 20, 2025 katika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma.

MADAKTARI WANAWAKE WA KIISLAM TANZANIA WAZINDUA MFUKO WA KUSAIDIA HUDUMA ZA AFYA KWA WATOTO WENYE UHITAJI

Katika kuunga mkono falsafa ya UTU NA MAENDELEO inayoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Madaktari Wanawake wa Kiislam nchini wamezindua rasmi Mfuko wa Kusaidia Huduma za Afya kwa Watoto Wenye Uhitaji, unaojulikana kama Muslimah Medical Support Fund (MMSF).

Mfuko huu ni mwendelezo wa juhudi za kujitolea ambazo madaktari hao wamekuwa wakizifanya kwa muda katika utaratibu usio rasmi, ambapo wamekuwa wakisaidia watoto kutoka familia zisizo na uwezo kupata matibabu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwenyekiti wa MMSF Dkt. Asha Omari Mahita alisema kuwa wazo hilo lilianza kupitia mawasiliano ya kawaida katika kundi la WhatsApp, baada ya madaktari kuguswa na mateso ya watoto wanaokosa huduma muhimu za afya kutokana na ukosefu wa rasilimali.

“Kwa mujibu wa maadili ya Uislamu, huduma ya afya ni haki ya msingi kwa kila binadamu. Tumeona ni wajibu wetu kusaidia kundi hili linaloathirika zaidi, kwa kuanzia na watoto, mpaka Sasa tumekwisha wakatia bima za Afya watoto 500 na malipo ya moja kwa moja hospitalini bila kujali ni dini gani” alisisitiza Dkt. Mahita.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Mstaafu, Prof. Mussa J. Assad, aliwapongeza Madaktari hawa Wanawake kwa moyo wao wa kujitolea na kuonyesha mfano bora wa uwajibikaji wa kijamii. Alisisitiza umuhimu wa kutumia uzoefu wa madaktari waliostaafu ili kupanua huduma kwa walengwa zaidi.

“Mfuko huu unaonyesha dira sahihi ya mshikamano wa kitaifa na matendo yenye kugusa maisha ya wengi. Ninafurahishwa na muundo wa MMSF ambao ni himilivu na unaolenga kupanua wigo wa huduma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,” alisema Prof. Assad.

Waanzilishi wa MMSF wamesema wanatarajia kushirikiana na hospitali, taasisi, watubinafsi na wahisani mbalimbali ili kuhakikisha kuwa watoto kutoka familia zisizo na uwezo wanapata huduma za kitabibu zenye ubora bila vikwazo vya kifedha.

Katika malengo mengine Karibu wa MMSF Dr Khadija Ibrahim alisema malengo ya mbeleni ni pamoja na kusaidia ada kwa waschana waliokwana wanotaka kuwa madaktari na pia kuweka Kambi za kitabibu (Medical camp) vijijini.


WABUNGE WAPONGEZA ONGEZEKO LA IDADI YA WATALII NA MAPATO NCHINI

Na Kassim Nyaki, Dodoma

Wabunge wameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa jitihada kubwa za kutangaza vivutio vya utalii, ambazo zimesaidia kuongeza idadi ya watalii wa kimataifa kutoka 922,692 mwaka 2021 hadi kufikia 2,141,895 mwaka 2024, huku watalii wa ndani wakiongezeka kutoka 788,933 hadi 3,218,352 katika kipindi hicho.

Kwa upande wa maduhuli ya Serikali yametajwa kuongezeka kutoka Shilingi bilioni 397.42 Mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 901.08 Mwaka 2023/2024. Aidha mwaka wa Fedha 2024/2025 kuanzia Julai 2024, hadi kufikia Aprili 2025, Wizara imekusanya jumla ya Shilingi bilioni 912.90 sawa na asilimia 94.2 ya lengo la makusanyo, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko wakati wowote kuwahi kupatikana katika historia ya sekta hii

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii 2025/26 iliyowasilishwa na Waziri Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana, ambaye ameomba Bunge liidhinishe Sh. bilioni 359.98.

Akichangia, Mbunge wa Moshi Vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi, ameipongeza Wizara, taasisi zake za uhifadhi, na wadau wa utalii kwa kazi kubwa ya kuitangaza nchi kimataifa na hivyo kuchangia ongezeko hilo la watalii.

“Tuendelee na mpango wa kutangaza vivutio vya utalii katika nchi za Uarabuni, Japan, Ufaransa, India, na Australia. Ikiwezekana, tutengeneze filamu za utalii kwa lugha za nchi hizo. Tuzitumie pia mashirika ya ndege, vyombo vya habari vya kimataifa, ligi maarufu za mpira duniani, na watu maarufu duniani kutangaza vivutio vyetu. Pia tuendelee kushiriki katika maonesho ya kimataifa kama ITB, ITN ya Ufaransa, na EAC Tourism Expo,” amesema Prof. Ndakidemi.

Naye, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Mhe. Timotheo Mnzava, ameshauri Serikali kuzipa taasisi za uhifadhi uwezo wa kukusanya mapato yatokanayo na utalii na uhifadhi ili kusaidia kuboresha miundombinu ya utalii, kujenga vituo vya askari, na kuweka uzio wa umeme kwenye mipaka ya hifadhi na kupunguza migogoro kati ya wanyamapori na wananchi.

Mbunge wa Kyerwa, Mhe. Innocent Bilakwate ameipongeza TANAPA na NCAA kwa kusimamia uhifadhi na utalii kwa mafanikio, huku akisisitiza kuwa shughuli za kutangaza utalii ziwe endelevu. Alihimiza matumizi ya programu za livestreaming na kuimarisha kituo cha matangazo ya kidijitali kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Kwa upande wake, Mbunge wa Hai, Mhe. Saashisha Mafue, ameiomba Serikali kuendeleza jitihada za kuainisha vivutio vya utalii wa miamba (Geoparks), hatua itakayoongeza bidhaa za utalii na kusaidia kusambaza wageni katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Mbunge wa Moshi Mjini, Mhe. Priscus Tarimo, ameeleza kuwa Serikali imefanya kazi kubwa kuboresha barabara ya Loduare hadi Golini katika Hifadhi ya Ngorongoro. Alishauri Serikali kuimarisha zaidi barabara za ndani (feeder roads) katika hifadhi ili kurahisisha upatikanaji wa vivutio vilivyotawanyika maeneo mbalimbali. 

Jumapili, 18 Mei 2025

President Samia Suluhu Hassan Congratulates Prof. Mohamed Yakub Janabi for being elected as WHO Regional Director for Africa


 Congratulations to Professor Mohamed Yakub Janabi for being elected the World Health Organization Regional Director for Africa, for the term 2025-2030. 


With decades of expertise and experience in the health sector, I have every confidence that you have all that it takes to serve our continent, and steer us all to greater heights.


The United Republic of Tanzania is thankful to every member state that believed in your skills, experience and vision for our continent.


Professor, you have my warmest wishes for a successful tenure.

Rais Mwinyi Ampongeza Prof. Janabi kwa kua Mkurugenzi was Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afeika

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amempongeza Profesa Mohamed Yakoub Janabi kwa kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika.


Uteuzi huu ni uthibitisho wa mchango mkubwa alioutoa Profesa Janabi katika sekta ya afya, pamoja na dhamira yake ya kuimarisha mifumo ya afya barani Afrika.


Zanzibar itaendelea kuunga mkono ajenda ya afya ya kikanda na kimataifa, pamoja na kushirikiana kwa karibu na Profesa Janabi katika juhudi za pamoja za kuboresha huduma za afya.

SERIKALI IPO KAZINI NA INAENDELEA KUFANYAKAZI-MAJALIWA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewahakikishia Watanzania kwamba Serikali ipo kazini na inaendelea kufanyakazi ya kuwahudumia na kuwatumikia wananchi katika maeneo yote nchini na bila ya ubaguzi wa aina yoyote.


Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wananchi waendelea kushirikiana     katika kudumisha amani na utulivu na kwamba wasiwasikilize watu wenye viashiria vya uvunjifu wa amani wanaopita katika maeneo yao.

Ameyasema hayo leo (Jumapili, Mei 18, 2025) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kwideko, Kata ya Ngudu wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.


”Huu ni wakati ambao watumishi wote wanatakiwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao na kuwaeleza miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kwa ajili ya maendeleo yao, ambapo alitolea mfano mradi wa VETA unaojengwa katika wilaya ya Kwimba kwa gharama ya takribani shilingi bilioni mbili.”

Waziri Mkuu amesema wakazi wa wilaya hiyo wanatakiwa kuchangamkia fursa ya ujenzi wa mradi huo kwa kwenda kusoma na kupata ujuzi wa fani mbalimbali ambazo zitawawezesha kujiajiri au kuajiriwa  hivyo kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza kuhusu upatikanaji wa mitaji, Waziri Mkuu amewasihi wananchi hao kuwasilisha mawazo yao ya biashara katika taasisi mbalimbalib za kifedha ambazo zinatoa mikopo.


Pia, Waziri Mkuu amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kwimba Dkt. Amon Mkonga na Maafisa elimu wafanye mapitio ya ikama ya walimu katika shule za wilaya hiyo na kuhamisha walimu kutoka kwenye shule zenye walimu wengi na kuwapeleka katika shule zenye walimu wachache ili nazo ziwe na walimu wa kutosha.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na maelekezo na maagizo anayoyatoa kwa Wizara hiyo ya kutatua changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.


Awali, Waziri Mkuu aweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza na amemtaka mkandarasi ahakikishe anakamilisha mradi huo kwa wakati.

Ujenzi wa jengo hilo la utawala unaotekelezwa katika kata ya Ngudu Wilaya ya Kwimba ulianza tarehe 27/12/2021 ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi bilioni 3.45. Mradi huo ambao upo katika hatua za ukamilishwaji utawawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

ZIARA YA KUSHTUKIZA VIWANDANI YAFANYWA NA KAMISHNA MKUU WA TRA


Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda amefanya ziara ya kushitukiza kwenye baadhi ya Viwanda vilivyopo wilayani Mkuranga mkoani Pwani na kubaini kuwepo kwa ukwepaji mkubwa wa Kodi.unaofanywa na wamiliki wa Viwanda hivyo.


Jana Mei 17, 2025 akiwa katika kiwanda cha kuzalisha viatu vya Plastiki maarufu kama Yeboyebo cha DOLIN Investment Company Ltd na Kiwanda cha nondo cha Fujian Hexingwang lndustry Tanzania Ltd vyote vikiwa vinamilikiwa na wageni, CG Mwenda amesema TRA itafanya uchunguzi wa kiwango Cha Kodi kilichokwepwa ambacho kitalipwa sambamba na Riba pamoja na adhabu.


Kamishna Mkuu Mwenda amesema walipata taarifa kutoka kwa wasamalia wema pamoja na Watumishi wa TRA kwenda kujiridhisha kuhusu kuwepo ukwepaji Kodi na alipofika amebaini kuwepo kwa hali hiyo hivyo Kodi yote ambayo haijalipwa, itapaswa kulipwa na Riba pamoja na adhabu.


“Watumishi wa TRA watakuwepo kwenye hivi Viwanda kwa mwezi mmoja kufanya uchambuzi na ufuatiliaji ili kupata thamani halisi ya Kodi ambayo inapaswa kulipwa” amesema Mwenda huku akiwapongeza wamiliki wa Viwanda kwa kufanya Uwekezaji mkubwa na kuwaajiri Watanzania.


Hata hivyo Kamishna Mkuu Mwenda amewaonya wote wenye tabia ya kukwepa Kodi kujisalimisha maana ukwepaji wa Kodi una athari kubwa na mwisho wa siku ni lazima ilipwe, hivyo amesema Kukwepa Kodi kwa sasa ni kuchelewesha kuilipa tu.

 

WAZIRI MAVUNDE AZINDUA MRADI WA MATUMIZI YA UMEME WA JUA MGODINI IGUNGA-TABORA

▪️Nishati ya umeme wa jua kupunguza gharama za uzalishaji kwa asilimia 65 migodini


▪️Aelekeza kufanyika mradi wa majaribio kwa wachimbaji wadogo


▪️Aipongeza Kampuni ya Madini Taur kwa matumizi ya Nishati safi na kupanua shughuli za mgodi


*Igunga,Tabora*


Imeelezwa kuwa mradi unaotumia teknojia ya kisasa ya uzalishaji umeme wa jua ni mkombozi kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini kwa kupunguza gharama za uzalishaji kwa zaidi ya asilimia 65.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde leo Mei 18, 2025  wakati akizindua mradi wa uzalishaji umeme wa jua uliopo katika kijiiji cha Nanga Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora ambao umesimikwa na Kampuni ya Uchimbaji madini ya Taur Tanzania.


Amesema kuwa, mradi wa uzalishaji umeme wa jua unaunga mkono juhudi za Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan  za kuhamasisha matumizi ya Nishati safi na kupambana na uchafuzi wa mazingira nchi kwa kupunguza matumizi yanayosababisha hewa ya ukaa.


Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amesema teknojia hiyo ya uzalishaji umeme wa jua itapelekwa katika maeneo mengine ya uchimbaji kwa lengo la kuwasaidia wachimbaji wadogo katika maeneo yao ili wachimbe kwa tija na kuchochea uchumi wa Taifa pamoja na kulinda mazingira.

Aidha, Mavunde amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya makubwa katika kuiendeleza Sekta ya Madini ambapo mpaka sasa sekta imeweza kuchangia katika pato la Taifa kwa asilimia 10.1 mwaka 2024 ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya lengo la mwaka 2025 kama ilivyoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi na Mpango wa Maendeleo wa miaka 5.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Mavunde amesema, katika mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora kuna miradi mikubwa ya Utafiti inaendelea katika maeneo hayo ambapo kuna uwezekano mkubwa wa kuanzishwa kwa mgodi mkubwa utakaopelekea kubadilisha maisha na uchumi wa watu katika maeneo hayo.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo amesema uwepo wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Taur Tanzania Limited wilayani Igunga umeleta maendeleo makubwa katika kijiiji cha Nanga na Wilaya ya Igunga kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuleta ajira na kukuza uchumi kwa jamii inayozunguka Mgodi.

Mtondoo amesema Mwaka 2023/24 Wilaya ya Igunga ilizalisha zaidi ya Kilo 400 za dhahabu na kuanzia June 2025 mpaka May Mwaka 2025 Igunga imeshazalisha zaidi kilo 300 za dhahabu, ambapo pia, ametumia fursa hiyo kumuomba Waziri Mavunde kupatiwa Soko la Madini wilayani Igunga.

Naye, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Taur Tanzania Limited Martin George amesema Kampuni hiyo imeanza shughuli za kuchenjua Madini Mwaka 2010 kwa kutumia Nishati ya mafuta (jenereta) na baadae umeme wa tanesco hivyo amesema teknojia ya uzalishaji umeme kwa kutumia jua umesaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa kiwango kikubwa.

 

Listen Mkisi Radio