Jumanne, 20 Mei 2025
HABARI KUBWA ZILIZO PEWA NAFASI KWENYE KURASA ZA MBELE YA MAGAZETI LEO TAREHE 20.05.2025
SERA MPYA YA MAMBO YA NJE IWE NYENZO YA KUTETEA MASLAHI YA TANZANIA KIMATAIFA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa uzinduzi wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ya mwaka 2001, toleo jipya la mwaka 2024, ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na ni nyenzo madhubuti ya kulinda na kutetea maslahi ya taifa ndani na nje ya mipaka.
Aidha, amesema kuwa Sera hiyo inalenga kufungua milango ya fursa mpya za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa pande zote za Muungano, hususan Zanzibar, ambayo kwa kiwango kikubwa inategemea sekta ya nje kwa maendeleo yake.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika uzinduzi wa Sera mpya uliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jana tarehe 19 Mei 2025, Jijini Dar es Salaam.
Vilevile, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kusimama imara maboresho ya Sera hiyo, pamoja na hatua kubwa zilizochukuliwa za kuimarisha diplomasia.
Halikadhalika Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa sekta ya utalii, usafirishaji wa baharini, uzalishaji wa bidhaa kama mwani na karafuu, pamoja na uwekezaji wa miradi ya maendeleo, ni mifano ya utegemezi mkubwa wa Zanzibar katika diplomasia ya kiuchumi.
Kwa upande mwingine Rais Dkt. Mwinyi ameihimiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha inashawishi mataifa rafiki kuanzisha ofisi za uwakilishi Zanzibar ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wageni. Amesema kuwa hatua hiyo itasaidia pia kukuza uwekezaji, kuimarisha sekta ya utalii, na kurahisisha mazingira ya ufanyaji biashara.
Jumatatu, 19 Mei 2025
MAKATIBU TAWALA WASAIDIZI WAPEWA SOMO USIMAMIZI WA MIRADI NA USULUHISHI WA AKAUNTI
Angela Msimbira, PWANI
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sospeter Mtwale, amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa kuhakikisha wanazisimamia Halmashauri zote kufanya usuluhishi wa akaunti za kibenki, hususani tunapoelekea mwishoni mwa mwaka wa fedha wa Serikali.
Akizungumza leo Mei 19, 2025 katika ufunguzi wa Mafunzo ya Uongozi kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa yanayofanyika mkoani Pwani, Mtwale amesema bado kuna baadhi ya Halmashauri ambazo zimekuwa na akaunti ambazo hazijafanyiwa usuluhishi kwa muda mrefu, hali inayokwamisha uwajibikaji na utawala bora wa fedha za umma.
“Mikoa ni taasisi wezeshi. Hakikisheni kuwa mnazisimamia Halmashauri zilizo chini yenu kuhakikisha usuluhishi wa akaunti unafanyika kikamilifu kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha,” amesisitiza.
Aidha, amewakumbusha viongozi hao wajibu wao wa msingi katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika maeneo mbalimbali ya mikoa, akiwataka kuhakikisha miradi hiyo inakidhi viwango na kuendana na thamani ya fedha inayotolewa na serikali.
Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa Makatibu Tawala Wasaidizi kushirikiana kikamilifu katika kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa wakati na kwa weledi, ili kupunguza idadi ya hoja za ukaguzi zinazojitokeza kila mwaka.
“Serikali ina sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya usimamizi wa rasilimali watu na fedha. Ikiwa viongozi mtaisimamia kikamilifu, hoja za ukaguzi zitapungua kwa kiasi kikubwa. Nendeni mkalisimamie hili kwa umakini mkubwa,” amesisitiza.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa serikali kupitia Taasisi ya Uongozi na Ofisi ya Rais – TAMISEMI wa kuimarisha uwezo wa viongozi wa ngazi ya mikoa katika kusimamia utekelezaji wa sera na miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
TUMEJIZATITI KUPUNGUZA CHANGAMOTO KATIKA SEKTA YA ELIMU
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejizatiti katika kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi zikiwemo za sekta ya elimu.
Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Mei 19, 2025) wakati akizungumza na wananchi katika mikutano wa hadhara iliofanyika Sengerema mjini na Buchosa wilaya ya Sengerema akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
Waziri Mkuu amesema miongoni mwa hatua ambazo Serikali imezichukua ni pamoja na kuendelea kutoa elimu msingi bila ya ada na hivyo kuwawezesha watoto wa kitanzania wenye umri wa kwenda shule kupata elimu.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa shule za msingi na sekondari katika maeneo mbalimbali nchini hususani katika yale yenye msongamano mkubwa wa wanafunzi.
”Mkakati mwingine mkubwa unaoendelea kutekelezwa na Serikali ni ujenzi wa mabweni, nyumba za walimu, pamoja na kujenga shule za amali ili wanafunzi watakapomaliza shule hizi waondoke na ujuzi.”
Akizungumzia kuhusu changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, Waziri Mkuu amesema kwa sasa Serikali inatekeleza miradi ya maji ikiwemo ya kutoa maji katika Ziwa Victoria na kuyasambaza kwa wananchi, hivyo amewataka waendelee kuwa na subira.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema uhakikishe unakamilisha mchakato wa ujenzi wa mradi wa soko la halmashauri hiyo ili Sengerema iweze kuwa kituo kikubwa cha biashara.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amewahakikishia wakazi wa wilaya ya Sengerema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kumkabidhi mkandarasi kazi ya ujenzi wa barabara ya Sengerema-Nyehunge ili aanze ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
RC SERUKAMBA AITAKA TRA KUDHIBITI RISITI FEKI, KUHAMASISHA ELIMU YA KODI
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe.Peter Serukamba, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo kuhakikisha wanadhibiti utoaji wa risiti feki kwa bidhaa mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki za kutoa risiti (EFD) ili kuongeza mapato ya serikali.
Akizungumza leo Mei 19, 2025 ofisini kwake baada ya kupokea ugeni wa Viongozi kutoka TRA Makao makuu uliofika kwa ajili ya kuanza kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi kwa njia ya "Mlango kwa Mlango", Serukamba alisema kuwa ni muhimu kwa maofisa wa TRA kutumia elimu na si nguvu wakati wa kukusanya kodi.
Aidha, Mhe Serukamba amewahimiza wafanyabiashara wote mkoani Iringa kupokea elimu hiyo kutoka kwa wataalamu wa TRA na si kufunga maduka au kuwaogopa.
Sambamba na hilo kampeni ya "Mlango kwa Mlango" inalenga kuelimisha wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari, matumizi sahihi ya mashine za EFD, na kutoa risiti kwa kila mauzo.
"Ni muhimu kwa kila mfanyabiashara kutoa risiti halali kwa kila mauzo na kulipa kodi stahiki na hii itasaidia serikali kupata mapato ya kutekeleza miradi ya maendeleo,"amesema Serukamba
MASHAHIDI WA MAJI DAR WAPAZA SAUTI UCHAFUZI WA MITO
Mbeto amtaka Jussa atangaze sera za ACT, Maalim Seif yuko mbele ya haki
Na Mwandishi Wetu ,Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi kimemkanya Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu ,kutaja sera za chama chake na kumtaka aache kulitumia jina la Hayati Maalim Seif Sharif Hamad kama msingi wa sera.
Pia kimesisitiza iwapo ACT hakina sera za kimaendeleo , akae kimya na kuacha kuwapumbaza wananchi kwa siasa za porojo na uchepe.
Matamshi hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanziabr, Idara ya itikadi ,Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis, aliyemtaka Jussa asilitumie jina la Maalim seif aliyetangulia mbele ya haki
Mbeto alisema kwa wananchi wa zanzibari hakuna hata mtu mmoja asiyejua Jussa alikuwa rafiki mwandani wa Maalim seif kwa ukuruba na mnasaba wao.
Alisema wananchi wanataka kusikia sera za ACT , kisha wazilinganishe na sera zilizoleta maendeleo chini ya serikali ya Rais Dk Hussein Ali Mwinyi .
"Kwa Chama cha siasa makini duniani sera huwa ndiyo dira ya ushindani badala ya porojo ,kejeli na matusi kama afanyavyo Jussa na wenzake" Alisema Mbeto.
Aidha alimtaka Jussa asiwafanye wazanzibari kama watu wasio na macho ya kuona yale yaliofanyika , au hawajui kutofautisha maendeleo yaliokuwepo awali na yaliopo sasa.
Mbeto alimtaka Jussa kuelewa kuwa wazanzibari ni watu werevu mno wana akili, maarifa na hekima hivyo hawaghilibiwi kwa porojo na siasa zake za chuki
'Wazanzibari hawako tayari kuendelea kugawanywa kwa siasa za chuki na hasama .Kiu yao ni maendeleo ya nchi yao ,Umoja ,Usalama na Ustawi wa Amani "Alieleza
Katibu huyo Mwenezi alimtaja Jussa na wenzake mara nyingi wamekuwa wakihubiri ubaguzi ambao kwa miaka mingi umechangia kuwagawa wananchi wa Unguja na Pemba
"Maalim Seif hana sifa ya kuitwa shujaa au jemedari wa Zanzibar. Jemedari Mkuu wa Mapinduzi yalioleta zanzibar ukombozi ni Hayati Mzee Abeid Amani Karume kupitia ASP " Alisema Mbeto.
Aliongeza kusema kuwa Maalim Seif ni atabaki kuwa kiongozj aliyekiwa na heshima baada ya kupikwa ,kuandaliwa kisiasa na kiuongozi toka akiwa mwanachama wa CCM.
Pia Katibu huyo Mwenezi alimkanya na kumueleimisha Makamu huyo Mwenyekiti wa ACT akimtaka aache kuvuruga historia ya zanzibar kwa kudai Maalim seif ni jemedari na shujaa wa Zanzibar.
"Maalim Seif ataheshimika kama Kiongozi aliyewahi kuwa Waziri wa Elimu ,Waziri Kiongozi pia Makamo wa kwanza wa Rais SMZ si vinginevyo " Alisiaitiza Mbeto .
Kwa upande mwingine Mbeto slimtaka Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Othman Masoud Othman ,ajiandae kushindwa katika uchaguzi mkuu ifikapo oktoba mwaka huu.
"Jussa huwezi kuzifananisha sifa za uongozi alizokuwanazo Hayati Maalim Seif na Othman .Wazanzibari wanahitaji kupata viongozi wenye maono na wapigania maendeleo hivyo asimlinganishe Othman na Maalim Seif "Alisema
Kadhalika Mwenezi huyo alisema Wazanzibari hawawezi kutoa kura zao na kumpigia othman kwa nafasi ya urais kwani hata hiyo kazi ya kuwa makamo wa Rais SMZ imekuwa ikimshinda
RAIS WA NAMIBIA DKT NETUMBO NANDI-NDAITWAH KUFANYA ZIARA NCHINI MEI 20-21,2025
Rais wa Jamhuri ya Namibia Dkt Netumbo
Nandi-Ndaitwah anatarajiwa kufanya ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini
Tanzania kuanzia kesho tar 20 hadi 21 Mei mwaka huu kwa mwaliko wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluh Hassan.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais,Ikulu Shaaban Kissu imeeleza kuwa Ziara hiyo ya kwanza
ya Rais Dkt Nandi-Ndaitwah chini Tanzania tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri
ya Namibia tar 21 Machi,2025 na inalenga kukuza ushirikiano wa kisiasa,kiuchumi
na kijamii ikiwemo katika nyanja za biashara,uwekezaji na elimu.
Tanzania na Namibia zimejenga uhusiano wa muda mrefu
wa kidugu na kidiplomasia,hivyo ziara hiyo itafungua fursa mpya za ushirikiano
zitakazowawezesha wananchi wan chi zote mbili kunufaika kiuchumi