Timu ya mpira wa miguu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje Sports) imeendelea kuonesha ubora mkubwa kwa kuichapa Wizara ya Afya na kufuzu hatua ya nusu fainali katika mchezo wa mashindano ya Mei Mosi uliopigwa katika uwanja vya Airtel, eneo la Mtipa mkoani Singida.
Mchezo huo uliokuwa wa kuvutia, ulimalizika kwa sare ya 1-1 katika dakika 90 za kawaida ambapo mshindi alipatikana kwa mikwaju ya penati na Nje Sports iliibuka kidedea kwa penati 4-2.
Kocha Mkuu wa Nje Sports, Bw. Shaban Maganga, ameonyesha furaha yake kutokana na juhudi kubwa za wachezaji wake waliopambana hadi mwisho wa mchezo. Ameeleza kuwa nidhamu na utekelezaji mzuri wa maelekezo ndio silaha ya ushindi wao.
"Nawapongeza wachezaji kwa kuonesha nidhamu na kufuata maelekezo, ndiyo siri ya ushindi wetu leo. Tunaendelea kujiandaa zaidi kwa nusu fainali." Alisema kocha Maganga.
Mwenyekiti wa timu, Bw. Ismail Abdallah, naye hakuficha furaha yake, akieleza kuwa ari ya wachezaji na sapoti waliyoipata kutoka kwa uongozi wa wizara ndiyo iliyowasaidia kupata matokeo mazuri.
"Wachezaji wameonyesha juhudi kubwa. Salamu za hamasa tulizopokea leo kutoka kwa Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Wizara yetu zimewapa nguvu ya ziada. Tunapambana hadi kulichukua kombe," alisema.
Mashindano haya ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Mei Mosi kitaifa, yakihamasisha mshikamano na afya miongoni mwa watumishi wa umma.