Mradi wa ujenzi wa daraja la Washi lililopo kata ya Heradu, Wilaya ya Same, ambalo linaunganisha mkoa wa Kilimanjaro na Tanga katika barabara kuu ya Same - Dar es Salaam lenye urefu wa mita 13 limefikia asilimia 45.
Daraja hilo pamoja na kipande cha barabara chenye urefu wa kilomita 0.675 inayojengwa katika barabara hiyo kwa gharama ya Sh 1.4 bilioni inatarajia kukamilika Agosti 28, mwaka huu.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, wakati kamati ya usalama ya Wilaya hiyo ilipofanya ziara ya kutembelea eneo hilo la mradi, Mhandisi Witness Maeda amesema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza changamoto ya mafuriko katika eneo hilo ambalo kipindi cha mvua kubwa barabara hiyo hujaa maji na kusababisha adha kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Aidha, Mhandisi Maeda amesema kukamilika kwa daraja hilo kutasaidia kurahisisha huduma za mawasiliano ya barabara hiyo kuu ambayo imekuwa ikikumbwa na mafuriko mara kwa mara kutokana na maji kujaa barabarani kutokana na changamoto ya daraja.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni amemtaka mkandarasi anayesimamia mradi huo kuhakikisha unajengwa kwa ubora na kwa viwango vinavyotakiwa na kuhakikisha unakamilika ndani ya muda uliopangwa.
0 comments:
Chapisha Maoni