TANZANIA YAJIKITA KUPAMBANA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA
Na, WAF-Dodoma
Tanzania imeongeza juhudi za kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kwa kuimarisha elimu ya afya kwa umma, kuhamasisha mabadiliko ya mtindo wa maisha, na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mkutano wa mwaka wa Chama cha Madaktari wa Magonjwa ya Ndani Tanzania (APHTYA), Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema kuwa Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo na saratani, ambayo yamekuwa chanzo kikubwa cha vifo na kupungua kwa tija ya nguvu kazi nchini.
Hatua hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa taifa katika kufikia dira ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Serikali inatambua kuwa mafanikio ya mpango huu yanategemea uwepo wa wataalam waliobobea katika taaluma zao pamoja na wananchi wenye afya njema, ambao kwa pamoja wataweza kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Dkt. Mollel ameeleza kuwa ongezeko la magonjwa haya linachangiwa na mabadiliko ya mtindo wa maisha, ikiwa ni pamoja na lishe duni, kutofanya mazoezi, matumizi ya tumbaku, na unywaji wa pombe kupita kiasi, hali ambayo inahatarisha ustawi wa taifa na kuathiri juhudi za maendeleo.
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya, inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kinga, lishe bora, na upimaji wa afya mara kwa mara. Vilevile, huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa haya zinaendelea kuimarishwa katika vituo vya afya nchini kote.
Pia, Dkt. Mollel, amebainisha kuwa juhudi hizi ni muhimu ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma stahiki, na taifa linakuwa na jamii yenye afya bora, tayari kushiriki katika kujenga uchumi imara unaojali ustawi wa watu wake.
0 comments:
Chapisha Maoni