JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Ijumaa, 23 Mei 2025

TBS IMEWATAKA WATANZANIA KUWA NA MAZOEA YA KUSOMA NA KUELEWA TAARIFA ZILIZOPO KWENYE VIFUNGASHIO

 

Dar es Salaam — Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewahimiza wananchi kuwa na mazoea ya kusoma na kuelewa taarifa zilizoandikwa kwenye vifungashio vya bidhaa kabla ya kuzinunua, likieleza kuwa taarifa hizo ni muhimu katika kuhakikisha ubora na usalama wa bidhaa zinazotumiwa.

Akizungumza na vyombo vya habari, Meneja wa Ukaguzi na Utekelezaji wa Sheria wa TBS, Nuru Mwasulama, alisema taarifa zinazopatikana kwenye vifungashio ni kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya mtengenezaji na mtumiaji. Alifafanua kuwa taarifa hizo zinahusisha jina la bidhaa, maelekezo ya matumizi, uthibitisho wa ubora, usalama pamoja na tarehe ya mwisho ya matumizi.

"Taarifa za kwenye vifungashio maana yake ni utambulisho wa bidhaa kwa mlaji. Zinakuambia bidhaa hiyo ni nini, inakupa maelekezo ya matumizi, uhakika wa ubora, usalama, na tarehe ya mwisho ya matumizi," alisema Mwasulama.
Kwa upande wake, Afisa Mkaguzi Mwandamizi wa TBS, Baraka Mbajije, alitoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda afya zao kwa kutoa taarifa pindi wanapokutana na bidhaa zilizoisha muda wa matumizi au zenye kasoro.

"Mtumiaji naye ana wajibu wa kuripoti bidhaa yoyote yenye dosari au iliyopita muda wa matumizi kabla mamlaka haijafika," alisema Mbajije.

TBS imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kusoma vifungashio, ikisisitiza kuwa ulinzi wa afya ya mlaji unaanzia katika uelewa wa kile anachonunua na kutumia.

0 comments:

Chapisha Maoni

Listen Mkisi Radio