JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Jumatatu, 2 Juni 2025

TAWA MGUU SAWA KUDHIBITI WANYAMAPORI WAKALI IKUNGI

.................

Ester Maile Dodoma

Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori(TAWA) imeanza kutekeleza mikakati ya kudhibiti makundi ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo katika wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Malisili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) alipokuwa akijibu swali la  Miraji Jumanne Mtaturu ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuondoa Tembo Singida Mashariki ambao wanasumbua na kuharibu mashamba ya Wananchi.

Aidha  Kitandula alisema Katika kudhibiti tembo wanaovamia na kuharibu mashamba ya wananchi wa Singida Mashariki, Serikali kupitia TAWA imeendelea  kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuweka vikosi viwili vyenye Askari 24 wakiwemo Wahifadhi 13 na Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) 11 na kutoa magari matatu (3).

Vilevile, TAWA imeimarisha matumizi ya ndege nyuki kwa kuwafukuza tembo kutoka kwenye maeneo ya wananchi na kuwarejesha hifadhini. Mathalan, kati ya mwezi Novemba 2024 na Mei 2025 kikosi maalum cha Askari Wahifadhi 18 na VGS 6 kikitumia ndege nyuki 2 na mabomu baridi kiliweka kambi katika Jimbo la Singida Mashariki, Wilayani Ikungi na kufanikiwa kudhibiti makundi 23 ya tembo kwa kuwarudisha ndani ya hifadhi. 

Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo tembo. Mathalan, kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Mei 2025 elimu hiyo imetolewa kwa wananchi 517 na Askari 110 wa Jeshi la Akiba katika Kata za Mkiwa, Igombwe, Iglansonia, Mang’onyi, Issuna, Ntuntu na Ikungi.

‘Serikali itaendelea kutumia teknolojia ikiwemo ndege nyuki na kufunga visukuma mawimb (GPS Satellite Collars) ili kufuatilia mienendo ya tembo na kuwadhibiti’ alisisitiza  Kitandula.

0 comments:

Chapisha Maoni

Listen Mkisi Radio