JSON Variables

Sunday, April 6, 2025

MAJALIWA: MEI MOSI INALENGA KUBORESHA USTAWI WA WAFANYAKAZI


_Achangisha zaidi ya sh. Bilioni 1.6 katika harambee ya Mei Mosi 2025_

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yana lengo la kuhamasisha utoaji wa haki za wafanyakazi, kuboresha masharti ya kazi na ustawi wa wafanyakazi kwa ujumla.


Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo jana usiku, Aprili 5, 2025 katika hafla ya chakula cha jioni kwa ajili ya kuchangisha fedha za kugharamia maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Singida. Hafla hiyo ilifanyika kwenye ukumbi wa Royal Village jijini Dodoma.


Amesema dhumuni jingine la maadhimisho hayo ni kutambua na kuenzi michango ya wafanyakazi katika maendeleo ya jamii na uchumi, Mei Mosi ni fursa ya kuonesha mshikamano kati ya wafanyakazi na kuhimiza usawa na haki katika maeneo ya kazi duniani kote.


Waziri Mkuu amesema mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Katika hafla hiyo jumla ya shilingi bilioni 1.62 zilikusanywa  zikiwa  ni ahadi na fedha taslimu, lengo lilikuwa ni kukusanya sh milioni 832.8.


Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete, rais wa TUCTA, Tumaini Nyamuhokya, Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, Martha Mlata.

CCM:Jina la Sheikh Abeid Amani Karume limebaki midomoni mwa wazanzibari wazalendo

 

 

Na Mwandishi  Maalum  , Zanzibar 


Chama Cha Mapinduzi  (CCM ) kimesema kitaendelea kuenzi yale yote yalioanzishwa katika utawala wa Awamu ya Kwanza  chini ya uongozi wa  Rais Hayati Mzee Abeid  Amani  Karume  aliyeuwawa kikatili  Aprili  7 mwaka 1972.


Pia chama hicho bado  kimeahidi   kuwa  kilichokufa ni kiwiliwili cha Mzee  Karume lakini fikra,upeo , vitendo na maono  yake yataendelezwa toka kizazi  hadi kizazi.


Msimamo  huo umetolewa na Katibu  wa Kamati  Maalum  ya NEC  Zanzibar  ,Idara ya Itikadi  , Uenezi na Mafunzo, Khamisi  Mbeto  Khamis , aliyesema  kifo cha Mzee Karume  miaka  53 iliopita,  kimeacha masikitiko na majonzi makubwa.


Mbeto  alisema CCM  kinaamini kuwa  kundi la Wapinga Mapinduzi  Matukufu na maharamia wa madaraka , ndio waliosuka njama za kukatisha maisha  ya kiongozi huyo na kuuridisha   nyuma maendeleo ya Zanzibar     .


Alisema kifo cha kiongozi huyo  jasiri na shupavu, kitaendelea kukumbukwa na kila mzanzibari  kutokana  na uwezo ,upeo na maono ya mbali aliojaliwa kuwa nayo  kiongozi  huyo mzalendo .


"CCM  inaahidi kuendelea kuenzi fikra,  Sera na mikakati  iliotumika katika  Awamu ya kwanza yaliowaletea wananchi maendeleo chini ya  ASP. Tuna jukumu la kuendeleza na kusimamia mema yote  kutekelezwa na kuendelezwa " Alisisitiza 


Aidha aliwahimiza wananachi wa zanzibar kutoacha kumuombea  duwa kwa mungu  Kiongozi  huy azidi kumpa makaazi mema huko aliko na kumsamehe makosa yake  yote.


"Alikuwa kiongozi shujaa na shupavu aliyewewaunganisha wazanzibari  tokea enzi za African  Association Mwaka 1935 hadi kilipoundwa ASP  mwaka 1957 .Lakini pia ndiye   Jemedari Mkuu wa Mapinduzi Zanzibar Januari  Mwaka 1964' Alieleza 


Katibu  huyo Mwenezi  alisema mema aliofanywa na serikali  ya  Mzee  Karume  katika uongozi wake wa miaka nane, yatazidi kukumbukwa na wananachi wa Zanzibar lakini  pia  kwa  kuanzisha mchakato uliounda  Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania  April  26 mwaka 1964 miaka 61 iliopita .


"Hatuwezi kuzungumzia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar   na kusahau  sera na juhudi  za  vyama vya ASP  na TANU. Uamuzi wa waasisi   wawili wa mataifa  yetu  Hayati  Sheikh  Abeid Karume na mwenzake Marehemu  Mwalimu Julius  Nyerere utaendelea kuenziwa "Alisema Katibu  huyo Mwenezi 


Kadhalika aliongeza kusema  pamoja na miaka 53 kupita  tokea Kiongozi  huyo alipouawawa na genge la wapinga Mapinduzi, jina lake  halijatoka midomoni mwa wazanzibari  Wazalendo.

MBOLEA YACHOCHEA MAPINDUZI KATIKA KILIMO CHA PARACHICHI: UZALISHAJI NA USAFIRISHAJI NJE WAONGEZEKA MARA DUFU*


 

BAADA ya wakulima wa zao la parachichi kuanza kutumia mbolea katika kilimo hicho, uzalishaji umeongezeka. 


Matumizi ya mbolea katika zao la parachichi yameongezeka kutoka wastani wa kilo 100 kwa hekta mwaka 2019/20 hadi kilo 150 kwa hekta mwaka 2023/24. 


Ongezeko hilo la matumizi ya mbolea limechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa parachichi inayouzwa nje kutoka tani 17,711 mwaka 2019/2020 hadi kufikia tani 35,627 mwaka 2023/2024.


Takwimu hizo zimetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bi. Elizabeth Bolle, wakati wa majadiliano ya mkutano wa kwanza wa kitaifa wa wadau wa zao la parachichi uliofanyika jijini Dodoma.


Bi. Bolle alieleza kuwa ongezeko hilo ni matokeo ya juhudi za Serikali kupitia TFRA za kuimarisha matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija katika Sekta ya Kilimo. 


“Hivi sasa wakulima wengi wa parachichi wameanza kutumia mbolea. Lengo la Serikali kupitia Ajenda 10/30 ni kuhakikisha kuwa matumizi ya mbolea yanafikia wastani wa kilo 250 kwa hekta ili kuongeza tija ya uzalishaji wa zao la parachihi kutoka wastani wa tani 6 kwa hekta hadi tani 10.8 kwa hekta ifikapo mwaka 2030,” alisema Bolle.


Aidha, alibainisha kuwa TFRA imeanzisha mfumo wa kidijitali wa kusajili wakulima, ili kuwa na takwimu sahihi ambazo pamoja na manufaa mengine zitawezesha kuwahudumia kwa ufanisi kulingana na mahitaji yao ya mbolea.


Mkakati mwingine muhimu ni kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wote ili kuwapunguzia gharama za uzalishaji.

Kwa mujibu wa Bi. Bolle, kutokana na utekelezaji wa mpango wa ruzuku, matumizi ya mbolea yameongezeka kwa kasi kutoka tani 363,599 mwaka 2021/22 hadi kufikia tani 840,714 katika msimu wa 2023/2024 — ishara ya mafanikio makubwa ya mikakati ya Serikali katika Sekta ya Kilimo.


Vilevile, Serikali inashirikiana na viwanda vya mbolea nchini ili kufanya tafiti zitakazowezesha upatikanaji wa mbolea maalum kwa ajili ya zao la parachichi.


Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Kati, Allan Mariki ametoa wito kwa wakulima kuendelea kujisajili kwenye mfumo wa kidijitali ili waweze kupata mbolea ya ruzuku itakayowaongezea tija kwenye shughuli zao.


Amesema Mamlaka inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kutumia mbolea kwenye shughuli zao pamoja na kuwahamasisha kujisajili kwenye mfumo wa kidijitali wa pembejeo za kilimo ili kunufaika na fursa zinazotolewa na Serikali kwa wakulima.

Saturday, April 5, 2025

MRADI WA KUFUA UMEME WA JNHPP WAKAMILIKA RASMI: DKT BITEKO

................
 
📌Asema ni ndoto ya watanzania,awataka wategemee umeme wa uhakika
 
📌Asisitiza kazi iliyobaki ni kuimarisha miundombinu ya kuwafikishia wananchi umeme
 
📌Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Misri kuuzindua rasmi
 
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kutegemea kupata umeme wa uhakika baada ya Mradi wa kufua umeme kutoka Bwawa la Julius Nyerere uliokuwa ukisubiriwa kwa shauku kubwa na Watanzania  kukamilika  rasmi.
 
Waziri Biteko ameyasema hayo leo April 5, 2025 baada ya kutembelea Mradi huo akiwa ameambatana na Mawaziri ambao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mha. Hamadi Masauni.
 
Amesema hivi sasa mitambo yote tisa inafanya kazi ambapo amefafanua kuwa  kukamilika kwa Mradi huo kumechangiwa na maono ya Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dokta Samia Suluhu Hassan ambaye aliupokea Mradi ukiwa katika asilimia 33 ya utekelezaji wake na ndani ya kipindi cha miaka minne ya Uongozi wake ameweza kuukamilisha Mradi. 
 
‘’Tumekuja leo tukiwa na furaha kubwa kwamba mitambo yote tisa imekamilika inazalisha umeme na nina furahi kuwajulisha Watanzania kuwa ile ndoto ya kuwa na umeme kutoka kwenye chanzo hiki kikubwa barani Afrika imekamilika, kazi iliyobaki ni kuimarisha miundombinu ya kuwafikishia watanzania umeme’’ Alisisitiza Dkt Biteko.
 
 
Dkt. Biteko amesema kutokana na nchi kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiwango kikubwa sasa Serikali iko katika mchakato wa kukamilisha mazungumzo na nchi ya Zambia kwa ajili ya kuwauzia umeme na tayari njia ya umeme ya kuunganisha nchi hizo mbili inajengwa.
 
‘’Kile ambacho tumekua tukikiongea miaka mingi kwamba Tanzania itakuwa na uwezo wa kuuza umeme nje ya nchi sasa imetimia katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya sita baada ya msukumo mkubwa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tuna mshukuru sana Mheshimiwa Rais’’

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Mhe.Profesa Kitila Mkumbo amesema kukamilika kwa Mradi huu ni ukombozi wa kiuchumi huku Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Hamadi Masaun amesema Tanzania imeingia katika historia barani Afrika ambapo amesema kazi kubwa iliyobaki ni kutunza vyanzo vya maji ili kuulinda Mradi.

Katika hatua nyingine Mhe Dkt Doto Biiteko amelishukuru Shirika la umeme Tanzania TANESCO kwa utekelezaji wa Mradi kwa kiwango cha kimataifa na kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Mha. Gissima Nyamo-Hanga kwa usimamizi na jitihada zake katika kusimamia miradi mbalimbali ya umeme.
 
Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere umegharimu zaidi ya Shilingi Trilioni 6.5 ambapo mpaka sasa serikali imeshalipa zaidi ya asilimia 99.5.



Friday, April 4, 2025

SHIRIKA LA MASOKO YA KARIAKOO KUJIENDESHA KWA TIJA -CPA ASHRAPH


.................. 

Watumishi wa Shirika la Masoko ya Kariakoo wametakiwa kufanya mageuzi katika utendaji kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na taaluma walizonazo ili kufikia malengo ya Taasisi na kuongeza tija.

Hayo yamesemwa na Meneja Mkuu wa Shirika hilo, CPA Ashraph Yusuph Abdulkarim wakati alipozungumza kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika leo (Aprili 4,2025) Dar es Salaam.

Meneja Mkuu huyo alisema endapo watumishi watafanya kazi kwa nidhamu na uadilifu ni dhahiri kwamba uzalishaji utaongezeka na mazingira ya kazi yataboreshwa na kuleta ufanisi mzuri katika utendaji kazi wa Shirika.

“Nitashirikiana na watumishi wenzangu kulifanya Shirika lisonge mbele na kujiendesha kwa tija pamoja na kudhibiti uvujaji wa mapato, kuongeza vyanzo vya mapato na kuweka mipango mizuri ya kibiashara” alisema CPA Ashraph.

CPA Ashraph amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumuamini na kumteua kuongoza Shirika la Masoko ya Kariakoo kwa nafasi ya Meneja Mkuu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo Hawa Ghasia, pamoja na kumkaribisha Meneja Mkuu huyo alimwagiza kusimamia kwa ukaribu mchakato wa maandalizi ya ufunguzi wa soko la Kariakoo uliopangwa ukamilike mwezi huu Aprili.

“Kazi yako kubwa kwa sasa ni kuhakikisha soko la Kariakoo linafunguliwa mwezi huu Aprili ili kuwezesha wafanyabiashara waweze kuingia ndani kuendelea na biashara kufuatia mradi wa ujenzi na ukarabati wa soko kukamilika,” alisema Ghasia.

Ghasia alisisitiza kuwa Bodi ya Wakurugenzi ina imani kubwa na Mtendaji Mkuu huyo kutokana na uzoefu alioupata alipokuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili hivyo aweke mipango ya kujenga masoko mengine maeneo ya Shirika ya Mbezi Beach na Tabata Bima.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Emma Lyimo aliyemwakilisha Katibu Mkuu kwenye hafla hiyo aliwasihi watumishi kutoa ushirikiano kwa Meneja Mkuu huyo ili atimize majukumu yake kwa ufasaha na kusaidia Shirika kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.

Mwisho


SERIKALI KUIMARISHA MFUMO WA UTAFITI  KATIKA  HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Mganga Mkuu wa Serikali,Dk Grace Maghembe,akizungumza wakati  wa  kongamano la Kisayansi   katika kuelekea Maadhimisho ya   wiki ya Afya Kitaifa 2025 jijini Dodoma .

Sehemu ya Washiriki wakisikiliza hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe,(hayupo pichani) wakati akifungua kongamano la Kisayansi  katika kuelekea Maadhimisho ya  wiki ya Afya Kitaifa 2025 kwa niaba ya Waziri wa Afya,Jenista Mhagama leo Aprili 4,2025 jijini Dodoma.

Sehemu ya Washiriki wakisikiliza hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe,(hayupo pichani) wakati akifungua kongamano la Kisayansi  katika kuelekea Maadhimisho ya  wiki ya Afya Kitaifa 2025 kwa niaba ya Waziri wa Afya,Jenista Mhagama leo Aprili 4,2025 jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua  kongamano la Kisayansi   katika kuelekea Maadhimisho ya   wiki ya Afya Kitaifa 2025 kwa niaba ya Waziri wa Afya,Jenista Mhagama leo Aprili 4,2025 jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua  kongamano la Kisayansi   katika kuelekea Maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa 2025 kwa niaba ya Waziri wa Afya,Jenista Mhagama leo Aprili 4,2025 jijini Dodoma.

........................

SERIKALI imesema  itaendelea kuimarisha Mfumo wa Utafiti na kutumia matokeo,kutenga fedha za kufanyia tafiti na  kusimamia tafiti lengo likiwa ni kuzidi kuiboresha sekta ya afya.
Hayo yameelezwa leo Aprili 4,2025 jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe,  kwa niaba ya Waziri wa Afya,Jenista Mhagama wakati akifungua kongamano la Kisayansi  katika kuelekea Maadhimisho ya  wiki ya Afya Kitaifa 2025.

Dk Shekalaghe amesema Utafiti wa magonjwa ya binadamu ni muhimu katika kuboresha huduma za afya na Kinga ambapo amedai Serikali itahakikisha inazitumia tafiti hizo.

"Miradi mingi ya Utafiti imetekelezwa na  Serikali imefanya mambo makubwa kwa kusaidiwa na tafiti hizo  ambapo dhamira ni kuimarisha tafiti kwa kutumia tafiti."amesema Dkt.Shekalaghe
Kwa upande wake,Mganga Mkuu wa Serikali,Dk Grace Maghembe amesema wameona hawawezi kuadhimisha wiki ya Afya bila kuwa na majadiliano ya kitaaluma.

Amesema forum hiyo imeleta wataalamu mbalimbali lengo ni kupata mawasilisho mbalimbali katika sekta ya afya,kubadiishana uzoefu na kuona namna gani ya kufanya vizuri zaidi.

Pia watapata Nafasi ya kujifunza kupitia wale ambao wanaofanya vizuri zaidi 
Amesema kupitia kauli mbiu tulipotoka tuendapo na tulipo katika sekta ya afya watajifunza mambo mbalimbali huku kwa upande wa tafiti wameweka wabobevu na wale wanaoelekea katika ubobovu.
Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  (TAMISEMI),Dk Rashid Mfaume amesema wanajivunia maboresho katika sekta ya afya kwa  kuwezesha vituo vya Afya kundaa mipango yao wenyewe.

Dk Mfaume ambaye ni Mkurugenzi wa Afya na Lishe Tamisemi amesema wanajivunia mifumo imara katika sekta ya afya ambayo imesaidia upatikaji wa bidhaa za afya kwa kuzidi kuimarika.
"TAMISEMI imeanza kusimamia suala la bima ya Afya kwa wote.Tunamshukuru Sana Mheshimiwa Rais kwenye rasilimali watu kwani katika kipindi Cha miaka minne zaidi ya watumishi 25,000 wameajiriwa.Hospitali 129 mpya zimejengwa majengo zaidi ya 14,"amesema Dk Mfaume.
Kwa upande wake,Mkuu shule ya Uuguzi kutoka Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM)  Prof Steven  Kigusi amesema  wao ni sehemu muhimu kama wadau katika sekta ya afya na dhamira yao ni kuendeleza wataalamu wa Afya wenye ujuzi kupitia shule zao udaktari na Uuguzi.

Amesema wanaendelea kuboresha huduma za afya kwa kuona huduma bora za afya zinawafikia watanzania wengi.

Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dk Edwin Swai amesema wataendelea kufanya tafiti lengo likiwa ni kuhakikisha wanakabiliana na changamoto zote zinazoikabili sekta ya afya.

MAKAMU WA RAIS AONGOZA KIKAO CHA KAMATI YA PAMOJA YA SJMT NA SMZ YA KUSHUGHULIA MASUALA YA MUUNGANO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameongoza Kikao cha 15 cha Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ya kushughulikia Masuala ya Muungano kilichofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 04 Aprili 2025.   

WAKAZI WA ZANZIBAR WATAKIWA KUJITOKEZA KUPIMWA AFYA YA MOYO

Afisa Muuguzi wa  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Happy Mabonka akimpima shinikizo la damu mkazi wa Zanzibar aliyefika katika uwanja wa Amaani kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa bila malipo na wataalamu wa taasisi hiyo katika kikao kazi  cha 20 cha Maafisa Habari, Uhusiano na Itifaki wa Serikali kilichoandaliwa na Idara za Habari - Maelezo za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Picha na JKCI

Na Mwandishi Maalumu – Zanzibar

 Wakazi wa Zanzibar wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa bila malipo na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Rai hiyo imetolewa jana na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aika Nnkya wakati akizungumza na wananchi waliofika katika uwanja wa Amaani uliopo Zanzibar kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za matibabu ya kibingwa zinazotolewa uwanjani hapo.

Huduma hizo zinatolewa kwa washiriki wa kikao kazi cha 20 cha Maafisa Habari, Uhusiano na Itifaki wa Serikali kilichoandaliwa na Idara za Habari - Maelezo za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Akizungumza kuhusu huduma hiyo Dkt. Aika alisema ni muhimu wananchi wakatumia siku nne za mkutano huo kupima afya za mioyo yao ili wajue hali zao kama wanashida waanze matibabu mapema na kama hawana shida wajue jinsi gani ya kujilinda wasipate maradhi ya moyo.

“Katika upimaji huu wale tunaowakuta na matatizo ya moyo tunawapatia dawa za kutumia pia wale ambao wana matatizo makubwa tunawapa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi yetu iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam”.

“Katika siku ya kwanza ya upimaji tumeona watu 64 kati ya hao watu watano tumewakuta na matatizo ya kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo na tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa katika taasisi yetu iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam”, alisema Dkt. Aika.

Nao wakazi wa Zanzibar waliopata huduma ya upimaji na matibabu ya moyo walishukuru kwa huduma hiyo na kusema kuwa imewasaidia kufahamu hali za mioyo yao.

“Nilikuwa na tatizo la presha kuna kipindi niliacha kutumia dawa baada ya presha yangu kukaa sawa, leo nimekuja kupima nimekutwa presha iko juu pia moyo wangu umeanza kutanuka. Daktari amenipa elimu ya matumizi sahihi ya dawa za presha nitaenda kuzingatia yote niliyoambiwa”, alisema Ally Amoor mkazi wa Mlandege.

“Nashukuru sana nimefika hapa nimepata huduma za matibabu na nimepewa dawa bure bila malipo yoyote yale, ninawaomba wananchi wenzangu mtumie nafasi hii kuja kupima na kujua afya zenu zikoje”, alishukuru Asha Salum mkazi wa Makunduchi.

Kikao kazi hicho cha  Maafisa Habari, Uhusiano na Itifaki wa Serikali kinakwenda sambamba za zoezi la utoaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa ya magonjwa mbalimbali zinatolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Hospitali ya Rufaa Lumumba.