Sunday, April 27, 2025
BENKI YA DUNIA YAIMWAGIA SIFA TANZANIA KWA KUSIMAMIA VIZURI UCHUMI WAKE
TANZANIA NA CHINA KUKUZA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI NA KIDIPLOMASIA
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akiwa ameongozana na Mhe. Tang Wenhong, Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na China.
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akiwa katika mazungumzo mafupi na Mhe. Tang Wenhong, Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, baada ya kumpokea katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na China.
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akipitia baadhi ya taarifa alizokabidhiwa na Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Bw. Melckzedeck Mbise, wakati alipoongoza ujumbe wa Tanzania kumpokea Mhe. Tang Wenhong, Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, ambaye amewasili nchini kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na China, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu wa Naibu Waziri Bw. Twaha Mwakioja.
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akisalimiana na Bw. Chu Kun, Kansela wa Uchumi na Biashara wa Ubalozi wa China nchini Tanzania, alipowasili kwa ajili ya kumpokea Mhe. Tang Wenhong, Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na China.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)
....................
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), ameongoza ujumbe wa Tanzania kumpokea Mhe. Tang Wenhong, Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, ambaye amewasili nchini kwa ziara ya kikazi kuanzia tarehe April 26 hadi 29, 2025.
Katika ziara hiyo inatarajiwa kuwa na vikao mbalimbali vya majadiliano kati ya ujumbe wa Tanzania na China, yanayolenga kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
MNDOLWA: 'MZIKI' WA RAIS SAMIA BADO UNAENDELEA UMWAGILIAJI
Mradi wa Membe Kunusuru SGR
Dodoma: Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa amesema kuwa kasi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan bado inandelea katika miradi ya umwagiliaji na kwamba kila mkoa utafikiwa.
Mndolwa amesema miradi yote inaendelea vyema na itakamilika kwa wakati lengo likiwa kuwawezesha wakulima nchini kulima kilimo biashara chenye tija na kuachana na kilimo cha mazoea kinachotumia nguvu nyingi lakini manufaa yake ni madogo.
Mkurugenzi Mndolwa amesema hayo katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo ilipotembea Mradi wa Bwawa la Umwagiliaji Membe mkoani Dodoma.
"Sisi Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji tuna nafuu sana. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na miradi yote inaendelea.
"Rais Samia anatekeleza kwa vitendo ahadi zake, kila mkoa utafikiwa na miradi ya umwagiliaji na uchimbaji wa visima, yote ni kuhakilisha serikali inawawezesha wakulima kupata tija, nchi iwe na chakula cha uhakika na ziada tuuze nje, " alisisitiza.
Mndolwa alisema mathalani kwa sasa Mkoa wa Manyara kuna miradi yenye thamani ya sh bilioni 80 inatekelezwa ukiwamo uchimbaji wa mabwawa na visima vya umwagiliaji, ufugaji wa samaki na utalii.
Akizungumzia Mradi wa Membe uliokamilika kwa zaidi ya asilimia 90, Mndolwa alisema bwawa hilo lenye ujazo wa lita bilioni 12 ambalo lina uwezo wa kumwagilia hekta 2,500 likikamilika litanufaisha watu zaidi ya 1,500.
Alisema mradi huo ni kati ya miradi 22 ukikamilia utawawezesha wakulima kulima na kuvuna mwaka mzima badala ya kusubiri kuvuna kwa msimu.
'Kubwa zaidi mradi huu ni kati ya miradi ya kimkakati wenye lengo la kudhibiti miundombinu ya Reli yetu ya Kisasa ya SGR isiharibike kwa mafuriko.
"Sote ni mashahidi eneo la Kilosa kila mwaka tunashuhudia uharibifu mkubwa unaotoka na mafuriko. Ukipita na SGR katika eneo hilo kuna maporomoko mengi ya maji na chanzo chake ni hiki lakini ujenzi wa Bwawa hili utasaidia maji kupugua na reli yetu kuwa salama kutoka na maji hayo. "
Alisema ujenzi wa mradi huo una faida kuu tatu, moja ni killimo na ufugaji ukiwamo wa samaki, utalii na uboreshaji wa miundombinu.
Alieleza kuwa, mradi huo utaokoa fedha nyingi zilizokuwa zikitumiwa na serikali kwa wanachi wa Kilosa kuokoa maisha, kununua chakula na kukarabati miundombinu mara kwa mara.
Katibu Tawala Msaidizi Sekfa ya Uchumi, Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba alisema changamoto kubwa kwa jiji la Dodoma ni maji na kwamba ujenzi wa bwawa hilo ni fursa kubwa kwani litasababisha wakulima kulima kwa uhakika.
"Mwaka huu Mkoa wa Dodoma tumepata mvua pungufu jambo ambalo ni hatari kwa kilimo chetu, lakini kuwepo kwa bwawa hili kutabadili kilimo chetu kiwe cha biashara na hali ya uchumi wa mwananchi mmoja itaboreka na hatimaye kuongeza pato la taifa," alifafanua Aziza.
PROF. MBARAWA AKUTANA NA NAIBU WAZIRI WA BIASHARA WA CHINA.
Na Mwandishi wetu
Dar es salam.
Waziri wa Uchukuzi Prof Makame Mbarawa amezungumza na Naibu Waziri wa Biashara wa China Mhe Tang Wenhong Jijini Dar es Salaam ambapo Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na China katika sekta ya usafirishaji na biashara, hasa kupitia maboresho ya miundombinu ya bandari, Reli ya TAZARA na Ujenzi wa Reli ya kisasa ya SGR
Kupitia Mkutano huo viongozi hao wamewejadili mikakati ya kuharakisha utiaji saini wa Mikataba ya miradi ya maboresho na ukarabati wa Reli ya TAZARA, kuongeza matumizi ya bandari yetu katika kusafirisha shehena, ambapo Naibu Waziri wa Biashara wa China amesisitiza dhamira ya serikali yao kuendelea kuwekeza nchini Tanzania, huku akieleza kuwa maendeleo yaliyofanyika kwenye bandari, Ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR unaoendelea, na ukarabati wa reli ya TAZARA utakaofanyika vitakuwa kichocheo kikubwa cha biashara na mahusiano ya kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.
Hata hivyo Prof.Mbarawa ameeleza kuwa ushirikiano uliopo baina ya Nchi hizi mbili ni muhimu kwa uchumi wa Taifa na unafungua fursa zaidi kwa wafanyabiashara wa ndani na wa kanda nzima ya Afrika Mashariki.
Aidha Mkutano huo unaenda kuimarisha zaidi urafiki na ushirikiano wa kimaendeleo.
Vilevile Mkutano huo umehudhuriwa na baadhi ya Viongozi na watumishi kutoka TPA,TAZARA, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
DKT. BITEKO AMWAKILISHA RAIS SAMIA UWEKWAJI WAKFU ASKOFU MTEULE JIMBO LA IRINGA
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akisalimiana na Askofu wa Mafinga, Mhashamu Vincent Mwagala wakati alipowasili katika Ibada ya kumsimika na kumuweka wakfu Askofu wa Jimbo la Iringa, Mhashamu Romanus Mihali iliyofanyika katika Viwanja vya Kichangani, Mjini Iringa, Aprili 27, 2025.
Dkt. Biteko anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe za kuwekwa wakfu Askofu Mteule, Romanus Elamu Mihali kuwa Askofu wa Jimbo la Kitume la Iringa.
KONGAMANO LA KWANZA LA KISWAHILI LAFANYIKA NCHINI NAMIBIA.
Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia kwa kushirikiana na Chuo cha Triumphant ziliandaa Kongamano la Kwanza la Kiswahili lililozungumzia mchango wa lugha ya Kiswahili katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika hususan Namibia.
Mgeni Rasmi katika Kongamano hilo lililofanyika Aprili 25, 2025 alikuwa Mheshimiwa Lt.Gen.(Rtd) Epaphras Denga Ndaitwah, Mwenza wa Mheshimiwa Rais wa Namibia.
Mtoa mada Mkuu kutoka Tanzania alikuwa Bi.Consolata Mushi, Katibu Mtendaji wa BAKITA ambaye alimwakilisha Mhe.Prof.Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (MB), Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Watoa mada wengine kutoka Tanzania walikuwa Balozi Lt.Gen.(Rtd) Abdulrahman Shimbo, Balozi Brig.Gen.(Rtd) Francis Mndolwa na Dkt .Eliah Victor, Mkurugenzi wa Vipindi kutoka TBC.
Kwa upande wa Namibia,mtoa mada alikuwa ni mmoja wa Wapigania Uhuru wa Namibia aliyeishi Kongwa, Dodoma nchini Tanzania.
Aidha ,Kongamano hilo lilihudhuriwa wa Wapigania Uhuru wa Namibia walioishi Tanzania,Vijana wa Namibia waliozaliwa uhamishoni, Mabalozi, Wanazuoni,Wanafunzi pamoja na Waandishi wa Habari.
JOWUTA , THRDC WALAANI WANAHABARI KUKAMATWA NA KUPIGWA
Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu nchini (THRDC) wamelaani kuanza kuibuka matukio ya waandishi wa habari na watangazaji kukamatwa na baadhi kupigwa na hata kuharibiwa vifaa vyao vya kazi na vyombo vya dola.
Kauli ya kulaani imetolewa leo Aprili 25 mwaka huu na Mwenyekiti wa JOWUTA Mussa Juma leo mkoani Mbeya, wakati wa mafunzo kwa wanahabari kuhusu uandishi wa habari za uchaguzi, ulinzi na usalama kazini.
Mafunzo hayo yamehusisha waandishi kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe, ambapo Juma amesema matukio ya kukamatwa, kupigwa na kuharibiwa vitendea kazi hayakubaliki katika nchi inayojinadi kuwa inazingatia misingi ya kidemokrasia.
Juma amesema katika siku za karibuni, kumeanza kutokea matukio ya baadhi ya wanahabari kukamatwa na vyombo vya dola, kupigwa na wengine kuzuiwa kufanyakazi, jambo ambalo sio sahihi.
Mwenyekiti huyo, amesema mahusiano mazuri baina ya vyombo vya dola na wanahabari, yalikuwa yameimarishwa katika siku za nyuma lakini sasa yanaanza kuharibika jambo ambalo halipaswi kuvumiliwa.
“Kama mwanahabari amekiuka taratibu zozote kuna utaratibu wa kufuata kisheria, badala ya kutumika nguvu kumkamata ama kumzuia kufanyakazi yake”amesema.
Hata hivyo, Juma amewataka wanahabari nchini, kufanyakazi kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa Habari, hasa kipindi hiki cha harakati za uchaguzi mkuu, ikiwepo kutoandika habari za upendeleo kwa chama chochote za siasa, kuacha kuwa washabiki wa vyama na watowe fursa sawa kwa vyama vyote.
“Msimamo wa JOWUTA kama mwanahabari unataka kujihusisha na masuala ya siasa ni bora kujiweka kando mapema na tasnia ya habari hadi chaguzi zipite, badala ya kutumia chombo chako cha habari kwa maslahi binafsi ya kisiasa”amesema.
Awali,Wakili Jones Sendodo wa kutoka THRDC, amesema mtandao huo unaungana na wadau wote kulaani matukio yoyote ya kunyanyaswa, kupigwa ama kuharibiwa vitendea kazi mtetezi wa haki za binaadamu, wakiwepo wanahabari.
Wakili Sendodo amesema ni vyema vyombo vya dola kuzingatia sheria za nchi wakati wa kutekeleza wajibu wao.
“Tunapinga matukio ambayo yanaendelea kwa vyombo vya dola kutumia nguvu kubwa kuwanyanyasa watetezi wa haki za binaadamu na sisi kama THRDC kwa kushirikiana na wadau wengine tutaendelea kuwatetea na kuwapa msaada wa kisheria, msaada wa ushauri wa kisaikolojia na hata makazi salama ya muda watetezi wa haki za binaadamu wakiwepo wanahabari wanapokabiliwa na majanga ama vitisho”amesema.
Wakili Sendodo pia akitoa mada katika mafunzo hayo ya uchaguzi kwa wanahabari, aliwataka kujua sheria mbalimbali ambazo zinawahusu ili kujitahidi kutozivunja, ikiwepo Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Takwimu, Sheria za Uchaguzi na nyingine.
Hata hivyo, alitaka wanahabari kujali usalama wao wakiwa kazini na kuchukuwa tahadhari mbali mbali ili kuhakikisha wakati wote wanabaki salama, wakati wakitekeleza wajibu wao.
Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya aliwataka wanahabari nchini, kuendelea kujiunga na JOWUTA kwani ndio chama pekee kinachotambulika kisheria kutetea maslahi ya wafanyakazi katika vyombo vya habari na mazingira bora ya kazi.
"Tumekuja kuwapa elimu ya uchaguzi, lakini pia nitumie nafasi hii kuwaomba wafanyakazi wa vyombo vya habari mjiunge JOWUTA, ili tuwe na nguvu moja ya kupigania maslahi yetu," amesema.
JOWUTA inaendelea na kutoa mafunzo kwa wanahabari nchini kuhusiana na kuripoti vyema uchaguzi mkuu mwaka huu na kubaki salama, mafunzo hayo yamedhaminiwa na Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ), Shirikisho la Waandishi wa Habari Afrika (FAJ),THRDC, Taasisi wa Wanahabari ya Kusaidia Jamii za Pembezoni (MAIPAC) na JOWUTA.
MWISHO.
MAJALIWA MGENI RASMI KATIKA MDAHALO WA FURSA ZA MAENDELEO YA USHIRIKA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Aprili 27, 2025 ni mgeni rasmi katika Mdahalo wa upatikanaji Mitaji ya Fedha na Fursa za Maendeleo ya Ushirika, mdahalo huo unafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Awali wakati akitembelea mabanda ya maonesho, Mheshimiwa Majaliwa alizindua mradi wa kwanza wa utekelezaji wa Programu ya BBT(BBT PROJECT 1) . Pia alizindua ramani ya Shoroba za Kilimo nchini.