JSON Variables

Tuesday, April 29, 2025

WAZIRI MKUU ATOA WITO KWA WAANDISHI WA HABARI NCHINI

 

_▪️Awataka watumie akili mnemba kama nyenzo na si kikwazo cha uhuru wao_▪️

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Waandishi wa Habari nchini kutumia Akili Mnemba (Artificial Inteligence) kama nyenzo ya kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo na sio kikwazo cha uhuru wao.


Amesema kuwa katika dunia ya sasa, vyombo vya habari vinakutana na changamoto mpya zinazotokana na maendeleo ya teknolojia, ambapo akili mnemba inachukua nafasi kubwa katika uzalishaji na usambazaji wa habari.


Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 29, 2025) katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, ambayo kitaifa inafanyika Jijini Arusha kwenye Hoteli ya Gran Melia.

Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuandaa sera maalum ya Akili Mnemba, ambayo itatoa mwongozo wa matumizi yake katika vyombo vya habari ili kuhakikisha kuwa teknolojia hiyo inaendana na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari, uwazi, na uadilifu wa uandishi wa habari.  


“Ni ukweli usiopingika kwamba, Akili Mnemba inaweza kuwa msaada mkubwa kwa wanahabari, lakini pia inaweza kuwa chanzo cha changamoto kubwa ikiwa haitatumika kwa busara. Hili linahitaji mjadala wa wazi, sera madhubuti, na ushirikiano wa karibu kati ya sekta zote.”


Amesema Serikali ya Tanzania inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika maendeleo ya Taifa, kwa kupitia vyombo vya habari, imeweza kuwahabarisha wananchi kuhusu shughuli na mipango ya Serikali, kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za kimaendeleo.

Amesema viongozi wanatambua na kuthamini mchango mkubwa wa waandishi wa habari na vyombo vya habari katika kuhabarisha jamii, kuhimiza uwajibikaji na kuimarisha demokrasia nchini. Aidha, wanawahimiza kuendelea kufanya kazi kwa weledi, maadili na uzalendo kwa ajili ya mustakabali wa wananchi na dunia kwa ujumla.


Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema vyombo vya habari vimekuwa sehemu muhimu katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na elimu ya uzalishaji, ujasiriamali, na maendeleo ya kijamii.


Waziri Mkuu ameongeza kwa kusema kuwa vyombo vya habari vimekuwa na nafasi kubwa katika kulinda na kudumisha amani, umoja, na mshikamano wa kitaifa na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuijenga taswira chanya ya Tanzania kimataifa.

Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa Akili Mnemba isiwafanye waandishi wa habari nchini wakafubaa na badala yake wahakikishe wanaitumia vizuri katika utekelezaji wa majukumu yao.


Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa ametumia fursa hiyo kuwapongeza waandishi wa habari kwa kuendelea kupambania matumaini ya wananchi.


Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa mwaka 2025 inasema: “Uhabarishaji kwenye Dunia Mpya: Mchango wa Akili Mnemba (AI) katika Uhuru wa Vyombo vya Habari.”

RC MTANDA AZITAKA TAASISI ZA KISEKTA KUSHIRIKIANA KATIKA KUTEKELEZA MAAGIZO YA WAZIRI MKUU

 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amezitaka Taasisi za kisekta kushirikiana kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa katika kikao kilichofanyika machi 24, 2025 ya kuhakikisha wanamaliza changamoto ya magugu maji katika ziwa victoria haraka iwezekanavyo.

Ametoa Rai hiyo  alipotembelea eneo la Kigongo Ferry, Wilayani Misungwi lililoathirika na Gugumaji Jipya (Salvina Species) ambapo naye ameshiriki zoezi la utoaji magugu maji.

Mhe. Mtanda amesema utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu si la watu wa Bodi ya maji Bonde la ziwa viktoria bali hata Taasisi zingine kama vile Uvuvi kwa kuwa shughuli za uvuvi na ufugaji wa samaki zinafanyika katika ziwa hilo na Ujenzi kwa kuwa kuna shughuli za usafirishaji wa abiria kwa vivuko lakini pia Taasisi za Mazingira pia.


“Hapa kuna athari mbalimbali na sote tunahitajika katika kufanya usafi ziwani, hii shughuli sio ya Bonde tu bali Taasisi na Wizara zingine zinaweza kuathirika lazima muwekeze fedha ili shughuli hii iende vizuri”.

Aidha Mkuu wa Mkoa ameishukuru Serikali kupitia Waziri Mkuu kwa kutoa maelekezo kwa Wizara ya fedha kutoa fedha ya dharura kiasi cha shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kuimarisha huduma katika ziwa viktoria na kukabiliana na gugumaji ikiwemo ununuzi wa mtambo wa uvunaji wa magugu maji katika ziwa viktoria.

Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la ziwa Viktoria Dkt. Renatus Shinhu amesema mpaka sasa tayari tani 441 za magugu maji yameopolewa na shughuli hiyo inaendelea ikiwa ni mpango wa muda mfupo mpaka pale mtambo wa kuvuna magugu maji utakapofika kwa kuwa tayari andiko la kupata fedha limeshawasilishwa Wizara ya Fedha kwa utekelezaji.

Katika kipindi cha mwezi January 2025 ilishuhudiwa ongezeko kubwa la gugumaji jipya na kuanza kuleta athari mbalimbali kwenye sekta ya uvuvi, ufugaji samaki (Vizimba-Luchelele na Bukumbi) na vyombo vya usafiri hususani vivuko katika eneo la Kigongo-Busisi na kuzorotesha huduma ya usafiri kati mkoa wa Mwanza kwenda kwenye maeneo mengine yanayozunguka

Ziwa ambayo yanategemea vivuko hivyo.


Hivyo kupatikana kwa mashine hiyo ya uvunaji itakwenda kusaidia kutatua na kumaliza changamoto hiyo.

SERIKALI YATATUA MGOGORO WA MWEKEZAJI NA WACHIMBAJI WADOGO IFUMBO, CHUNYA-MBEYA

 

▪️Ni maelekezo ya Rais Dkt. Samia kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo


▪️ Waziri Mavunde aelekeza Wanakijiji kupewa Leseni kuhalalisha uchimbaji wao


▪️Mwekezaji aruhusiwa kuendelea na uwekezaji kwa Leseni za eneo la Lupa Market


▪️Uchimbaji wa Eneo la Ifumbo wasimamishwa mpaka vibali vya Mazingira


▪️Naibu Waziri Khamis Chilo asisitiza utunzaji wa mazingira wa Mto Zira


📍 Chunya, Mbeya.


Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameeleza kuwa wananchi wa Kata ya Ifumbo Wilayani Chunya watapewa leseni 2 kati ya 14 za uchimbaji madini zinazomilikiwa na Kampuni ya G & I  katika bonde la Mto Zira na kutambulika rasmi kama wachimbaji halali ili wafanye shughuli za uchimbaji bila usumbufu ikiwa ni hatua ya utatuzi wa mgogoro baina  ya wananchi hao na mwekezaji.

Alisema hayo jana Aprili 28, 2025 wakati akizungumza katika Mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata na Kijiji cha Ifumbo Wilayani Chunya ambapo aliambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.  Khamis Hamza Chilo.


“Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake kushughulikia haya mambo kwa uharaka sana na tuko hapa kwa utekelezaji wa maelekezo yake.


Baada ya kusitisha shughuli za uchimbaji madini katika bonde hilo mwishoni mwa mwezi Desemba 2024 niliunda Kamati ya Wataalam ya kutathmini athari za mazingira yaliyotokana na shughuli za uchimbaji madini katika mto Zira.

Kwa kuwa wananchi wa hapa shughuli zenu zinategemea Mto Zira, nimemwelekeza mwekezaji ili aendelee kudumisha ujirani mwema, tumekubaliana katika leseni 14 anazomiliki, atoe leseni 2 kwa ajili ya wananchi wa Ifumbo na Lupa Market ikiwa ni leseni moja kwa kila kijiji, ambako atafanya tathmini ya mazingira kabla hajakabidhi kwa serikali ya kijiji, tathmini hii ni kwa leseni 7 zilizopo Ifumbo kwa kuwa 7 zilizopo Lupa Market zimeshafanyiwa tathmini.


Kampuni ya G & I ihakikishe kuwa mazingira yanarejershwa kama yalivyokuwa awali kabla uchimbaji huu haujaanza (restoration); iweke mipaka ya leseni zao zinapoishia; Uchimbaji wa eneo la ifumbo uendelee kusimama mpaka utaratibu wa kimazingira utakapokamilika.


Kwa leseni zilizopo Kijiji cha Lupa Market, mwekezaji anaweza kuendelea na uchimbaji kwa kuwa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilishafanya tathmini ya mazingira lakini za Ifumbo zinaendelea kusimama mpaka ukaguzi wa mazingira utakapokamilika baada ya siku 21.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Khamis Hamza Chilo alielekeza kazi ya upandaji miti katika eneo hilo lifanywe haraka sambamba na kuzingatia utaratibu wa kufanya shughuli za kibinadamu umbali wa mita 60 kutoka kwenye ukingo wa mto kwa mujibu wa sheria.


“Nitoe maelekezo kwa NEMC itoe vibali vya ndani ya siku 21 baada ya wahusika kuomba vibali na kukamilsha utaratibu ili kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli zao kwa tija na bila kubughudhiwa lakini pia Mameja wa NEMC wa Kanda zote kufuatilia tathmini ya mazingira yote ambako shughuli za uchimbaji madini zinafanyika  hapa nchini” alisema Chilo.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mkuu wa Wilaya Chunya, Mbaraka Batenga, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Chunya Noel Chiwanga na Mbunge wa Jimbo la Lupa Mhe. Masache Kasaka walieleza kuwa wananchi wa Chunya wamenufaika sana na shughuli za madini katika kipindi cha uongozi wako katika sekta na kuwa wananchi wa Ifumbo wakushukuru sana kwa kulipa jambo hili uzito na kulifanya kwa uharaka na hatimaye leo wamepata mrejesho.

Desemba 30, 2024 Waziri Mavunde alitangaza kusitisha shughuli za uchimbaji madini katika bonde la mto Zira na kuahidi kuunda Kamati Maalum itakayofanya tathmini ya uharibifu wa mazingira uliotokana na shughuli za uchimbaji madini na baada ya kamati hiyo kukamilisha kazi yake ataleta mrejesho.

UCHAGUZI SI MBWEMBWE NA MATUSI NI MAANDALIZI YA USHINDI -MBETO

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar 


Chama Cha Mapinduzi kimesema ACT wapande au washuke  ikiwa kisiwani  Pemba au Unguja  kijue  kitapigwa kumbo la aina yake mwaka huu na kishindo cha ushindi  wa Rais Dk Hussein Ali Mwinyi .


CCM kimewahakikishia wananchi  wa Pemba kuwa  mgombea urais wa ACT  Wazalendo Othman Masoud Othman  hana ubavu wa kumshinda kiongozi aliyeiletea Mageuzi ya kimaendeleo  Zanzibar. 


Hayo yameelezwa na Katibu  wa Kamati  Maalum ya NEC Zanzibar, Idara  ya Itikadi ,Uenezi na Mafunzo , Khamis Mbeto Khamis, aliyesema nguvu  ya umma ndio itakayomrudisha tena Rais Dk Mwinyi  madarakani. 


Mbeto  alisema  uchaguzi  wowote ili chama cha siasa kiweze kushinda ni  mpango wa maandalizi na mikakati  kabambe si mbwembwe, fedhuli wala mikogo.


Alisema CCM kinaamini  kazi kubwa ya mikakati ya kimageuzi kuelekea maendeleo ya kweli  Zanziabr, imefanywa na Rais Dk Mwinyi kwa jinsi anavyoendelea kuitumikia Zanzibar .


"ACT  kiseme na kuonyesha kimefanya nini katika kuwatumikia wananchi .Kiache kulitaja jina la Hayati  Maalim  Seif Sharif  Hamad kama mtaji  wa kupata  kura. CCM kimetenda na yaliofanyika yanaonekana kwa macho " Alisema Mbeto. 


Akijibu madai yaliotolewa na Makamu Mwenyekiti wa ACT Ismail Jussa Ladhu akiwa jimbo la Mtambwe, aliyedai  ACT  kitashinda Uchaguzi  ,ajiandae kushuhudia kikipeperushwa na kimbunga Hidaya .


"Jussa ndiye mgombanishi mkubwa baina ya  viongozi  wenzake na Hayati Maalim  Seif .Wewe Jussa ni  kirusi hatari na mchafuzi wa mahusiano toka mkiwa  CUF na sasa amkiwa ACT "Alisema Mbeto. 


Aidha Katibu  huyo Mwenezi alimtaka Jussa  asimame kama Mwanasiasa mwenye uwezo wa kujieleza na kushawishi wananchi kwa  sera za chama chake na kuacha kukitumia  jina la Maalim seif  kwani sio sera  wala maendeleo. 


"CCM haina kabrasha la  makubaliano  yoyote yaliofanyika kati ya Rais  Dk Mwinyi na  Maalim   Seif.  Kama Jussa ana ushahidi huo auonyeshe na kutaja yalioazimiwa ,  lini na wapi yalikofanyika "Alieleza


Hivyo basi, Mbeto alimtaka Makamu huyo Mwenyekiti ACT  ,aache kubwabwaja  hovyo kwa maneno  ya kutunga na kutamka maneno ya kipuuzi na yenye ujinga mwingi. 


"Jussa  huna siri zozote unazozijua  za Maalim  Seif katika siasa za Zanzibar bali wewe  ni mzandiki na mzushi baada ya Maalim Seif kufariki na kuzikwa kwa heshima  zote " Alisema


Mbeto aliwataja baadhi ya wanasiasa ndani ya ACT ambao walikuwa karibu na Maalim Seif ni kina Hamad  Rashid Mohamed na Juma Duni Haji  lakini si yeye mtoto  wa watu" Alisisitiza Mbeto

HABARI KUBWA ZILIZO PEWA NAFASI KWENYE KURASA ZA MBELE YA MAGAZETI LEO 29.04.2025

 


Good morning, Habari gani popote ulipo Nikukaribishe kupitia vichwa vya habari kwenye magazeti ya leo tarehe 29.04.2025












SERIKALI IMEWEKA MSINGI IMARA KUHAKIKISHA WAANDISHI WA HABARI WANAFANYA KAZI KWA UHURU,BILA BUGHUDHA

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari–MAELEZO, Gerson Msigwa.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari na kujenga mazingira salama kwa waandishi wa habari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha uhuru wa kujieleza unaimarika nchini.


Akizungumza leo Aprili 28, 2025 jijini Arusha katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari–MAELEZO, Gerson Msigwa, amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imeweka msingi imara wa kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi kwa uhuru na bila bughudha.


"Ninawashukuru kwa mijadala yenu kuhusu Akili Mnemba; ni muhimu sana katika kazi za uandishi wa habari. Nimesikia kuhusu maazimio yenu na tutayafanyia kazi," amesema Msigwa. 

Ameeleza kuwa serikali inatekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tangu siku ya kwanza alipoingia madarakani, kuhakikisha vyombo vya habari vinafanya kazi kwa uhuru na waandishi wanalindwa dhidi ya bughudha.

Msigwa amebainisha kuwa serikali itaendelea kulinda haki za waandishi wa habari, kuimarisha uhuru wa kujieleza, na kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha sekta ya habari nchini. 


"Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa hakuna mwandishi anayebughudhiwa na itaendelea kujenga mazingira bora zaidi ya kazi kwa waandishi wa habari," amesisitiza.

Mkurugenzi wa Jamii Africa, Maxence Melo

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jamii Africa, Maxence Melo, ameeleza kuwa uhuru wa vyombo vya habari ni haki ya msingi na siyo hisani, akisisitiza kuwa kila mwananchi ana jukumu la kuutetea.


Melo amesema katika dunia ya sasa yenye wingi wa taarifa, akili mnemba ni silaha muhimu katika kulinda uhuru wa habari. 


Ameongeza kuwa mageuzi ya teknolojia yamepanua uwanja wa habari kutoka kwa vyombo vya jadi hadi kwa watengeneza maudhui wa kidijitali, hivyo kila anayesambaza taarifa anapaswa kulindwa.


Hata hivyo, ametoa tahadhari kuhusu matumizi ya teknolojia mpya kama akili mnemba (AI), akieleza kuwa zinahitaji matumizi ya umakini mkubwa hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ili kuepusha usambazaji wa taarifa potofu.

Katika maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Jamii Africa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, UNESCO na wadau wengine, viongozi wa kimataifa akiwemo Balozi wa Sweden na mwakilishi wa UNESCO wametoa wito wa kuimarisha uhuru wa habari na kuwalinda wanahabari dhidi ya vitisho vinavyochochewa na matumizi ya teknolojia mpya.

Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani mwaka 2025 yanaendelea jijini Arusha hadi Aprili 30, 2025, yakilenga kujadili mafanikio, changamoto, na njia bora za kuimarisha tasnia ya habari kwa maendeleo ya taifa.


Monday, April 28, 2025

RAIS SAMIA IPONGEZA TIMU YA TAIFA YA WANAWAKE KWA KUFUZU KATIKA MASHINDANO YA FUTSAL KWA AFRICA


 Hongereni wanangu Timu ya Taifa ya Wanawake katika Mchezo wa Futsal kwa kufuzu kuingia fainali ya mashindano hayo kwa Bara la Afrika, na wakati huo huo kufuzu kucheza Mashindano ya Kombe la Dunia la Futsal kwa Wanawake 2025 ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), yatakayofanyika huko Manila, Ufilipino baadaye mwaka huu. 

Nimefurahishwa na juhudi na nidhamu yenu katika mashindano haya. Ushindi wenu ni heshima kwa nchi yetu, na hamasa zaidi kwa watoto wa kike kushiriki katika michezo, si tu kwa burudani lakini pia kama ajira. Ninawapenda na ninawatakia kila la kheri.


MAONO YA RAIS DKT. SAMIA YAMEIPAISHA SEKTA YA ANGA-MAJALIWA

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yameiwezesha Tanzania kupiga hatua kubwa za kimaendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo ya Anga.

 

Amesema hayo leo Jumatatu (Aprili 28, 2025) wakati alipofungua Mkutano wa 73 wa Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege kwa Ukanda wa Afrika (ACI Afrika) unaofanyika kwenye Hotel ya Mount Meru.

 

Amesema kuwa moja ya eneo ambalo Rais Dkt. Samia ameendelea kusimamia ni ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege nchini ikiwemo ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege cha msalato kilichopo jijini Dodoma.

 

Ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia anaendelea na uboreshaji wa viwanja vingine vya kimkakati vya Kilimanjaro, Unguja, Pemba, Mwanza, Kigoma, Tabora, Shinyanga na Sumbawanga. “Pia tunaendeleza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti unaolenga kukuza utalii wa mazingira huku tukihifadhi mfumo ikolojia wa Serengeti”.

 

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imewekeza katika ununuzi wa vifaa vya kisasa vya mawasiliano kwenye viwanja wa ndege na masafa marefu ili kuhakikisha kunakuwa na usalama wa ndege na abiria.

 

Amesema kuwa kutokana na jitihada mbalimbali za Serikali za kuiimarisha Sekta ya anga, Tanzania imetajwa na Shirika la ICAO kushika nafasi ya nne barani Afrika kwenye masuala ya usalama wa anga

 

Kadhalika Uwanja wetu wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere umefanikiwa kushinda Tuzo ya Usalama ya Baraza la Viwanja vya Ndege Duniani, katika viwanja vyenye miruko ya ndege 50000 kwa mwaka”

 

Akizungumzia kuhusu shirika la ndege la Tanzania (ATCL) Waziri Mkuu amesema hivi sasa ndege zake zinatoa huduma ya usafiri katika viwanja 15 vya ndani na nje ya nchi katika nchi za Dubai, Mumbai, Guangzhou, Johannesburg, Nairobi, Harare, Lusaka, Entebe na Kinshasa

 

“Shirika pia linatarajia kuongea safari zake katika miji ya London, Lagos, Accra, Juba, Muscat na maeneo mengine ya masoko ya kimkakati ili kuiunganisha Tanzania Kikanda na Kimataifa”

 

Kwa Upande wake, Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa mkutano huo Inatoa jukwaa adimu linalowaleta pamoja viongozi na wasimamizi wa usafiri wa anga, waendeshaji wa viwanja vya ndege kujadili na kubadilishana mawazo katika kuboresha na kuikuza sekta ya usafiri wa Anga.

 

Naye Rais wa Baraza la Viwanja vya Ndege Afrika Emmanuel Chaves amesema kuwa mafanikio endelevu sekta ya anga afrika sio tu kwenye utungaji wa Sera bali kwenye maamuzi tunayoyafanya sasa katika kushirikiana “Kama tutaamua kwa dhati tutajenga Afrika yenye muunganiko na ushindani katika sekta ya anga”