JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Jumapili, 18 Mei 2025

WAKAZI 11,628 MKOANI MTWARA KUONDOKANA NA KERO YA MAJI, RUWASA MILIONI 310 KUJENGA MRADI

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara Abdala Mwaipaya kushotoa,akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa Kijiji cha Michiga Wilayani Nanyumbu Zuwena Kambutu mara baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Ismail Ali Ussi kuweka jiwe la msingi ujenzi wa mradi wa maji utakaogharimu kiasi cha Sh.milioni 310.

Baadhi ya Wakazi wa Kijiji cha Michiga Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara,wakichota maji katika moja ya vituo vya kuchotea maji vilivyojengwa na Wakala wa Maji na Usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Wilaya ya Nanyumbu baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Ismail Ali Ussi kuweka jiwel la msingi ujenzi wa mradi wa maji Michiga utakaogharimu zaidi ya Sh.milioni 310.

Muonekano wa Tenki la kuhifadhi lita 50,000 za maji linalojengwa katika kijiji cha Michiga kwa ajili ya kuhudumian wakazi zaidi ya elfu 11 wa vijiji vya Michiga,Mnazimmoja na Pachani Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara.

.......

Na Mwandishi Maalum, Nanyumbu

WANANCHI zaidi ya 11,628 wa vijiji vya Michiga,Mnazimmoja na Pachani Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara,wameanza kuwa na matumaini ya kuondokana na changamoto ya maji safi na salama baada ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini(Ruwasa) Wilayani humo kuanza ujenzi wa mradi wa maji ya bomba utakaogharimu Sh.310,034,722.20.

Hayo yamesemwa jana na Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Nanyumbu Mkoani humo Simon Mchucha, wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi.

Alisema,mradi huo ulianza kutekelezwa Mwezi Mei 2024 na ulitarajia kukamilika mwezi Aprili 2025 lakini kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza zikiwemo kuchelewa kwa malipo ya Mkandarasi na mvua,muda wa kutekeleza wake umeongezwa hadi Mwezi Julai mwaka huu.

Alisema,chanzo cha mradi huo ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 3,500 kwa saa ambacho kipo kijiji cha Mnazi mmoja.

Mchucha alisema,mradi huo ukikamilika utatoa huduma ya maji safi na salama katika vijiji hivyo na vijiji vya jirani na katika utekelezaji wa mradi wakazi 19 akti yao wanawake 5 na wanaume 14 wamefanikiwa kupata ajira za muda.

Kwa mujibu wake,mradi unatekelezwa kupitia program ya malipo kwa matokeo(PforR) kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 na Mkandarasi amelipwa Sh.152,434,916.92 kati ya fedha hizo Sh.39,411,193.50 malipo ya awali na Sh. 113,023,723.42 fedha za hati ya kwanza ya malipo.

Alisema,utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 81 na kazi zilizopangwa kufanyika ni ujenzi wa nyumba ya uendeshaji wa pampu na uzio ambao umefikia asilimia 90,ujenzi wa tenki la lita 50,000,ujenzi wa vituo 10 vya kuchotea maji,ununuzi na uletaji wa bomba mita 5,596 kuchimba mitaro na kulaza bomba pamoja na ununuzi na ufungaji wa pampu.

Mchucha amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake ya awamu ya sita kuleta fedha hizo ambazo zinakwenda kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.

Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ismail Ali Ussi,amewapongeza wataalam wa Ruwasa kwa usimamizi mzuri na Mkandarasi kutekeleza mradi huo kwa viwango vinavyotakiwa,hata hivyo amemuagiza Mkandarasi kuhakikisha anakamilisha kazi haraka ili wananchi wapate huduma ya maji.

Alisema,Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji ili kuwaondolea wananchi adha ya kukosa huduma za kijamii na kuwapunguzia kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma hizo.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Abdala Mwaipaya alisema,wananchi wa vijiji hivyo wana changamoto kubwa ya huduma ya maji safi na salama,hivyo mradi huo utakuwa suluhisho la changamoto ya maji iliyokuwepo kwa muda mrefu.

WAZIRI MKUU AKGUA UJENZI WA KITUO CHA MAENDELEO YA MICHEZO MALYA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa chuo cha Maendeleo Michezo Malya wilayani Kwimba mkoa wa Mwanza, Mei 18, 2025. Wa tatu kushoto ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi, wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)  

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mshauri Mwelekezi wa Mradi wa Ujenzi wa chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, Peter Naingo, alipokagua mradi huo akiwa katika ziara ya kikazi mkoa wa Mwanza, Mei 18, 2025. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, wa tatu kulia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi , wa nne kulia ni Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega na wa tano kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni , Sana na Michezo, Gerson Msigwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Rais Mwinyi ajivunia utendaji wa Serikali yake Zanzibar



Na Mwandishi  Wetu, Zanzibar 


Chama  Cha Mapinduzi  kimesema kina matumaini makubwa ya kushinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba  Mwaka  huu, baada ya  kutekeleza ahadi  zake za kisera zilizoleta maendeleo na kuwatumikia wananchi kwa Haki na Usawa.


Kimesisitiza kitashinda tena na kuongoza Serikali  ya zanzibar  kwa ridhaa na matakwa ya wananchi ili kukata ngebe za upinzani  Visiwani humu.


Makamu Mwenyekiti  wa CCM  Zanzibar  na Rais wa SMZ  , Dk Hussein Ali Mwinyi , ameeleza hayo katika mkutano  wa hadhara akifungua  Tawi la CCM  la kisasa huko Mpendae Juu ,Mkoa wa Mjini Magharibi Kisiwani Unguja. 


Rais Dkt  Mwinyi  alisema CCM kitashinda kwa kishindo na kupata kura nyingi   bada ya kutekeleza wajibu wake wa kuwatumikia wananchi kwa  vitendo ,hali ilioleta mabadiliko ya kimaendekeo ,.


Alisema kutokana na  CCM kutimiza ahadi zake zilizoleta mageuzi  katika  sekta muhimu za maendeleo ,hatua hizo zimekuza ustawi kwa wananchi kupitia  ilani ya uchaguzi ya CCM Mwaka 2020/2025.


"Wananchi  na wana CCM  wa Mkoa wa Mjini Magharibi nina furaha kuona  mmejiandikisha kwa wingi katika  Daftari la Kudumu la Mpiga Kura. Kazi iliobaki na jukumu  lenu ni kupiga  kura ifikapo oktoba mwaka huu"Alisema Rais Dk Mwinyi 


Aidha Makamu  huyo Mwenyekiti wa CCM  Zanzibar ,alisema kujitokeza kwenu na kupiga kura kwa mgombea  urais wa zanzibar kupitia  CCM , Wabunge ,  Wawakilishi na Madiwani wa chama chenu  kutaka ngebe za wapinzani  wetu .


Aliwasisitiza wananchi na wana CCM,Rais huyo  wa Zanzibar alisema kazi kubwa iliobaki iko mikononi mwa wananchi ya kujitokeza mapema na kupiga  kura.


"Kazi imebaki kwenu ya kukirudisha chama chenu madarakani. Tutahakikisha Zanzibar  inazidi kupaa  kimaendeleo kuliko ya miaka mitano ya kwanza. Hiyo ni ahadi yangu  kwenu na kwa wazanzibari  wote "Alisisitiza Rais Dk Mwinyi

Jumamosi, 17 Mei 2025

TANZANIA YAPOKEA MSAADA WA SH. BILIONI 185 KUTOKA CHINA


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China zimetia Saini mikataba miwili ya msaada wa jumla ya Yuan za China milioni 500, sawa na shilingi bilioni 185 kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete pamoja na kusaidia program ya ushirikiano wa kiuchumi na kitaalamu. 


Mikataba hiyo imesainiwa Ofisi za Wizara ya Fedha (Treasury Square) na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian. 


Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo, Dkt. Nchemba, alisema kuwa Mkataba wa kwanza ni wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Kitaalam wenye thamani ya Yuan za China milioni 200 sawa na shilingi bilioni 74.2 na Mkataba wa pili kwa ajili ya mradi wa Upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kuwa Kituo cha Umahiri cha matibabu na upasuaji wa moyo Afrika Mashariki na Kati wenye thamani ya Yuan za China milioni 300, sawa na shilingi bilioni 111.2.

“Lengo la misaada hii ni kuwezesha utekelezaji wa miradi itakayochaguliwa na kukubalika kwa pamoja na Serikali za Tanzania na China, na mkataba wa pili una lengo la kujenga Kituo cha Umahiri cha Matibabu ya Magonjwa ya Moyo ya Watoto kwa ajili ya Tanzania na nchi za Afrika Mashariki na Kati”, alieleza Dkt. Nchemba. 

Dkt. Nchemba alisema kuwa, msaada wa Ushirikiano wa kiuchumi na Kitaalamu ni ahadi aliyoitoa Mhe. Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, wakati wa kikao chake na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Tisa la Kilele la Ushirikiano wa China na Afrika la mwaka 2024, uliofanyika jijini Beijing.  


Alisema kuwa msaada wa ujenzi wa hospitali ya magonjwa ya moyo kwa watoto Mloganzila - unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kama vile upatikanaji wa huduma bora za afya, kukuza uchumi kupitia kuongeza ajira na kuchochea biashara kwa wananchi ili kuboresha maisha yao, kukuza utafiti katika masuala ya afya na elimu na kuendeleza miundombinu.

Alisema kuwa misaada hiyo inadhihirisha kwamba Jamhuri ya Watu wa China inabaki kuwa rafiki wa kweli na wa kutumainiwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo na kuendelea kudumisha urafiki wa muda mrefu kwa manufaa ya pande hizo mbili.


Aidha amemhakikishia Balozi huyo wa China utayari wa Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya China. 


Kwa upande wa Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe.Chen Mingjian, alisema kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania kutokana na ushirikiano wa kihistoria wa muda mrefu na pia imani ya Tanzania kwa nchi hiyo katika kukuza maendeleo ya wananchi.

Aidha alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi kinara yenye ushirikiano bora wa kiuchumi na kijamii na imeshirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya TAZARA, mradi ambao umekuwa wa kielelezo cha uhusiano huo.


Alisema kuwa msaada wa sekta ya afya kupitia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambao umelenga kunusuru maisha ya watoto wanaougua maradhi ya moyo, pia utakuza ajira na kuwa sehemu ya utalii wa kimatibabu watakaokuja nchini kutoka mataifa mengine.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dkt. Peter Kisenge, aliishukuru China kwa ufadhili huo utakao kuwa mkombozi mkubwa wa matibabu ya moyo kwa watoto kupitia ujenzi wa Kituo hicho cha Umahiri kitakachojengwa katika Hospitali ya Mloganzila.

Alisema kuwa changamoto ya kiafya kwa watoto inayosababishwa na maradhi ya moyo ni kubwa ambapo takwimu zinaonesha kuwa kati ya Watoto 200 wanaozaliwa, Watoto wawili wanazaliwa wakiwa na matatizo ya moyo na kwamba ujenzi wa Kituo hicho cha umahiri utaondoa changamoto ya matibabu.


Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya na Naibu Katibu Mkuu  Wizara ya Afya, Mhe. Ismail Rumatila, ambaye aliahidi kuwa Serikali itasimamia utekelezaji wa mradi huo kama ilivyokusudiwa ili kuleta tija na kuboresha upatikanaji wa huduma na matibabu ya magonjwa ya moyo nchini.

TANZANIA YAUNGA MKONO AZIMIO LA AFYA KWA WOTE NA UBORESHAJI HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA MSINGI KATIKA MKUTANO WA 37 WA JUMUIYA YA MADOLA


Na WAF, Geneva Uswisi.


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeungana na nchi wananchama wa Jumuiya ya Madola kuendelea kuweka msisitizo wa kufikia lengo la Afya kwa wote pamoja na uboreshaji wa huduma za afya ngazi ya msingi.


Hayo yamebainishwa leo Mei 17, 2025 na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wakati akiwasilisha tamko la Tanzania kwenye Mkutano wa 37 wa Jumuiya ya Madola kwenye kikao cha Mawaziri wa Afya kinachofanyika Geneva, Uswisi.


“Tanzania inaendelea kuunga mkono juhudi za Jumuiya ya Madola za kuongoza kasi ya uboreshaji wa huduma za afya kwa wote pamoja na kuendelea kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za afya ngazi ya msingi, tunaamini kwa kuwekeza kwenye mifumo ya utoaji huduma za afya tutaweza kufikia malengo endelevu,” amesema Waziri Mhagama.


Waziri Mhagama amesema ili kufikia malengo hayo ni lazima nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kuungana pamoja kutekeleza vipaumbele vya kuboresha huduma za afya ili kukabiliana na vikwazo vya ugharamiaji huduma za afya.


Amebainisha kuwa tayari Serikali ya Tanzania imepitisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ikiwa ni lengo moja wapo la kufikia afya kwa wote.


“Sheria hii imelenga kuweka mkakati jumuishi na endelevu wa kuendelea kugharamia mifumo ya utoaji wa huduma za afya na kuhakikisha Watanzania bila ya kujali hali zao za kiuchumi wanapata huduma bora za afya bila ya kuwa na kikwazo cha kifedha,” amefafanua Waziri Mhagama.


Katika hatua nyingine, ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Afya Tanzania Bara Mhe. Jenista Mhagama, Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Mazrui wamemnadi mgombea wa Tanzania katika uchaguzi wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani kwa Kanda ya Afrika (Prof. Mohammed Janab) kwa Mawaziri wa Afya na Viongozi kutoka nchi za Bara la Afrika ambao ni wananchama wa Jumuiya ya Madola.

 

KAMPENI YA KITAIFA YA AFYA YA AKILI YAENDELEA KWA KISHINDO JIJINI DODOMA


Majid Abdulkarim, Dodoma


Hospitali Bingwa ya Taifa ya Magonjwa ya Akili ya Mirembe imehimiza umuhimu wa kufanya mazoezi ya mwili na kula mlo kamili kama njia ya msingi ya kulinda na kuimarisha afya ya akili.


Hayo yamesemwa Mei 17, 2025, na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili kutoka hospitali hiyo, Dkt. Enock Chagarawe, kuwa hatua hiyo ni  mwendelezo wa Kampeni ya Kitaifa ya Afya ya Akili inayoendelea jijini Dodoma inayolenga kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu ustawi wa afya ya akili.


Dkt. Chagarawe, amesema afya ya akili ni hali ya kuwa na utimamu wa kiakili na uwezo wa kushirikiana na watu wengine bila kujitenga. 


Amebainisha kuwa matatizo ya afya ya akili huanza kwa mtu kuwa na msongo wa mawazo, hali ya kuwa na mawazo mazito au hofu bila kuwa na dalili za wazi za ugonjwa wa akili.


"Dalili nyingine ni pamoja na mtu kuamini kwamba amerogwa au kwamba watu wanamnyemelea kwa nia mbaya, kusikia sauti ambazo hazipo, kujitenga, kujiona hana thamani na hata kutamani kifo na wengne kuonesha tabia za hasira za mara kwa mara na kuwa wagomvi," ameeleza Dkt  Chagarawe.


Amefafanua kuwa watu wenye ugonjwa wa akili wanapaswa kupata matibabu ya kitaalam katika hospitali na wakati mwingine kulazwa kwa ajili ya uchunguzi na tiba sahihi sambamba na huduma ya ushauri nasaha kutoka kwa wataalam wa saikolojia pia ni muhimu katika mchakato wa matibabu.


Kampeni ya kitaifa ilianza

mkoani Dodoma, na tayari imeshatembelea mikoa ya Singida na Iringa, huku mikoa ya Morogoro na Manyara ikiwa katika ratiba inayofuata. Kaulimbiu ya kampeni inasema:

"Afya ya Akili ni Afya – Jikubali, Jijali."


Kampeni hii ni sehemu ya jitihada za kitaifa za kubadili mtazamo wa jamii kuhusu afya ya akili na kuhamasisha watu kutafuta msaada mapema.

 

NISHATI SAFI YA KUPIKIA NI KIPAUMBELE CHA SERIKALI - MHANDISI MRAMBA



📌 *Ashiriki Marathon ya Kuhamasisha Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia*


📌 *Asema Nishati Safi ya Kupikia itapunguza uharibifu wa mazingira na kulinda afya*


Katibu Mkuu wa Wizara Ya Nishati Mha. Felchesmi Mramba amesema kuwa, suala la upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ni moja ya vipaumbele vya nchi na kwamba Serikali inahakikisha kuwa Mpango Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unatekelezwa kwa kasi na kwa umakini ili kutimiza azma ya nchi kuhama kutoka matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia kwenda kwenye nishati safi.


Amesema hayo tarehe 17 Mei, 2025 jijini Dar es Salam wakati akishiriki Marathon ya Nishati Safi ya Kupikia oiyofanyika katika viwanja wa Oysterbay..


“Serikali imeamua kwenda nalo kasi suala hili la nishati safi ya kupikia ili kuepusha uharibifu wa mazingira kwani nishati ambayo si salama kama kuni na mkaa inatumika kwa kiasi kikubwa kwa kupikia hivyo tukitekeleza Dira hii, kwa kiasi kikubwa tutapunguza uharibifu wa mazingira pamoja na kulinda afya za wananchi.” Amesema Mramba


Mha. Mramba, amewapongeza waandaaji wa Marathon hiyo Shirika la Wafanyabishara Wanawake (TABWA) ambayo imelenga kuhamasisha Nishati Safi ya Kupikia  kwa Wananchi.


Aidha, amewaasa  Wadau mbalimbali kuzidi kujitokeza ila kuzidi kuendeleza mikakati ya kusambaza elimu ya Nishati Safi ya Kupikia kwa Watanzania wengi zaidi.

WAZIRI MKUU ARIDHISHWA NA MABORESHO YANAYOENDELEA KWA MKAPA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Mei 17, 2025 amekagua ukarabati wa uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kukagua maboresho ya viwanja kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya AFCON na CHAN yanayotarajiwa kufanyika nchini hivi karibuni.


Akiwa uwanjani hapo, Mheshimiwa Majaliwa ambaye aliambatana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gerson Msigwa, amesema ameridhishwa na hatua za ukarabati zinazoendelea kiwanjani hapo.

Waziri Mkuu amesema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wakandarasi wanaokarabati uwanja huo ni kuwa upo tayari kwa michezo yoyote hata ya kimataifa na kwamba utakamilika kabla ya kuanza kwa mashindano ya CHAN na AFCON.


Aprili 7, 2025 Mheshimiwa Majaliwa alikagua ukarabati na ujenzi wa Viwanja vya Amani, Maisara na Mao Zedong Zanzibar, ambapo alisema  Watanzania watapata fursa ya kuendeleza michezo na kuhamasisha wachezaji kufanya mazoezi zaidi ili wapate sifa za kucheza michuano hiyo. Kwa upande wa Tanzania Bara alikagua viwanja vya Shule ya Sheria, Gymkhan na Jenerali Isamuhyo.


Alisema uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wa kuridhia michuano hiyo kufanyika nchini utasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza na kukuza sekta ya michezo na utalii nchini.

Aidha Mheshimiwa Majaliwa amesema ameridhishwa na kasi na bora wa ukarabati wa viwanja hivyo na jukumu lililopo kwa sasa ni kuilinda miundombinu hiyo ili ubora uliofikiwa baada ya ukarabati uendelee kuwepo hadi michuano hiyo itakapofanyika.

Listen Mkisi Radio