JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Jumatano, 21 Mei 2025

ULEGA AWATAKA WAKANDARASI DODOMA RING ROAD KUONGEZA KASI

 


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amekagua  na kuridhishwa na utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya jiji la Dodoma (km 112.3) ambapo kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 85 ya utekelezaji wake.


Ulega ameeleza hayo leo Mei 21, 2025 jijini Dodoma wakati alipokagua hatua za maendeleo ya mradi huo ambapo  amewaagiza wataalam wa Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha wanawasimamia Makandarasi wa mradi huo kukamilisha kwa wakati na ubora. 

“Nimekagua na nimeridhishwa na hatua zilizofikiwa katika awamu zote mbili na malengo ya Serikali ni kuwa mradi huu ukamilike kwa wakati na nimeelekeza wataalam kutoka TANROADS hadi kufikia mwezi Juni wawe wamefika asilimia 90”, amesisitiza Ulega.


Kuhusu uboreshaji  wa miundombinu ya barabara katika jiji la Dodoma Waziri Ulega amesema kuwa Serikali inatarajia kujenga barabara ya njia nne na sita kuanzia Chamwino Ikulu hadi katikati ya jiji hilo  ambapo kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za manunuzi za kumpata mkandarasi wa kujenga mradi huo.

Ameongeza kuwa katika eneo la Ihumwa Serikali ina mpango wa kujenga barabara ya kisasa ya njia za kupishana (interchange), ili kuruhusu magari kupita katika mji wa Serikali wa Magufuli na yaendayo mjini bila kuwa na kizuizi chochote.


Vilevile, Waziri Ulega amezungumzia umuhimu wa Taasisi za TANROADS, TRC na TPA kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuwezesha mradi huo wa kimkakati kukamilika kwa wakati.


Aidha , akiwa katika ziara hiyo Ulega pia alifafanua kuhusu ujenzi wa miundombinu ya barabara  za juu (flyovers) katika eneo la Morocco na Mwenge jijini Dar es salaam ambapo amesisitiza kuwa miradi hiyo ipo kwenye mpango mzuri na hatua iliyofikiwa sasa ni kuwa Wizara inaendelea kukamilisha taratibu za kitaalam ili kuendelea na utekelezaji wa miradi hiyo.

“Nitumie fursa hii kuwaambia watanzania kwamba bado Serikali inayo mpango wa kuzijenga Flyover za Mwenge na Morocco na hatua iliyopo wataalam wameniambia wanakamilisha taratibu na wafadhili wa mradi JICA hadi kufikia mwezi Julai fedha za mkopo zitakuwa zishasainiwa ”, amesisitiza Ulega.


Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Aloyce Matei amesema kuwa hadi kufikia mwezi wa saba matarajio yao ni kwamba fedha za mradi wa ujenzi wa barabara za juu za  Morocco na Mwenge zitasainiwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Naye, Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS, Mhandisi Japheson  Nnko amemhakikishia Waziri Ulega kuwa watasimamia Makandarasi hao kuhakikisha mradi wa mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma unakamilika kwa ubora na wakati kama ilivyosainiwa kwenye mkataba.

Amebainisha  kuwa  mradi huo umegawanywa sehemu mbili ambapo Mkandarasi China Civil Engineering  Construction Corporation (CCECC) anayejenga sehemu ya Nala-Veyula-Mtumba-Ihumwa bandari kavu (km 52.3) anatarajiwa kukamilisha ifikapo mwezi Julai, 2025 na Mkandarasi Avic International anayejenga sehemu ya Ihumwa bandari kavu-Matumbulu-Nala (km 60) anatarajiwa kukamilisha ifikapo mwezi Agosti, 2025.

MKOPO WA BILIONI 240 KUJENGA SKULI ZA GHOROFA 23

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa mkopo wa Shilingi Bilioni 240 kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya CRDB kwa ajili ya ujenzi wa skuli 23 za kisasa za ghorofa hapa nchini.


Hafla hiyo imefanyika Ikulu ambapo Benki ya CRDB iliwakilishwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Ndg. Abdulmajid Nsekela na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi – Afisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dkt. Juma Malik Akil.


Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa mkataba huo ni hatua kubwa kwa Zanzibar ambayo kwa mara ya kwanza imefanikiwa kupata mkopo mkubwa kutoka nje ya nchi bila ya kuwa na dhamana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwezeshwa na benki za ndani ya nchi tangu Mapinduzi ya mwaka 1964.

Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa mkopo huo wa Euro milioni 79 (sawa na Shilingi Bilioni 240) utatumika kujenga skuli za kisasa za ghorofa 23 katika maeneo yenye uhitaji mkubwa wa skuli Unguja na Pemba.


Aidha, amebainisha kuwa mkopo huo umewezeshwa kupitia ushirikiano wa Benki ya CRDB na Benki ya Udachi (Deutsche Bank), kwa dhamana ya Bima ya CESCE kutoka Uhispania. Fedha hizo zitatumika pia kununua vifaa vya kisasa vya Maabara, Maktaba, Kompyuta, na Samani.

Amesema kuwa kwa muda mrefu, Serikali ilikuwa na njia mbili pekee za kupata mikopo kwa kupitia dhamana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au kutegemea bajeti za ndani ambazo zote zilichukua muda mrefu na kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Kupitia mpango huu mpya, Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar sasa inaweza kutekeleza miradi mingi ya kimkakati kwa haraka ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo.


Akitaja baadhi ya miradi ya kimkakati itakayotekelezwa ndani ya miaka mitano ijayo, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa itajumuisha ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Uwanja wa Ndege wa Pemba, barabara za Chake Chake–Mkoani, Kisauni–Fumba, Uwanja wa Soka wa kisasa wa michuano ya AFCON 2027, Uwanja wa Ndege wa Pemba, Hospitali za Mikoa, na Kituo cha Umahiri cha Matibabu ya Saratani.

Ameongeza kuwa Serikali inakopa kwa umakini mkubwa na ina akaunti maalum ya kulipa mikopo, ambapo takriban dola milioni 10 hutengwa kila mwezi kwa ajili ya marejesho.


Vile vile, Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Benki ya CRDB pamoja na PDB kwa kusaidia kupata mkopo huo kwa haraka, na ameahidi Serikali kuendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za kifedha za ndani na ametoa wito kwa benki kutochelewesha pale Serikali inapohitaji mikopo ili miradi ya maendeleo itekelezwe kwa wakati.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela, amesema kuwa benki hiyo inajivunia mpango unaofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwashirikisha wadau katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

WAKULIMA ZAIDI YA MILIONI NANE WAMEAHIDI KUMPA KURA RAIS SAMIA- MHE. DITOPILE


 Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dodoma Mhe. Mariam Ditopile, ameliambia Bunge kuwa kutokana na Mapinduzi makubwa ya sekta ya Kilimo pamoja na manufaa yaliyopatikana kwa wakulima ndani ya Miaka minne ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Wakulima zaidi ya Milioni nane wa Tanzania wameahidi kumpa kura za kishindo kama ahsante ya tija kubwa iliyopatikana kwenye sekta hiyo.


Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2025/26, leo Jumatano Mei 21, 2025 Bungeni Jijini Dodoma, Mhe. Mariam  Ditopile amebainisha kuwa mafanikio hayo makubwa yanayoshuhudiwa kwa kipindi kifupi yametokana na utashi binafsi na imani ya Rais Samia kwenye sekta ya Kilimo.


"Wakulima wa nchi hii wanasema wanatambua kuwa tayari CCM imempitisha rasmi Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya Urais kwenye uchaguzi utakaofanyika Oktoba 2025,Kwa Tanzania nzima wapo zaidi ya Milioni 8 na tena wamesajiliwa, wanatambuana na wamejiandikisha kupigakura, Wanamuambia atoe shaka kura zote za wakulima ndani ya nchi hii zitaenda kwake na nia wanayo na sababu za kumuunga mkono wanazo." Amekaririwa Mhe. Ditopile.


Akizungumzia mafanikio ya Miaka minne ya Rais Samia ameeleza kwamba ruzuku zimekuwa zikitolewa kwenye Korosho, pamba na Tumbaku, ambapo kwa Tumbaku pekee jumla ya Bilioni 21 zimetolewa kwa wakulima, suala ambalo limesababisha Tanzania kuwa nafasi ya pili kwa uzalishaji wa tumbaku barani Afrika.


Ameeleza kwamba ni serikali ya Rais Dkt. Samia pia iliyoimarisha na kufufua ushirika nchini ambapo kwa mara ya kwanza pia ndani ya serikali ya Rais Samia, Ushirika umefanikiwa kuwa na Benki yake ya Taifa ya Ushirika iliyo na Makao yake Jijini Dodoma.


Aidha ongezeko la matumizi ya mbolea nchini limeongezeka kutoka tan 363,599 mwaka 2021/22 hadi tani 580, 628 mwaka 2022/23, ongezeko ambalo limetajwa kutokana na serikali kutoa mbolea ya ruzuku, kuimarisha uwezo wa kampuni ya mbolea (TFC) kwa kuipatia mtaji wa jumla ya Shilingi Bilioni 116.


Aidha Mhe. Ditopile pia ameeleza kuwepo kwa ongezeko kubwa la bajeti ya wizara ya kilimo ndani ya miaka minne ya Rais Samia, miradi mikubwa ya umwagiliaji pamoja uanzishwaji wa mashamba makubwa ya kilimo, suala ambalo amesema limesababisha sekta binafsi na sekta ya umma kujadili na kuingia kwa wingi kwenye kilimo nchini.


Ditopile anaungana na Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe ambaye wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara hiyo, mbali ya kuzungumzia mafanikio yaliyopatikana, alieleza kwamba wakulima wa Tanzania ni miongoni mwa wapigakura muhimu na wa uhakika kwa Rais Samia, akieleza kwamba wanafikika kirahisi na wameunganishwa katika mtandao mmoja, wakifikia zaidi ya Milioni nane.

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU TAHADHARI YA MAGONJWA YA MFUMO WA NJIA YA HEWA NA MAGONJWA YANAYOENEZWA NA MBU

 


TAREHE 20 MEI, 2025 

Wizara ya Afya imeendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu na kutoa taarifa za kila siku kuhusu magonjwa ya mlipuko pamoja na tetesi za uwepo wa magonjwa hayo nchini. Katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Aprili 2025, tumeshuhudia ongezeko la tetesi zinazohusiana na magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa katika jamii hapa nchini, hasa katika mkoa wa Dar es Salaam.


 Kwa kutumia mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa, ambayo imekuwepo tangu mwaka 2008, tumekuwa tukifuatilia mwenendo wa magonjwa haya ili kubaini aina za vimelea vinavyosababisha maambukizi, ongezeko la visa, pamoja na uwezekano wa kujitokeza kwa kirusi kipya chenye uwezo wa kusambaa kwa haraka. Vipimo vya maabara vimebaini kuongezeka na kupungua kwa virusi vya influenza hali ambayo imekuwa ikionekana pia katika miaka iliyopita na ndiyo maana hujulikana kama ‘Seasonal influenza”. Aidha vipimo hivyo vimeonesha kuwa hakuna kirusi kipya kinachoweza kusambaa kwa haraka na kusababisha mlipuko wa aina ya Pandemiki.


 Ugonjwa wa UVIKO-19, ambao ulitangazwa kwa mara ya kwanza hapa nchini mwezi Machi 2020, umeendelea kuwepo kwa kiwango cha chini kama yalivyo magonjwa mengine ya mfumo wa njia ya hewa. Tangu Februari hadi Aprili 2025, ufuatiliaji wa virusi hivi umeonesha ongezeko la visa vya UVIKO-19 kutoka asilimia 1.4 (wagonjwa 2 kati ya watu 139 waliopimwa) mwezi Februari hadi asilimia 16.3 (wagonjwa 31 kati ya 190 waliopimwa) mwezi Machi, na kisha asilimia 16.8 (wagonjwa 31 kati ya watu 185 waliopimwa) mwezi Aprili 2025. Hali ya kuongezeka na kupungua kwa ugonjwa huu imekuwepo kila mwaka tangu kutangazwa kwa ugonjwa huu mwaka 2020. Kwa kipindi hiki ongezeko hili linaonekana zaidi katika mkoa wa Dar es Salaam. 


Wizara ya Afya inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa nchini na kutoa taarifa. Kupitia vituo vyake vya kutolea huduma, Wizara imeelekeza wataalam kuhakikisha wanaendelea kufanya utambuzi wamagonjwa haya kwa kutumia vipimo vya maabara na kutoa matibabu stahiki kwa wagonjwa wote wanaobainika kuwa na maambukizi.


Aidha, natoa rai kwa wananchi wote kuzingatia kanuni za afya ili kujikinga na kuwalinda wengine dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa ikiwa ni pamoja na:

 • Kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya, pamoja na kuvaa barakoa pale inapohitajika; 

• Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi mara kwa mara;

 • Kudumisha usafi wa mwili binafsi na wa mazingira yanayotuzunguka.

 Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi, hususan katika mikoa ya pwani mwa Tanzania, kumekuwa na ongezeko la hatari ya kuenea kwa magonjwa yanayoenezwa na mbu, kama vile Homa ya Dengue, Malaria, na magonjwa mengine ya aina hiyo. Ili kujikinga na madhara yatokanayo na magonjwa haya, nawasihi wananchi wote kuchukua tahadhari kwa kuzingatia yafuatayo:

 1. Kuangamiza mazalia ya mbu – kuondoa maji yaliyotuama karibu na makazi, ikiwemo madimbwi, ndoo, chupa, matairi ya zamani, na vifaa vingine vinavyoweza kuhifadhi maji;

 2. Kutumia vyandarua vyenye dawa;

 3. Kupulizia viuatilifu (sprays) ndani ya nyumba mara kwa mara ili kuua mbu waliopo ndani;

 4. Kuvaa nguo ndefu zinazofunika mwili hasa wakati wa jioni na alfajiri;

 5. Kufunga madirisha na milango au kutumia wavu ili kuzuia mbu kuingia ndani ya nyumba.

 Magonjwa haya yanayosababishwa na virusi yana dalili zinazoshabihiana hivyo ni vigumu kuyabaini bila kupata vipimo vya maabara. Hivyo, nawasihi kuwahi katika vituo vya kutolea huduma mara mnapopata dalili zozote za homa, maumivu ya kichwa, macho, misuli, viungo, au vipele mwilini au dalili za magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa kama vile kikohozi, mafua, kuwashwa koo au kupumua kwa shida ili kupata vipimo na matibabu stahiki. 

Serikali kupitia Wizara ya Afya ina uwezo, utaalamu, na mifumo madhubuti ya kufuatilia, kutambua, na kudhibiti magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa pamoja na magonjwa mengine ya mlipuko. Tutaendelea kutoa taarifa sahihi kwa wakati kwa lengo la kuwalinda na kuhakikisha usalama wa afya za Watanzania wote.

 Mwisho, nawasihi tuendelee kushirikiana kwa karibu, tufuate maelekezo ya wataalam wa afya, na tuendelee kuilinda jamii yetu dhidi ya magonjwa yanayoambukiza.

Imetolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace E. Magembe

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiongoza moja ya vikao vya kikosi kazi


 Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiongoza moja ya vikao vya kikosi ambacho hatimaye kilitimiza azma yake mnamo Jumapili, Mei 18, 2025, kwa ushindi wa kishindo wa mgombea wa Tanzania Profesa Mohamed Yakub Janabi, alipopata kura 32 kati ya 47 zilizopigwa kwa siri na wajumbe wa nchi wanachama wa WHO Afrika, kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa WHO.


Dkt. Kikwete amepongezwa kwa kutumia umahiri na uhusiano wake wa kidiplomasia kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa, mchango ambao umetajwa kama kichocheo muhimu kilichowezesha Tanzania kupata ushindi dhidi ya wagombea kutoka CΓ΄te d’Ivoire, Guinea na Togo.


Uchaguzi huo umefanyika kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa Mkurugenzi mteule, Dkt. Faustine Ndugulile, mnamo Novemba 2024. Nafasi hiyo ilivuta wagombea mahiri kutoka mataifa kadhaa, lakini Profesa Janabi alifanikiwa kuungwa mkono kwa wingi, akionesha kuwa jina la Tanzania bado lina nguvu katika diplomasia ya afya barani Afrika.


Kwa mujibu wa taratibu za Shirika la Afya Duniani, jina la Profesa Janabi sasa litawasilishwa kwa ajili ya kuthibitishwa rasmi na Bodi ya Utendaji ya WHO katika kikao chake cha 157 kitakachofanyika Mei 28–29, 2025, mjini Geneva, Uswisi.

WAZIRI MAVUNDE AONGOZA KIKAO CHA KIMKAKATI WA KIUCHUMI WA NCHI KUPITIA SHIRIKA LA MADINI LA TAIFA (STAMICO)


▪️Lengo ni kuiwezesha Taifa Kushiriki kikamilifu katika uvunaji Rasilimali Madimi kupitia uwekezaji Mkubwa wa STAMICO 


▪️STAMICO kuweka nguvu kubwa katika madini mkakati na adimu


▪️Mapato ya Shirika yatarajiwa kuongezeka kwa asilimia zaidi ya 500 ifikapo mwaka 2029


▪️Yaja na kauli mbiu mpya ya π™ˆπ˜Όπ™Žπ™π˜Όπ™Žπ™ƒπ˜Ό(π™ˆπ™–π™ π™š π™Žπ™π˜Όπ™ˆπ™„π˜Ύπ™Š π™Žπ™π™žπ™£π™š π˜Όπ™œπ™–π™žπ™£)


Dodoma


Shirika  la  Madini la Taifa  (STAMICO) limekaa Mguu Sawa kuhamia kwenye Uwekezaji Mkubwa wa  Madini Muhimu na Madini Mkakati huku tayari likiwa na mafanikio kadhaa ikiwemo kuachana na utegemezi kwa Serikali kwa asilimia 100 na likiwa limekwisha toa gawio kwa Serikali  ya kiasi cha shilingi bilioni 9.


Mbali na hayo, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Shirika hilo linakua kubwa kama ilivyo malengo ya kuanzishwa kwake ya kuwekeza kwa niaba ya Serikali ambapo miongoni mwa majukumu yake ni pamoja na kuwekeza  kwenye miradi ya kimkakati ya utafutaji na uchimbaji madini  ili kuongeza manufaa zaidi kwa taifa.


Hayo  yamebainishwa Mei 19, 2025 zikiwa zimepita siku kadhaa tangu Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lipitishe Bajeti ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2025/26 ambapo miongoni mwa yaliyopangwa kutekelezwa mwaka ujao ni pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na kuendeleza mnyororo wa thamani katika madini muhimu na mkakati.


Kikao hicho ni cha pili baada ya kikao cha kwanza kilichofanyika Mei 12, 2025 jijini Dodoma ambavyo vyote vimeongozwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde vikihusisha Menejimenti ya Wizara na Taasisi zake ili kujadili kwa pamoja andiko la kuiwezesha STAMICO) kuwekeza katika uchimbaji mkubwa wa madini nchini.


Awali, STAMICO liliwekwa kwenye orodha ya mashirika yanayopaswa kufutwa na Serikali  na miaka ya karibuni, kupitia Falsafa ya 4 Rs za Mhe. Rais wa Awamu ya sita Dr. Samia Suluhu Hassan Shirika lineweza kuishi mageuzi jayo kwa vitendo na kuweza kujipambanua  kuwa miongozi mwa mashirika ya mfano yanayofanya vizuri na sasa  limejikita kuwekeza katika shughuli za uchimbaji mkubwa na wa Kati wa madini muhimu na mkakati pamoja na dhahabu katika zama hizi  ambazo mataifa mengi duniani yanapambana  kuhakikisha yananufaika na rasilimali madini zilizopo kwenye nchi zao.


Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Mavunde amesema miradi inayotarajiwa kufanywa na STAMICO italirejesha tena shirika hilo kwenye ramani ya dunia na kusisitiza kwamba, matamanio yake ni kuliona  shirika  hilo linakua  kubwa kama ilivyo kwa Kampuni kubwa kama  Barrick Gold Mine na AngloGold Ashanti  ili liweze kuongeza manufaa zaidi kwa  nchi kupitia rasilimali madini zinazopatikana nchini.


‘’ Ninawapongeza STAMICO kwa hatua kubwa mliyopiga hadi mlipo sasa. Miradi hii pindi itakapotekelezwa, kama taifa tutakwenda kunufaika ipasavyo na kusema, ‘’tukipata nafasi ya kuifanya kazi wenyewe, manufaa yake ni makubwa.


Shirika hili ni muhimu sana katika kuisaidia nchi yetu kunufaika na rasilimali madini,tutatumia maarifa na ujuzi wote kuhakikisha STAMICO inakuwa moja kati ya mashirika makubwa ya umma katika kushiriki kikamilifu kwenye sekta ya madini barani Afrika kwa kuja na kauli mbiu ya  MASTASHA (π™ˆπ™–π™ π™š π™Žπ™π˜Όπ™ˆπ™„π˜Ύπ™Š π™Žπ™π™žπ™£π™š π˜Όπ™œπ™–π™žπ™£)kulirudishia ari,nguvu na malengo iliyokuwa nayo wakati  wa uanzishwaji wake’’ amesema Waziri Mavunde.


Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amekielekeza kikao hicho kuhusu mipango kabambe iliyopangwa kutekelezwa na shirika hilo, pamoja na kueleza manufaa ya miradi hiyo ikiwemo kutoa ajira za moja kwa moja, mapato kwa serikali, kuongeza ushindani na  uwekezaji kutoka nje  kwa lenfo la kuongeza tija na kuchochea maendeleo ya teknolojia.


Dkt. Mwase ameongeza kwamba, miongoni mwa miradi itakayotekelezwa, ipo ambayo itatekelezwa na shirika lenyewe na ile itakayotekelezwa kwa ubia na kuongeza kwamba tayari STAMICO inazo leseni zake  nyingine za uchimbaji zikihusisha madini ya dhahabu na kinywe.


STAMICO lilianzishwa Mwaka 1972 kwa lengo la kuwekeza kwa niaba ya Serikali katika mnyororo mzima wa thamani wa madini.


*#π™ˆπ™–π™ π™šπ™Žπ™π˜Όπ™ˆπ™„π˜Ύπ™Šπ™Žπ™π™žπ™£π™šπ˜Όπ™œπ™–π™žπ™£#

Mhe. Thabo Mbeki Ashiriki Mjadala Kujadili Uendelezaji Uchumi wa Buluu na Utalii Afrika

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mheshimiwa Thabo Mbeki ameshiriki mjadala wa kuendeleza uchumi wa buluu na utalii Afrika uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuendeshwa na kauli mbiu ya “Kuinua Uchumi wa Bluu na Utalii kwa Ajili ya bara la  Afrika”.


Majadiliano hayo yalilenga kusisitiza umuhimu wa usimamizi endelevu wa bahari, maziwa, na mito pamoja na kukuza utalii wa kikanda na kimataifa kama nyenzo za kuimarisha uchumi, ajira, na utambulisho wa Kiafrika.

Akizungumza katika mjadala huo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa amesema Afrika iko katika kipindi nyeti  ambacho kinahitaji vitendo thabiti, dhamira isiyotetereka, na suluhisho bunifu na zinapaswa kuelekeza nguvu katika maeneo muhimu. “Hatua si chaguo tena, bali ni lazima zichukuliwe ili kudhibiti maendeleo holela ya maeneo ya pwani.” alisema.


“Ninaamini kuwa majadiliano haya yatachangia katika kuendeleza malengo ya kimkakati ya Afrika ya kuunda, kushirikiana, na kusambaza maarifa. Ninafahamu kuwa tuna timu za utafiti kutoka vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za tafiti barani Afrika zinazoshughulika na masuala yanayohusiana na bahari na mazingira ya majini. Katika mkutano huu, watawasilisha mafanikio yaliyopatikana kupitia ushirikiano wao na wenzao kutoka sehemu mbalimbali za Afrika,” alisema.


Aliwasihi washiriki wakumbuke umuhimu wa ushirikiano na kwamba hakuna taifa moja linaloweza kukabiliana na changamoto peke yake na kuongeza kuwa dhamira ya pamoja ya kushirikiana, tukitumia maarifa na uzoefu wetu wa pamoja, ndiyo itakayokuwa msingi wa mafanikio ya mkakati huu na kusisistiza umoja, ubunifu, na kutambua kwamba Waafrika wote ni walezi wa rasilimali muhimu za majini kwa uhai wa viumbe vyote.

Mhe. Thabo Mbeki yuko nchini kwa ajili ya kushiriki programu mbalimbali zilizoandaliwa na Taasisi yake kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Afrika itakayofanyika tarehe 25 Mei 2025 ambapo Mhadhara wa 15 wa Mbeki Foundation utafanyika nchini tarehe 24 Mei 2025 jijini Dar es Salaam na utawakutanisha wana majumui mbalimbali kutoka barani Afrika .

Jumanne, 20 Mei 2025

Tanzania na Namibia Fursa za mpya kufunguliwa

Karibu Tanzania, Karibu Nyumbani. 


Ikulu jijini Dar es Salaam leo nimempokea Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mheshimiwa Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah. Kama ilivyokuwa enzi za waasisi wa mataifa yetu, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Sam Nujoma, tunaendelea kuimarisha udugu na ushirikiano ambao ulianza tangu kipindi cha kupigania uhuru, ambapo baada ya kupata uhuru wa kisiasa, sasa tunajikita katika kuimarisha uchumi na ustawi wa nchi zetu.


Katika mazungumzo yetu tumeazimia kukuza uhusiano uliopo, na kufungua fursa mpya za ushirikiano kupitia sekta mbalimbali zikiwemo biashara na uwekezaji, mifugo na uvuvi, uchumi wa buluu, utalii na lugha ya Kiswahili, kwa manufaa ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Dkt. Netumbo ni dada kwangu. Nimefarijika kumkaribisha tena nchini Tanzania, mahali alipoishi kuanzia mwaka 1980 hadi 1986 akiwa nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi nchini Namibia.

 

Listen Mkisi Radio