JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Jumatano, 12 Machi 2025

Dr. Godwin Mollel amefanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya.

 

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya, Bi. Christine Grau, kujadili njia za kuboresha sekta ya afya nchini, huku wakisisitiza umuhimu wa teknolojia katika kuimarisha huduma na kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga.


Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili mchango mkubwa wa maabara tembezi (mobile laboratories) katika kugundua na kudhibiti magonjwa ya mlipuko, hasa katika maeneo ya mipakani na nchi jirani kama Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zambia, na nyinginezo. Maabara hizi zitarahisisha uchunguzi wa haraka, hivyo kusaidia kuchukua hatua za mapema kuzuia kusambaa kwa magonjwa hatari.


Aidha, wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa kupitia mashirika kama Red Cross na CDC, ambayo hutoa msaada wa kiufundi katika kuimarisha mifumo ya afya. Viongozi hao wamekubaliana kwamba uwekezaji zaidi katika teknolojia na miundombinu ya afya ni muhimu ili kufanikisha lengo la Huduma ya Afya kwa Wote (UHC).


Dkt. Mollel ameishukuru Umoja wa Ulaya kwa msaada wao endelevu, akibainisha kuwa ushirikiano huu utasaidia Tanzania kukabiliana na changamoto za kiafya kwa ufanisi zaidi. 


Bi. Grau ameahidi kuwa Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na salama, hasa katika maeneo yenye changamoto kubwa za kiafya.

DKT. BITEKO AWASILI BARBADOS KUNADI NISHATI SAFI KIMATAIFA

..............

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewasili nchini Barbados kushiriki Mkutano wa Kimataifa kuhusu matumizi ya Nishati endelevu utakaofanyika katika jiji la Bridgetown kuanzia tarehe 12 hadi 14 Machi, 2025.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Grantley Adams nchini humo, Dkt. Biteko amepokelewa na Waziri wa Nishati wa Nchi hiyo Mhe. Lisa Cummins pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Cuba na mwakilishi katika eneo la Caribean, Mhe. Humphrey Polepole

Aidha, Dkt. Biteko atashiriki katika majadiliano mbalimbali kuhusu matumizi ya Nishati endelevu kimataifa ikiwemo Nishati safi ya kupikia ambayo ni ajenda muhimu kwa ajili ya kuwakomboa wananchi dhidi ya matumizi ya nishati isiyokuwa safi.

Dkt. Biteko ameongozana na Mshauri wa Rais masuala ya Wanawake, Mhe. Angellah Kairuki, Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Mhe. Shaib Hassan Kaduara na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha. Felichesmi Mramba.


UWANJA WA MKAPA WAFUNGIWA

..............

Shirikisho la mpira wa miguu Afrika ( CAF) wamefungia uwanja wa Benjamin Mkapa kutokana na kukosa ubora eneo la kuchezea ( Pitch ) huku wakieleza kuwa yanahitajika maboresho yafanywe haraka ili kuepusha uwanja huo kufungwa kwa muda mrefu.

Klabu ya Simba Sc ambayo ilipanga kucheza mchezo wake wa robo fainali kombe la Shirikisho dhidi ya Al Masri April 9 mwaka huu hivyo kuepuka usumbufu Shirikisho la mpira wa miguu TFF limetakiwa kutuma jina la uwanja mbadala utakaotumiwa na klabu ya Simba kufikia Machi 14 .

CAF imepanga kufanya ukaguzi wa uwanja wa Benjamin Mkapa ifikapo machi 20 ili kuona kama maboresho yamefanyika ili kuona kama unafaa kutumika au uendelee kufungiwa.

Mbali na mashindano hayo uwanja Benjamin Mkapa pia umepangwa kutumika kwenye mashindano ya fainali za CHAN yatakayofanyika Agosti 2025.


Jumanne, 11 Machi 2025

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAJIIMARISHA KIUTENDAJI

 


*********

Na Sixmund Begashe - Dodoma

Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kujiimarisha katika Ufuatiliaji na Tathmini ya utendaji wa shughuli mbalimbali za Serikali zinazofanywa kupitia idara, vitengo na taasisi zake ili kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yake.

Akifungua kikao kazi cha wataalam wa Ufuatiliaji na Tathmini wakiwemo M&E Champions kutoka idara, vitengo na taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii, Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikali, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bi. Sakina Mwinyimkuu amewataka washiriki kujiimarisha zaidi kielimu katika suala zima la Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) ili kupata uelewa mpana maana kazi yao ni muhimu katika kuchochea ufanisi na mafanikio makubwa kazini.

Bi. Mwinyimkuu ameipongeza Wizara hiyo kwa kuandaa mafunzo hayo yenye lengo la kutoka na nyaraka muhimu zitakazo imarisha zaidi Upimaji na Ufuatiliaji wa utekelezaji wa kazi za Wizara.

"Ninyi ndio chachu ya Mabadiliko ya utendaji mzuri kwenye Taasisi zenu, hakikisheni mnafuatilia na kutathmini mipango kazi iliyopo, elimisheni watendaji ili watekeleze kazi zao kulingana na wakati uliopangwa na kwa tija iliyokusudiwa". Bi. Mwinyimkuu.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Bure Nassibu, amesema Wizara hiyo imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha wataalam wake wanapata mafunzo ya mara kwa mara ili kuwapatia uwezo wa Kufuatilia, Kutathmini na kuandaa Taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Taasisi na Idara zao.

Mafunzo hayo yanayowezeshwa na wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, yatafanyika kwa siku 12 huku wataalam hao wakitarajiwa kutoka na nyaraka muhimu za kuimarisha Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara.

WANANCHI MKOA WA MARA WATAKIWA KUTUMIA KWA USAHIHI MIKOPO

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bw. Gerald Kusaya, akizungumza kuhusu changamoto za mikopo umiza wakati alipokutana na Timu ya Wataalam ya Wizara ya Fedha ambao walifika ofisini kujitambulisha kwa lengo la zoezi la kutoa elimu ya fedha katika mkoani huo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Bw. Gerald Kusaya, akiagana na Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bw. Salim Khalfan Kimaro, baada ya Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kufika ofisini kwake kujitambulisha kwa lengo la kuanza kutoa elimu ya fedha mkoani humo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Bw. Gerald Kusaya, akiagana na Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bw. Stanley Kibakaya, baada ya Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kufika ofisini kwake kujitambulisha kwa lengo la kuanza kutoa elimu ya fedha mkoani humo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bw. Gerald Kusaya, akieleza kuhusu tatizo la mikopo umiza kwa wananchi wa mkoa wa Mara, kushoto ni Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro  na kulia ni Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha Mkoa wa Mara Bw. Gamba, wakati Timu ya Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha ilipofika ofisini hapo kujitambulisha.
Baadhi ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake wakiwa ofisini kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Bw. Gerald Kusaya, ambao walifika kujitambulisha kwa lengo la kuanza kutoa elimu ya fedha mkoani humo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bw. Gerald Kus6aya, (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, Taasisi na Waratibu wa Elimu ya Fedha ngazi ya Mkoa baada ya kumaliza kujitambulisha kabla ya kwenda kuanza kutoa elimu hiyo kwa wananchi.
 
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Mara)

.............................
Na. Josephine Majura na Peter Haule , WF, Mara

Katibu Tawala Mkoa wa Mara Gerald Kusaya amewataka wananchi wa mkoa huo kutumia mikopo inayotolewa na Serikali kwa manufaa na kuirejesha kwa wakati ili iweze kuwanufaisha wengine wenye uhitaji.
 
Rai hiyo imetolewa Mkoani Mara, alipokutana na kufanya mazungumzo na Timu ya Wataalamu ya Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha ambayo imewasili mkoani hapo kwa ajili ya kutoa elimu katika baadhi ya vijiji vya Wilaya za Mkoa huo.
 
Alisema kuwa uelimishaji umma kuhusu masuala ya huduma za fedha ni jambo la msingi kwa kuwa linatoa fursa kwa wananchi kuweza kufahamu ni namna gani wanaweza kunufaika na mikopo wanayoipata kutoka Serikalini na Taasisi nyingine zinazotoa huduma za Fedha.
 
“Uzoefu unaonesha kuwa wakati mwingine mwananchi anakuwa na shida lakini pale anapodhani anapata fedha za kujikwamua anajikuta amejiingiza kwenye shimo lingine na kuzalisha matatizo makubwa kwake binafsi, familia na jamii inayomzunguka kwa kukosa uelewa”, alieleza Bw. Kusaya.
 
Bw. Kusaya alisema kuwa Serikali imekuwa na mpango mahususi wa kutoa mikopo kwenye vikundi kupitia Halmashauri, lakini utafiti unaonesha kuwa pamoja na jitihada za Serikali kuna watu hawajanufaika na mikopo hiyo kutokana na uelewa mdogo wa masuala ya mikopo.
 
Aliwataka wananchi wa mkoa huo kutambua kuwa mikopo inayotolewa na Serikali haitolewi kwa maana ya zawadi bali inatolewa kwa kusudi la kumwinua mwananchi kwa suala la kipato na inatakiwa irudishwe ili wengine waweze kunufaika pia.
 
Kwa upande mwingine Bw. Kusaya alishangazwa na tabia za wananchi kukopa kwenye taasisi za “mikononi” ambazo hazina ofisi, ambazo ni dhahiri kuwa ufuatiliaji wa marejesho hauwezi kuwa na ustaarabu, alisema taasisi ya ukopeshaji ni lazima iwe na ofisi, anuani na usajili.
 
Alitoa rai kwa wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wakiwemo wa Halmashauri za Wilaya na Mkoa wakiwa na wasiwasi kuhusu taasisi za ukopeshaji kwa kuwa viongozi hao wapo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na milango ipo wazi.
 
Bw. Kusaya aliwataka wananchi wa mkoa wa Mara, kuhudhuria kwenye mafunzo ya elimu ya fedha katika kipindi ambacho timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha itakuwa Mkoani humo kwa kuwa mafunzo yatatolewa bila gharama.
 
Alisema utoaji wa elimu ya fedha hususani kwa Mkoa wa Mara ni faraja kwa kuwa wananchi wanaweza kuelimishwa zaidi kuhusiana na matumizi mazuri ya fedha na kujinasua mikononi mwa matapeli wanaotoa mikopo inayotambulika kama kausha damu.
 
Awali Kiongozi wa Timu ya wataalamu wa utoaji wa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha Bw. Salim Kimaro, alisema kuwa, watu wengi wanakabiliwa na matatizo yanayohusiana na masuala ya fedha yanayowasababishia hasara kubwa kutokana na kukosa elimu ya fedha.
 
Alisema Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha nchini, wametakiwa kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2025/2026 asilimia 85 ya wananchi iwe imefikiwa na elimu hiyo.
 
Alisema Serikali imeandaa Programu ya Kutoa Elimu ya Fedha kwa Umma ya Mwaka 2021/22-2025/26 ikiwa ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/21 hadi 2029/30. 
 
Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika Sekta ya Fedha imeandaa Nyenzo ya Kufundishia Elimu ya Fedha ambayo imeainisha maeneo muhimu ya kuzingatia wakati wa utoaji wa elimu ya fedha kwa umma ikiwa ni pamoja na usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji wa akiba, mikopo, uwekezaji, bima, bima ya amana, kodi na kujipanga kwa Maisha ya uzeeni.
 
Mwisho.

RAIS SAMIA ATEMBELEA MABANDA YA MAONESHO MKUTANO MKUU WA (ALAT)

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt,Samia Suluhu Hassan akitembelea Maonyesho ya Mabanda mbalimbali wakati wa Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) uliofanyika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center Dodoma leo Machi 11,2025.  

TANZANIA KUENDELEA KUJENGA MAJENGO YA BALOZI ZAKE NJE YA NCHI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Miradi na Majengo wa Wizara, Balozi Said Shaibu Mussa amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kujenga na kukarabati majengo ya Balozi zake ili kupunguza gharama za kukodi na kupanga majengo nje ya nchi.

Balozi Mussa ameyasema hayo jijini Harare tarehe 10 Machi, 2025 alipotembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Zimbabwe na kukagua majengo Nane yanayomilikiwa na Ubalozi huo ikiwemo Jengo la Ofisi za Ubalozi na nyumba za Watumishi.

Balozi Mussa ambaye alipokelewa ubalozini hapo na Balozi wa Tanzania Zimbabwe, Inspekta Jenerali wa Polisi Mstaafu, Mhe. Simon Sirro amesema azma ya Serikali ni kuendelea kujenga majengo ya Balozi na vitega uchumi katika nchi mbalimbali ambazo tayari Tanzania inayo maeneo ili kuondokana na gharama kubwa za kukodi.

Amesema tayari Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo mifuko ya Jamii kama NSSF na PSSSF inatelekeza miradi mikubwa ya ujenzi wa majengo ya Balozi na vitega uchumi kama wa Nairobi, Kenya na Ukumbi wa kisasa wa mikutano wa kimataifa wa Kilimanjaro utakaojengwa jijini Arusha.

Akiwa Ubalozini hapo, Balozi Mussa amesema anaona fahari na kufarijika kuona Ubalozi unamiliki majengo nane ambayo miongoni mwake jengo moja linatumika kama kitega uchumi.

“Nafarijika kuona majengo haya yote ni ya kwetu, hakuna ambalo tumekodi, hii ni faraja kubwa kwani inatusaidia kama Wizara kupunguza gharama za kutumia fedha nyingi katika kukodi majengo. Tunataka zaidi tupate mapato kutokana na vitega uchumi lakini vilevile kutokana na uwepo wa majengo yetu” alisema Balozi Mussa.

Balozi Mussa pia alitumia nafasi hiyo, kutoa rai kwa watumishi wa Ubalozi huo kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana kwa hali na mali ili kuwezesha malengo ya Serikali kwenye Ubalozi huo kutimia.

“Balozi Sirro anaondoka nyie mtakuwepo, nyinyi ndiyo mtamsaidia Balozi ajaye kutekeleza majukumu yake kikamilifu, Afande Kaganda ni mama hodari wa kazi kwa hiyo mumpatie ushirikiano na mumsaidie” alisisitiza Balozi Mussa.

Pia alipongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Ubalozi katika kutekeleza diplomasia ya uchumi na kuwataka kuendelea kuishauri Serikali kuhusu namna ya kunufaika na fursa na ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo baina ya Tanzanja na Zimbabwe.

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Sirro ambaye anamaliza muda wake wa utumishi kituoni hapo, amemshukuru Balozi Mussa kwa kutenga muda wake na kuutembelea Ubalozi huo ambapo kwa niaba ya Watumishi, ameahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa.

Kadhalika, alieleza kuwa hali ya ushirikiano baina ya Tanzania na Zimbabwe ni nzuri ambapo nchi hizi zinaendelea kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji na masuala yanayohusu Kanda ya Kusini mwa Afrika.

Balozi Mussa yupo nchini Zimbabwe kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika utakaofanyika nchini hapa kuanzia tarehe 12 hadi 14 Machi 2025. Mkutano huo ulitanguliwa na vikao vya Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu ambapo Balozi Mussa aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye vikao hivyo.  

MAMA MARIAM MWINYI ATOA MSAADA WA FUTARI KWA WAZEE NA WATOTO YATIMA


......................

NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Anna Atanas Paul, akimkabidhi Hamid Khatib Hamid boksi la tende wakati wa Ugawaji wa futari Kwa watoto Yatima wenye mahitaji maalum wanaolelewa Katika kituo cha 'Zanzibar Aids association and support of orphans Mambosasa, kwaniaba ya Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindunzi, mama Mariam Mwinyi. ( PICHA NA FAUZIA MUSSA).

Na Ali Issa Maelezo

Mwenyekiti wa Maisha Bora Foundation Mama Mariam Mwinyi ametembelea na kutoa Msaada wa futari mbali mbali katika nyumba za Wazee wa Seblen na kituo cha kulelea watoto yatima Fuoni Mambo sasa.

Akikabidhi msaada huo kwa niaba Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Anna Athanas Poul katika vituo hivyo amesema ni kawaida ikifika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwatembelea wazee na watu wenye uhitaji maalum kuwasalimia na kuwapatia futari kwa ajili kujikimu.

Amesema wazee wanahitaji kutunzwa na kulelewa  na kupatiwa mazingira mazuri kwa kuzingatia hali zao na mahitaji muhimu pamoja na kupewa chakula kizuri ili kuongeza faraja katika funga zao.

Ameeleza kuwa taasisi ya Mama Mariamu itandelea kuisadia jamii na kuwajali watu wenye mahitaji hasa katika kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ili wapate fadhila na matumaini mazuri katika kutekeleza ibada ya funga.

 Nae Mkurugenzi wa kituo cha kulelea watoto yatima Fuoni Mambo sasa Aboud Maulid Haji akipokea Msaada huo alimshukuru Mama Mariam Mwinyi kwa jitihada zake anazochukua kwa kuwatambua watoto wenye mahitaji malumu akiwa kama ni mlezi wao kwa kuwapatia msaada wa chakula cha Futari katika kipindi hiki cha Mwezi mtukufu wa Ramadhani.

“Watoto wangu ni wenye mahitaji maalum lakini wote wanafunga kwa kushindana kuazia miaka sita na kuendelea hivyo sadaka tuliyoipata itatusaidia sana katika kipindi hiki cha Ramadhani”, alisema Mkurugenzi huyo

Aidha alipongeza jitihada zinazofanywa Dkt. Mwinyi na Mama Mariamu kuimarika na kusaidia wananchi mbalimbali jambo ambalo linapaswa kushukuriwa na kuigwa na watu wengine kutoa sadaka zao katika kipindi hiki cha Ramadhani.

Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa jamii kuwa na utamaduni wa kuvitembelea vituo vya kulelea watoto yatima kwani kufanya hivyo kunatengeneza furaha mapenzi kwa watoto.

Amesema kituo chake kina watoto 48 wanaume 26 na 22 wakike ni watoto wenye uhitaji maalum ambao msaada huo utawasaidia kwa ajili ya kujikimu na kujiendeleza kimaisha

Msaada uliotolewa ni pamoja na unga wa ngano, sukari, tende, mafuta ya kupikia  na mchele ambavyo vitasaidia futari katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Listen Mkisi Radio