Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Finland zimeazimia kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kupitia sekta za kimkakati kama vile nishati, biashara na uwekezaji, ili kukuza diplomasia ya uchumi.
Azma hiyo imefikiwa katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika Ofisi Ndogo ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam, kikihusisha viongozi waandamizi kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Naibu Waziri wa Biashara za Kimataifa wa Finland, Mhe. Jarno Syrjälä.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, amesema Tanzania inaendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kushirikiana na mataifa rafiki kama Finland, kwa lengo la kufungua fursa zaidi za maendeleo. Amesisitiza kuwa ushirikiano huo una mchango mkubwa katika kuleta teknolojia, mitaji, na ujuzi unaoweza kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Mhe. Syrjälä amepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia wawekezaji wa kimataifa. Amesema Finland iko tayari kushirikiana na Tanzania katika maeneo yenye maslahi kwa pande zote, hususan nishati jadidifu, teknolojia ya kisasa na elimu ya ufundi stadi.
Katika kikao hicho, ujumbe wa Tanzania uliwasilisha vipaumbele vya Serikali katika kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda, kilimo, nishati na utalii. Pia, ujumbe huo umetoa wito kwa wawekezaji kutoka Finland kutumia fursa zilizopo kuwekeza nchini.
Ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho ulijumuisha viongozi na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
0 comments:
Chapisha Maoni