JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Ijumaa, 30 Mei 2025

JICA YAAHIDI KUENDELEA KUISHIKA MKONO SERIKALI YA TANZANIA-MAJALIWA


JICA YAAHIDI KUENDELEA KUISHIKA MKONO SERIKALI YA TANZANIA-MAJALIWA


_▪️JICA, Benki ya Dunia na AFDB watoa Dola za Marekani mil 516 miradi ya kilimo_


_▪️Washauri elekezi wawili Mjapan na Mtanzaniia wawekwa TIC kurahisha uwekezaji_

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) limeihakikishia Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa itaendelea kushirikiana nayo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.


Hatua hiyo imetokana na namna ambavyo Serikali imekuwa ikisimamia kikamilifu matumizi ya fedha mbalimbali zinazotolewa na wadau wa maendeleo likiwemo shirika hilo. Waziri Mkuu amesema “Serikali itaendelea itaendelea kusimamia ipasavyo fedha zote za maendeleo zinazoletwa nchini na kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.”


Ameyasema hayo juzi (Jumatano, Mei 28, 2025) alipokutana na Makamu wa Rais wa JICA, Miyazaki Katsura kwenye ukumbi wa Mikutano wa Tachibana uliopo katika hotel ya New Otani, Tokyo nchini Japan akiwa katika ziara yake ya kikazi.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa JICA kuendelea kutafuta wadau zaidi wa maendeleo kwa ajili upatikanaji wa fedha zitakazowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwafanya Watanzania kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.


Amesema lengo la wito huo ni kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa wanafungua milango ya kiuchumi ili wananchi wengi washiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo na kujiongezea kipato.


“Lengo la kutafuta wadau hawa ni kuwawezesha wananchi washiriki kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi, wanaotaka kuingia kwenye biashara, wanaotaka kuingia kwenye kilimo, sekta ya madini, sekta ya uvuvi na ufugaji haya ni maeneo ambayo tumeyawekea umuhimu.”


Waziri Mkuu amesema Serikali inataka kuona wananchi wanaendesha shughuli za kibiashara kukiwa na huduma zote katika mazingira rahisi, ikilinganishwa pia na utekelezaji wa miradi ya elimu, afya, miundombinu, nishati, ujenzi wa barabara pamoja na kilimo ni maeneo yanayotiliwa mkazo.


Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa JICA, Miyazaki Katsura alisema shirika lao linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali nchini kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo Benki ya Dunia katika mradi wa Ustahimilivu wa Chakula.


Makamu huyo wa Rais wa JICA alisema kuwa shirika lao litaendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini ikiwemo ya kuimarisha sekta ya miundombinu na usafirishaji.


Naye, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde ametumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa JICA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 516 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kilimo.


Mheshimiwa Silinde ametaja miradi hiyo kuwa ni Mradi wa Ustahimilivu wa Chakula (TSRP) unaogharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 371 ambazo kati yake Benki ya Dunia imetoa Dola milioni 300.05 na JICA imetoa Dola milioni 71.09, ambapo utekelezaji wa mradi huo unafanyika kwa miaka mitano kuanzia 2025 hadi 2030.


Amesema mradi mwingine ni wa Tanzania Agricultural Inputs Support Project (TAISP) unaotekelezwa kwa ubia kati ya Benki ya Maendeleo Afrika na JICA unaohusika na utoaji wa ruzuku katika pembejeo za kilimo.


Waziri Shilinde amesema mradi huo unaotarajiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 145, ambapo kati ya fedha hizo, JICA wanatoa dola milioni 70 na AfDB dola milioni 75.49 na ulianza kutekelezwa mwaka 2024 na utakamilika 2028. Tayari dola milioni 40 zimelipwa kwa kampuni 17 kwa ajili ya usambazaji wa mbolea.


Waziri Silinde amesema fedha hizo zimetolewa baada ya wadau hao kuridhishwa na namna ambavyo Serikali inasimamia sekta ya kilimo kwa mafanikio makubwa. Hata hivyo amewaomba wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan waje kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji hususan kwenye teknolojia ya umwagiliaji.


Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar, Ali Mohamed Ameir amesema katika vikao hivyo amewahakikishia wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan uwepo wa mazingira wezeshi ya kutekeleza majukumu yao Zanzibar ikiwemo hali ya amani na utulivu.


Pia, Mheshimiwa Ameir ametumia fursa hiyo kuiomba JICA kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kukamilisha miradi miwili ya ujenzi ikiwemo upanuzi wa soko na jiko la samaki katika eneo la Malindi hususani kutoa vifaa kwa wafanyabiashara pamoja na mradi wa usambazaji maji mijini katika Mkoa wa Mjini Magharibi. Miradi yote inatekelezwa kwa awamu ya pili.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri ameishukuru Serikali ya Japan kupitia JICA kwa kugharamia washauri elekezi wawili ambao watakuwa kiungo kati ya wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan na Tanzania.


Amesema washauri hao elekezi ambao watakuwepo TIC mmoja ni Mtanzania na mwingine Mjapani watakuwa na majukumu ya kutoa taarifa za namna ya kufanikisha uwekezaji kati ya Tanzania na Japan.


“Lengo la huyu mwelekezi kutoka Japan ni kuzungumza na kusaidia makampuni na wawekezaji kutoka Japan kupata taarifa za namna ya kuja kuwekeza Tanzania na huyu wa Tanzania ni kusaidia Watanzania wote wanaotaka kuuza bidhaa zao Japan waweze kupata usaidizi kupitia kituo cha uwekezaji.”


Awali, Meneja Uenezi na Masoko wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Khamis Dunia alisema ushiriki wa Tanzania kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Osaka (World Expo Osaka 2025) yanayoendelea nchini Japan umeiwezesha mamlaka yao kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo Zanzibar.


Alisema mbali na maonesho hayo, pia kitendo cha kushiriki katika mikutano iliyomhusisha Waziri Mkuu pamoja na wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa wa Kijapan vilivyofanyika jijini Tokyo alipata fursa ya kuelezea vipaumbe vya uwekezaji vilivyopo Zanzibar ikiwemo uchumi wa buluu na utalii jambo ambalo liliwavutia wawekezaji hao ambao tayari baadhi yao wameonesha nia ya kuwekeza Zanzibar.

Mbeto : Wana CCM wameondoka Dodoma kibabe ,vifua mbele tayari kwa ushindi


 Mbeto : Wana CCM wameondoka Dodoma kibabe ,vifua mbele tayari  kwa ushindi


Na Mwandishi  Wetu, Dodoma 



Chama Cha Mapinduzi kimesema Wajumbe wake wa Mkutano  Mkuu wa  Taifa , wanaondoka katika Jiji la Dodoma huku  wakiwa wamebeba  matumaini  ya kupata  ushindi kuliko  wakati  wowote. 


Mamia  ya  Wajumbe hao  toka Mikoa  ya Tanzania Bara na Zanzibar  wameliacha Jiji Kuu hilo la Tanzania ,wakiamini chama  chao kitashinda uchaguzi  Oktoba  Mwaka huu. 


Matamshi hayo yametamkwa na Katibu  wa Kamati  Maalum  yya  NEC Zanzibar  , Idara ya itikadi , Uenezi na Mafunzo,  Khamsi Mbeto Khamis ,aliyesema  kazi iliobaki  ni kuinadi Ilani  mpya  ya CCM ya Uchaguzi   Mwaka 2025 -2030 kwa nguvu zote .


Mbeto  alisema hakuna Chama cha Siasa wala mgombea atakaehimili  kimbunga cha Kampeni  za CCM ambazo zitaanza Miezi michache ijayo toka sasa.


Alisema Uwasilishaji wa  taarifa ya matokeo ya Ilani  Uchaguzi ya Mwaka 2020-2025, tija na  mafanikio ya utekelezaji wa maendeleo  ya kisekta , kumedhihirisha nia thabit walionayo Marais ,  Dk Samia  Suluhu  Hassan na mwenzake , Dk Hussein  Ali Mwinyi .


"Wajumbe  wa Mkutano Mkuu wameondoka  Dodoma  wakiwa wamebeba vikapu vya matumaini ya ushindi . Silaha ya ushindi  wa chama cha siasa hutokana na ubora wa Ilani ,  sera  na mipango ya maendeleo " Alisema Mbeto .


Aidha, Katibu huyo Mwenezi , alisifu kazi kubwa iliiofanywa na Serikali zote mbili  katika  azma ya kutumikia wananchi na kuweka mkazo  katika utatuzi wa changamoto za  maendeleo ya kisekta. 


Alisema  matokeo  ya utekelezaji wa Ilani iliopita ya Mwaka  2020-2025 , imeelezea mafanikio ya Sekta za Afya , Elimu , Uwekezaji , Miundombinu , Nishati ya Umeme na gesi  , Ufugaji na  ukuzaji Kilimo.


 'Taifa limepiga hatua nyingi za kimaendeleo hususan  katika sekta ya Usafiri,  Mawasiliano  na Makaazi ya Nyumba  bora za  kisiasa, ujenzi  wa Masoko, Barabara ,  Shule  za Msingi na 

Sekondari ikiwemo  Ujenzi wa Vituo vya Afya na Zahanati " Alieleza 


Pia alisema  Ilani iliopita imetaja na kuonyesha mafanikio  katika ukuaji wa  Uchumi  wa Taifa , pato la Taifa,   Viwanda, Uhusiano wa Kimataifa , Diplomasia, Michezo na Siasa  pia mikopo ya  taaisis za  kimatiafa na Elimu ya juu .


Kadhalika  Mbeto  alisema taarifa katika  ilani iliopita  imeonyesha jinsi halmashauri   za wilaya zilivyoanzisha miradi ya Maji Safi na Salama ,  Barabara za Vijijini, Wilaya na Mikoa hadi  kukamilika kwake.


"Matumaini makubwa ya Wananchi yamebebwa na ilani mpya Uchaguzi wa  Mwaka huu  2025-2530 .Utekelezaji  wa mipango iliiomo katika   ilani hiyo itaipaisha na kuifanya Tanzania kuwa miongoni   mwa Nchi za uchumi  Kati "Alieleza katibu  huyo Mwenezi

Vijana 26 Kushiriki progranu ya Mandela Washington Fellowship 2025 nchini Marekani



 Vijana 26 Kushiriki progranu ya Mandela Washington Fellowship 2025 nchini Marekani 


Vijana waliochaguliwa kushiriki progranu ya Mandela Washington Fellowship kwa mwaka 2025, wamekumbushwa kuwa fursa waliyoipata haikuja kwa bahati, isipokuwa kutokana na majukumu wanayoyafanya ambayo yana mchango mkubwa kwa jamii.


Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa wakati anawapa nasaha za kuwaaga vijana hao 26 jijini Dodoma Mei 30, 2025.

Balozi Mussa aliwataka kutumia fursa hiyo kujifunza mambo mapya kwa kuwa nchi wanayokwenda imeendelea kiuchumi na kiteknolojia duniani na itawapa fursa pia ya kukutana na raia wa mataifa mbalimbali wenye uzoefu na mila tofauti.


Vijana hao ambao wanatarajiwa kwenda nchini Marekani Juni na kurejea Agosti 2025,  wametakiwa kulitangaza jina la Tanzania kwa watu watakaokutana nao. "Mtalitangaza jina la nchi yetu kwa kuheshimu sheria za nchi mnayokwenda,  kutangaza utamaduni mzuri wa Tanzania na kuelezea kwa ufasaha mambo makubwa na mazuri ya nchi kama vile mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama, maziwa, mito na maendeleo ya miundombinu", Balozi Mussa alisema. 


Balozi Mussa alisema kuwa kuwepo kwao katika programu hiyo ni kielezo cha uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Marekani ambao umedumu tokea ulipoanzishwa mwaka 1961.


Pogranu ya Mandela Washington Fellowship ilizinduliwa mwaka 2014 na hadi sasa vijana 6500 kutoka nchi za Afrika wamefaidika na mpango huo ambao unalenga kuwajengea uwezo vijana, kupata mbinu na ujuzi wa uongozi utakaosaidia kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi, kisiasa na kijamii barani Afrika.

WAKULIMA WA PARACHICHI WAPONGEZA RUZUKU YA MBOLEA

................

Wakulima wa parachichi mkoani Njombe wameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapatia mbolea ya ruzuku ambayo imewasaidia kuongeza tija na uzalishaji katika zao hilo.

Wakizungumza na wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) walipotembelea Chama cha Msingi cha Ng’anda AMCOS na kampuni ya mkulima wa parachichi ya Avo Nemes Green Limited, tarehe 28 Mei, 2025, wakulima hao walisema ruzuku hiyo imepunguza gharama za uzalishaji na kuwawezesha kuajiri nguvu kazi zaidi kwenye mashamba yao.

Mkulima mkubwa wa parachichi, Bw. Stephen Mlimbila, alieleza kuwa kupitia ruzuku hiyo, amepunguza gharama na fedha alizokuwa akizitumia kununua mbolea sasa zimeelekezwa kwenye ulipaji wa vibarua wanaohudumia shamba lake lenye ukubwa wa ekari 210 na kuwa chanzo cha ajira kwa wananchi wengi wasiokuwa na kazi.

Akijibu ombi la wakulima wa chama cha Ushirika Ng’anda cha kusajiliwa kuwa wakala wa mbolea za ruzuku, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA,  John Cheyo, amemwelekeza Meneja wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Joshua Ng’ondya, kuhakikisha Chama hicho  kinasajiliwa na kusaidia kusambaza pembejeo hiyo kwa wanachama wake na kutatua changamoto ya ucheleweshaji pindi inapohitajika.

Cheyo alisisitiza kuwa serikali inatamani kuona wakulima wanaongeza tija na uzalishaji, akiwahimiza kulima kwa bidii ili kuzalisha mara mbili zaidi ya msimu uliopita ili kukuza uchumi wao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya GBRI Business Solutions Company Limited,  inayojihusisha na ununuzi na uongezaji thamani wa zao la parachichi  Hadija Jabir, amewasihi wakulima kuzingatia matumizi sahihi ya mbolea kwenye zao la parachichi  ili wazalishe kwa wingi na ubora unaohitajika kwenye soko la nje.


 

Alhamisi, 29 Mei 2025

WATUHUMIWA 12 WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA MAKOSA YA UHUJUMU UCHUMI

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke,  Holle Makungu akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa taarifa ya utendaji wa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2025.

Wanahabari na maafisa TAKUKURU walioshiriki kwenye mkutano wa Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke,  Holle Makungu akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa taarifa ya utendaji wa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2025.

..........

NA MUSSA KHALID

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Temeke imewafikisha mahakamani  watuhumiwa kumi na wawili kwa mashtaka ya uhujumu uchumi,Ubadhirifu na Utakatishaji fedha kiasi cha zaidi ya milioni 165.14

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es salaam na Mkuu wa TAKUKURU (M)Temeke,Holle Makungu  wakati akizungumza na wananahabari akitoa taarifa ya kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu ambapo amesema mashtaka hayo yamefunguliwa katika mahakama ya Wilaya Kigamboni.

Mkuu huyo wa TAKUKURU Temeke amewataja baadhi ya washtakiwa hao kuwa ni pamoja na Annie Nyabugumba Maugo ambaye ni Afisa Hesabu(Ofisi ya Rais TAMISEMI)Tumsifu Christopher Kachira,(afisa mwandamizi OR-TAMISEMI) na Aidani Zabron Mponzi (Ofisa hesabu OR-TAMISEMI).

Wengine ni Jonathan Stanley Manguli (aliyekuwa Afisa hesabu OR TAMISEMI),Godrey James Martiny(aliyekuwa mkuu wa kitengo cha Fedha na Uhasibu),Juvenalis Mauna(Mkuu wa kitengo cha udhibiti taka na Usafi wa Mazingira),Josephat Mtembei(Mhandisi),Bibiana Mdete (Mtunza Bohari)na  Henry Herman(Afisa Ugavi).

Mbali na Watendaji hao wapo pia wakandarasi walioshatakiwa katika kesi hiyo ni Hamis Kashinje Manfred,Paulo Sam Mwakyusa na Godwin Adamson Cheyo ambao kampuni zao zinatumika kutakatisha fedha hizo.

 Aidha,Makungu,amesema kwa mujibu wa hati ya mashtaka,makosa wanayoshtakiwa nayo ni kusababisha hasara kinyume cha kifungu cha 10(1) cha jedwali la kwanza na kifungu cha 57 na 60(2) cha sheria ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 mapitio ya 2022,kosa la utakatishaji fedha k/f cha 12(1)(a) na 13(1) (a) cha Sheria ya utakatishaji fedha sura 423 ya mapitio 2022,ubadhirifu kinyume na k/f cha 28(2) cha Sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa sura ya 329.

 Aidha Makungu,amesema washtakiwa hao wamepelekwa mahabusu kwa kuwa makosa yao hayana dhamana hadi kesi yao itakapokuja tena mahakamani hapo tarehe 12/6/2025 kwa ajili ya kutajawa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, watuhumiwa wanakabiliwa na kosa la kusababisha hasara, kinyume na kifungu cha 10(1) cha Jedwali la Kwanza pamoja na vifungu vya 57 na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 (Marejeo ya 2022).

Kosa la utakatishaji fedha, kinyume na vifungu vya 12(1)(a) na 13(1)(a) vya Sheria ya Utakatishaji Fedha, Sura ya 423 (Marejeo ya 2022) pamoja na kosa la ubadhirifu, kinyume na kifungu cha 28(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329

Katika hatua nyingine,TAKUKURU mkoa wa Temeke imefuatili miradi 13 yenye thamani ya TZS zaidi Bilioni 11,ambapo kati ya miradi 13 miradi mitano (5) ilitolewa ushauri wa kurekebisha mapungufu yaliyobainika.

Hata hivyo Taasisi hiyo imetaja mikakati yake kwa kipindi cha April mpaka Juni mwaka huu kuwa ni kuimarisha juhudi za kuzuia rushwa kwa kuongeza ushiriki wa kila mwananchi na wadau mbalimbali katika kukabili tatizo la rushwa hasa katika uchaguzi wa viongozi wa kisiasa unaotarajiwa kufanyika kwa mwaka.

pIA TAKUKURU inaendelea kuelimisha jamii kwa njia mbalimbali, zikiwemo kuimarisha klabu za wapinga rushwa katika shule za msingi, sekondari, na vyuo, kufanya mikutano ya hadhara na semina, kushiriki maonesho mbalimbali pamoja na kurusha vipindi vya televisheni na redio

KAPINGA ATAJA VIGEZO VYA ZIADA UPELEKAJI UMEME VITONGOJINI


........................

  Lengo ni kuhakikisha kila Jimbo linakuwa na vitongoji vingi vilivyofikiwa na umeme

 Vinahusisha mahitaji ya kiuchumi na Kijamii, ukubwa wa Jimbo na Kitongoji

  Mkurugenzi Mkuu REA atakiwa kumsimamia kwa karibu Mkandarasi wa miradi ya Vitongoji Ziwa Tanganyika

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza miradi ya umeme katika Vitongoji kwa kuzingatia vigezo vya ziada ikiwemo ukubwa wa vitongoji, ukubwa wa Jimbo pamoja na mahitaji ya kiuchumi na kijamii.

Lengo la kuweka vigezo hivyo ni kuhakikisha kuwa kila jimbo linakuwa na vitongoji vingi vilivyofikiwa na nishati ya umeme.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Mei 29, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Simanjiro, Mhe. Christopher Olesendeka aliyeuliza kwamba  Serikali imejipangaje kutekeleza miradi ya Vitongoji kulingana na jiografia ya Wilaya ya Simanjiro ambapo umbali kutoka Kitongoji kimoja hadi kingine ni zaidi ya kilometa kumi.
 
"Mheshimiwa Naibu Spika, tunatekeleza miradi hii ya Vitongoji kwa kuzingatia vigezo vya ziada, tumeangalia ukubwa wa jimbo husika, ukubwa wa Vitongoji na mahitaji ya kiuchumi na kijamii katika jimbo husika. Niwahakikishie Wabunge mtaona utofauti katika miradi hii tunayoitekeleza hivi sasa."  Amesema  Kapinga

Akijibu swali la Mbunge wa Nyasa Mhe. Stella Manyanya aliyeuliza kuhusu kitongoji cha  Songea Pori kilichopo katika Kijiji cha Lunyele  na Kitongoji cha Nindi kilichopo Kijiji cha Konganywita kufikishiwa nishati ya umeme, Mhe. Kapinga amesema Vitongoji hivyo vimefanyiwa upembuzi yakinifu na kubainika vinahitaji njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kati kwa umbali wa kilometa tatu.

Amesema  Serikali inatarajia kuvipelekea umeme vitongoji hivyo kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili B  (HEP IIB) ambao utekelezaji wake utaanza mwaka wa fedha 2025/2026. 

Kuhusiana na kasi ndogo ya Mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme katika Jimbo la Nyasa Mhe. Kapinga amesema tayari Serikali imeshakutana na Mkandarasa na kumuagiza kuweka Wakandarasi wadogo (sub contractors) katika miradi yake anayotekeleza.

Akijibu swali la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Mhe. Aida Khenani aliyetaka  kauli ya Serikali kuhusu kusuasua kwa Mkandarasi ambaye amepewa kazi ya kupeleka umeme kwenye Vitongoji vilivyozunguka ziwa Tanganyika, Mhe. Kapinga amesema katika utekelezaji wa miradi ya Vitongoji Serikali imehakikisha inawapata wakandarasi wenye weledi.

Kuhusu Wakandarasi ambao wanasuasua,  Kapinga kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kumsimamia Mkandarasi anayetekeleza mradi huo wa umeme kwenye Vitongoji vilivyozunguka ziwa Tanganyika.

Aidha, amemuagiza kuchukua hatua za ziada kwa Mkandarasi huyo kuhakikisha anatekeleza mradi huo kwa haraka na kwa weledi
 

WAZIRI MKUU MAJALIWA AKUTANA NA WAZIRI MKUU WA JAPAN

.................

_▪️Asema Japan itaendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Tanzania_

_▪️Aagiza tathmini ya barabara za Kibiti-Lindi na Morogoro-Dodoma_

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na Waziri Mkuu wa Japan, Ishiba  Shigeru ambaye amemuhakikishia kuwa nchi hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania jambo ambalo linalenga kuchochea ukuaji wa uchumi kutokana na fursa zitakazoendelea kupatikana kupitia mahusiano hayo.

Amekutana na kiongozi huyo leo (Alhamisi, Mei 29, 2025) katika ofisi ya Waziri Mkuu Tokyo, Japan, ambapo Mheshimiwa Majaliwa amesema ahadi hiyo inazidi kutoa fursa ya wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan pamoja na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kumueleza Waziri Mkuu huyo kuwa  pamoja na miradi mingine wanayotekeleza nchini, Japan kupitia JICA iangalie uwezekano wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuzifanyia ukarabati mkubwa barabara za Morogoro-Dodoma na barabara ya Kibiti-Lindi ambayo imeharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.

Amesema Waziri Mkuu wa Japan baada ya kupata maelezo hayo ameuelekeza uongozi wa JICA pamoja na Balozi wa Japan nchini Tanzania Youichi Mikami kwenda kutembelea barabara hizo na kuzifanyia tathmini ya uharibifu na kisha kuwasilisha taarifa ili Serikali ya Japan ione namna itakavyoshirikiana na Tanzania katika utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan amepongeza kuendelea kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Japan na kwamba ameahidi kuhakikisha makampuni mbalimbali ya Japan yataendelea kufanyakazi na Tanzania ili kuisaidia katika kukuza uchumi, kuendelea masuala ya kijamii na teknolojia kwani wanatambua idadi ya watu nchini inaendelea kuongezeka.


 

Jumatano, 28 Mei 2025

SERIKALI YAKAGUA MIGODI 13, 279, BOHARI ZA BARUTI 164 KUDHIBITI USALAMA

 JUMLA ya migodi 13,279 pamoja na bohari za baruti 164 zimekaguliwa nchini kuanzia Julai 2024 hadi Machi 2025.

Hayo yameelezwa leo Mei 28, 2025 jijini Mwanza na Mkurugenzi wa Idara ya Leseni wa Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Mhandisi Ramadhan Lwamo, katika kikao kazi cha wakaguzi wa migodi na baruti kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Amesema kuwa miongoni mwa migodi hiyo iliyokaguliwa ni migodi mikubwa saba, migodi ya kati 46, migodi midogo 13,226 pamoja na bohari za baruti 164.

“Kaguzi hizi zimeimarisha Sekta ya Madini na kuongeza makusanyo ya Serikali kupitia maduhuli, hivyo kuchangia katika kuimarisha uchumi na Pato la Taifa,” amesema Mhandisi Aziza.

Ameongeza kuwa, “Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ina matarajio makubwa kwa Sekta ya Madini kutokana na mchango wake mkubwa katika Pato la Taifa. Kufikia mwaka 2024, sekta hii ilichangia asilimia 10.1 ya Pato la Taifa, ikiwa ni zaidi ya lengo la asilimia 10 lililowekwa kufikiwa mwaka 2025.”

Mhandisi Aziza ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na kazi kubwa ya Idara ya Ukaguzi wa Migodi, ambayo ndiyo chanzo kikuu cha maduhuli ya Serikali katika sekta hiyo.

Aidha, amewakumbusha wakaguzi kuzingatia Sheria ya Madini Na. 123 katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu masuala ya afya na usalama mahali pa kazi, uhifadhi wa mazingira, na matumizi salama ya baruti ili kuepuka ajali.

“Naagiza kila mkoa kutambua maeneo yenye hatari kubwa ya ajali na kuyawasilisha kwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi, ili kuweka mikakati shirikishi ya kuzuia ajali katika maeneo hayo,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Hamisi Kamando, amesema kikao hicho cha nne kwa wakaguzi wa migodi kinalenga kujengeana uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao, kwa kuwa wao ni uti wa mgongo wa usimamizi wa Sekta ya Madini.

“Wakaguzi wa migodi wana jukumu kubwa. Malengo ya ukusanyaji wa maduhuli yaliyowekwa na Serikali hutegemea vyanzo vya mapato vinavyosimamiwa na wakaguzi. Bila kulinda vyanzo hivyo, mapato hayawezi kupatikana. Tutaendelea kujifunza na kuboresha utendaji ili kuhakikisha tunafikia malengo,” amesema Mhandisi Kamando.

Aidha, amebainisha madhara ya kutofanya ukaguzi, yakiwemo ajali katika migodi zinazosababisha vifo, kusimamishwa kwa shughuli za uchimbaji, na kupungua kwa mapato ya Serikali.

OFISI YA TRA MBULU KUJENGWA 2026/27

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akijibu swali la  Mbunge wa Mbulu Mjini, Mhe. Zacharia Paulo Issaay, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kujenga Ofisi ya TRA katika Wilaya ya Mbulu, jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini- Wizara ya Fedha)

......................

Na. Josephine Majura, WF, Dodoma

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), amesema kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ina mpango wa kuanza ujenzi wa Ofisi ya TRA katika Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, katika mwaka 2026/27. 

Aliyasema hayo bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Mjini, Mhe. Zacharia Paulo Issaay, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kujenga Ofisi ya TRA katika Wilaya hiyo.

Alifafanua kuwa katika kipindi ambacho hakuna Ofisi ya TRA, shughuli za ukusanyaji wa mapato ya Serikali zinafanyika kwenye jengo la iliyokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu.

Mwisho.

TFRA YAWATAKA WAKULIMA WA KAHAWA KUZINGATIA KANUNI NA TEKNOLOJIA KWENYE KILIMO

Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA Akipata ufafanuzi kutoka kwa Meneja wa TFRA Nyanda za Juu Kusini, Joshua Ng'ondya wa kahawa iliyokobolewa kutoka katika _CPU central pulpery unit_ na baadae kuanikwa katika kichanja tayari kwa kupelekwa katika viwanda vya kukoboa kahawa na baadaye kuuzwa mnadani. Wajumbe wa bodi ya TFRA Dkt. Peter Shimo ( kushoto) na Hadija Jabir wakifurahia matunda yaliyosheheni kwenye mti wa kahawa wakati wa ziara ya kikazi kwa mkulima LOHE TANZANIA LIMITED, tarehe 27 Mei, 2025 Mbinga mkoani Ruvuma  Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo akiwa katika picha na wajumbe alioambatana nao wakati wa ziara yenye lengo la kufuatilia utekelezaji wa mpango wa ruzuku katika mazao ya kimkakati ya kahawa na parachichi kwa mikoa ya nyanda za juu kusini, ikiwa ni mkoa wa Ruvuma tarehe 27 Mei, 2025

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo akizungumza na wajumbe wa Bodi wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Kahawa Mbinga (MBIFACU) Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma tarehe 27 Mei, 2025.

Wajumbe wa bodi ya TFRA, Dkt. Peter Shimo (kulia) akifuatiwa na Lilian Gabriel na Hadija Jabir (Kushoto) wakimsikiliza Meneja wa shamba la kahawa lenye ukubwa wa ekari 113 linalomilikiwa na kampuni ya LOHE Tanzania Limited, Regnald Mapunda wakati wa ziara ya bodi tarehe 27 Mei, 2025

Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo wa pili kutoka kushoto akiwa na wajumbe wa bodi, menejimenti ya TFRA na Wajumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Miwa mara baada ya kikao kilichofanyika katika ukumbi wao wa mikutano Mbinga mkoani Ruvuma tarehe 27 Mei, 2025

...................

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) amewataka wakulima wa Kahawa Mbinga Mkoani Ruvuma kuzingatia kanuni na teknolojia bora za kilimo cha kahawa ili waweze kuongeza tija ya uzalishaji, fursa ya kujiajiri na kuondokana na umaskini. 

Dkt. Diallo ametoa ushauri huo tarehe 27 Mei, 2025, Mkoani Ruvuma ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya Bodi ya TFRA kwenye Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Kahawa (MBIFACU), lengo kuu likiwa ni kufuatilia utekelezaji wa mpango wa ruzuku katika mazao ya kimkakati ya kahawa na parachichi kwa mikoa ya nyanda za juu kusini.

Dkt. Diallo amesema, gharama na nguvu anayoitumia mkulima kuwekeza kwenye ekari moja ya shamba la kahawa, lazima ilingane na thamani ya uzalishaji anaoutarajia ambao ili kuupata ni lazima mkulima azingatie kutumia maarifa na sayansi katika uzalishaji wa zao hilo.

Aidha, Dkt. Diallo amewasihi wakulima kuondokana na tabia ya kukalili majina ya mbolea na badala yake wazingatie aina ya virutubisho vinavyohitajika kwenye mashamba yao na kununua mbolea yenye sifa zinazoendana na mahitaji ya udongo wa shamba lake. 

Akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya mbinga, Kanisius Marco, Dkt. Diallo alimuomba kufuatilia taarifa ya wakulima waliopimiwa afya ya udongo na maafisa kilimo waliowezeshwa kwa vifaa hivyo (Soil Scanner) ili kuwasaidia wakulima kuondokana na hasara ya kutumia mbolea kimazoea na kuishia kupata hasara.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Kanisius Marco ameeleza kuridhishwa na ushirikiano baina ya TFRA na watendaji ngazi ya Mkoa, Wilaya hadi vijiji unaowezesha kuwafikia wakulima na kutatua changamoto zao huku akikiri tangu afike wilayani hapo hajakutana na changamoto ya upatikanaji wa mbolea kwa wakulima.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo wa Mkoa wa Ruvuma, Afisa Kilimo Onesmo Mpuya, ameishukuru Serikali kwa mpango wa ruzuku, akisema kabla ya mpango huo walikuwa wakikadiria kiwango cha matumizi ya mbolea kwa wakulima wao, lakini sasa kupitia mfumo wa pembejeo za kilimo, wanaweza kupata taarifa sahihi za matumizi na kufanya makadirio sahihi kwa misimu inayofuata ya kilimo.

Naye Michael Kanduyu Mwenyekiti wa MBIFACU ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutekeleza mpango wa mbolea ya ruzuku iliyowezesha kuongeza uzalishaji wa kahawa kutoka tani 16,000 hadi kufikia tani 24,000.</

Jumanne, 27 Mei 2025

MILIONI 815.453 KUMALIZA KERO YA MAJI VIJIJI VINNE WILAYANI MTWARA

Picha no 382 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,akiangalia kisima cha maji katika kilichofanyiwa ukarabati mkubwa kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji kwa Wananchi wa Vijiji vya Ndumbwe,Dihimba,Mpondomo na Kinyamu Wilayani Mtwara,kushoto Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mtwara Hamis Mashindike na kulia Mkuu wa Wilaya hiyo Abdala Mwaipaya.

Picha no 387 Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mtwara Mkoani Mtwara Hamis Mashindike kushoto,akitoa maelezo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi kuhusu ukarabati wa Mradi wa Maji  Dihimba unaohudumia zaidi ya Wakazi 7,489 wa vijiji vinne Wilayani Mtwara. Na Mwandishi Maalum, Mtwara SERIKALI kupitia Wizara ya Maji,imetoa Sh.815,453,185 ili kukarabati mradi wa Maji Dihimba utakaohudumia wakazi zaidi  7,489 wa Vijiji vya Dihimba,Mpondomo,Kinyamu na Ndumbwe vilivyopo Halmashauri ya Wilaya Mtwara Mkoani Mtwara. Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mtwara Hamis Mashindike  alisema,kati ya fedha  hizo Sh.694,271,895 zimetumika kulipa Mkandarasi na Sh.121,181,200 zimetumika kwa ajili ya kununua bomba na Ruwasa Makao Makuu kwa kumtumia Mkandarasi M/S Zonghi Plumbing&General Supplies  Company Ltd. amesema,mradi huo ulianza kufanyiwa ukarabati Mwezi Januari 2024 na ulitakiwa kukamilika Mwezi Septemba, lakini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwa malipo ya hati ya madai na mvua nyingi umeshindwa kukamilika kwa muda,hivyo uliongezwa muda  na utakamilika Mwezi Juni Mwaka huu. Mashindike amesema,mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi M/S Seba Construction umefikia asilimia  75 na Mkandarasi amelipwa  malipo ya awali kiasi cha Sh.100,766,635.90 na  ulianzishwa ili kusogeza huduma ya majisafi na salama kwa Wananchi wa Vijiji hivyo na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji katika  Wilaya Mtwara. Alisema,ukarabati  huo umehusisha ujenzi wa tenki moja la lita 100,000 katika kijiji cha Mpondomo,ukarabati wa matenki mawili ya lita 200,000 katika Kijiji cha Ndumbwe na ujenzi wa vituo 17 vya kuchotea maji. Alitaja kazi nyingine zilizofanyika ni ujenzi wa nyumba ya muhudumu,ujenzi wa ofisi ya Jumuiya ya watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO),ununuzi na ulazaji wa bomba za maji umbali wa kilometa 9.74 zilizonunuliwa na Mkandarasi na ulazaji  wa bomba umbali wa kilometa 14.781 zilizoletwa na Ruwasa Makao Makuu. Kwa mujibu wa Mashindike,faida zilizopatikana kutokana na mradi huo ni pamoja na kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa Wananchi kutoka asilimia 37.04 ya awali hadi asilimia 93.47 mwaka 2025  ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 56.43. “Faida nyingine zilizopatikana ni kutatua changamoto ya maji iliyokuwepo katika vijiji vya Dihimba na Mpondo,Kinyamu na Ndumbwe,kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya mlipuko katika jamii yanayotokana na matumizi ya maji yasio safi na salama,kuchochea maendeo na umetoa ajira za muda mfupi na mrefu kwa baadhi ya Wananchi”alisema. Alieleza kuwa,mradi umezingatia sera ya maji ya kumtua mama ndoo kichwani  kwa kuzingatia umbali usiozidi mita 400 kutoka kituo kimoja cha kuchotea maji kwenda kingine na hadi sasa jumla ya kaya 48,taasisi 2 za umma zimeunganishiwa maji na vituo 12 vipya vya kuchotea maji vimejengwa. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Patrick Sawala alisema,mradi wa maji Dihimba ulizinduliwa mwaka 1989, lakini tangu wakati huo haujafanyiwa ukarabati  wowote hivyo ulishindwa kutoa maji ya kutoshelezaji mahitaji ya Wananchi wa vijiji husika. Alisema,kutokana na changamoto hiyo Serikali imeamua kutoa fedha  ili kukarabati mradi huo ambao sasa umewezesha wananchi kupata huduma ya majisafi na salama na kupunguza muda kwa kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi yao. Alisema,katika Mkoa wa Mtwara kuna miradi mikubwa na midogo ya maji inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo mradi wa Maji wa Miji 28 wa Mto Ruvuma unaotarajiwa kupeleka maji katika Mji wa Mangaka,Masasi na Nachingwea Mkoa jirani wa Lindi. Alisema,miradi hiyo ikikamilika itaongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 71 maeneo ya Vijijini hadi asilimia 85 ifikapo mwaka 2030 ambapo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi ili kuwaondolea Wananchi changamoto ya majisafi na salama. Mkazi wa Kijiji cha Dihimba Mwanahawa Rashid alisema,kabla ya ukarabati huo walitembea kilometa 2 hadi 3 kila siku  kwenda vijiji vya jirani kutafuta maji kwa kuwa katika kijiji chao kulikuwa na bomba moja tu lililojengwa kupitia mradi wa Jaica ambalo halikutosheleza kutoa maji ya uhakika. “Tunaishukuru sana Serikali yetu ya awamu ya sita iliyofanikisha kukarabati   mradi wa maji katika Kijiji chetu cha Dihimba,nawapongeza watendaji wa Ruwasa kusimamia vizuri mradi ambao umetusaidia sana kupata maji ya uhakika”alisema.

MABADILIKO YA MITAALA NGUZO MUHIMU YA KUIMARISHA ELIMU NCHINI - PROF MKENDA


...........................

 Na Ester Maile: Dodoma 

Serikali  kupitia  wizara ya Elimu,sayansi na Teknolojia inaendelea  Kuboresha   mfumo wa elimu kupitia maboresho makubwa ya mitaala katika ngazi zote za elimu nchini.

Maboresho hayo, yanalenga kuongeza ujuzi, maarifa na stadi za wanafunzi, ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kuhakikisha elimu inakuwa chachu ya maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.

Hayo yamebainishwa  leo 27 may 2025 jijini Dodoma na Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia  Prof Adolf Mkenda wakati akizungumza     na waandishi  wa habari  akieleza mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita Waziri Mkenda amesema kuwa Serikali imeanzisha mikondo miwili ya elimu ya Sekondari, Mkondo wa Jumla na Mkondo wa Amali, pamoja na kuweka mfumo wa elimu kuwa nyumbufu, ili kuhakikisha wanapokea ujuzi na maarifa yanayozingatia mahitaji halisi ya taifa na soko la ajira.

Tumeweka somo la lazima la elimu ya Biashara na Historia ya Tanzania, huku tukiboresha mifumo ya ufundishaji lugha ili kuongeza ufanisi wa ujifunzaji,” amesema Waziri Mkenda.

Aidha, amebainisha kuwa mitaala 389 katika elimu ya ufundi na mitaala 563 katika elimu ya juu imeboreshwa ili kuendana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, pamoja na kuzingatia stadi za karne ya ishirini na mahitaji ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Waziri Mkenda pia ameeleza kuwa Serikali inaendelea kufanya mapitio ya Sheria ya Elimu (Sura 353) ili kuendana na mabadiliko haya ya sera na mitaala.

 “Tunaendelea kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu ili kuhakikisha Sheria yetu inakidhi mahitaji ya sasa,” amesema.

Aidha, Serikali imehuisha miongozo mbalimbali ikiwemo Mwongozo wa Taifa wa Tuzo na Sifa Linganifu za Kitaaluma (TQF), Mwongozo wa Uanzishaji na Usajili wa Shule, Mwongozo wa Utambuzi wa Vipawa na Vipaji, pamoja na Mwongozo wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini.

Pia, Waziri Mkenda ametangaza utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika elimu, ikijumuisha miongozo ya matumizi ya teknolojia katika shule, vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu, pamoja na matumizi ya Akili Bandia (Artificial Intelligence) kwa mwaka 2025.

Amesema Serikali imeandaa Mfumo wa Kielektroniki wa Tathmini ya Ujifunzaji unaolenga kurahisisha upimaji wa wanafunzi katika shule za msingi na kuimarisha huduma kwa walimu na wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Katika sekta ya elimu ya juu, Waziri Mkenda amesema Serikali imeanza ujenzi wa majengo ya madarasa, maabara na mabweni katika kampasi kuu na za pembezoni katika mikoa 16 ambayo haikuwa na taasisi za elimu ya juu. 

Mradi huo wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), wenye thamani ya shilingi bilioni 972, utaongeza uwezo wa taasisi hizi katika kudahili wanafunzi zaidi na kupunguza uhaba wa wahadhiri kwa asilimia 20.

“Tunahakikisha kwamba elimu yetu inazalisha wataalamu wenye ujuzi na stadi zinazohitajiwa katika soko la ajira ili kuchangia maendeleo ya Taifa letu,” alisisitiza Waziri Mkenda.

Waziri amewataka wananchi na wadau wa elimu kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mfumo wa elimu nchini.

Listen Mkisi Radio