JSON Variables

Wednesday, April 30, 2025

WIKI YA UTALII TANZANIA ILIVYONOGESHA OSAKA EXPO 2025.

 

Wiki ya Utalii Osaka Expo 2025 iliyoanza rasmi tarehe 25  Aprili, 2025  inatarajiwa kumalizika  tarehe 6  mwezi  May, 2025 ambapo mojawapo ya tukio kubwa linaloloendelea kufanyika  katika  wiki hii ni pamoja na Tanzania kuonesha vivutio vya Utalii vilivyopo nchini ikiwakilishwa na Bodi ya Utalii Tanzania pamoja na taasisi zilizopo chini ya wizara ya Maliasili na Utalii.


Hifadhi ya Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro, Visiwa vya Zanzibar, Serengeti pamoja na vivutio vingine vya malikale na urithi wa utamaduni vimeweza kuwa na mvuto mkubwa kwa wageni mbalimbali wanaofika katika Banda la Tanzania nchini Japan na kujionea namna nchi hiyo ilivyoweza kuwa na rasilimali nyingi na za kuvutia.


Balozi wa Tanzania nchini Japan Mheshimiwa Baraka Luvanda aliongoza timu ya Tanzania katika ufunguzi wa maonesho hayo katika banda la Tanzania na kupongeza juhudi zinazofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii katika kuhakikisha kuwa wageni wengi wanafikiwa kwa kupata taarifa ya vivutio vilivyopo na namna ya kuweza kuvitembelea vivutio hivyo.


“Hongereni sana TTB na TanTrade kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuitangaza nchi yetu katika maonesho kama haya, hii inasaidia kwa kiasi kikubwa kuendelea kuwavutia wageni wengi kuja kuona vivutio tulivyonavyo na hapa kwa kweli tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii wetu”,alisema Balozi Luvanda.


Mkurugenzi wa Masoko kutoka Bodi ya Utalii Tanzania Ernest Mwamwaja alieleza kwamba sekta ya utalii imekuwa ikifanya vizuri kadri miaka inavyosonga mbele hasa kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa za kutangaza vivutio vyote vilivyopo kwa nguvu kubwa ambapo kwa sasa imekuwa ikiingiza asilimia katika ya 17 mpaka 20 ya pato la taifa.


“Sekta hii inakua na ndiyo maana mpaka sasa tumevuka lengo la watalii milioni tano kama ilivyoelekezwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi, tutaendelea kuutangaza utalii katika kila matukio kwani hii ndiyo njia sahihi ya kupeleka taarifa kwa wadau na watumiaji wa sekta hii.”alisema Mwamwaja.


Meneja wa banda la Tanzania nchini Japan bwana Deo Shayo alisema kuwa Tantrade imekuwa ikiwaunganisha wadau wa sekta mbalimbali katika maonesho makubwa kama EXPO 2025 ili kutoa fursa kwa kila sekta kuweza kujitangaza katika masoko ya kimataifa na kusaidia pia kuvutia wawezekezaji kutoka mataifa mengine.


Kwa upande wake Afisa Makoso Mkuu kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro bwana Michael Makombe alisema EXPO 2025 inaonesha kuwa na faida kubwa kwa Tanzania na Ngorongoro kwa ujumla kutokana na wageni wengi kuonesha kuvutiwa na utalii wa wanyama na hivyo maonesho hayo yatasaidia kuongezeka kwa idadi ya wageni msimu ujao wa utalii.


Maonesho ya EXPO 2025 yanaendelea nchini Japan ambapo kwa wiki mbili hizi wadau wa sekta ya utalii wamekuwa katika pilika pilika kubwa ya kutangaza vivutio na kujiandaa kwa mikutano ya wadau wa sekta hiyo ili kuweza kubadilishana mawazo na kuainisha maeneo ambayo wanaweza kutembelea.

NIMERIDHISHWA NA MAANDALIZI KUELEKEA SHEREHE ZA MEI MOSI-MAJALIWA

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na Maandalizi kuelekea sherehe za siku ya wafanyakazi duniani zitakazofanyika kesho Mei mosi, 2025 kitaifa Mkoani Singida katika Uwanja wa Bombadia

 

Ameyasema hayo leo Jumatano (Aprili 30, 2025) alipopokea taarifa na kukagua maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe hizo. Mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza kamati inayoratibu sherehe hizo na kuwataka kuhakikisha wanakamilisha maeneo machache yaliyobaki ambayo yanahitaji maboresho.

 

Awali, akitoa taarifa ya maandalizi hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete amesema maandalizi yamekamilika kwa kiasi kikubwa na wapo tayari kumpokea Rais Dkt. Samia kwa ajili ya sherehe hizo.

JESSICA MSHAMA MGENI RASMI KATIKA KONGAMANO LA BINTI NA DKT. SAMIA.

 

Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi wa UVCCM Taifa, Ndugu *Jessica Mshama*, atakuwa mgeni rasmi katika *Kongamano Maalum la Mabinti na Dkt. Samia* litakalofanyika   tarehe 1 Mei 2025 katika ukumbi wa Kibo Garden. Kongamano hili limeandaliwa na *UVCCM UDSM MLIMANI* kwa lengo la kuwaunganisha vijana wa elimu ya juu na kuwawezesha kubadilishana mawazo, kuongeza uelewa wa masuala ya uongozi n.k. kama ilivyo elezwa hapo juu.


🇹🇿 Ndugu *Jessica Mshama* anatarajiwa kutoa hotuba ya kuhamasisha, kuelimisha  mabinti na vijana wote wa UDSM kushiriki kikamilifu katika kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. Kongamano hili litakuwa jukwaa muhimu kwa vijana wasomi wa kike na wa kiume kujifunza na kupata mwanga kuhusu nafasi ya vijana katika siasa na Uongozi  hasa kupitia dira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, *Dkt. Samia Suluhu Hassan*. 


 "KAZI NA UTU TUNASONGA MBELE" 

RAIS MWINYI:SMZ KUVIONDOA VIKWAZO VINAVYOKWAMISHA UENDESHAJI WA BIASHARA.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi ameahidi Serikali kuviondoa Vikwazo vyote vinavyochangia Kukwamisha Uendeshaji wa Biashara hapa nchini.


Rais Dkt,Mwinyi amesema hayo alipoizindua Sera ya Biashara ya 2024 na Tathmini ya Uimarishaji wa Mazingira ya Biashara (Zanzibar Blue Print) 2025 Hafla iliofanyika New Amani Hotel , Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 30 Aprili 2025.

Aidha Rais Dkt, Mwinyi amebainisha kuwa bado lipo Tatizo la  kuwepo kwa Urasimu,Ucheleweshaji wa Watu kufanya Biashara zao na Utendaji usio na Ufanisi kwa baadhi ya Watendaji katika Sekta ya Biashara.


Rais Dkt Mwinyi amesema Serikali haiwezi Kuendelea na  Watendaji wanaosababisha kuwepo kwa Vikwazo katika Uendeshaji wa Biashara.


Vilevile Rais Dkt.Mwinyi amewatoa hofu Wadau na Taasisi   zinazosimamia Sekta ya Biashara  kuwa Serikali imedhamiria kuweka Mazingira mazuri ya  Ufanyaji wa Biashara.

Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa licha ya kuwepo kwa Sera ya Biashara na Ripoti ya Tathmini lazima kuwepo na Msimamizi Mwenye dhamira ya Kweli ya  kusimamia Utekelezaji wa Sera Hiyo na kuahidi kulivalia njuga Suala Hilo na  Utekelezaji wa Sera Hiyo.

 Ameziagiza Taasisi zote za Umma na Binafsi kutekeleza kikamilifu Sera ya Biashara 2024 na tathmini ya Uimarishaji wa Mazingira ya Biashara.(Zanzibar Blue Print) 2025.


Akizungumzia Uzinduzi huo wa Sera amesema itasaidia kwa kiwango kikubwa kuleta Ufanisi wa Utekelezaji wa Sekta ya Biashara  na kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha Biashara.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt Mwinyi amesema kuwa Sera hiyo ni hatua ya Kufanikisha Ahadi ya Ilani ya CCM ya 2020-2025  ilioitaka Serikali Kuandaa Mazingira Bora ya Biashara Nchini.


"ACT BILA KULITAJA JINA LA MAALIM SEIF HAKUNA JIPYA KWA WAZANZIBARI" ASEMA MBETO

 

Na Mwandishi  wetu,Micheweni 


Chama Cha Mapinduzi kimesema  Viongozi  wa   ACT  Wazalendo bila   kulitaja jina la Marehemu   Maalim  Seif Sharif Hamad, hawana uwezo wa kukubalika katika jamii na kupata viti  vya  udiwani ,uwakilishi ubunge na kuongeza kura za urais. 


Kimesisitiza kuwa ndio maana hueneza na kuhubiri    Siasa za utengano , shari au kukimbilia kukosoa  mfumo  wa  Muungano wa serikali  mbili si sahihi ili wapatwe kusikilizwa 


Katibu wa Kamati Maalum  ya NEC  Zanzibar  Idara  ya itikadi  ,Uenezi na Mafunzo,  Khamisi  Mbeto  Khamis, ameeleza hayo akiwa katika ziara ya kizazi huko  Micheweni Mkoa wa Kaskazini  Pemba



Akizungumza na wanachama wa  CCM  Wilaya  hiyo , Mbeto  alisema kisiasa ACT  Wazalendo  kimeshakwama, hakina maneno ya kuwashawishi wananchi ili kiweze kukubalila  na kuchagulika katika  uchaguzi mkuu wa oktoba  Mwaka huu.


Mbeto  alisema baada ya chama hicho  kukosa sera zenye matumaini kwa wananchi,  kinga yao kuu ni  kulitumia jina la Maalim  Seif, kuhubiri Siasa za fitna ,majungu na ubaguzi  au kuzungumzia muundo wa Muungano .


"Juussa na viongozi  wenzake  hawana uwezo  wa kuwaeleza lolote wazanzibari wakasilizwa na kufahamika.Wana dosari  na shutuma  katika  jamii zisizowapa heshima.Baada ya kujua  wana udhaifu huo   jina la Maalim  Seif kwao huwa ngao  yao  "Alisema Mbeto 


Aidha  alisema iwapo kungekuwa na tija ya  kuzungumzia kasoro za  chaguzi zilizopita CCM kingezungumzia chaguzi za  mwaka  1957, '61 na '63,  lakini  hakioninkama kuna  umiumu  wowote.


Alisema ACT  kinapozungumzia chaguzi  za  mwaka 1995 hadi 2015 ni katika  kuiaminisha jamii katika uongo wao wa kudai kuwa hakuna  ambao CCM kilishinda kama kinavyojidanganya. .


"Kuzungumzia Uchaguzi uliopita  ni   kutonesha vidonda vilivyoanza kupona .CCM na ACT vyote havitakiwi  kuzumgumzia  chaguzi zilizopita.Kufanya hivyo  ni kupoteza wakati  bure. Ni  sawa na kufufua makaburi ya  wafu  "Alieleza 


Alisema kwa vyovyote itakavyokuwa ,  Zanzibar  haiwezi kujitoa katika  Muungano wa serikali  mbili ili mataifa  ya Tanganyika na zanzibar yawe na mamlaka kamili kama ilivyokuwa kabla ya Aprili 26  mwaka 1964.


"Serikali ya Rais Dk   Hussein Ali Mwinyi ina cha kuwaonyesha wananchi kwa  iliofanyika miaka mitano  iliopita .Yaliofanyika yanaonekana na kila mzanzibari .Rais Dk Mwinyi hana kazi ngumu Oktoba  mwaka huu" Alisema Mbeto.


Hata hivyo, Katibu  huyo Mwenezi  aliwataka wananchi wa mkoa wa  Kaskazini  Unguja kutazama mema waliofanyiwa na serikali ya awamu ya nane  Zanzibar na manufaa walioyapata.

WAZIRI CHANA AKUTANA NA SEKRETARIETI YA MKATABA WA LUSAKA

 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Sekretarieti ya mkataba wa Lusaka (Lusaka Agreement) kuhusu Mkutano wa 14 wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba wa Lusaka(LATF) unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha kuanzia Mei 6-8, 2025.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dodoma leo Aprili, 30 2025 Mhe. Chana amesema Tanzania iko tayari kupokea  wageni zaidi ya 100 kutoka Nchi wanachama na Nchi waalikwa na kuwahakikishia usalama wao kwa kipindi chote wawapo nchini. 

Naye, Mkurugenzi wa Sekretarieti ya Mkataba wa Lusaka, Bw. Edward Phiri amesema maandalizi  ya mkutano huo yamekamilika  na  tayari viongozi mbalimbali kutoka nchi wanachama wa Mkataba wa Lusaka wameshathibitisha kushiriki.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii (anayeshughulikia maliasili), CP Benedict Wakulyamba , Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii (anayeshughulikia utalii), Bw. Nkoba Mabula, Mkurugenzi wa Wanyamapori, Dkt. Alexander Lobora pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.



TIJA KWA NCHI NDIYO KIPAUMBELE CHA UTEKELEZAJI WA MRADI WA KUCHAKATA NA KUSINDIKA GESI ASILIA (LNG)- DKT.BITEKO


 Asema kiu ya Serikali ni kuona mradi unatekelezwa ila maslahi ya Taifa ndiyo kipaumbele

 Alieleza Bunge hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhamasisha ujenzi wa vituo vya gesi (CNG) na matumizi

 Aeleza kuhusu kuundwa kwa Timu kuangalia unafuu wa gharama za umeme kwa Wananchi

 Kapinga azungumzia kazi za kupeleka umeme wa Gridi Rukwa, Kagera, Katavi, Lindi na Mtwara

 Shilingi Bilioni 9.89 kupeleka umeme jua kwenye visiwa 118

 Bunge lapitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati 2025/2026 kwa asilimia 100

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko amesema dhamira ya Serikali ni kutekeleza mradi mkubwa wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) kutokana na faida zake kiuchumi ila kwa sasa kuna maeneo ambayo Serikali inayafanyia kazi kwa kina kupitia majadiliano na Wawekezaji ili mradi husika uwe na tija kwa nchi na wananchi.

Ameyasema hayo tarehe 29 Aprili 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Wabunge kuhusu Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati ya shilingi Trilioni 2.2 kwa mwaka 2025/2026 kabla ya kupitishwa kwa kishindo na Bunge hilo kwa asilimia 100.

“ Mradi wa LNG umeanza kusemwa kwa muda mrefu na kila mmoja angetamani mradi huu ukamilike jana lakini lazima tukubaliane kuwa lazima tujadiliane kwa kina na wawekezaji ili kupata kilicho bora na kuleta tija, ninachotaka kuwahakikishia ni kuwa timu ya majadiliano ya Serikali na Wawekezaji wanaendelea na majadiliano na tunatarajia kuwa ndani ya mwaka huu 2025 kama tutakuwa tumemaliza masuala matatu yaliyosalia kujadiliwa, mkataba huo utasainiwa ili mradi uanze mara moja.” Amesema Dkt.Biteko

Ameongeza kuwa, Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan ana kiu ya kuona mradi huo unaanza na alishatoa maagizo kwa Wizara ya kuhakikisha kuwa mradi unaanza kutekelezwa.

Akijibu hoja kuhusu vituo vya mafuta vinavyoongezeka na kujengwa kwa kukaribiana,

Dkt.Biteko amesema kuwa Wizara ya Nishati imeanza mazungumzo na Wizara ya Ardhi ili kuongeza umbali kati ya kituo kimoja na kingine kutoka mita 200 za sasa kwa lengo la kuleta usalama wa watu, mazingira na shughuli za kijamii.

Kuhusu msamaha wa kodi mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa gesi inayotumika kwenye vyombo vya moto kama vile magari (CNG), Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali ilishatoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa vifaa na mashine mbalimbali zinazotumika katika mnyororo wa thamani kwa miradi ya CNG kama vile mitungi ya CNG pamoja na vifaa vya kuwezesha kufunga mfumo kuwezesha magari kutumia gesi hiyo.

Ameongeza kuwa, katika mwaka 2024/2025 Wizara ya Nishati imewasilisha Wizara ya Fedha mapendekezo ya maboresho ya kodi katika gesi asilia inayotumika kwenye magari ili kuzidi kuhamasisha matumizi ya CNG na wawekezaji wanaowekeza kwenye miradi hiyo wapate faida na kurudisha gharama wanazowekeza kwa haraka.

Akijibu hoja za Wabunge kuhusu gharama za kuunganisha umeme vijijini na mijini, Dkt.Biteko amesema kuwa imeundwa timu kwa ajili ya kuangalia namna gani gharama hizo zitapunguzwa lengo likiwa ni kuleta unafuu kwa wananchi.

Kuhusu usambazaji wa umeme Vijijini, Dkt.Biteko amesema kuwa, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anapaswa kupongezwa kwa kufikisha umeme katika Vijiji vyote 12,318 kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 huku kazi ya kupeleka umeme vitongojini ikiendelea kwa kasi.

Akizungumzia ujenzi wa vituo vya kupoza umeme katika wilaya zote nchini kupitia mradi wa gridi imara, Dkt. Biteko amesema kuwa tayari Serikali imeshanunua viwanja kwa ajili kujenga vituo hivyo na katika awamu ya kwanza vitajengwa vituo 14 huku utekelezaji ukiendelea na katika laini za umeme ambazo ni ndefu sana Serikali itaweka switching stations.

Aidha, kuhusu suala la kukatika kwa umeme nchini, Dkt.Biteko amesema kuwa limepungua kwa asilimia 48 huku dakika za kukatika umeme zikipungua kwa asilimia 64 na kwa sasa umeme ukikatika ni kwa sababu tu ya matengenezo ya miundombinu. Hata hivyo amesema Serikali inaendelea kuimarisha kituo cha huduma kwa Wateja TANESCO ili taarifa ziwafikie wananchi kwa wakati pale umeme unapokatika ikiwemo kila wilaya kuwa na kundi sogozi.

Awali, wakati wa kuhitimisha Hotuba hiyo ya Wizara ya Nishati, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga alimpongeza Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya katika Taifa hususan kwenye Sekta ya Nishati akieleza kuwa moja ya misingi ya ukuaji wa kiuchumi na maendeleo katika Taifa lolote ni uwekezaji katika Sekta ya Nishati.

Akizungumzia mikoa ambayo bado haijaunganishwa katika gridi ya Taifa ya umeme, Kapinga alisema kuwa kuna miradi mbalimbali inayoendelea ambapo katika Mkoa wa Rukwa kuna mradi mkubwa wa kusafirisha umeme unaoendelea wa kutoka Iringa-Tunduma hadi Rukwa na kipande kingine cha mradi kitakachounganisha gridi ya Tanzania na Zambia.

“Mhe.Spika katika Mkoa wa Mtwara na Lindi tayari mkandarasi yupo eneo la kazi, mradi umeanza kwa kujenga njia ya umeme kutokea Songea-Tunduru-Masasi hadi Mahumbika na tumeshaanza kulipa fidia katika eneo la Tunduru hadi Masasi takriban shilingi bilioni 4.6 na eneo lililobakia la Songea kuelekea Namtumbo na Tunduru tutaendelea kulipa fidia ya takriban shilingi bilioni 2.7.” Alisema Kapinga

Kuhusu kupeleka gridi ya Taifa katika Mkoa wa Kagera alisema kuwa kazi inaendelea kupitia ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya Benaco-Kyaka na katika Mkoa wa Katavi mradi wa kupeleka umeme wa gridi mkoani humo uko katika hatua za mwisho.

Akizungumzia kazi ya kupeleka umeme kwenye visiwa mbalimbali nchini, Kapinga alisema kuwa, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 9.89 ili kupeleka mifumo ya umeme jua katika visiwa 118 ambavyo vipo katika mikoa zaidi ya mitano hususan Wilaya ya Ukerewe.

Kuhusu maboresho miundombinu ya umeme katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Kapinga alieleza kuwa kuna kazi zinaendelea kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata umeme wa uhakika ikiwemo uboreshaji wa kituo cha Mbagala ambacho kilikuwa na transfoma yenye uwezo wa MVA 50 lakini sasa inawekwa transfoma mpya yenye uwezo wa MVA 120 ili kukiongezea uwezo kituo hicho ili wananchi wa Mbagala, Temeke, Yombo, Mkuranga na baadhi ya maeneo ya Kigamboni waendelee kupata umeme wa uhakika.

Alieleza kuwa kazi hiyo imefikia mwishoni na muda wowote transfoma hiyo itaanza kufanya kazi. Kwa eneo la Kigamboni amesema maboresho pia yanaendelea kufanyika na kwamba wananchi tayari wameshaanza kuona mabadiliko ya upatikanaji umeme kupitia maboresho hayo.

                                               

Tuesday, April 29, 2025

MALIASILI SC YATIKISA SINGIDA.


Na Sixmund Begashe 

Club ya Michezo ya Wizara ya Maliasili na Utalii maarufu kama MNRT SPORTS CLUB imeibua gumzo la shangwe Mkoani Singida kwenye mashindano ya Maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi Duniani MEI MOSI 2025, Mkoani Singida, kutokana ushujaa wa timu zake hususani timu ya mchezo wa kuvuta kamba wanaume iliyofanya vizuri mpaka mwisho.

Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Singida na viunga vyake wamesikika wakiwapongeza wachezaji wa timu za Club hiyo yenye wachezaji wenye mbinu na ujuzi mkubwa, kwa kupambana vikali kwenye michuano hiyo hali inayoleta hamasa ya watu kupenda michezo na burudani ya aina yake.

Akizungumza na Maliasili Media, Bi. Mwantum Shabani wa Manyoni Singida amesema japo timu ya Maliasili Sports Club Wanaume Kamba imeshika nafasi ya pili lakini imeonesha upinzani mkali dhidi ya timu zingine pinzani.

" Singida kama burudani tumepata, mimi timu yangu ilikuwa Maliasili, si kwa sababu tu wanatulindia Maliasili zetu na kutuletea mapato kupitia Utalii, pia kwa namna walivyojipanga kwenye michezo hii, yaani ukishangilia hii timu haikuangushi, najivunia kuona wameibuka na Kombe hili naamini mwakani watakuwa washindi wa kwanza". Aliongeza Bi. Shabani.

Akizungumzia mashindano hayo makubwa hapa nchini, Mwenyekiti wa MNRT SPORTS CLUB Bw. Gervas Mwashimaha ameushukuru uongozi wa Wizara hiyo kwa kuiunga mkono club hiyo hali iliyowatia moyo na hari kubwa Kipindi chote cha michuano hiyo na kuahidi kuendelea kufanya vyema zaidi katika michezo mingine watakayo shiriki.

Katika mchezo wa Fainali wa Kamba wanaume, timu ya Maliasili imeshika nafasi ya pili dhidi ya timu 47 zilizoshiriki mashindano hayo huku timu ya Uchukuzi wanaume Kamba ikishika nafasi ya kwanza.