JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Jumanne, 13 Mei 2025

MACHINGA DODOMA WAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA UJENZI WA SOKO LA KISASA

 

▪️Ni soko kubwa la kipekee la Machinga Complex


▪️Machinga Wanawake Dodoma wazindua Umoja wao


▪️RC Senyamule ataka Jiji kuongeza maeneo ya kufanyia biashara 


▪️Mbunge Mavunde awataka Machinga Dodoma kuchangamkia Mkopo wa Bilioni 7 za Jiji


*Dodoma*


Umoja wa Wanawake Machinga Dodoma(UWAMADO) wamempongeza Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa ujenzi wa soko la kisasa la Machinga Complex na miundombinu ya kisasa ya soko hilo ambalo ni la kipekee nchini.


Hayo yamesemwa jana wakati wa uzinduzi wa chama cha UWAMADO uliofanyika kwenye eneo la soko la Machinga Complex kwa kuzinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mh. Rosemary Senyamule

Akisoma Risala Katibu wa UWAMADO Bi. Mariam Kajembe amesema umoja huo umelenga kuwaleta wanawake Machinga pamoja ili kujijenga na kujiimarisha uchumi.


Aidha pia UWAMADO umempongeza Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa ujenzi wa Soko la Machinga Complex ambalo limesaidia kuwaleta pamoja wafanyabiashara wengi wadogo pamoja ambao awali hawakuwa katika maeneo rasmi na hivyo kuwafanya kutokuwa rasmi.


Akitoa hotuba yake,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mh. Rosemary Senyamule amewapongeza UWAMADO kwa kuamua kuanzisha umoja wao ambao utawasaidia kujiendeleza zaidi na kujiimarisha kiuchumi.

“Jambo hili la kuanzisha umoja ni jambo jema,hakikisheni umoja unafikia malengo mliyokusudia.


Mh. Rais kawajengea soko kubwa na zuri,soko hili liwe kichocheo cha ukuaji wenu kimtaji na kibiashara.


Niwatake Uongozi wa Jiji la Dodoma kuendelea kubuni na kuanzisha maeneo mapya ya kuwapanga vizuri wafanyabiashara wadogo wa Dodoma”Alisema Senyamule

 

Akitoa salamu zake Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde amewapongeza UWAMADO kwa kuona umuhimu wa kukaa pamoja kujiinua kiuchumi na kuwataka kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10% ya mapato ya ndani ya Jiji ambayo kiasi cha Shilingi Bilioni 7 kimetengwa kwa ajili ya kuwawezesha wakina mama,vijana na watu wenye ulemavu.

Jumatatu, 12 Mei 2025

INEC YAGAWA MAJIMBO YAANZISHA CHAMAZI NA KIVULE DAR

........................

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imeanzisha majimbo mapya nane nchini kote, ambapo jijini Dar es Salaam, majimbo mawili ya Chamazi na Kivule yameanzishwa kutokana na mgawanyo wa majimbo ya Mbagala wilayani Temeke na Ukonga Wilaya ya Ilala.

Majimbo mapya yatakuwa sehemu ya Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, ambapo Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani Jacob Mwambegele, amesema tume yake imefikia uamuzi huo baada ya kupitia maombi kutoka kwenye mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Jaji Mwambegele amesema uamuzi huo umefanyika kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 75(1), (2) na (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Kanuni ya 18(7) ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024.

Ameyataja majimbo hayo kuwa ni Jimbo la Kivule amabalo limegawanywa kutoka Jimbo la Ukonga na Jimbo la Uchaguzi la Chamazi lililogawanywa kutoka Jimbo la Mbagala yote ya mkoani Dar es Salaam.

“Mkoani Dodoma limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Dodoma Mjini limegawanywa na kuanzishwa jimbo jipya la Uchaguzi la Mtumba na Mkoani Mbeya limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Mbeya Mjini limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Uyole,” amesema.

Jaji Mwambegele ameongeza kuwa, Mkoani Simiyu limeanzishwa jimbo jipya moja ambapo Jimbo la Uchaguzi la Bariadi limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la uchaguzi la Bariadi Mjini.

“Huko Geita yameanzishwa majimbo mawili, Jimbo la Busanda limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Katoro na Jimbo la Chato likigawanywa pia na kuanzishwa Jimbo jipya la Chato Kusini.

“Mkoani Shinyanga limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Solwa limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Itwangi,” amesema Jaji Mwambegele mbele ya wanahabari.

SERIKALI INABORESHA MIUNDOMBINU YA UMEME KIBITI KUONDOA CHANGAMOTO YA UMEME- KAPINGA


.......................

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inatekeleza miradi mbalimbali ya matengenezo na ukarabati wa njia za kusafirisha na kusambaza umeme katika Wilaya ya Kibiti ili kuondokana na tatizo la kukatika kwa umeme kunakotokana na uchakavu wa miundombinu hiyo.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Mei 12, 2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kibiti, Mhe. Twaha Mpembenwe aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali kutatua tatizo la kukatika kwa umeme Jimbo la Kibiti. 

Ameitaja Mikakati hiyo ni kubadili nyanya za umeme kwa kuweka zenye uwezo mkubwa, kubadili nguzo za umeme na kuweka za zege, kubadili Pin insulators na kuweka mpya, na kufunga vidhibiti matatizo (fault auto recloser) kwenye line zenye urefu wa zaidi ya Kilomita 50.


 

WACHIMBAJI GEITA WAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA MAFANIKIO MAKUBWA YA SEKTA YA MADINI

 

▪️Wachimbaji Madini wapongeza upatikanaji wa Leseni na mazingira rafiki ya biashara


▪️Waziri Mavunde aainisha mafanikio 16 ya Rais Samia kwenye sekta ya Madini


▪️Aagiza uanzishwaji wa Soko la Dhahabu Katoro


▪️RC Shigela aja na mikakati mizito ya kupaisha sekta ya madini Geita


*Katoro,Geita*


Wachimbaji na Wafanyabiashara wa Madini wa Mkoa wa Geita wamempongeza Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia sekta ya madini katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.

Hayo yamesemwa jana kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na wachimbaji hao katika eneo la mnada wa zamani Katoro,Geita kwa lengo la kumpongeza Rais Samia kwa mafanikio yaliyopatikana kupitia sekta ya madini.


Akitoa maelezo ya awali,Mwenyekiti wa Chama cha Wachimba Madini Mkoa wa Geita(GEREMA) Ndg. Titus Kabuo amesema dhumuni kubwa la kusanyiko hilo ni kumpongeza Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kuiboresha sekta ya madini na kuweka mazingira rafiki ya uchimbaji na ufanyaji biashara hali inayopelekea kukua kwa shughuli za uchimbaji na kuathiri chanya maendeleo ya wachimbaji na uchumi wa nchi.

Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimba Madini Tanzania(FEMATA) Ndg. John Bina amesema katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia  sekta ya madini imeshuhudia mabadilko makubwa hasa katika upatikanaji wa Leseni kwa wachimbaji na hatua iliyoanzwa na serikali ya kufanya utafiti wa kina ili kuwaongoza vyema wachimbaji madini nchini.


Akiwasilisha hotuba yake,Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde ameyataja mafanikio 16 ya Rais Samia S. Hassan katika kuipaisha sekta ya madini kubwa ikiwa ni kuongezeka kwa mchango wa sekta ya madini kwenye pato la Taifa kufikia 10.1%,ununuzi wa Dhahabu kupitia Benki Kuu,Kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuli kuelekea lengo la kukusanya Shilingi Trilioni moja na upatikanaji wa mitambo ya kuchoronga 15 kwa ajili yaa wachimbaji wadogo.

Aidha, Waziri Mavunde ametumia fursa hiyo kukipandisha hadhi kituo cha ununuzi wa dhahabu cha Katoro na kuwa soko kamili la Dhahabu la Katoro.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti wabunge Joseph Msukuma na Tumaini Magesa wamempongeza Rais Samia kwa kuweka mazingira rafiki ya biashara ambayo yamesaidia kupatikana kwa maendeleo makubwa na kukuza uchumi wa watu wa Geita.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Mh. Martin R. Shigela amesema Mkoa wa Geita umejipanga kuchochea shughuli za madini kwa kuboresha mazingira ya uchimbaji ili kukuza uchumi wa  wananchi wa mkoa wa Geita kupitia upatikanaji wa Leseni zaidi ya 5308 na mitambo ya Uchorongaji ambayo Mh. Rais ameitoa kwa kwa wachimbaji wadogo.

Jumapili, 11 Mei 2025

NYAHOZA AKIPONGEZA CHAMA CHA CCK KWA KUMPATA MGOMBEA URAIS

Naibu Msajili wa vyama vya siasa nchini Sisty Nyahoza akizungumza na wajumbe wa Chama Cha Siasa Cha Kijamii (CCK) katika mkutano Mkuu maalum wa Chama hicho kwa ajili ya kuwachagua na kuwapitisha wagombea nafasi ya Urais wa Tanzania Bara na Zanzibar ambao umefanyika tar 10/5/2025 jijini Dar es salaam.

Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Kijamii cha CCK David Daudi Mwaijolele ambaye pia amepitishwa kwa kupigiwa kura kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bara akizungumza katika mkutano Mkuu maalum wa Chama hicho ambao umefanyika tar 10/5/2025 jijini Dar es salaam.

Aisha Salum Hamadi ambaye amepitishwa kugombea nafasi ya Urais kupitia Chama cha Kijamii cha CCK Zanzibar akizungumza na wajumbe wa chama hicho katika mkutano Mkuu maalum wa Chama hicho ambao umefanyika tar 10/5/2025 jijini Dar es salaam.

Viongozi wa Kitaifa wa Vyama vya siasa waliohudhuria katika katika mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha siasa cha Kijamii cha CCK ambao umefanyika tar 10/5/2025 jijini Dar es salaam.

Wajumbe mbalimbali waliohudhuria katika mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha siasa cha Kijamii cha CCK ambao umefanyika tar 10/5/2025 jijini Dar es salaam. 

........................

NA MUSSA KHALID

Naibu Msajili wa vyama vya siasa nchini Sisty Nyahoza amekipongeza Chama Cha Siasa Cha Kijamii - CCK kwa kufanya Uchaguzi wa wazi na demokrasia wa kumchagua Mgombea Urais wa Tanzania bara na Zanzibar kupitia Chama hicho.

Katika Uchaguzi huo uliofanyia jijini Dar es salaam wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama hicho wamepiga kura na kumchagua Mwenyekiti wa Chama hicho David Daudi Mwaijojele kuwa mgombea Urais kwa Tanzania Bara huku  Isha Salum akiteuliwa na Halmashauri kuu kuwa mgombea Pekee wa Nafasi ya Urais Kupitia Chama Cha CCK  Zanzibar.

Akizungumza kwenye mkutano huo Naibu Msajili wa vyama vya siasa Sisty Nyahoza amevisisitiza Vyama vya siasa nchini kueendelea kudumisha amani na kulinda umoja wetu wakati huu wa kuelekea uchaguzi ili nchi iweze kupita salama.

Nyahoza amesema mkutano huo umefanyika kwa sababu taifa lina amani na hivyo mtu yeyote mwenye nia ya kuvunja amani ni vyema akakemewa mapema.

‘Umoja wetu ndio unatufanya tuwe Pamoja hapa tukiwa wazanzibari na watu wa bara hivyo tulinde umoja wetu ili tfanye siasa kwa amani na utulivu’amesema Nyahoza

Kwa upande wake Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Kijamii cha CCK David Daudi Mwaijolele amesema kuwa wananchi watarajie makubwa pindi atakapofanikiwa kuitangaza mikakati mbalimbali wakati wa kampeni.

Amesema kuwa malengo yao ni kutaka kuhakikisha jamii ya kitanzania inaishi maisha bora katika maeneo mbalimbali ya kilimo ,uvuvi,ujasiriamali ikiwemo makundi maalum.

‘Chama cha CCK tutakapopewa ridhaa kupitia tume Tutahakikisha vijana wanaweza kujiajiri wenyewe pindi wanapomaliza elimu,lakini pia wanawake kunufaika na uchumi wao’amesema Mwaijolele

Naye Aisha Salum Hamadi ambaye amepitishwa kugombea nafasi ya Urais kupitia chama chake cha CCK Zanzibar amesema kuwa anajivunia kuwa mwanamke wa kwanza chama chake kumuamini kuiepeperusha bendera ya chama katika visiwa hivyo.

Amesema kuwa yupo tayari kukipambania chama cha CCK kwa Zanzibar ambapo vipaumbele vyake ni kuwasaidia watui wenye uhitaji wakiwemo walemavu.

Amewasisitiza watanzania kuwaonyesha mshikamano kwa kuwaunga mkono kukichagua chama chao ili kiweze kuwasaidi kuzitatua changamoto mbalimbali kwenye maeneo yao.

   

CHARLES HILLARY AFARIKI DUNIA LEO ALFAJIRI


Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Znz ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais wa Zanzibar Charles Hillary, amefariki alfajiri ya leo May 11 2025 katika Hospitali ya Muhimbili Mloganzila, alikokuwa akipatiwa matibabu.


Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar Mhandisi Zena Ahmed Said, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kutoa pole kwa Familia, Ndugu, Jamaa na Marafiki wote walioguswa na msiba huu.

Charles Hillary ni miongoni mwa Watangazaji bora wa Redio na Televisheni Nchini Tanzania ambaye amefanya kazi katika vituo mbalimbali vya ndani na nje ya Tanzania ikiwemo Radio One 

Jumamosi, 10 Mei 2025

Rais Mstaafu Dkt. JM Kikwete pamoja na Mkewake wahani msiba wa Hayati Cleopa Msuya.

 


RIAS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete pamoja na Mkewake wahani msiba wa Hayati Cleopa Msuya, Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu nyumbani kwake Upanga Jijini Dar es Salaam leo 10 Mei, 2025.


Dkt. Kikwete ameungana na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa pamoja na waombolezaji wengine.



DINI ZINA MCHANGO MKUBWA KATIKA KUIMARISHA USTAWI WA JAMII


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema madhehebu ya dini yana mchango mkubwa katika kuimarisha ustawi wa jamii na kutoa huduma za kiroho.

 

Amesema kwa kutambua hilo, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wote amekuwa akitekeleza kwa vitendo dhamira ya kukuza ushirikiano kati ya Serikali na madhehebu ya dini.

 

Amesema hayo leo Jumamosi (Mei 10, 2025) alipomuwakilisha Mheshimiwa Dkt. Samia katika kilele cha dua maalum ya kuombea viongozi wa Kitaifa, amani, uchaguzi mkuu pamoja na kuwaombea mamufti na masheikh waliotangulia mbele za haki, kwenye Viwanja vya Msikiti wa Mohammed VI, Kinondoni Dar es Salaam.

 

“Ni ukweli usiopingika sote tumeshuhudia kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jinsi gani anawathamini, anawasilikiza na kuwashirikisha viongozi wa madhehebu ya dini katika masuala muhimu ya kitaifa”.

 


Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amempongeza Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir bin Ali Mbwana kwa kuandaa dua hiyo kwa ajili ya baraka na amani ya Tanzania wakati wa uchaguzi mkuu.

 

“Nikiri kwamba Serikali inatambua umuhimu wa sala na dua. Viongozi tunatekeleza majukumu yetu kwa salama kwa kuwa viongozi wetu wa dini na waumini wote mnatuombea dua. Hii ndiyo sababu Serikali imekuwa ikishirikiana na madhehebu ya dini katika shughuli zake.”


Ameongeza kuwa Serikali inathamini kazi kubwa inayofanywa katika maeneo mbalimbali hususan katika kutoa huduma za kijamii na hivyo kuchangia kasi ya maendeleo ya Taifa letu. “Huduma hizo ni pamoja na zile za elimu, afya, maji, nishati, mafunzo kuhusu kilimo bora na ufugaji, na huduma nyingine mbalimbali.”

 

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya dua hiyo Kitaifa Hajati Mwamtumu Mahiza amesema kuwa dua hiyo ni kwa ajili ya kuwaombea masheikh na Mamufti walioleta mchango chanya katika dini ya kiislamu.

 

Amesema kuwa dua hiyo ambayo imefanyika kwa siku tatu ililenga kuombea viongozi wakuu wa nchi na wote wanaoingia kwenye mchakato wa uchaguzi pamoja na kuombea amani nchini,

 

“Tunahitaji kuwa wanyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu anasema katika Quran kuwa niombeni nami nitawapa, tunataka kuingia kwenye uchaguzi mkuu na kutoka tukiwa salama na wamoja”.

 

Listen Mkisi Radio