JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Jumamosi, 17 Mei 2025

SERIKALI INAFIKIRIA KUJA NA MPANGO WA UUZAJI WA SARAFU ZA DHAHABU KWA WANANCHI


▪️Lengo ni kuwaongezea Watanzania wigo wa uwekaji akiba na uwekezaji kupitia dhahabu


▪️Waziri Mavunde azitaka Taasisi za Fedha kuwawezesha watanzania kimtaji


▪️Afungua Tawi jipya la STANBIC GEITA


▪️Wachimbaji wadogo kukopa fedha isiyozidi 115,000,000 bila dhamana


▪️STANBIC kuja na riba ndogo ya mikopo kwa wachimbaji nchini


*Geita*


Ikiwa ni hatua ya kuwaongezea watanzania wigo wa uwekaji akiba na uwekezaji kupitia ununuzi wa dhahabu, Serikali ipo mbioni kuanzisha uuzaji wa Sarafu ya dhahabu nchini.


Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 17 Mei, 2025 na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb) akiwa Mkoani Geita aliposhiriki katika uzinduzi wa tawi la benki ya Stanbic Geita.


"Mheshimiwa Rais wetu mpendwa *Dkt. Samia S. Hassan* amefanya makubwa katika sekta yetu ya madini, na ndiyo maana tumeweza kuchangia katika pato la Taifa kufikia asilimia 10.1 kwa mwaka 2024, mwaka mmoja kabla ya mwaka 2025 kama ilivyokuwa imeelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi na Mpango wa Maendeleo wa miaka 5.

Wizara kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzanania(BOT) tunajadiliana namna bora  ya uanzishwaji wa Sarafu za dhahabu(𝙜𝙤𝙡𝙙 𝙘𝙤𝙞𝙣𝙨) ili kuongeza umiliki wa dhahabu miongoni mwa wananchi, kuimarisha soko la ndani la dhahabu na mzunguko wa fedha ndani ya nchi yetu.


Hatua hiyo ya uanzishwaji wa uuzaji wa Sarafu ya dhahabu ni sehemu ya maboresho ya mpango wa ununuzi wa dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania ili kufikia malengo tarajiwa ya kuwa na ununuzi wa dhahabu endelevu na wenye tija nchini.


Nawapongeza Benki ya STANBIC kwa kusogeza huduma  rafiki ya kibenki kwa wananchi wa Geita hususani wadau wa madini na hivyo kuzitaka Benki nyingine kuiangalia sekta ya madini kwa upekee ili kuwezesha mitaji kwa watanzania ili washiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, kwani sekta hiyo ina utofauti mkubwa na sekta nyingine za uzalishaji nchini” Alisema Mavunde

Awali, akitoa maelezo kuhusu uanzishwaji wa Tawi hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic, *Bw. Fredrick Maxi* aliishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara na kubainisha kuwa Benki ya Stanbic kwa sasa ina matawi 15 nchini na inaendelea kufungua matawi mengine mengi kwenye maeneo ya uchimbaji ili kuwafikia wadau wengi zaidi kwenye sekta ya madini,na pia Benki inakuja na mpango maalum wa kutoa riba ndogo isiyo ya kibiashara kwa sekta ya madini ili kuchochea shughuli za madini nchini ambapo kwa sasa wachimbaji wadogo wanaweza kuchukua mikopo isiyozidi Tsh 115,000,000 bila kuwa na dhamana.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mh. Martin Shigela aliishukuru benki ya Stanbic kwa kuleta Tawi Mkoani Geita na kusisitiza kwamba, ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwezesha sekta za uzalishaji zinazochochea ukuaji wa biashara na kuzifanya benki za biashara kuchangamkia fursa zinazoendelea kuibuka mkoani hapo na kuwataka wananchi wa Geita kuchangamkia huduma zitolewazo na taasisi hizo za fedha katika kujiimarisha kimtaji.

BIL.2.25/- ZATOLEWA KWA WANUFAIKA WA SHUGHULI ZA UTALII


.....................

Na Mwandishi wetu

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, amekabidhi hundi zenye jumla ya Sh.bilioni 2.25  kwa wanufaika wa shughuli za utalii katika maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Wanufaika wa mgao huo ni pamoja na Jumuiya sita za Hifadhi za Wanyamapori (WMA) ambazo zimepokea Sh.bilioni 1.5, Halmashauri za Wilaya 20 ambazo zimepata jumla ya sh. milioni 368.7, na Halmashauri za Vijiji 25 ambazo zimepokea sh.milioni 385.5.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hundi hizo, Waziri Chana amesema kuwa ni ukweli usiopingika kwamba ongezeko la watalii nchini linaongeza mapato ya Serikali, ambapo sehemu ya mapato hayo yanarejeshwa kwa jamii kupitia migawo iliyoainishwa katika sheria, kanuni na miongozo ya usimamizi wa utalii.

“Miongozo hiyo inaielekeza Serikali kukusanya mapato yatokanayo na shughuli za utalii na kuyaelekeza kwa wanufaika – ambao ni halmashauri za wilaya, vijiji na WMA husika – kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii. Hafla hii ya kugawa mgao ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuzingatia sheria, uwazi na kuwajali wananchi wake,” amesema Waziri Chana.

Ameongeza kuwa fedha hizo zitasaidia utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika maeneo husika, na kutoa wito kwa vijiji, halmashauri, na hata Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kuweka ajenda ya utalii kwenye vikao vyao, ili kuhamasisha uanzishwaji wa WMA zaidi. 

Aidha, Waziri Chana amesisitiza kuwa Wizara kupitia taasisi zake, hususan TAWA, itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha shughuli za utalii na kuhakikisha mgao unaowastahili wanufaika unatolewa kwa mujibu wa sheria.

Amesema serikali inatarajia kuona fedha hizo zinatumika kwa ufanisi na kwa mujibu wa malengo yaliyowekwa – ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za wanyamapori, kukuza utalii na kuongeza mapato katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA.

MAJALIWA: SANAA INAMCHANGO MKUBWA KATIKA KUKUZA UCHUMI


_▪️Awataka wasanii wawekeze zaidi katika sanaa ili kuongeza wigo wa ajira_

 


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema sekta ya utamaduni na Sanaa ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wasanii na Taifa, kuongeza fursa za ajira, kurasimisha kazi za sekta sambamba na kuimarisha maadili ya jamii.


Waziri Mkuu ametoa wito kwa wasanii nchini waweke kipaumbele cha kuwekeza mapato yatokanayo na kazi zao katika shughuli za mnyororo wa thamani wa sanaa ili kuongeza wigo wa kuajiri vijana katika sekta hiyo na kuongeza pato la Taifa.

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Mei 17, 2025) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Pili wa Wadau wa Utamaduni na Sanaa uliofanyika kwenye Ukumbi wa Millenium Tower jijini Dar es Salaam. Amesema sekta hizo zimeajiri makundi yote jumuishi yakiwemo ya watu wenye ulemavu, vijana, wazee na watoto kwa jinsia na hali tofauti na watu wote.


Waziri Mkuu amesema zaidi ya hayo, sekta hiyo inakuza ujasiriamali na biashara ndogondogo na za kati. ”Sote tumewashuhudia wasanii wakianzisha biashara, kuzirasimisha na kuziweka katika mfumo unaotambuliwa na mabenki ili  kuzitumia kama dhamana kwenye taasisi za kifedha ili kupata mitaji kwa shughuli mbalimbali.”


Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wasanii wote nchini wajitahidi kutengeneza kazi bora zaidi na kurasimisha shughuli zao za sanaa katika mamlaka husika za binafsi na Serikali ili kila msanii awe rasmi na aweze kunufaika na fursa zilizopo.

Amesema Sekta za Utamaduni na Sanaa inatoa mchango mkubwa katika uchumi kote ulimwenguni, ambapo Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) ya mwaka 2022, imebainisha kuwa sekta hizo zilichangia asilimia 3.1 ya Pato la Dunia (GDP), huku ikitoa asilimia 6.2 ya ajira sawa na ajira milioni 50 duniani kote.


Waziri Mkuu amesema kwa kutambua umuhimu wa sekta za utamaduni na sanaa, Serikali imefanya jitihada mahsusi za kuendeleza sekta hizo.  Jitihada hizo ni pamoja na kuimarisha mifumo kisera na rasilimalifedha kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kisekta.

Pia, Waziri Mkuu amesema sambamba na kutunga sera, Serikali imetunga sheria na kanuni zilizoleta mageuzi ya shughuli za utamaduni na sanaa. ”Mifumo hiyo ya kisheria, imewezesha shughuli za utamaduni na sanaa kuondoka kwenye dhana ya kuwa burudani pekee na kuwa ajira rasmi zinazochangia kukuza pato kwa mtu binafsi na Taifa.


Amesema hatua hiyo kwa upande mwingine ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 Ibara ya 241 inayoielekeza serikali kuboresha tasnia ya sanaa nchini ili kuiendesha kibiashara  na  kuongeza upatikanaji wa fursa zaidi za ajira kwa makundi yote ya jamii.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi amesema Mkutano huo ni wa pili katika mfululizo wa mikutano ya wadau wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania inayolenga kuwakutanisha ili kubadilishana uzoefu, kujadili mafanikio na changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana nazo.


Akizungumzia kuhusu mahitaji ya mikopo kwa wasanii amesema ni makubwa kuliko mtaji walionao na kwa upande mwingine wadau wanaomba kiasi cha juu cha mkopo kinachotolewa cha shilingi milioni 100 kiongezwe mara dufu ili kiendane na uhalisia wa uwekezaji kisekta.


“Tumetoa mikopo yenye masharti nafuu kwa zaidi ya miradi 580 ya wasanii, hii inaonesha kwamba Serikali imedhamiria katika kuiinua sekta ya Utamaduni na Sanaa kama kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Hadi sasa tumefanikisha marejesho kwa asilimia 96 hadi sasa, jambo ambalo linaonesha uwajibikaji wa wanufaika.”


Amesema wakati wizara inaendelea na jitihada za kutafuta vyanzo vingine endelevu vya fedha, wanamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za makusudi za kuhakikisha bajeti ya Mfuko wa Utamaduni inaongezeka kila mwaka ambapo katika mwaka wa fedha 2025/2026 imefikia sh bilioni nne kutoka shilingi bilioni 1.6 mwaka 2023/2024.

RAIS MWINYI:TUWAOMBEE MAHUJAJI NA KUIOMBEA NCHI AMANI


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewaaga rasmi Mahujaji wa Zanzibar wanaotarajiwa kuelekea katika miji mitakatifu ya Makka na Madina mwaka huu kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hija huku akiwaasa kushikamana na mafunzo ya dini na kuiombea nchi amani, mshikamano na maendeleo zaidi.


Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika hafla maalum ya kuwaaga Mahujaji hao iliyofanyika katika Msikiti wa Jamii Zinjibar, Mazizini, Mkoa wa Mjini Magharibi, leo tarehe 17 Mei 2025.

Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana kwa karibu na Umoja wa Taasisi za Hija Zanzibar (UTAHIZA) pamoja na Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana ili kuondoa changamoto zinazowakabili Mahujaji na kuhakikisha utekelezaji mzuri wa ibada hiyo tukufu.


Vilevile, Alhaj Dkt. Mwinyi amethibitisha kupokea risala ya UTAHIZA kuhusu changamoto kadhaa, ikiwemo ucheleweshaji wa michango ya Mahujaji, haja ya eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya UTAHIZA, na pendekezo la kuanzisha Mifuko Maalum ya Hija. Ameahidi kuwa Serikali italifanyia kazi suala hilo. 

Katika hatua nyingine, Alhaj Dkt. Mwinyi ametoa shukrani maalum kwa Shirika la Ndege la Saudi Arabia kwa kuridhia ombi la kuwa na safari za moja kwa moja kwa Mahujaji wa Zanzibar, sambamba na pongezi kwa Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia kwa mchango wao katika kufanikisha utaratibu huo.


Halikadhalika Alhaj Dkt. Mwinyi amewataka Waislamu wote kuwaombea Mahujaji na kuiombea nchi amani, umoja na maendeleo, akibainisha kuwa mafanikio ya taifa letu yanahitaji mshikamano wa kila mmoja.

KIKWETE AKUTANA NA BALOZI WA USWISI, WAWEKA MIKAKATI USHIRIKIANO ZAIDI NA UKUZAJI UJUZI KWA VIJANA.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Nicole Providoli, jijini Dar es Salaam leo Mei 16, 2025 ambaye alifika kujitambulisha.

Katika kikao hicho, Mhe. Kikwete amesema kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa Serikali ya Uswisi kupitia shirika la Swiss Aid kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, maendeleo ya jamii pamoja na masuala ya ukuzaji ujuzi kwa vijana.


Aidha, Waziri Kikwete amepongeza ubalozi wa Uswisi kwa mchango wake katika kufanikisha kukamilika Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana (2007), Toleo la Mwaka 2024 ambayo inatoa mwongozo kwa vijana na wadau wengine kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. 

Kwa upande wake, Balozi wa Uswisi hapa nchini, Mhe. Nicole Providoli amesema kuwa Uswisi itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili Sera hiyo mpya ya vijana toleo la 2024 inawafikia vijana wengi.

TANZANIA NA FINLAND KUSHIRIKIANA KATIKA DIPLOMASIA YA UCHUMI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Finland zimeazimia kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kupitia sekta za kimkakati kama vile nishati, biashara na uwekezaji, ili kukuza diplomasia ya uchumi.


Azma hiyo imefikiwa katika kikao cha pamoja kilichofanyika  katika Ofisi Ndogo ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam, kikihusisha viongozi waandamizi kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Naibu Waziri wa Biashara za Kimataifa wa Finland, Mhe. Jarno Syrjälä.


Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, amesema Tanzania inaendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kushirikiana na mataifa rafiki kama Finland, kwa lengo la kufungua fursa zaidi za maendeleo. Amesisitiza kuwa ushirikiano huo una mchango mkubwa katika kuleta teknolojia, mitaji, na ujuzi unaoweza kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.


Kwa upande wake, Mhe. Syrjälä amepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia wawekezaji wa kimataifa. Amesema Finland iko tayari kushirikiana na Tanzania katika maeneo yenye maslahi kwa pande zote, hususan nishati jadidifu, teknolojia ya kisasa na elimu ya ufundi stadi.


Katika kikao hicho, ujumbe wa Tanzania uliwasilisha vipaumbele vya Serikali katika kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda, kilimo, nishati na utalii. Pia, ujumbe huo umetoa wito kwa wawekezaji kutoka Finland kutumia fursa zilizopo kuwekeza nchini. 


Ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho ulijumuisha viongozi na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

 

RAIS MWINYI AZINDUA VIWANJA VYA MAISARA COMPLEX


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameiagiza Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kutafuta wawekezaji wazuri watakaoviendesha viwanja vya michezo kwa ubora na ufanisi.


Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipovizindua rasmi Viwanja vya Michezo vya Maisara Sports Complex vilivyopo Maisara, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 16 Mei 2025.

Aidha, amesema kuwa Zanzibar sasa haina sababu tena ya kushindwa kuendesha michezo yoyote kutokana na ukosefu wa viwanja, kwani tayari viwanja vya kisasa na vya kutosha vimejengwa vyenye michezo mchanganyiko 10, ikiwemo: viwanja viwili vya tenisi, viwili vya mchezo wa padel, viwili vya mpira wa miguu, na vinne vya michezo mchanganyiko kama mpira wa kikapu, mpira wa mikono, pete na wavu.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi ameagiza viwanja hivyo vitunzwe ipasavyo ili vibaki katika ubora wake wakati wote na viweze kutumika kwa muda mrefu.

Viwanja vya Maisara Sports Complex vimejengwa na fedha za Serikali kupitia kampuni ya Reform Sports kutoka Uturuki kwa gharama ya Shilingi Bilioni 7. 

Uzinduzi huo uliambatana na mechi ya kirafiki iliyochezwa viwanjani hapo kati ya Ramsquad na Miembeni, ambapo Miembeni iliibuka mshindi kwa magoli ya penati  5-3.

Ijumaa, 16 Mei 2025

SERIKALI YAJIZATITI KUDHIBITI MUINGILIANO KATI YA BINADAMU NA WANYAMAPORI


Na Sixmund Begashe


Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Kitaifa wa kutatua changamoto za muingiliano kati ya binadamu na wanyamapori kwa kutoa mafunzo maalum kwa Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza wakati wa kufunga Kozi Maalum Na. 22/2025 ya VGS katika Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii – Likuyu Sekamaganga, mkoani Ruvuma, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi (ACC), Hadija Malongo, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuongeza ushiriki wa jamii katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kwa kushirikiana na Jeshi la Uhifadhi.

“Ni matumaini yangu kuwa mbinu mlizojifunza mtazitumia kwa weledi mkubwa katika maeneo yenu. Tunahitaji askari waaminifu na waadilifu watakaosaidia kulinda maisha ya wananchi, mali zao na rasilimali za taifa,” amesema Kamishna Malongo.

Aidha, amepongeza chuo hicho kwa mchango wake mkubwa katika kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za maliasili, na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kukiunga mkono ili kiweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo, ACC Japhary Lyimo, amesema kuwa wahitimu wamepata stadi mbalimbali zikiwemo za usimamizi wa rasilimali, mwitikio wa haraka kwa changamoto za wanyamapori, pamoja na ulinzi wa chakula, watu na mali katika maeneo ya vijijini.

Listen Mkisi Radio