JSON Variables

Saturday, April 26, 2025

RAIS MWINYI:SMZ ITAHAKIKISHA MUUNGANO UNAENDELEA KUIMARIKA.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt, Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi Kuendelea kutoa Ushirikiano  Kuhakikisha Muungano  unaimarika  kufikia dhamira ya Waasisi  wake  ya kudumisha Uhuru,Umoja na Mshikamano wa Watanzania. 


Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo   katika hafla ya Kutunuku Nishani za Kumbukumbu ya Muungano ilioambatana na  Uzinduzi wa Kitabu cha MWALIMU JULIUS NYERERE PHOTOGRAPHIC JOURNEY cha  Historia ya Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  uliofanyika Ikulu  ya Chamwino, Dodoma.

Ameeleza kuwa Watanzania Wana kila sababu ya kudumisha Muungano kwani ni Tunu ya Taifa  ya kujifaharisha nayo na ni kielelezo cha Muungano wa Mafanikio Barani Afrika.


Rais Dkt,Mwinyi  amesema Waasisi Mwalimu Julius Nyerere na   Mzee Abeid  Karume walikuwa na dhamira thabiti ya kuwaunganisha Watanzania Kisiasa,Kiuchumi na Kijamii kwa faida ya Vizazi vya sasa na Vijavyo Jambo linalopaswa kudumishwa na kila Mtanzania.

Halikadhalika Rais Dkt , Mwinyi amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa Juhudi anazozitekeleza za kumaliza Changamoto za Muungano kupitia Vikao  vya Majadiliano  hadi kubakia  Changamoto Tatu  hivi sasa Miongoni mwa  25 zilizokuwepo awali.



Aidha amesema Kitabu hicho kitawasaidia Watanzania waliozaliwa Baada ya Muungano  Kujifunza na kumtambua Muasisi Huyo wa Muungano na faida  ya Muungano huo tangu Kuasisiwa kwake Miaka 61iliyopita.

Kwa upande mwingine Rais Dkt, Mwinyi ameipongeza Kazi nzuri iliofanywa na Watunzi wa Kitabu hicho ilioonesha kuthamini Mchango wa  Baba wa Taifa na kutoa Rai ya kuchapishwa kwa wingi kopi za Kitabu hicho na kupatikana katika Maktaba Kuu zote hapa Nchini pamoja na  kwenye Mitandao ya Kijamii.

Kitabu hicho kimezinduliwa wakati Watanzania wanaadhimisha Miaka 61 ya Mafanikio ya Muungano wa Tanzania.

TFS YATUMIA MKUTANO WA UN TOURISM KUINUA UTALII WA IKOLOJIA KUPITIA VYAKULA ASILIA

 

Arusha, Aprili 2025 – Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendeleza juhudi zake za kukuza utalii wa kiikolojia kupitia vyakula asilia vinavyotokana na misitu ya Tanzania, katika mkutano wa UN Tourism on Gastronomy for Africa unaoendelea jijini Arusha.


Katika mkutano huo, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, na Mwenyekiti wa Bodi ya TFS, Meja Jenerali Dkt.Mbaraka Naziad Mkeremy, walifanya mazungumzo ya kimkakati na wadau mbalimbali kuhusu mchango wa misitu katika kutoa ladha halisi ya utamaduni wa wenyeji kwa watalii.


Prof. Silayo alisema kuwa misitu ya Tanzania siyo tu chanzo cha rasilimali za kiuchumi, bali pia hazina ya vyakula asilia na mimea ya dawa vinavyoweza kuendelezwa kama vivutio muhimu vya utalii wa chakula (gastronomy tourism).

“Tunatambua kuwa mapishi ya jadi, uyoga wa misitu, mimea ya dawa, na mazao mengine ya asili vinatoa fursa ya kipekee kwa watalii wanaotafuta uzoefu wa kiutamaduni na ikolojia,” alisema Prof. Silayo.


Kupitia ushirikiano na jamii zinazozunguka misitu, TFS inalenga kuhakikisha kuwa utalii wa chakula unachangia moja kwa moja katika uhifadhi wa mazingira, kuongeza kipato cha wananchi, na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii endelevu nchini.


Meja Jenerali Dkt.Mbaraka Naziad Mkeremy alisisitiza kuwa mafanikio ya kukuza utalii wa gastronomy yanategemea matumizi endelevu ya rasilimali za misitu na mafunzo kwa jamii kuhusu thamani ya vyakula vya asili.


Mkutano huo wa UN Tourism umewakutanisha wadau kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika, ukilenga kuibua mbinu bora za kuendeleza utalii wa chakula kama njia ya kuongeza thamani ya utalii na kuinua uchumi wa jamii zinazohifadhi mazingira..

MAKAMU WA RAIS MH.DKT.PHILIP MPANGO AMESEMA NAMNA NZURI YA KUMUENZI ALIYEKUWA KIONGOZI WA KANISA KATOLIKI DUNIANI.

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema namna bora ya kumuenzi aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani hayati. Baba Mtakatifu Francisko ni kudumisha amani pamoja na kujali masikini.

 

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa mazungumzo mara baada ya kumalizika kwa Misa ya Mazishi ya aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani hayati. Baba Mtakatifu Francisko iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro - Vatican. Amesema Papa Francisko alikuwa mnyenyekevu na mtu aliyefanya jitihada kubwa za utafutaji amani maeneo mbalimbali duniani na kuacha alama ikiwemo tukio la kuwabusu miguu viongozi wa Sudan ili waweze kuachana na mapigano.

 

Makamu wa Rais amesema kati ya nyaraka za mwisho alizosaini hayati Papa Francisko ni pamoja na barua aliyomwandikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumtakia heri ya siku njema ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

 

Katika Misa hiyo ya Mazishi, Makamu wa Rais ameongozana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania Vatican Mhe. Balozi Hassan Mwameta pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi. Swahiba Mndeme.

 

Misa ya Mazishi ya Papa Francisko imehudhuriwa na zaidi ya watu 250,000 ikiwemo viongozi wakuu kutoka mataifa mbalimbali duniani. Maziko ya Papa Francisko yamefanyika katika Basilika ya Santa Maria Maggiore leo tarehe 26 Aprili 2025.

 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

26 Aprili 2025

Vatican.

SEKTA YA UTALII TANZANIA KIVUTIO MAONESHO YA EXPO 2025 JAPAN

 


Na Hamis Dambaya, Osaka-Japan

Tanzania imeendelea kuvutia watazamaji wengi wa kimataifa katika maonesho ya Expo 2025 yaliyoanza tarehe 13 aprili, 2025 katika Jiji la Osaka nchini Japan.

Katika maonesho hayo Mkurugenzi wa Masoko kutoka Bodi ya Utalii Tanzania Bwana Ernest Mwamwaja amesema kuwa tangu wiki ya utalii iliponza banda la Tanzania limekuwa limekuwa kivutio na kupokea wageni wengi wanaotembelea na kutaka kujua fursa vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji kwenye maeneo ya utalii yaliyopo Tanzania.

Bwana Mwamwaja amesema kuwa Tanzania itatumia maonesho hayo makubwa duniani pamoja na kupokea watembeleaji na kuwapa maelezo kuhusu fursa zilizopo Tanzania na kushiriki mijadala ya kimkakati yenye lengo la kuvutia wageni kutembelea Tanzania.

Amesema kuwa Tanzania imekuwa ikitumia fursa ya Maonesho hayo ya kimataifa kuelezea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo kama mbuga za Wanyama zikiwepo Ngorongoro, Serengeti,Manyara, Mikumi, Mlima Kilimanjaro na maeneo ya fukwe ikiwemo  zilizopo Zanzibar.

Kwa upande wake Afisa Utalii Mkuu,masoko kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bwana Michael Makombe amesema watembeleaji wengi katika maonesho hayo wamekuwa wakijifunza kuhusu namna Tanzania ilivyofanikiwa kuimarisha uhifadhi wa wanyama pori.

Maonesho ya mwaka huu yanakadiriwa kutembelewa na watazamaji zaidi ya milioni 26 yakihusisha waoneshaji kutoka mataifa mbalimbali duniani.

JOWUTA NA THRDC WALAANI VIKALI KUKAMATWA NA KUPIGWA KWA WAANDISHI WA HABARI

 


NA MWANDISHI WETU, MBEYA

CHAMA cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu nchini (THRDC) wamelaani kuanza kuibuka matukio ya waandishi wa habari na watangazaji kukamatwa na baadhi kupigwa na hata kuharibiwa vifaa vyao vya kazi na vyombo vya dola.


Kauli ya kulaani imetolewa leo Aprili 25 mwaka huu na Mwenyekiti wa JOWUTA Mussa Juma leo mkoani Mbeya, wakati wa mafunzo kwa wanahabari kuhusu uandishi wa habari za uchaguzi, ulinzi na usalama kazini.


Mafunzo hayo yamehusisha waandishi kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe, ambapo Juma amesema matukio ya kukamatwa, kupigwa na kuharibiwa vitendea kazi hayakubaliki katika nchi inayojinadi kuwa inazingatia misingi ya kidemokrasia.


Juma amesema katika siku za karibuni, kumeanza kutokea matukio ya baadhi ya wanahabari kukamatwa na vyombo vya dola, kupigwa na wengine kuzuiwa kufanyakazi, jambo ambalo sio sahihi.


Mwenyekiti huyo, amesema mahusiano mazuri baina ya vyombo vya dola na wanahabari, yalikuwa yameimarishwa katika siku za nyuma lakini sasa yanaanza kuharibika jambo ambalo halipaswi kuvumiliwa.


“Kama mwanahabari amekiuka taratibu zozote kuna utaratibu wa kufuata kisheria, badala ya kutumika nguvu kumkamata ama kumzuia kufanyakazi yake”amesema.


Hata hivyo, Juma amewataka wanahabari nchini, kufanyakazi kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa Habari, hasa kipindi hiki cha harakati za uchaguzi mkuu, ikiwepo kutoandika habari za upendeleo kwa chama chochote za siasa, kuacha kuwa washabiki wa vyama na watowe fursa sawa kwa vyama vyote.


“Msimamo wa JOWUTA kama mwanahabari unataka kujihusisha na masuala ya siasa ni bora kujiweka kando mapema na tasnia ya habari hadi chaguzi zipite, badala ya kutumia chombo chako cha habari kwa maslahi binafsi ya kisiasa”amesema.


Awali,Wakili Jones Sendodo wa kutoka THRDC, amesema mtandao huo unaungana na wadau wote kulaani matukio yoyote ya kunyanyaswa, kupigwa ama kuharibiwa vitendea kazi mtetezi wa haki za binaadamu, wakiwepo wanahabari.


Wakili Sendodo amesema ni vyema vyombo vya dola kuzingatia sheria za nchi wakati wa kutekeleza wajibu wao.


“Tunapinga matukio ambayo yanaendelea kwa vyombo vya dola kutumia nguvu kubwa kuwanyanyasa watetezi wa haki za binaadamu na sisi kama THRDC kwa kushirikiana na wadau wengine tutaendelea kuwatetea na kuwapa msaada wa kisheria, msaada wa ushauri wa kisaikolojia na hata makazi salama ya muda watetezi wa haki za binaadamu wakiwepo wanahabari wanapokabiliwa na majanga ama vitisho”amesema.


Wakili Sendodo pia akitoa mada katika mafunzo hayo ya uchaguzi kwa wanahabari, aliwataka kujua sheria mbalimbali ambazo zinawahusu ili kujitahidi kutozivunja, ikiwepo Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Takwimu, Sheria za Uchaguzi na nyingine.


Hata hivyo, alitaka wanahabari kujali usalama wao wakiwa kazini na kuchukuwa tahadhari mbali mbali ili kuhakikisha wakati wote wanabaki salama, wakati wakitekeleza wajibu wao.


Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya aliwataka wanahabari nchini, kuendelea kujiunga na JOWUTA kwani ndio chama pekee kinachotambulika kisheria kutetea maslahi ya wafanyakazi katika vyombo vya habari na mazingira bora ya kazi.


"Tumekuja kuwapa elimu ya uchaguzi, lakini pia nitumie nafasi hii kuwaomba wafanyakazi wa vyombo vya habari mjiunge JOWUTA, ili tuwe na nguvu moja ya kupigania maslahi yetu," amesema.


JOWUTA inaendelea na kutoa mafunzo kwa wanahabari nchini kuhusiana na kuripoti vyema uchaguzi mkuu mwaka huu na kubaki salama, mafunzo hayo yamedhaminiwa na Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ),  Shirikisho la Waandishi wa Habari Afrika (FAJ),THRDC, Taasisi wa Wanahabari ya Kusaidia Jamii za Pembezoni (MAIPAC) na JOWUTA


TANZANIA GOSPEL MUSIC AWARDS KUFANYIKA MEI 23, 2025

 

 Walioingia kwenye kinyang'anyiro wawekwa hadharani.


NA MWANDISHI WETU 

TUZO za Muziki wa Injili Tanzania (Tanzania Gospel Music Awards (TGMA)) zinatarajia kufikia kilele Mei 23, 2025 kwa utoaji wa Tuzo na fedha kwa washindi katia hafla itakayofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Hayo yamebainishwa jana Aprili 25, 2025 na  Msemaji wa Kamati ya Maandalizi ya Tuzo hizo Mchungaji Haris Kapiga akizungumza na waandishi wa habari wakati akibainisha watu walioingia kwenye kinyang'anyiro cha tuzo hizo zenye vipemgele 20.

Mchungaji Kapiga amesema kuwa mchakato wa Tuzo hizo ulianza tangu Novemba Mwaka jana kwa kufungua dirisha la kila Msanii wa Muziki wa Injili kuwasilisha kwa hiari yake nyimbo zake anazotaka ziingie kwenye kinyang'anyiro hicho huku sharti likiwa ni lazima nyimbo hizo ziwe ni za Mwaka Jana.

"Tuliwaomba watu wawasilishe kazi zao wenyewe kwa vipemgele wanavyoona vinawafaa wao, kazi ya TGMA ni kuwatia moyo watu wenye vipawa ambavyo Mungu amewapatia," amesema Mchungaji Kapiga.

Mchungaji Kapiga ameeleza kuwa jumla ya kazi 529 zilipokelewa ambapo wahusika walipigiwa kura na kupatikana watu watano kwa kila kipemgele na kwamba hatua inayofuata wataendelea kupigiwa kura na kubakia watu watatu kwa kila kipengelea ambapo washindi watapatikana siku ya kilele cha tuzo hizo.

Ametaja vipemgele vya tuzo hizo kuwa ni pamoja na wimbo Bora wa kuabudu wa Mwanamuziki wa Injili wa Mwaka, wimbo Bora wa Muziki wa Sifa, Wimbo Bora wa Muziki wa Injili wa Mwaka na Wimbo Bora wa Injili wa Mwaka kwa wanamuziki wa nje ya Nchi.

Vipengele vingine ni Msanii Bora wa Muziki wa Injili wa Mwaka, Msanii Chipukizi wa Muziki wa Injili, Mwimbaji Bora wa kiume wa Muziki wa Injili wa Mwaka, na Mwimbaji Bora wa Kike wa Muziki wa Injili wa Mwaka.

Akiendelea kutaja vipengele vingine Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Tuzo hizo Nina Mbura, amesema ni Kwaya/bendi bora ya Muziki wa Injili ya Mwaka, Video Bora ya Muziki wa Injili, Mtayarishaji Bora wa Video ya Muziki wa Injili wa Nota na mtunzi Bora wa Muziki wa Injili wa Mwaka.

Vingine ni Mwandaaji Bora wa Muziki wa Injili wa Mwaka, Mtayarishaji wa bora wa Muziki wa Injili wa Mwaka, Kiongozi wa Miziki wa Injila wa Mwaka, ushirikiano wa bora wa Muziki wa Mwaka na tuzo ya heshima Kwa mtu mwenye mchango mkubwa kwenye ukuaji wa Tasnia ya Muziki wa Injili nchini.

Baadhi ya wasanii wanaowania tuzo hizo ni Paul Clement, Water Chilambo, Japheth Zabron wa Zabron Singers, Joel Lwaga, Rehema Simfukwe, Zabron Singers na kadhalika. 

Hata hivyo Mchungaji Kapiga amebainisha kuwa hadi sasa maandalizi ya hafla hiyo yamefikia asilimia 80.

RECAP : WASIRA AMTAHADHARISHA MARTHA KARUA WA KENYA KUJIPIMA UBAVU NA CCM

 

Amesema kama anajiona anaweza kutatua migogoro aende nchi nyingine za Afrika


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amemjia juu Mwanasheria maarufu na mwanasiasa wa nchini Kenya Martha Karua,  ambaye amekuja nchini kumtetea Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu,  anayekabiliwa na tuhuma za uhaini na kuchapisha picha za uongo mtandaoni.

Wasira amemtaka mwanasheria huyo kuacha kujipima uzito na Chama Cha Mapinduzi huku akimwambia pia kuwa Chama kinaheshimu mamlaka ya Mahakama na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).

Amesisitiza kama Karua anajiona anaweza kushughulika na migoro basi atatue matatizo yaliyoko nchini kwake au mgogoro unaoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Congo (DRC). 

Akizungumza mbele ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma Leo Aprili 25, 2025 , akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuelezea faida za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Wasira alitumia nafasi hiyo kumjibu Karua hatua kwa hatua na kumtaka aache kuingilia mambo asiyoyajua vizuri.

“Tanzania hatuvurugi amani ya Afrika Mashariki isipokuwa tunaendesha mambo yetu kwa amani na salamu ninazompatia Mwanasheria Martha Karua ni kwamba aache kujipima na CCM, CCM ni chama kikubwa Afrika kinachoanza na nyumba kumi," alisema.

Aliongeza kuwa "CCM haina hofu na chama chochote lakini hatuwezi kuingilia kazi ya Mahakama na hatuwezi kuingilia shughuli za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuwa ni vyombo vyenye mamlaka, lakini kama ni mjuzi ashughulike na mambo ya Kenya."


"Akishindwa arudi nyumbani akaendeshe chama chake ambacho sera zake hazijulikani. Atuache Tanzania tuchaguane kwa utaratibu wetu hata mwenyewe na zungumza hapa nilichaguliwa kwa kishindo katika nafasi hii ndani ya Chama, naamini dozi hii inamtosha," amesema 

Wakati Wasira anamjibu mwanasheria huyo wa Kenya alisema Chama kinamheshimu kwa kuwa ni mtu wa Afrika Mashariki, pia kinaheshimu taaluma yake ya sheria.

Martha ni Mwenyekiti  wa Chama cha People’s Liberation Party (PLP) cha Kenya.

“Anahaki kama mwanasheria kama ameitwa na watu wanaoshtakiwa, sasa pale kuna 'katatizo' tuna Polisi, Mahakama na Tundu Lissu. Sasa Polisi wakikukuta umekosea hawaendi kwa Wasira kusema kwamba umekosea wao wamesomeshwa kujua kama umekosea, wakikuchukua hawaruhusiwi kukaa na wewe muda mrefu.

TFS LINDI YAGAWA MICHE 300 YA MATUNDA NA MBAO KUCHOCHEA MAPINDUZI YA LISHE BORA NA UHIFADHI MAZINGIRA

 

TFS Lindi Yagawa Miche 300 ya Matunda na Mbao, Yachochea Mapinduzi ya Lishe Bora na Uhifadhi Mazingira


Lindi – Katika kuadhimisha Miaka 61 ya Muungano wa Tanzania, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Ofisi ya Mkoa wa Lindi, imeshiriki kikamilifu katika sherehe hizo kwa kugawa miche 300 ya miti ya mbao, matunda na kivuli kwa wananchi.

Shughuli hiyo imefanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Nyengedi, iliyopo katika Halmashauri ya Mtama, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mheshimiwa Victoria Mwanziva, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi.


Akizungumza wakati wa hafla hiyo mapema leo, Mheshimiwa Mwanziva aliipongeza TFS kwa juhudi kubwa katika kuhifadhi mazingira kupitia upandaji wa miti, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu muhimu ya kutunza rasilimali za taifa na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tuna kila sababu ya kuunga mkono juhudi hizi, kwani miti inabeba uhai wa Taifa letu. Tuipokee na kuitunza miche hii ili iwe urithi wa kizazi kijacho. Zoezi hili pia linaunga mkono kaulimbiu ya kitaifa kuhusu lishe bora kupitia upandaji wa miche ya matunda, hivyo kusaidia kuboresha afya za wananchi wetu,” alisema Mwanziva.


Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Rondo, PCO John Olomi, aliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na TFS katika juhudi za kulinda mazingira, huku akieleza utaratibu wa upatikanaji wa miche kutoka kwa Wakala huo.

“TFS itaendelea kutoa elimu ya mazingira na kuhamasisha upandaji wa miti kwa maendeleo endelevu. Wananchi wote wanakaribishwa kutembelea bustani zetu za miche na kujipatia miche bure kwa ajili ya kupanda kwenye maeneo yao binafsi, mashamba madogo, shule na taasisi mbalimbali,” alisema Olomi.


Aidha, alifafanua kuwa, “Kwa wakulima na wananchi wa kawaida, miche ya miti hutolewa bila malipo. Hata hivyo, kwa wale wanaohitaji miche kwa ajili ya mashamba ya miti ya kibiashara, mche mmoja huuza kwa bei ya serikali ya Shilingi 500 hadi 600.”

Akibainisha zaidi utaratibu wa maombi, Mhifadhi Olomi alisema kuwa, “Mahitaji ya miche kwa mwananchi mmoja mmoja hutumwa kwa kupitia uongozi wa vijiji vyao, ambao hufanya majumuisho ya maombi yote na kuyawasilisha kwa Meneja wa Wilaya au Meneja wa Shamba husika. Utaratibu huu umewekwa mahsusi kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji sahihi wa taarifa na ufuatiliaji wa matumizi ya miche inayotolewa.”


“Tunawakaribisha wote kutumia fursa hii kuanzisha mashamba au bustani za miti, kwa ajili ya kuhifadhi mazingira na kuongeza kipato kupitia kilimo cha miti na mazao ya matunda,” alisisitiza Mhifadhi Olomi.


Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ilikuwa:

“Muungano Wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa – Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025,” ikisisitiza mshikamano, amani na umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia.


TFS inaendelea kuhamasisha wananchi kuwa sehemu ya juhudi za kitaifa za kulinda na kuhifadhi misitu na mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.