Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza na viongozi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake wakati wa kikao cha tathmini ya utendaji kazi wa Wizara hizo na Taasisi kilichofanyka tarehe 03 Mei, 2025 Jijini Dodoma. Kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhadisi Felchesmi Mramba.
Jumatano, 4 Juni 2025
UTENDAJI KAZI WA WIZARA YA NISHATI NA TAASISI ZAKE WAIMARIKA KWA ZAIDI YA ASILIMIA 95
VITONGOJI 284 ARUMERU MASHARIKI VYAFIKIWA NA UMEME
π Ni kati ya Vitongoji 330 vya Jimbo la Arumeru Mashariki.
πKapinga asema upelekaji umeme unafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imevifikishia huduma ya umeme Vitongoji 284 katika Jimbo la Arumeru Mashariki kati ya Vitongoji 330.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Juni 03, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Arumeru Mashariki, Mhe. Dkt. John Danielson Pallangyo aliyeuliza ni lini Serikali itakamilisha kusambaza umeme wa REA katika Vitongoji 37 ambavyo vipo gizani katika Jimbo la Arumeru Mashariki.
"Mheshimiwa Mwenyekiti, Vitongoji 17 vipo katika hatua ya utekelezaji kupitia Mradi wa Ujazilizi (Densification IIB) na mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji Awamu ya Pili A (HEP IIA), aidha, katika Vitongoji 29 zabuni imetangazwa ili kupata Wakandarasi wa kutekeleza miradi kupitia mradi wa kupeleka umeme Vitongojini Awamu ya Pili B (HEP IIB).
Amesema kukamilika kwa miradi hiyo, kutawezesha vitongoji vyote vya Jimbo la Arumeru Mashariki kufikiwa na umeme.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Arumeru Mashariki, Mhe. Dkt.John Danielson Pallangyo aliyeuliza kuhusu Kata za Arumeru Mashariki zinazo pata maji kutoka msitu wa mlima Arumeru na kuwa na flouride ambapo Kampuni ya Kweka imejitolea kuweka mtambo wa kusafisha lakini kinachohitajika ni umeme, Mhe. Kapinga amesema tayari Serikali imetenga fedha katika mwaka ujao wa fedha kukipelekea umeme wa uhakika Kitongoji cha Seneto Kata ya Legeruki kwa ajili ya kutibu flouride katika maji.
Akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini, Mhe. Profesa Patrick Alois Ndakidemi aliyeuliza Serikali itakiunganishia lini umeme Kitongoji cha Orera kilichopo Kijiji cha Mweka, Mhe. Kapinga amesema katika Jimbo la Moshi Vijijini yupo Mkandarasi anayetekeleza miradi ya kupeleka umeme kwenye Vitongoji 15 vya kila Mbunge na kuongeza kuwa kitongoji hicho kipo katika orodha hiyo ya Mkandarasi.
Akijibu swali la Mbunge wa Kondoa Mjini, Mhe. Ally Makoa aliyeuliza Serikali itapeleka lini umeme kwenye mitaa ya Mongoroma, Chandimo na Hachi, Mhe. Kapinga amesema Serikali imeipelekea umeme mitaa ya Kondoa Mjini ambapo imebaki mitaa hiyo mitatu na kuongeza kuwa itatengwa fedha katika bajeti ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuifikishia mitaa hiyo umeme.
Mhe. Kapinga ameongeza kuwa upelekaji wa umeme unafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha na bajeti ambayo imetengwa.
Akijibu swali la Mbunge wa Mwibara, Mhe. Charles Kajage aliyeuliza kuhusu lini Serikali itavipelekea umeme Vitongoji vya Jimbo la Mwibara ambavyo havina umeme, Mhe. Kapinga amesema Jimbo la Mwibara lina miradi ya Vitongoji ambayo inaendelea kutekelezwa.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Rita Kabati aliyeuliza kauli ya Serikali kuhusu uwepo wa nguzo Kata ya Ilula Wilaya ya Kilolo toka mwezi wa 11 mwaka jana na hadi leo umeme haujawaka, Mhe. Kapinga amesema hadi kufikia mwezi wa saba eneo hilo litakuwa limefikiwa na huduma ya umeme.
Jumatatu, 2 Juni 2025
WAZIRI AWESO ATAKA WANANCHI WALINDE VYANZO VYA MAJI
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amewataka wananchi kulinda mazingira ya vyanzo vya maji kwa kuacha kukata miti ovyo na kufanya shughuli za kibinadamu ili kuepuka ukame.
Ametoa wito huo mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo Juni 2, 2025 yanayoendelea kwenye Viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Mhe. Aweso amesema kuwa uwepo kwa rasilimali za maji toshevleu ni usalama wa taifa kwakuwa uwepo wa maji ni uhakika wa chakula, nishati ya umeme pamoja na mipango ya kimaendeleo ambapo yote hayo yanategemea na mazingira endelevu.
Pia, Waziri Aweso alisema ni wakati sasa Watanzania watambue kuwa athari za mazingira ziwe funzo, akitolea mfano Mto Ruvu mkoani Pwani ulivyokauka kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yalisababishwa na binadamu wenyewe.
“Athari za mazingira ziko wazi kwa mfano ukienda Pangani athari zikio wazi, leo tunaona bahari imekula mji na hivyo kina cha maji kinaongezeka kina kwahiyo changamoto hizi za kimazingira tunazoziona sasa ziwe funzo kwetu,” alisema.
Pamoja na changamoto hizo, alishukuru na kuipoingeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuandaa mikakati thabiti na hatua madhubuti inazochukua katika kuyasimamia na kuyatunza mazingira.
Amesema hayo yote yanafanyika kutokana na jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa kusimamia agenda ya mazingira.
“Nashukuru
kwa kupata nafasi ya kutembelea mabanda haya, hakika Ofisi ya Makamu wa Rais mmejipanga
na sisi kama Wizara ya Maji tutaendelea kushirikiana na wadau wote katika
kuyalinda na kuyatunza mazingira ili kuhakikisha Tanzania inakuwa bora na salama,
kama mtakumbuka tumefanya mabadiliko ya Sera ili yaendane na mazingira,”
alisema Mhe. Aweso.
Maonesho
hayo ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanatarajiwa
kuhitimishwa Juni 5, 2025 ambayo ndio kilele.
TAWA MGUU SAWA KUDHIBITI WANYAMAPORI WAKALI IKUNGI
Ester Maile Dodoma
Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori(TAWA) imeanza kutekeleza mikakati ya kudhibiti makundi ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo katika wilaya ya Ikungi mkoani Singida.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Malisili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) alipokuwa akijibu swali la Miraji Jumanne Mtaturu ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuondoa Tembo Singida Mashariki ambao wanasumbua na kuharibu mashamba ya Wananchi.
Aidha Kitandula alisema Katika kudhibiti tembo wanaovamia na kuharibu mashamba ya wananchi wa Singida Mashariki, Serikali kupitia TAWA imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuweka vikosi viwili vyenye Askari 24 wakiwemo Wahifadhi 13 na Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) 11 na kutoa magari matatu (3).
Vilevile, TAWA imeimarisha matumizi ya ndege nyuki kwa kuwafukuza tembo kutoka kwenye maeneo ya wananchi na kuwarejesha hifadhini. Mathalan, kati ya mwezi Novemba 2024 na Mei 2025 kikosi maalum cha Askari Wahifadhi 18 na VGS 6 kikitumia ndege nyuki 2 na mabomu baridi kiliweka kambi katika Jimbo la Singida Mashariki, Wilayani Ikungi na kufanikiwa kudhibiti makundi 23 ya tembo kwa kuwarudisha ndani ya hifadhi.
Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo tembo. Mathalan, kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Mei 2025 elimu hiyo imetolewa kwa wananchi 517 na Askari 110 wa Jeshi la Akiba katika Kata za Mkiwa, Igombwe, Iglansonia, Mang’onyi, Issuna, Ntuntu na Ikungi.
‘Serikali itaendelea kutumia teknolojia ikiwemo ndege nyuki na kufunga visukuma mawimb (GPS Satellite Collars) ili kufuatilia mienendo ya tembo na kuwadhibiti’ alisisitiza Kitandula.
Jumapili, 1 Juni 2025
PROFESA MDEBE: MATUMIZI YA NISHATI JADIDIFU YAMESAIDIA KUPUNGUZA VIFO VYA WATOTO NJITI
Na Mwandishi Wetu
MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Shule ya Madini na
Jiosayansi , Profesa Evelyne Mbede amesema matumizi ya Nishati Jadidifu
yamesaidia kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya miezi yao kutimia
(njiti).
Profesa Mbede ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Maadhimisho
ya Wiki ya Kitaifa ya Nishati Jadidifu aliyasema hayo Mei 29, 2025 wakati
akifunga maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa
cha Julius Nyerere (JNICC) jijini
Dar es Salaam.
“Zamani wajawazito walikuwa wakijifungua kwa shida vijijini kutokana
na kukosa umeme hadi kusababisha watoto waliozaliwa chini ya muda wao (njiti)
kupoteza maisha lakini leo hii kwa kutumia nishati jadidifu imesaidia kuokoa
maisha ya watoto hao,” alisema Mbede.
Alisema nishati jadidifu hivi sasa inatumika katika vituo vya afya
na zahanati mbalimbali nchini na si kwa Tanzania tu bali dunia nzima kusaidia
nishati ya umeme kwenye vituo hivyo muhimu kwa jamii.
Profesa Mdebe alisema kumalizika kwa maadhimisho hayo ndio mwanzo
wa maandalizi ya maadhimisho ya msimu mwingine wa 2026 mwakani.
Alisema maadhimisho hayo yamekuwa yakipanua wigo wa ubunifu, kwani
vijana wengi wamekuwa wakiibuka na bunifu mbalimbali na kuongeza matumizi ya
nishati jadidifu na kusaidia maeneo yenye uhitaji, ambako hakuna umeme wa
TANESCO na REA na kutatua changamoto za wananchi.
Profesa huyo alisema Tanzania kushiriki katika maadhimisho hayo ni
kuendana na hali ya mazingira dunia ili kufikia malengo ya 2030 ya kukabiliana
na tabianchi.
“Maonesho haya yanatija sana, kama nchi tumetoka mbali
zamani tulikuwa tukitegemea umeme wa Tanesco pekee lakini hivi sasa tunazalisha
umeme kwa kutumia vifaa mbalimbali na hii ni hatua kubwa,” alisema Mbede.
Maadhimisho hayo yaliandaliwa na Jumuiya ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA) kwa
kushirikiana na Wizara ya Madini na wadau mbalimbali wa sekta hiyo.
Jumamosi, 31 Mei 2025
WAZIRI MKUU AKUTANA NA MWENYEKITI WA CHAMA CHA URAFIKI WA WABUNGE WA JAPAN NA AFRIKA
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa Mei 29, 2025 alikutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge wa Japan cha Urafiki na Afrika (Africa Union Parliamentarians Friendship) Mheshimiwa Ichiro Aisawa, kwenye Ofisi za Bunge la Japan.
Katika mazungumzo yao walijadili kuhusu kuendeleza urafiki kati ya Bunge la Tanzania na Bunge la Japan.
Pia, walijadili kuhusu masuala mbalimbali ya uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Japan, pamoja na kumkaribisha kutembelea Tanzania ili kujionea vivutio mbalimbali ya utalii.
Ijumaa, 30 Mei 2025
STAMICO YAANIKA FURSA YA NISHATI MBADALA KWA WAJASIRIAMALI MANISPAA YA UBUNGO
Afisa Masoko Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Bw. Mark Stephano (wa kwanza kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Afisa Mazingira wa Manispaa ya Ubungo Bi. Jesca Stanley kuhusu nishati mbadala ya Rafiki Briquettes inavyofanya kazi kwa ufanisi, wakati semina ya wajasiriamali iliyofanyika leo Mei 30, 2025, Dar es Salaam.
Afisa Mazingira wa Manispaa ya Ubungo Bi. Jesca Stanley akimkabidhi Cheti cha pongezi Afisa Masoko Mwandamizi wa STAMICO, Bw. Bilton Otto ikiwa ni sehemu shukrani kwa Shirika hilo baada ya kudhamini mafunzo wajasiriamali zaidi ya 700 kutoka Manispaa hiyo.
Picha za matukio mbalimbali.
.............
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SAlAAM
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limewajengea uwezo wajasiriamali zaidi ya 700 kutoka Manispaa ya Ubungo kuhusu namna ya kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika nishati mbadala ya Rafiki Briquettes, ambayo ni rafiki kwa mazingira na nafuu kwa matumizi ya kila Mtanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo wakati akifungua semina hiyo, iliyofanyika leo, Mei 30, 2025, jijini Dar es Salaam, Afisa Mazingira wa Manispaa hiyo, Bi. Jesca Stanley, amesisitiza umuhimu wa kutumia nishati mbadala si tu kwa ajili ya kulinda mazingira, bali kama fursa ya kiuchumi kwa vijana na jamii kwa ujumla.
Bi. Stanley amesema kuwa Manispaa ya Ubungo itaendelea kutengeneza mazingira rafiki pamoja na kuwawezesha vijana kwa kuwajengea uwezo katika matumizi ya nishati mbadala, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu na uhifadhi wa mazingira Kitaifa.
"Watu wenye sifa wafike katika Ofisi ya Maendeleo ya jamii Manispaa ya Ubungo kwa ajili ya kupewa utaratibu wa kupata mikopo na baada ya kupata tunaomba watumie kulingana na vigezo walivyopewa kupata mikopo jambo ambalo litasaidia kufanya marejesho" amesema Stanley.
Kwa upande wao, Afisa Masoko Mwandamizi wa STAMICO, Bw. Bilton Otto, pamoja na Afisa Masoko, Bw. Mark Stephano, wameeleza kuwa kuna fursa kubwa ya biashara katika nishati mbadala ya Rafiki Briquettes kutokana na gharama yake kuwa nafuu na manufaa ya kimazingira.
"Tumefadhili wajasiriamali zaidi ya 700 ili waweze kupata mafunzo katika semina hii, mwitikio ni mkubwa na wengi wameonesha nia ya kuwa mawakala wa bidhaa ya nishati mbadala ya Rafiki Briquettes baada ya kuona umuhimu na faida katika matumizi ukilinganisha na nishati nyengine" amesema Bw. Bilton Otto.
Bw. Stephano amesema kuwa STAMICO imekuja na bidhaa hiyo kwa lengo la kuwasaidia watanzania kuondokana na ukosefu wa nishati ya kupikia, hivyo ni wakati wa vijana kuanzishaji vikundi kwa ajili ya kupata mkopo kwa kushirikiana na Manispaa ya Ubungo kwani uhitaji ni mkubwa.
Amebainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu mbalimbali, Mkoa wa Dar es Salaam ni miongoni mwa mikoa yenye matumizi makubwa ya mkaa, ambapo takribani tani milioni moja hutumika kwa mwaka.
"STAMICO tumekuja na bidhaa hii kwa lengo la kuonesha fursa zilizopo, tukishirikiana na Manispaa ya Ubungo ili kuwawezesha wajasiriamali kupitia mikopo rasmi na kuhamasisha vijana kuwa mawakala wa nishati mbadala ya Rafiki Briquettes," amesema
Nao baadhi ya wajasiriamali wa Manispaa ya Ubungo walioshiriki semina hiyo, akiwemo Asinath Jameson na Julius Msele, wamelishukuru Shirika la STAMICO kwa kudhamini mafunzo kwani yamekuwa na msaada mkubwa kwao pamoja na kupatiwa fursa ya kipekee ya kuingia katika biashara ya nishati mbadala ya Rafiki Briquettes
CHAMA CHA MAPINDUZI CHAZINDUA ILANI YAKE YA UCHAGUZI MKUU MWAKA 2025
Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 yazinduliwa leo katika mkutano mkuu maalum wa chama cha mapinduzi (CCM) Taifa unaonedelea katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center Jijini Dodoma.
Akizundua ilahi hiyo Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) na Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Katibu Mkuu na mgombea mwenza wa Chama cha Mapinduzi Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, makamu mwenyekiti wa CCM Mhe. Stephen Wasira pamoja na viongozi wengine wa chama hicho.
JICA YAAHIDI KUENDELEA KUISHIKA MKONO SERIKALI YA TANZANIA-MAJALIWA
JICA YAAHIDI KUENDELEA KUISHIKA MKONO SERIKALI YA TANZANIA-MAJALIWA
_▪️JICA, Benki ya Dunia na AFDB watoa Dola za Marekani mil 516 miradi ya kilimo_
_▪️Washauri elekezi wawili Mjapan na Mtanzaniia wawekwa TIC kurahisha uwekezaji_
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) limeihakikishia Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa itaendelea kushirikiana nayo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi.
Hatua hiyo imetokana na namna ambavyo Serikali imekuwa ikisimamia kikamilifu matumizi ya fedha mbalimbali zinazotolewa na wadau wa maendeleo likiwemo shirika hilo. Waziri Mkuu amesema “Serikali itaendelea itaendelea kusimamia ipasavyo fedha zote za maendeleo zinazoletwa nchini na kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.”
Ameyasema hayo juzi (Jumatano, Mei 28, 2025) alipokutana na Makamu wa Rais wa JICA, Miyazaki Katsura kwenye ukumbi wa Mikutano wa Tachibana uliopo katika hotel ya New Otani, Tokyo nchini Japan akiwa katika ziara yake ya kikazi.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa JICA kuendelea kutafuta wadau zaidi wa maendeleo kwa ajili upatikanaji wa fedha zitakazowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwafanya Watanzania kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Amesema lengo la wito huo ni kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa wanafungua milango ya kiuchumi ili wananchi wengi washiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo na kujiongezea kipato.
“Lengo la kutafuta wadau hawa ni kuwawezesha wananchi washiriki kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi, wanaotaka kuingia kwenye biashara, wanaotaka kuingia kwenye kilimo, sekta ya madini, sekta ya uvuvi na ufugaji haya ni maeneo ambayo tumeyawekea umuhimu.”
Waziri Mkuu amesema Serikali inataka kuona wananchi wanaendesha shughuli za kibiashara kukiwa na huduma zote katika mazingira rahisi, ikilinganishwa pia na utekelezaji wa miradi ya elimu, afya, miundombinu, nishati, ujenzi wa barabara pamoja na kilimo ni maeneo yanayotiliwa mkazo.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa JICA, Miyazaki Katsura alisema shirika lao linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali nchini kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo Benki ya Dunia katika mradi wa Ustahimilivu wa Chakula.
Makamu huyo wa Rais wa JICA alisema kuwa shirika lao litaendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini ikiwemo ya kuimarisha sekta ya miundombinu na usafirishaji.
Naye, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde ametumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa JICA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 516 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kilimo.
Mheshimiwa Silinde ametaja miradi hiyo kuwa ni Mradi wa Ustahimilivu wa Chakula (TSRP) unaogharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 371 ambazo kati yake Benki ya Dunia imetoa Dola milioni 300.05 na JICA imetoa Dola milioni 71.09, ambapo utekelezaji wa mradi huo unafanyika kwa miaka mitano kuanzia 2025 hadi 2030.
Amesema mradi mwingine ni wa Tanzania Agricultural Inputs Support Project (TAISP) unaotekelezwa kwa ubia kati ya Benki ya Maendeleo Afrika na JICA unaohusika na utoaji wa ruzuku katika pembejeo za kilimo.
Waziri Shilinde amesema mradi huo unaotarajiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 145, ambapo kati ya fedha hizo, JICA wanatoa dola milioni 70 na AfDB dola milioni 75.49 na ulianza kutekelezwa mwaka 2024 na utakamilika 2028. Tayari dola milioni 40 zimelipwa kwa kampuni 17 kwa ajili ya usambazaji wa mbolea.
Waziri Silinde amesema fedha hizo zimetolewa baada ya wadau hao kuridhishwa na namna ambavyo Serikali inasimamia sekta ya kilimo kwa mafanikio makubwa. Hata hivyo amewaomba wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan waje kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji hususan kwenye teknolojia ya umwagiliaji.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar, Ali Mohamed Ameir amesema katika vikao hivyo amewahakikishia wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan uwepo wa mazingira wezeshi ya kutekeleza majukumu yao Zanzibar ikiwemo hali ya amani na utulivu.
Pia, Mheshimiwa Ameir ametumia fursa hiyo kuiomba JICA kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kukamilisha miradi miwili ya ujenzi ikiwemo upanuzi wa soko na jiko la samaki katika eneo la Malindi hususani kutoa vifaa kwa wafanyabiashara pamoja na mradi wa usambazaji maji mijini katika Mkoa wa Mjini Magharibi. Miradi yote inatekelezwa kwa awamu ya pili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri ameishukuru Serikali ya Japan kupitia JICA kwa kugharamia washauri elekezi wawili ambao watakuwa kiungo kati ya wawekezaji na wafanyabiashara wa Japan na Tanzania.
Amesema washauri hao elekezi ambao watakuwepo TIC mmoja ni Mtanzania na mwingine Mjapani watakuwa na majukumu ya kutoa taarifa za namna ya kufanikisha uwekezaji kati ya Tanzania na Japan.
“Lengo la huyu mwelekezi kutoka Japan ni kuzungumza na kusaidia makampuni na wawekezaji kutoka Japan kupata taarifa za namna ya kuja kuwekeza Tanzania na huyu wa Tanzania ni kusaidia Watanzania wote wanaotaka kuuza bidhaa zao Japan waweze kupata usaidizi kupitia kituo cha uwekezaji.”
Awali, Meneja Uenezi na Masoko wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Khamis Dunia alisema ushiriki wa Tanzania kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Osaka (World Expo Osaka 2025) yanayoendelea nchini Japan umeiwezesha mamlaka yao kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo Zanzibar.
Alisema mbali na maonesho hayo, pia kitendo cha kushiriki katika mikutano iliyomhusisha Waziri Mkuu pamoja na wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa wa Kijapan vilivyofanyika jijini Tokyo alipata fursa ya kuelezea vipaumbe vya uwekezaji vilivyopo Zanzibar ikiwemo uchumi wa buluu na utalii jambo ambalo liliwavutia wawekezaji hao ambao tayari baadhi yao wameonesha nia ya kuwekeza Zanzibar.
Mbeto : Wana CCM wameondoka Dodoma kibabe ,vifua mbele tayari kwa ushindi
Mbeto : Wana CCM wameondoka Dodoma kibabe ,vifua mbele tayari kwa ushindi
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Chama Cha Mapinduzi kimesema Wajumbe wake wa Mkutano Mkuu wa Taifa , wanaondoka katika Jiji la Dodoma huku wakiwa wamebeba matumaini ya kupata ushindi kuliko wakati wowote.
Mamia ya Wajumbe hao toka Mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar wameliacha Jiji Kuu hilo la Tanzania ,wakiamini chama chao kitashinda uchaguzi Oktoba Mwaka huu.
Matamshi hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum yya NEC Zanzibar , Idara ya itikadi , Uenezi na Mafunzo, Khamsi Mbeto Khamis ,aliyesema kazi iliobaki ni kuinadi Ilani mpya ya CCM ya Uchaguzi Mwaka 2025 -2030 kwa nguvu zote .
Mbeto alisema hakuna Chama cha Siasa wala mgombea atakaehimili kimbunga cha Kampeni za CCM ambazo zitaanza Miezi michache ijayo toka sasa.
Alisema Uwasilishaji wa taarifa ya matokeo ya Ilani Uchaguzi ya Mwaka 2020-2025, tija na mafanikio ya utekelezaji wa maendeleo ya kisekta , kumedhihirisha nia thabit walionayo Marais , Dk Samia Suluhu Hassan na mwenzake , Dk Hussein Ali Mwinyi .
"Wajumbe wa Mkutano Mkuu wameondoka Dodoma wakiwa wamebeba vikapu vya matumaini ya ushindi . Silaha ya ushindi wa chama cha siasa hutokana na ubora wa Ilani , sera na mipango ya maendeleo " Alisema Mbeto .
Aidha, Katibu huyo Mwenezi , alisifu kazi kubwa iliiofanywa na Serikali zote mbili katika azma ya kutumikia wananchi na kuweka mkazo katika utatuzi wa changamoto za maendeleo ya kisekta.
Alisema matokeo ya utekelezaji wa Ilani iliopita ya Mwaka 2020-2025 , imeelezea mafanikio ya Sekta za Afya , Elimu , Uwekezaji , Miundombinu , Nishati ya Umeme na gesi , Ufugaji na ukuzaji Kilimo.
'Taifa limepiga hatua nyingi za kimaendeleo hususan katika sekta ya Usafiri, Mawasiliano na Makaazi ya Nyumba bora za kisiasa, ujenzi wa Masoko, Barabara , Shule za Msingi na
Sekondari ikiwemo Ujenzi wa Vituo vya Afya na Zahanati " Alieleza
Pia alisema Ilani iliopita imetaja na kuonyesha mafanikio katika ukuaji wa Uchumi wa Taifa , pato la Taifa, Viwanda, Uhusiano wa Kimataifa , Diplomasia, Michezo na Siasa pia mikopo ya taaisis za kimatiafa na Elimu ya juu .
Kadhalika Mbeto alisema taarifa katika ilani iliopita imeonyesha jinsi halmashauri za wilaya zilivyoanzisha miradi ya Maji Safi na Salama , Barabara za Vijijini, Wilaya na Mikoa hadi kukamilika kwake.
"Matumaini makubwa ya Wananchi yamebebwa na ilani mpya Uchaguzi wa Mwaka huu 2025-2530 .Utekelezaji wa mipango iliiomo katika ilani hiyo itaipaisha na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa Nchi za uchumi Kati "Alieleza katibu huyo Mwenezi
Vijana 26 Kushiriki progranu ya Mandela Washington Fellowship 2025 nchini Marekani
Vijana 26 Kushiriki progranu ya Mandela Washington Fellowship 2025 nchini Marekani
Vijana waliochaguliwa kushiriki progranu ya Mandela Washington Fellowship kwa mwaka 2025, wamekumbushwa kuwa fursa waliyoipata haikuja kwa bahati, isipokuwa kutokana na majukumu wanayoyafanya ambayo yana mchango mkubwa kwa jamii.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa wakati anawapa nasaha za kuwaaga vijana hao 26 jijini Dodoma Mei 30, 2025.
Balozi Mussa aliwataka kutumia fursa hiyo kujifunza mambo mapya kwa kuwa nchi wanayokwenda imeendelea kiuchumi na kiteknolojia duniani na itawapa fursa pia ya kukutana na raia wa mataifa mbalimbali wenye uzoefu na mila tofauti.
Vijana hao ambao wanatarajiwa kwenda nchini Marekani Juni na kurejea Agosti 2025, wametakiwa kulitangaza jina la Tanzania kwa watu watakaokutana nao. "Mtalitangaza jina la nchi yetu kwa kuheshimu sheria za nchi mnayokwenda, kutangaza utamaduni mzuri wa Tanzania na kuelezea kwa ufasaha mambo makubwa na mazuri ya nchi kama vile mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama, maziwa, mito na maendeleo ya miundombinu", Balozi Mussa alisema.
Balozi Mussa alisema kuwa kuwepo kwao katika programu hiyo ni kielezo cha uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Marekani ambao umedumu tokea ulipoanzishwa mwaka 1961.
Pogranu ya Mandela Washington Fellowship ilizinduliwa mwaka 2014 na hadi sasa vijana 6500 kutoka nchi za Afrika wamefaidika na mpango huo ambao unalenga kuwajengea uwezo vijana, kupata mbinu na ujuzi wa uongozi utakaosaidia kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi, kisiasa na kijamii barani Afrika.