JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Jumamosi, 10 Mei 2025

RAIS MWINYI AZINDUA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amezindua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia na kuiagiza Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais – Katiba, Sheria na Utawala Bora kutenga fedha maalum kwa ajili ya utekelezaji endelevu wa kampeni hiyo.


Amesema ili kufanikisha kampeni hiyo, ni muhimu kuandaa mkakati madhubuti wa kutafuta rasilimali fedha, nyenzo, na utaalamu, ili kufikia lengo la kuwafikishia wananchi wengi huduma za msaada wa kisheria kote nchini.


Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika Uwanja wa Donda, Mtende, Mkoa wa Kusini Unguja.


Aidha, amezitaka wizara zote mbili zinazoshughulikia masuala ya sheria kuongeza ushirikiano, kufanya kazi kwa ukaribu, na kubadilishana uzoefu ili kufanikisha kampeni hiyo.


Ameeleza kuwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ni nguzo muhimu ya kuimarisha utawala bora, upatikanaji wa haki na kichocheo cha amani, utatuzi wa migogoro, utulivu, na ustawi wa jamii.


Rais Dkt. Mwinyi pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake ya mbali, huruma, na upendo kwa Watanzania, kwa kuanzisha kampeni hiyo inayolenga kutoa huduma za sheria kwa wananchi wasio na uwezo wa kupata huduma hizo kwa njia ya kawaida, ameahidi kuziunga mkono kikamilifu juhudi hizo.


Amesisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuimarisha utawala wa sheria kupitia ujenzi wa mahakama saba za mikoa na mbili za wilaya, ambapo tano ni za mikoa na mbili ni za wilaya.


Vilevile, kupitia Mradi wa Maboresho ya Mahakama, Serikali inalenga kuongeza ufanisi katika utendaji wa mahakama na kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kikamilifu katika mchakato wa upatikanaji wa haki, sambamba na kuongeza rasilimali watu.


Mwisho, Rais Mwinyi ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo, hususan kwa wale wenye malalamiko yanayohusu udhalilishaji wa kijinsia, mirathi, na masuala ya wanawake na watoto.


Kampeni hii ya msaada wa kisheria ni mpango wa miaka mitatu unaolenga kuwafikia wananchi katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

WAZIRI MAVUNDE: MGODI WA MAGAMBAZI WILAYANI HANDENI KUANZA KAZI JULAI 2025


◾️ Kampuni ya kuendeleza mgodi kupatikana mwezi wa 5 mwishoni


◾️ Wananchi wamshukuru Rais Samia kwa kusimamia kuanza tena kwa shughuli za Mgodi Magambazi


▪️Wilaya ya Handeni kuongeza mapato zaidi


▪️Waziri Mavunde asisitiza ajira kwa wananchi wanaouzunguka Mgodi


📍Handeni, Tanga


Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ameeleza kuwa Mgodi wa Kati wa Dhahabu wa Magambazi uliopo Wilayani Handeni Mkoani Tanga utaanza kufanya kazi rasmi ifikapo Julai 2025 na unatarajiwa kuleta tija kwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Kijiji cha Nyasa na Wilaya ya Handeni kwa ujumla.


Waziri Mavunde ameeleza hayo leo Mei 10, 2025, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Nyasa, Kata ya Kang’ata, Wilaya ya Handeni, ambapo amekuja kuleta mrejesho wa ahadi aliyotoa Aprili 6, 2025 kuhusu hatma ya uendelezaji wa mgodi huo uliosubiriwa kwa muda mrefu.

“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake kuhakikisha Mgodi huu wa Magambazi unaanza kufanya kazi na kuwainua wananchi wa hapa na mnyororo mzima wa shughuli za maendeleo.


Baada ya kuchukua hatua ya kupata muafaka wa kuhakikisha mgodi huo unaanza kufanya kazi, Kampuni nyingine ya tatu itateuliwa ndani ya siku 14 kuanzia Mei 12 hadi Mei 26, ambayo itaungana na Kampuni za PMM na East African Metals/CANACO ili kuendesha mgodi huo.

Kipekee nawashukuru sana wananchi wa Nyasa kwa uvumilivu wenu, hili jambo lilikuwa la muda mrefu tangu tumeanza kulifanyia kazi, mlikubali kukaa hapa na kunyeshewa na mvua, na leo mmekuja tena na kukubali kukaa nami kwenye mvua ili kuwapa mrejesho wenu.


Kampuni zinazoendesha mgodi huo kuhakikisha zinatoa kipaumbele kwa wakazi wa Nyasa katika ajira ili wananchi wa Nyasa wanufaike moja kwa moja na uwepo wa mgodi huo katika Kijiji chao.


Faida zitakazopatikana ikiwa ni pamoja na kuinua mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, uboreshaji wa miundombinu ya afya, elimu, barabara na mengine kupitia Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) pamoja na ushiriki wa Watanzania katika mgodi huo kwa kutoa huduma na kuuza bidhaa (Local Content)”amesema Mavunde

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Handeni, Mhe. Amiri Changogo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Japhari Kubecha, na Mbunge wa Handeni Vijijini, Mhe. John Sallu, wamemshukuru Waziri Mavunde kwa kufanyia kazi suala hilo na hatimaye kuondoa kiu ya muda mrefu ya wananchi wa Nyasa na Handeni kwa ujumla.


Naye, Wakili Albert Msando (aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Handeni, hivi sasa ni Mkuu wa Wilaya Ubungo) ameeleza hisia zake za kufurahishwa na hatua hiyo kwani alikuwa akilisimamia kwa ukaribu kipindi akiwa Mkuu wa Wilaya hiyo na kwamba hana deni na wananchi wa Kata ya Kang’ata na Kijiji cha Nyasa baada ya kutatuliwa kwa changamoto hiyo iliyokuwa inawakabili kwa muda mrefu.

RC CHALAMILA AZINDUA MPANGO WA KUFANYA BIASHARA SAA 24 WILAYA YA UBUNGO

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amezindua mpango wa ufanyaji biashara kwa saa 24 kwenye soko la Mbezi eneo la stendi ya Malamba Mawili wilayani Ubungo na kuwahakikishia usalama wafanyabiashara huku akiwataka maafisa biashara kutowaonea wafanyabiashara


Akizungza wilayani Ubungo Jijini Dar es salaam katika uzinduzi huo uliofanyika usiku wa kuamkia leo kwenye soko la mbezi mbele ya mamia ya wafanyabiashara wa Soko hilo waliokusanyika kumsikiliza Mkuu wa Mkoa huyo amesema jiji hilo ni kitovu cha biashara inayochagizwa na uwepo wa bandari,kituo cha mabasi cha Magufuli na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl Nyerere hivyo hakuna sababu ya kulala


Aidha RC Chalamila amewataka wafanyabiashara kutohofia usalama wao kwani Serikali Mkoani humo inazidi kuimarisha ulinzi na usalama ili jiji hilo liwe na amani zaidi huku akimuagiza mkuu wa wilaya ya Ubungo kutoruhusu maafisa biashara kuwaonea wafanyabiashara hao kwani vitendo hivyo ni kinyume na utaratibu


Hata hivyo RC Chalamila ametumia nafasi hiyo kuitaka Halmashauri ya Ubungo kutengeneza vizimba vya mfano vya kufanyia biashara ambapo ametoa muda wa wiki moja kukamilisha kazi hiyo ili wafanyabiashara wenyewe watengeneze vizimba vyao


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Wakili Albert Msando amewahakikishia usalama wafanya biashara, madereva pamoja na wananchi huku Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Hassan Mkwawa akiwahakikishia kuwa pamoja na taa zilizofungwa kwenye maeneo mengi wataendelea kuweka taa za kutosha ili biashara ifanyike saa 24 kwa ufanisi


Shamra shamra za uzinduzi huo zimefanyika usiku mzima hadi asubuhi huku jukwaa likipendezeshwa na wasanii mbalimbali pamoja na Rdj kutoka Efm redio amkiambatana na MC Pilau kutoka Efm.

DKT. MWIGULU AWATAKA WATUMISHI WA WIZARA YA FEDHA KUZINGATIA MISINGI YA KAZI NA UTAWALA BORA

 

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewataka Watumishi wa Wizara ya Fedha, kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa kuzingatia misingi ya kazi na utawala bora ili kuepusha malalamiko yasiyo na lazima kutoka kwa wadau wake wakiwemo wananchi.


Mhe. Dkt. Nchemba alisema hayo wakati akifungua Mkutano wa 38 wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Fedha, lililofanyika katika katika Kituo cha Mikutano cha APC, kilichoko Bunju mkoani Dar es Salaam.


Aidha, Mhe. Dkt. Nchemba aliutaka Uongozi wa Wizara kumchukulia hatua stahiki kwa mujibu wa taratibu mtumishi yeyote atakayebainika na kuthibitika kwenda kinyume na misingi ya maadili katika utendaji kazi ili kulinda heshima ya Wizara.


‘’Ninatambua kwamba mnafahamu misingi ya utendaji kazi katika utumishi wa umma, hivyo, si jambo jema kusikia mtumishi yeyote wa Wizara ya Fedha anakiuka misingi ya utawala bora katika utumishi wa umma’’, alisema Mhe. Dkt. Nchemba.

Pia, Mhe. Dkt. Nchemba aliwapongeza watumishi wote wa Wizara hiyo kwa kazi na mchango wao moubwa uliofanikisha majukumu yake ya kuismamia uchimi wa nchi na kuwezesha upatikanaji wa Fedha zinazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.


Aliwataka Watumishi wa Wizara kuendelea kufanyakazi kwa ushirikiano kati ya Watumishi ndani ya Idara, Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha, na kuzielekeza Taasisi kutekeleza majukumu yao ya msingi kama inavyoratajiwa na Serikali pamoja na wadau wengine.


Mhe. Dkt. Nchemba aliongeza kuwa kutokana na Uwekezaji mkubwa uliofanywa na Wizara katika kuwapatia mafunzo Watumishi wake, hivyo ni lazima matokeo ya mafunzo hayo yaonekane kwa vitendo kupitia utendaji wa kila mtumishi, na kusisitiza umuhimu wa Watumishi kuendelea kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili kuboresha utendaji na kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

Awali, akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Baraza hilo la Watanyakazi ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, alisema kuwa lengo kuu la Baraza la Wafanyakazi ni kuwashirikisha Wafanyakazi katika utekelezaji wa shughuli za Wizara kwa kushirikiana na Uongozi ikiwa ni pamoja na kuishauri Wizara juu ya ufanisi wa kazi na hatua zinazofaa kuchukuliwa ili huduma zinazotolewa na Wizara zikidhi matarajo ya wateja.


Dkt. Mwamba aliongeza kuwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/25, Wizara imepata mafanikio mbalimbali yakiwezo kupandishwa vyeo kwa Watumishi 484 wa kada mbalimbali na kulipa jumla ya shilingi 521,980,765/= yakiwa ni malimbikizo ya mishahara kwa Watumishi wa Wizara.


‘’ Aidha, katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali imeshatoa kibali ili watumishi wenye sifa waweze kupandishwa vyeo. Uchambuzi wa awali umebaini kwamba watumishi 313 wana sifa za kupandishwa vyeo’’ alisema Dkt. Mwamba.

Dkt. Mwamba aliongeza kuwa Mkutano wa 38 wa Baraza la Wafanyakazi ni mwendelezo wa mikutano mingine ambayo imekuwa ikifanyika kila mwaka ambapo kupitia mikutano hiyo wajumbe wamekuwa wakitoa maoni na mapendekezo ambayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha maslahi ya watumishi na utendaji kazi wa Wizara.


Mkutano wa 38 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha, umekutanisha Wajumbe kutoka Makao Makuu ya Wizara, Wakuu wa Hazina Ndogo na Wahakikimali kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara.

Kongamano la Kimataifa la 18 la Elimu Mtandao kwa Afrika lafikia kilele, Mhe. Zainab Katimba (Mb) Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi (Elimu) akishiriki katika kilele hicho.

 

Mhe. Zainab Katimba (Mb) Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI (ELIMU)  tarehe 9 Mei, 2025 amehudhuria kilele cha Kongamano la Kimataifa la 18 la Elimu Mtandao kwa Afrika ‘eLearning Africa’ ambapo Mgeni rasmi alikuwa Mhe. Hemed Abdulla Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akimwakilisha Mhe Dkt. Hussein Mwinyi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.


Mhe. Hemed Abdulla amewataka washiriki wote kuendelea kuunga jitihada za pamoja katika kukuza matumizi ya TEHAMA katika elimu kwa mustakabali wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika. Aidha, amewaalika wafanyabiashara, wawekezaji na taasisi kuja kuwekeza na kuongeza wigo wa ushirikiano Tanzania Bara na Zanzibar katika teknolojia ya digiti hususani elimu na biashara.

Ijumaa, 9 Mei 2025

THE ROYAL TOUR YAZIDI KUIFUNGUA SEKTA YA UTALII. 

...........

Na Mwandishi wetu 

Filamu ya The Royal Tour imezidi kuleta matokeo chanya katika sekta ya Utalii kutokana na mwamko mkubwa kwa wawekezaji hususan wa Hotel za kitalii kuendelea kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali hasa kwenye Hifadhi za Taifa ili kwendana na kasi kubwa ya watalii wanaoingia nchini.

Akizungumza baada ya kutembelea Hoteli ya Serengeti Explore by Elewana na Hoteli ya Serengeti Lake Magadi, Mkoani Mara, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amesema ujenzi wa Hoteli hizo ni mwitikio wa kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuinua sekta ya Utalii hasa kupitia Filamu ya “Tanzania-The Royal Tour,” ambayo imechagiza zaidi kuleta wageni wengi na kufungua fursa zaidi kwa wawekezaji kuwekeza katika malazi.

“Tunamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia kwa kujitoa kwake kutangaza Utalii wa Tanzania ambapo leo matunda yake yanaonekana, wawekezaji wanaendelea kujitokeza kuwekeza kwa kujenga hoteli za kisasa na za kimataifa ambazo zitavutia wageni wengi zaidi kwenye Hifadhi zetu,” alisema Dkt. Abbasi.

Dkt. Abbasi pia ameendelea kutoa wito kwa wawekezaji kuchangamkia fursa adhimu kuwekeza kwa kujenga hoteli katika hifadhi za kusini ikiwa ni mkakati wa Serikali katika kuifungua zaidi Kusini pamoja na kutangaza vivutio vipya vya utalii.

Aidha Dkt. Abbasi asema, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika kwa wadau wote wenye nia ya kuwekeza kwenye maeneo ya vivutio, kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo. 

Hoteli ya Serengeti Explore ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100 na Lake Magadi ambayo ujenzi wake unaendelea kwa jumla zina vyumba 150, hivyo zinaongeza zaidi wigo wa Hoteli za Kitalii katika kuwahudumia wageni wengi zaidi wanaoingia nchini.

MNEC GHULAM AONYA WANAOICHONGANISHA CCM NA WANANCHI


Na Shushu Joel, Kisarawe 


MJUMBE wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa anayetokana na Umoja wa Wanawake Tanzania Bi, Nadra Ghulam amewaonya watumishi wa umma wenye tabia ya kuichonganisha ccm na wananchi.


Onyo hilo amelitoa alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mafumbi kata ya Chole Wilaya ya Kisarawe alipotembelea na kujionea jinsi wananchi walivyoungana na kujenga zahanati hiyo kwa nguvu zao.


"Watumishi wengi wa umma wamekuwa wakikisemea vibaya chama jambo ambalo wananchi wanakiona chama akifanyi kazi kumbe ni uongo mtupu hivyo niwaombe wananchi muwapuuze wote wenye nia mbaya na ccm" Alisema Mnec Nadra Ghulam. 


Aidha amewapongeza wananchi wa kijiji hicho kwa umoja wao wanaouonyesha katika ujenzi wa maendeleo ya kijiji chao.


Pia amewataka wananchi hao kuendelea kutembea kifua mbele kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan anawatendea haki kubwa watanzania katika sekta ya maendeleo. 


Kwa Upande wake Diwani wa kata ya Chole Moshi Mgalu amempongeza Mnec Nadra Ghulam kwa jinsi ambavyo ametatua changamoto za papo kwa papo za wananchi.


Aliongeza kuwa hakika Mnec Nadra Ghulam ameonyesha kuwa ni msaidizi mkubwa wa Rais Dkt Samia. 

KAPINGA AZINDUA KITUO MAMA CHA GESI ASILIA ILIYOSHINDILIWA (CNG) JIJINI DAR ES SALAAM

.............................

Ni cha Pili kwa ukubwa barani Afrika; Cha Kwanza kwa ukubwa EAC

 Kujaza Gesi Asilia kwenye magari 1200 kwa siku

 Ampongeza Dkt. Samia kutatua changamoto za wananchi kwa vitendo

Aipongeza TPDC; Ataka Vituo vya CNG kuendelea kujengwa

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amezindua Kituo Mama cha Gesi Asilia iliyoshindiliwa (CNG) ambacho kina uwezo wa kujaza Gesi Asilia kwenye magari 1200 kwa siku huku kikifanya kazi kwa muda wa saa 24. 

Kapinga amezindua kituo hicho tarehe 9 Mei, 2025 jijini Dar es Salaam akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambapo uzinduzi huo ulienda sambamba na uzinduzi wa basi la mfano la Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) ambalo litaendeshwa kwa kutumia nishati ya Gesi Asilia.

Akizungumza na halaiki iliyohudhuria hafla hiyo, Kapinga amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono, mtazamo na maelekezo yake kwa Wizara ya Nishati ambayo yanaleta matokeo chanya kielelezo mojawapo kikiwa ni uzinduzi kwa kituo hicho cha CNG.

Pia, amemshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko kwa uongozi wake ambao unapelekea upatikanaji wa nishati ya uhakika ambayo ni rafiki kwa mazingira na afya za wananchi.

“ Hapo nyuma kumekuwa na malalamiko ya uwepo wa foleni kubwa za ujazaji wa gesi kwenye vyombo vya moto katika vituo vya CNG ikiwemo kituo cha Ubungo Maziwa, lakini uwepo wa kituo hiki unaonyesha jinsi Serikali inavyotekeleza kwa vitendo ahadi inazotoa kwa wananchi za kupunguza kero ya upatikanaji wa CNG, nampongeza Rais Samia kwa kuendelea kutatua changamoto za wananchi na pia naipongeza Bodi na Menejimenti ya TPDC kwa hatua hii.” Amesema Kapinga

Ameeleza kuwa, kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kujaza Gesi kwenye magari nane kwa wakati mmoja, kuchochea ongezeko la vituo vingine vya CNG na kuwapatia huduma ya gesi watumiaji wengine kama viwanda, shule, hoteli n.k

Kapinga ameiagiza TPDC kuhakikisha kuwa, kituo hicho kinakuwa mfano wa kutoa huduma bora na za viwango kwa wateja huku kikizingatia masuala ya usalama na utunzaji wa mazingira.

Pia ameiagiza TPDC kuendelea kujenga vituo vya CNG katika maeneo mengine ya nchi ikiwemo Lindi na Mtwara, pia kutoa ushirikiano kwa sekta binafsi ili kuendelea kuchochea uwekezaji kwenye sekta ya CNG. 

Naibu Waziri Kapinga pia ameishukuru Sekta binafsi kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali kwenye ujenzi wa vituo vya CNG.

Aidha, amewaasa Watanzania kuchangamkia fursa ya kuweka mifumo ya matumizi ya gesi kwenye magari yao kwani mifumo hiyo haiharibu magari hayo na pia watapata nafuu ya gharama za uendeshaji. 

Kuhusu kampuni ya UDART ambayo kwa mara ya kwanza imezindua basi jipya linalotumia Gesi Asilia, ikiwa ni moja ya mabasi mengi yakayotumia gesi hiyo, Kapinga amesema kuwa ushirikiano kati ya TPDC na UDART utaendelea kuchochea uwekezaji kwenye CNG na kuendelea kuboresha huduma za usafiri jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ameipongeza wizara ya Nishati kwa kazi kubwa inayofanyika ili kupata matokeo makubwa kwenye sekta na kuahidi ulinzi katika miundombinu hiyo ambayo ni muhimu katika kutoa huduma kwa wananchi.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe.Kilumbe Ng’enda amesema Bunge limeridhishwa na hatua zinazochukuliwa kwa kasi na Serikali katika kuendeleza Sekta ya Gesi akieleza kuwa unapotumia gesi asilia kuendesha gari unapata unafuu kwa asilimia 40 ukilinganisha na mafuta. 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio ameipongeza Bodi na Menejimenti ya TPDC kwa kutekeleza mradi huo kwa mafanikio, pia ameipongeza UDART ambao watakuwa wateja wakubwa wa CNG.

Amesema mradi huo ni wa kujivunia kwani kituo hicho kilichozinduliwa ni cha Pili kwa ukubwa barani Afrika na cha kwanza kwa ukubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki

Mwenyekiti Bodi TPDC, Mhe. Balozi Ombeni Sefue amesema Bodi na Menejimenti ya Taasisi hiyo itahakikisha changamoto ya wananchi kupanga foleni ndefu kwenye vituo vya CNG inaisha na watahakikisha rasilimali ya gesi asilia inapatikana wakati wote kupitia huduma mbalimbali ikiwemo ya kupikia na kuendeshea vyombo vya moto.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Francis Mwakapalila amesema kuwa katika kuchochea matumizi ya Gesi Asilia kwenye vyombo vya moto nchini, TPDC imeamua kuweka mkazo kwa kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya kujazia gesi asilia kwenye vyombo vya moto ikiwemo magari na bajaji kwenye maeneo mbalimbali nchini na kwa sasa tayari wameanza mchakato wa manunuzi ya vituo vitano vya CNG vinavyohamishika ambavyo vitawejwa kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.

Awali Mkurugenzi wa Idara ya Biashara ya Mafuta kutoka TPDC, Mhandisi Emmanuel Gilbert alisema kuwa kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha CNG kiasi cha futi za ujazo milioni 4.2 sawa na kilo 120 kwa siku, kina pampu nne zenye jumla ya nozeli nane na hivyo kukifanya kituo kuwa na uwezo wa kuhudumia magari nane kwa wakati mmoja ambapo kwa siku kitatoa huduma kwa magari takriban 1200.

Ameongeza kuwa, kituo kina pampu maalum tatu kwa ajili ya kujaza magari maalum ya kusafirisha CNG kwenda kwenye vituo vidogo vya kujaza gesi kwenye magari (Offline CNG Filling Stations), viwandani, taasisi na majumbani.  

Listen Mkisi Radio