JSON Variables

Showing posts with label Top Stories.. Show all posts
Showing posts with label Top Stories.. Show all posts

Friday, May 9, 2025

MUENDELEZO WA ZIARA YA KAMATI YA SIASA CCM MKOA DAR ES SALAAM KUKAGUA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM KWA MIRADI YA KIJAMII NA MIRADI YA MAENDELEO

 

📍Ubungo

🗓08 May 2025


Abasi Mtemvu Mwenyekiti wa CCM Mkoa ameongozana na wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa katika Ukaguzi utekelezaji wa ilani ya CCM Wilaya ya Ubungo.  Mwenyekiti *Mtemvu* amewapongeza watendaji wa serikali katika kutekeleza miradi hiyo na amewasisitiza wananchi kutunza miradi hiyo ambayo imetumia gharama kubwa kwa ajili ya maendeleo ya wana Ubungo. Miradi iliyokaguliwa ni:- 


🎤 ~*Mradi wa maji wa booster* (DAWASA)- KIBAMBA ambao unagharimu *Tsh Bilioni 36.9* ambapo mradi huo unatarajia kunufaisha zaidi ya wananchi takribani *77000* wa wilaya ya ubungo, Temeke na Ilala kwani maji yatakuwa yanatoka mara mbili kwa wiki

🎤~*Mradi wa ujenzi wa vyumba 4 vya madarasa na matundu 8 ya vyoo* katika shule ya sekondari ya Mbezi Inn, ambapo mradi huo umegharimu *Tsh milioni 114* mpaka kukamilika kwake

 


🎤~*Mradi wa ujenzi wa uboreshaji wa kituo cha afya makulumla* ambao unatekelezwa kwa pesa za ndani kwa gharama ya *Tsh milioni 380* ambao ulianza 2022 na unatarajiwa kukamilika mapema tarehe 1/6/2025 ambapo mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar Es salaam ndugu *Abasi Mtemvu* amewasihi mafundi katika mradi huu kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha haraka mradi huu.

🎤~ *Mradi wa ufungaji wa Ufungaji wa Transforma 4* kubwa kituo cha umeme cha NIT ambao unafadhiliwa na pesa za ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa gharama ya *Tsh Bilioni 125* ambapo unatarajiwa kukamilika tarehe 3/11/2025 kwani vifaa vimekamilika kwa 95%


Kadhalika; Mkuu wa mkoa wa Dar Es salaam ndugu *Albert Chalamila* ameijulisha kamati ya siasa ya CCM mkoa wa Dar Es salaam kuwa ameziagiza Halmashauri zote zinazounda mkoa wa Dar Es salaam kuhakikisha *zinatenga Fedha ili kujenga vituo vya polisi kwa kushirikiana na jeshi la polisi* ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao ndani ya jiji la Dar Es salaam.

Pongezi kwa serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi  wa Rais *Dkt Samia Suluhu Hassan* kwa kuendelea kusogeza huduma za kijamii kwa wananchi wa Ubungo


*Imetolewa na Idara ya siasa na uenezi mkoa wa Dar Es saalam*


#Ccm Imara

#Kaziiendelee

# DktSamiaMitanoTena🖐🏿


©️Kazi na Utu Tunasonga mbele 2025

WAZIRI MAVUNDE AZINDUA TAARIFA YA UCHAMBUZI UONGEZAJI THAMANI MADINI MUHIMU TANZANIA


◾️ Asema Tanzania imeanza Safari ya Mageuzi ya Sekta ya Madini kuchochea ukuaji wa viwanda. 


◾️ Asisitiza dhamira ya Tanzania kuwa kitovu cha bidhaa zitokanazo na madini muhimu. 


◾️ Balozi wa Uingereza nchini asema hatua hiyo ni kielelezo cha ushirikiano kati ya Tanzania na Uingereza. 


📍 *Dodoma*


Waziri wa Madini Mhe.  Anthony Mavunde ameeleza kuwa, Serikali ya Tanzania imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuelekea mageuzi ya kweli ya Sekta ya Madini hapa nchini kwa kuanza rasmi mkakati wa kuongeza thamani ya madini muhimu yanayopatikana nchini. 


Alieleza hayo Mei 8, 2025  wakati akizindua rasmi  Taarifa ya Uchambuzi wa Kina wa Uongezaji Thamani Madini Muhimu na Mkakati ya Tanzania (Manufacturing Africa – Critical Minerals Value Addition Study), katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma

Akizungumza katika Mkutano huo uliohudhuriwa na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. Marianne Young akiongozana na maafisa wandamizi wa Ubalozi huo, wadau wa Sekta ya Madini, Wawekezaji, na wawakilishi, Waziri Mavunde alisema kuwa utafiti huo ni hatua muhimu katika kufanikisha azma ya Taifa ya kuyachakata madini muhimu na mkakati ndani ya nchi hadi kufikia bidhaa za mwisho kwa matumizi ya ndani na nje.


“Ni maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunaweka Mkakati kuyaongeza thamani madini muhimu yanayopatikana nchini hapa hapa ndani ya nchi. Dhamira ni kuyatumia madini yetu kama nyenzo ya kujenga uchumi wa viwanda na kupanua fursa za ajira na teknolojia,” amesema Waziri Mavunde. 


Waziri Mavunde alisisitiza kuwa, Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za madini muhimu kama vile nickel, graphite, rare earth elements, na lithium, madini ambayo ni mhimili wa teknolojia za kisasa, magari ya umeme, na nishati mbadala duniani.

“Kwa kuwekeza katika uongezaji thamani wa madini haya, tunajipanga kuwa kitovu cha uzalishaji wa malighafi ya kisasa kwa ajili ya soko la kimataifa,” amesisitiza Mavunde.


Aidha, Waziri Mavunde alieleza kuwa, Serikali imeweka mazingira rafiki kwa uwekezaji kwa kuboresha miundombinu, kujenga uwezo wa kitaalamu, na kuweka sera na motisha zinazowezesha uwekezaji katika mitambo ya uchenjuaji, uchenjuzi, na uzalishaji wa bidhaa za mwisho.


“Utafiti huu pia utaisaidia Serikali kutambua maeneo mahsusi ya kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuchakata madini, pamoja na fursa mpya za kiuchumi zitakazochochea maendeleo hapa nchini” ameongeza Mavunde. 

Kwa upande wake, Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Marianne Young alisema kuwa taarifa hiyo ni sehemu ya ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili (Tanzania na Uingereza) katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya Sekta ya Madini ambao pia ameeleza Mkakati wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini ya Uingereza kushirikiana na GST kubadilishana uzoefu katika eneo la utafiti wa kina wa madini. 


Uchambuzi huo ni sehemu ya mpango mkubwa wa ushirikiano wa kimkakati wa Ushirikiano wa Ustawi wa Pamoja (Mutual Prosperity Partnership - MPP) kati ya Tanzania na Uingereza uliozinduliwa mwaka jana. Mpango huo pia unalenga kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kwenye Sekta ya Viwanda, hasa kwa kutumia madini muhimu/mkakati kama malighafi ya msingi.

WATUMISHI SEKTA YA AFYA ZINGATIENI MAADILI YA KAZI ZENU – DKT. MAGEMBE


Na. WAF, Arusha

 

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amewataka watumishi wa sekta ya afya nchini kuzingatia maadili ya kazi zao na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

 

Dkt. Magembe ameyasema hayo Mei 8, 2025 jijini Arusha, wakati akizungumza na watumishi katika ziara yake ya kikazi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru.

 

Amesema kuwa kila mtumishi wa afya anatakiwa kufanya kazi kwa weledi  na  kuwa na mawasiliano mazuri baina yao na wagonjwa, ndugu wa wagonjwa pamoja na kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa wote wanaokwenda kupata huduma katika hospitali hiyo na kuongeza kuwa hatua za kisheria zichukuliwe kwa mtumishi atakayekwenda kinyume na kanuni na sheria za kiutumishi kwa kuwafikisha

kwenye mabaaraza ya kitaaluma.

 

“Ndio maana kuna Mabaraza ya Kitaaluma ambayo kazi yao kubwa ni kulinda taaluma na kuhakikisha maadili yanazingatiwa kinyume cha hapo ni kumchukulia hatua stahiki kwa mujibu wa sheria mtumishi anayekiuka maadili ya taaluma yake, ikumbukwe pia kila mtumishi wa afya alikula kiapo kuwa atawahudumia wananchi kwa nguvu zote na sio vinginevyo, hivyo tuyazingatie hayo na kufanya kazi kadri inavyopaswa na isitokee mwananchi amepoteza maisha kwa uzembe,” amesema Dkt. Magembe.

 

Aidha, Dkt. Magembe ameeleza kuwa Mkoa wa Arusha umejipambanua katika eneo la utalii na agenda ya Royal Tour imeubeba sana  mkoa huo hivyo ni vyema kuwahakikishia wananchi na watalii kiujumla wana uhakika wa matibabu pale wanapopata changamoto ya kiafya.

 

“Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Arusha - Mount Meru imekuwa kimbilio kwa watalii wengi wanaokuja kwenye vivutio vilivyopo nchini pale wanapopata changamoto ya kiafya na hospitali ya Mount Meru imekuwa ikifanya vizuri na niwaombe muendelee hivyo ili muwe mfano wa kuigwa,”amesisitiza Dkt. Magembe.

Dkt. Magembe amewashukuru watumishi wote kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuwahudumia wananchi na kusisitiza kuzingatia miiko, na maadili ya taaluma zao ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Thursday, May 8, 2025

MKE WA RAIS WA MSUMBIJI AVUTIWA NA HUDUMA ZA KIBINGWA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI


Mke wa Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mheshimiwa Gueta Selemane Chapo, ametembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) za jijini Dar es Salaam.


Katika ziara hiyo Mheshimiwa Mama Gueta amepongeza ubora wa huduma za kibingwa na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika utoaji wa matibabu.


Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Mama Gueta Chapo amepokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi, na kufafanuliwa kuhusu huduma zinazotolewa katika vitengo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Kitengo cha Tiba ya Uzazi kwa Njia ya Kisasa (IVF), wodi ya kina mama waliojifungua, na huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto na watu wazima zinazotolewa JKCI.


Aidha, akiwa katika wodi ya wanawake waliojifungua, Mheshimiwa Mama Chapo amepata fursa ya kukutana na akina mama waliolazwa, ambapo alitoa zawadi na kusisitiza umuhimu wa kutoa huduma bora kwa mama na mtoto, akitaja kuwa huo ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii.


Katika Kitengo cha IVF, Mheshimiwa Mama Chapo ameelezwa kwa kina kuhusu huduma zinazotolewa kwa wanawake na wanaume wenye changamoto za uzazi kwa kutumia teknolojia ya kisasa.


Mama Chapo ameonesha kuvutiwa na mafanikio ya huduma hiyo na kubainisha umuhimu wa kuimarisha huduma kama hizo nchini Msumbiji.


Vilevile, akiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Mheshimiwa Mama Chapo amepata maelezo kuhusu huduma za kibingwa za upasuaji na matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima.


Pia ameshuhudia kazi ya madaktari bingwa na kupongeza ubora wa huduma zinazotolewa, pamoja na mchango wa ushirikiano wa kimataifa katika kuboresha huduma hizo.


Katika mazungumzo yake na viongozi wa hospitali hizo, Mheshimiwa Mama Chapo ameeleza kufurahishwa na kiwango cha huduma na teknolojia inayotumika katika MNH na JKCI, huku akisisitiza kuwa uzoefu alioupata utasaidia kuanzisha ushirikiano wa kina kati ya Msumbiji na Tanzania, hususan katika maeneo ya afya ya moyo, huduma za uzazi na matibabu ya kibingwa.

TANZANIA NA MSUMBIJI ZA SAINI MAKUBALIANO KATIKA NYANJA YA UCHUMI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Raisi wa Jamhuri ya Msumbiji Mh. Daniel Francisco Chapo wamekubaliana kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na Msumbiji hususani katika eneo la biashara na uwekezaji kwa kuunda Tume ya pamoja ya Uchumi (JEC) ili kutatua changamoto za kiuchumi.

 



RAIS SAMIA AZIDI KUINUA SEKTA YA UTALII" DKT. ABBASI

Na Mwandishi wetu.

Jitihada kubwa za kukuza Utalii nchini zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, zinazidi kushamiri katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa Gofu nje kidogo ya Hifadhi hiyo ilioko Mkoani Mara.

Akikagua ujenzi wa uwanja huo wenye mvuto wa kipekee, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amesema ujenzi wa uwanja huo ni jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendelea kukuza sekta ya Utalii ili kuongeza zaidi furasa kwa watanzania kupitia watalii wanaoingia nchini pamoja na kukuza pato la Taifa.

Aidha Dkt. Abbasi ameridhishwa na kasi ya ujenzi unaendelea ambao umefikia hatua nzuri na pindi utakapo kamilika utaongeza mchechemko wa watalii nchini hususani wa michezo.

Dkt. Abbasi licha ya kupongeza kwa kazi nzuri ya usimamizi wa unjenzi huo, amesisitiza kasi zaidi ili ukamilike kwa wakati uliopangwa na kutoa nafasi ya kuendelezwa kwa viwanja vingine kadha vya michezo ambayo yatakuwa ni mazao mapya ya Utalii wa Michezo.

Uwanja huo unaojengwa nje kidogo ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kama sehemu ya kuibua zao jipya la utalii wa michezo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwaka huu.

BALOZI MBUNDI AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA MAKATIBU WAKUU WA EAC

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen P. Mbundi leo tarehe 8 Mei, 2025 ameongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kikao cha Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kinachofanyika jijini Arusha.


Kikao hicho na kikao cha maafisa waandamizi wa EAC kilichofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 7 Mei, 2025 sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 25 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya wa Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 9 Mei, 2025.


Kikao hicho cha Makatibu Wakuu kinaangazia vipaumbele vya sekta ya afya katika Jumuiya ikiwemo: Maboresho ya mifumo ya afya inayosomana, ushirikiano katika uchunguzi wa magonjwa ya milipuko na ya kuambukiza, upatikanaji wa teknolojia ya kisasa na bora katika huduma za afya na uimarishaji wa mfumo wa usimamizi wa sekta ya afya.


Akitoa salamu za Serikali katika ufunguzi wa kikao hicho Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia masuala ya sayansi, Prof. Daniel Mushi kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi ameipongeza Sekretarieti pamoja na maafisa waandamizi kwa uratibu na maandalizi mazuri ya nyaraka ili kuwezesha Baraza la Mawaziri kutoka na miongozo mizuri ya kisera na kupata uelewa wa pamoja juu ya masuala ya kitaalamu katika masuala ya afya


‘’ Nina imani kuwa majadiliano haya yatatoa uelekeo kwa nchi wanachama katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za sekta ya afya zilizopo na zinazoendelea kujitokeza ulimwenguni ili kujenga utayari wa pamoja wa kukabiliana nazo’’ Prof. Mushi.


Kadhalika, ameainisha jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutatua changamoto za afya ambazo ni: Kuendelea kuimarisha mfumo wa afya katika pande zake mbili za muungano (Tanzania Bara na Zanzibar) kwa kuboresha miundombinu; uwekezaji wa rasimali watu pamoja na kuwajengea uwezo.


Jitihada nyingine ni pamoja na matumizi ya vifaa tiba vya kidigitali na msisitizo wa ujumuishi na usawa wa upatikanaji wa huduma bora za afya kwa jamii zenye uwezo mdogo na zilizo mbali na huduma za afya.


Viongozi wengine walioshiriki mkutano huu ni pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Maghembe, Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Benjamini Mkapa-Dodoma Prof. Abel Makubi na maafisa wengine waandamizi kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

MAMA MARIAM MWINYI AZINDUA ZANZIBAR AFYA WEEK

 

Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi amesema  Maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Nchi yoyote yanahitaji  jamii yenye Watu wenye Afya Bora.


Mama Mariam ambae pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Zanzibar Zanzibar Maisha Bora Foundation(ZMBF) amesema hayo alipoizindua  Zanzibar Afya Week  katika Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege , Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 8 Mei 2025.


Amesema Zanzibar Afya Week ni fursa nyengine Muhimu  ya Kuhakikisha  Wananchi wànapata huduma Bora za Afya ikiwemo Elimu ya Afya na Uchunguzi wa Magonjwa mbalimbali Ikiwemo Kisukari, Presha, Saratani ya Matiti , Macho  na  Moyo.


 Mariam Mwinyi ameeleza kuwa Zanzibar Maisha Bora Foundation imejizatiti  kushirikiana na Serikali  Kuimarisha huduma za Afya na Kuifanya Zanzibar kuwa na  Watu wenye Afya Bora na kituo Muhimu cha Utabibu kinachotambulika.


Aidha, Mariam Mwinyi amesema hatua zinazochukuliwa na Wizara ya Afya hivi sasa zinaakisi dhamira ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi ya kuifanya Zanzibar kutoa huduma za Matibabu, Kupunguza Rufaa za kwenda nje ya Nchi kufuata Matibabu na kupunguza bajeti za Matibabu na Wageni wanaofika Zanzibar Kupata huduma  za Uhakika za Matibabu.


Halikadhalika Mariam Mwinyi amefahamisha kuwa kupitia Kampeni ya Afya Bora Maisha bora ZMBF imeweza kuwafikia Wananchi 21, 500 kupitia Kambi nne za Afya kuwapatia  Wananchi Elimu ya Afya , Unguja na Pemba 


Vilevile Zanzibar Maisha Bora Foundation  imefanikiwa kupitia Mpango wa Lishe imeweza  kuwafikia Wanawake 2,830 Unguja na Pemba   kuwapatia Elimu ya Lishe na Afya  ya Uzazi na mama wajawazito huduma za Kliniki. 



Kwa upande mwingine Mariam Mwinyi amefahamisha kuwa Programu ya Tumaini Initiative ya ZMBF imeweza  kuwafikia Wasichana balehe 8,676 Unguja na Pemba  wa Skuli za Msingi na Sekondari na kuwapatia Tumaini kits na Elimu ya hedhi Salama na kuchangia Mahudhurio Skuli na kusoma kwa  Waweze kusoma kwa kujiamini.


Mama Mariam Mwinyi amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika  kuimarisha Hospitali na Vituo vya Afya pamoja na Sera na Teknolojia ya Utoaji wa huduma katika Sekta ya Afya na kuipongeza kwa Mafanikio hayo.  


Uzinduzi huo uliambatana na Programu za Lishe Bora 2025, Afya Mama na Mtoto 2025 na Shehia Afya Programu 2025

RAIS MWINYI:TUENDELEE KUDUMISHA AMANI KWA UMOJA NA MSHIKAMANO NCHINI

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewanasihi Wananchi wa Tanzania kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na amani kwa mustakabali mwema wa Taifa kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo na kujiepusha na matendo yanayoweza kuleta mgawanyiko.


Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipofungua  Dua Maalum ya kumuombea Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Mamufti, Masheikh, na Waislamu waliotangulia mbele ya haki  iliofanyika katika Msikiti wa Mohamed VI-Bakwata Makao Makuu, Kinondoni Jijini Dar es Salaam tarehe 8 Mei 2025.


Aidha , Rais Dkt.Mwinyi amewapongeza Uongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kuendeleza utaratibu wa Dua ya kila Mwaka na kuiombea nchi amani .


Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa amani ina umuhimu mkubwa katika  Uchaguzi Mkuu Mwaka huu kabla , wakati na baada ya Uchaguzi huo.


Rais Dkt.Mwinyi amesema jukumu la kuwaombea Dua Masheikh,  Walimu, na Waislamu waliohai na waliotangulia  mbele ya haki na kuiombea amani   Nchi ni miongoni mwa dalili za imani ya kweli kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu kwa mikusanyiko yenye kheri kwa mustakabali wa Taifa.

KIKWETE ATETA NA UONGOZI WA KIWANDA CHA DANGOTE- MTWARA.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete leo Alhamisi amefanya mazungumzo na Ujumbe wa Kiwanda cha Kutengeneza Cement Cha Dongote kutokea Mtwara walipokuja kumtembea Ofisini Dodoma wakiongozwa na Meneja wa Kiwanda hicho Nchini Bwana Adeyemi Fajobi. 

Mazungumzo yao yamejikita zaidi kuzungumzia maeneo yenye changamoto na utatuzi wake. Pia Serikali kuwakumbusha umuhimu wa kiwanda hicho kwa Watanzania haswa ajira na kukuza uchumi wa miji ikianza na Mkoa wa Mtwara. 


Kwa upande wake Bwana Adeyemi amemsisitizia Waziri kuendelea kufanya kazi kutatua changamoto zinazotoka mahala pa kazi na kuiomba Serikali kuendelea kushirikiana nao huku Waziri Kikwete akimuahidi kuwa serikali itaendelea kufanya kazi nao kwa pamoja kustawisha kiwanda kicho kikubwa kwa ustawi wa uchumi wa Tanzania. 

#KaziInaendelea #DangoteCement

MAJALIWA AHANI MSIBA WA MHE. CLEOPA DAVID MSUYA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Mei 8, 2025 amehani msiba wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Cleopa David Msuya, Upanga Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na wanafamilia pamoja na waombolezaji wengine, Mheshimiwa Majaliwa, amewasihi kuendelea kumuombea Mhe. Msuya na wawe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Marehemu Cleopa Msuya alifariki Mei 07, 2025 katika hospitali ya Mzena Jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu.

TANAPA YAENDESHA MAFUNZO YA USIMAMIZI WA VIATARISHI


Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limefanikiwa kuendesha mafunzo muhimu ya Usimamizi wa Viatarishi kwa Wakuu wa Kanda, Wasimamizi wa Ofisi Viunganishi, Maafisa wa Hifadhi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.


Mafunzo hayo, yaliyofanyika katika ofisi ya Kiunganishi ya TANAPA, Dodoma kuanzia Mei 5 hadi 9, 2025, yamelenga kuimarisha ufanisi katika usimamizi wa viatarishi kwa kutoa ujuzi na mbinu bora za kutambua, kudhibiti, na kuripoti viatarishi katika ngazi zote za Shirika.


Akizungumza katika katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo haya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Godwell Meng’ataki ambaye pia ni Mkuu wa Kanda ya Kusini alieleza kuwa Semina hii elekezi inalenga kuimarisha ujuzi, uelewa wa pamoja na mbinu bora za kusimamia vihatarishi jambo ambalo ni msingi wa Utawala Bora na uwajibikaji wa TANAPA.


“Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za TANAPA, katika kuhakikisha kuwa utawala bora na uwajibikaji unazingatiwa katika usimamizi wa Hifadhi za Taifa, hivyo kuimarisha Uhifadhi na Utalii endelevu nchini ni matarajio yangu kuwa tukirejea katika maeneo yetu ya kazi tutakuwa na nguvu mpya ya kuhakikisha viatarishi vinatambuliwa, mikakati ya kuvithibiti inatekelezwa ipasavyo, na taarifa sahihi zinaandaliwa kwa wakati katika ngazi zote za shirika.” alisema Kamishna Meng’ataki


Semina hii elekezi, iliongozwa na wataalamu kutoka Wizara ya Fedha wakiongozwa na Msaidizi Mkaguzi Mkuu wa ndani Bw. Abrahamu Elisamia Msechu, ambaye aliendesha mafunzo katika kuimarisha utekelezaji wa Usimamizi wa Viatarishi, huku Dkt. Bernard Mnzava kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) akitoa mafunzo ya kina kuhusu mbinu bora za usimamizi wa viatarishi ili kufikia malengo.


Sambamba na hayo, mafunzo ya vitendo yalifanyika kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Viatarishi wa TANAPA, Risk Information Management System (RIMS), ambapo Maafisa wa kutoka kitengo cha TEHAMA walionyesha namna bora ya matumizi ya  mfumo huo katika usimamizi wa viatarishi.

Wednesday, May 7, 2025

KERO YA MAJI KIJIJI CHA MLOKA, MBUNJU MVULENI NA NDUNDUTAWA YAPATIWA UFUMBUZI.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI na Mbunge wa Rufiji Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameshuhudia hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa miradi ya Maji itakayojengwa katika Vijiji vitatu vya Mloka, Mbunju Mvuleni pamoja na Ndundutawa ambayo itahudumia Wananchi 16, 593 hali itakayosaidia kupunguza kero ya Maji katika maeneo hayo.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani Rufiji Mhandisi Alkam Sabuni, alisema ujenzi wa Miradi ya Maji katika Vijiji hivyo utagaharimu kiiasi cha Shilingi 791,068,682.56.


"Katika Kipindi Cha Mwezi Juni 2025 hadi Oktoba 2025 Wananchi wapatao 16,593 wa Vijiji vitatu vya Mloka, Mbunju Mvuleni na Ndundutawa wanaenda kunufaika na huduma ya Maji safi na salama na yenye kutosheleza, ambapo miradi hii itakapokamilika itaongeza hali ya upatikanaji wa Maji kutoka asilimia 86.6 ya sasa hadi asilimia 97.3" alisema Sabuni

Hafla ya Utiaji Saini wa Mikataba ya ujenzi wa miradi hiyo imefanyika katika Kijiji Cha Mloka Kata ya Mwaseni Jana Mei 6, 2025.


Sabuni aliongeza kuwa RUWASA Wilayani Rufiji inatoa huduma katika Vijiji 38 vyenye Jumla ya Watu 157,412 kwa Mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa alisema uwepo wa miradi iyakapokamilika itasaidia kupunguza adha ya Wananchi kwenda kuchoma Maji katika Mto Rufiji.


"leo tumeandika historia katika changamoto ambazo tumekuwa tukizipata kwa muda mrefu leo tumezimaliza na matarajio yangu kwamba Mkandarasi sasa ataanza kazi mara Moja" alisema Mchengerwa.


Rais Mwinyi Afanya Uteuzi Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mh. Dkt. Hussein Ally Mwinyi amefanya uteuzi leo kwa kumteua Ndugu Madina Mjaka Mwinyi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar.

Ndugu Madina ni Mstaafu katika Utumishi wa Umma Zanzibar.


KAMATI YA SIASA YA CCM MKOA WA DAR ES SALAAM YAKAGUA MIRADI YA MAENDELEO WILAYA YA TEMEKE

 

-Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na kutoa Shukrani kwa Rais Dkt Samia kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo.  

Kamti ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam leo Mei 7, 2025 ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo Mhe Abbas Mtemvu imetembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha nyingi zinazotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ambapo kwa ujumla Kamati hiyo imeridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo.

Akiongea wakati wa Ukaguzi wa miradi hiyo Mhe Abbas Mtemvu amempongeza Mkuu wa Mkoa na viongozi wote waliochini yake kwa kazi nzuri wanayoifanya hususani utekelezaji wa mzuri wa miradi ya maendeleo yenye masilahi mapana kwa umma pamoja na ushirikiano mkubwa walionao kati ya Chama na Serikali.

Aidha kwa upande wa Mkuu wa Mkoa Mhe Albert Chalamila amesema miradi yote katika Mkoa huo, itakamilika kwa wakati kwa viwango na kuzingatia thamani ya fedha "Value for Money " 

Vilevile amesema mkakati wa Mkoa kwa sasa kutokana na ufinyu wa Ardhi na ongezeko kubwa la idadi ya watu, majengo mengi ya umma ikiwemo shule, vituo vya Afya kwa sasa vitajengwa kwa Ghorofa ili kutumia vizuri Ardhi iliyopo.


Mwisho Kamati hiyo ikiwa katika muendelezo wa kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo imekagua ujenzi wa Jengo la Ghorofa la Shule ya Sekondari Mangaya linalojengwa Mbagala, Maradi wa Hospitali ya Wilaya ya Temeke unaojengwa Chamazi na Kituo cha Polisi cha Kisasa kinachojengwa Toangoma.

Mkutano wa 14 wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba wa Lusaka kuanza Arusha kesho

 



ARUSHA


Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 14 wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba wa Lusaka (14TH Governing Council Meeting of Parties to the Lusaka Agreement) utakaofanyika jijini Arusha katika Hoteli ya Gran Melia kuanzia Mei 8,2025.


Hayo yamesemwa leo Mei 7,2025 jijini Arusha na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana wakati akizungumza na wanahabari.

"Tumekutana hapa hii leo kwa lengo la kuwaomba kutumia vyombo vya habari mnavyoviwakilisha kufikisha ujumbe kwa Watanzania kuhusu mkutano mkubwa na wa kipekee wa masuala ya Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu unaoatarajiwa kufanyika hapa nchini kwetu hususani katika Jiji hili la Utalii la Arusha."


Amesema,mkutano huu hufanyika mara moja kila baada ya miaka miwili ambapo kwa mara ya mwisho ulifanyika nchini Zambia mwezi Machi, 2022.


Balozi Dkt.Chana amesema,Baraza la Usimamizi wa Mkataba wa Lusaka, ulianzishwa mwaka 1994 kwa lengo la kuziwezesha nchi za Afrika kusaidiana katika kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya nyara yakiwemo mazao ya misitu inayovuka mipaka ya nchi.

Tanzania ilijiunga na Mkataba huu mwaka 1999 na imekuwa ikiutekeleza kwa kushirikiana na nchi wanachama ambazo ni pamoja na Congo-Brazzaville, Kenya, Lesotho, Liberia, na Zambia.


"Kupitia Mkataba huu, Tanzania imenufaika katika nyanja mbalimbali ikiwemo kubadilishana taarifa za uhalifu wa makosa yanayohusu wanyamapori na misitu."


Mafanikio mengine amesema ni kufuatilia na kukabiliana na mitandao ya ujangili wa wanyamapori na misitu,kufanya operesheni na doria na mafunzo ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

"Katika mkutano huu wa 14 ambao utafanyika hapa nchini kwetu katika Jiji hili la Arusha, pamoja na mambo mengine utapokea taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa 13 wa Baraza na utaidhinisha Mpango Mkakati wa Mkataba wa Miaka mitano (2025-20230)."


Aidha, Tanzania kupitia Waziri wa Maliasili na Utalii, itapokea nafasi ya Urais wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba kwa kipindi cha miaka miwili ijayo kutoka kwa Waziri wa Maliaisili wa Kenya.


Waziri Chana amesema, kufanyika kwa mkutano huu katika jiji la Arusha ni fursa ya kutangaza utalii, kufanya biashara na kushiriki katika juhudi za kikanda na kimataifa za kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori na mazao ya misitu.

Kwa mujibu wa Kanuni za Uendeshaji wa Mikutano ya Baraza, mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na takribani Mawaziri 19 wanaoshughulikia masuala ya Maliasili na Mazingira kutoka katika nchi 19 za Afrika.


Sambmba na wawakilishi kutoka katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UNEP, UNODC, UNDP, INTERPOL WCWG) na Katibu Mkuu wa Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyamapori na Mimea Iliyohatarini kutoweka (CITES).


Aidha, kwa Tanzania,Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na taasisi zake zinazounda Wakala wa Utekelezaji wa Mkataba (National Bureau) zitashiriki.

NHIF SASA KUGHARAMIA MATIBABU YA AFYA YA AKILI, KUFUATA MWONGOZO

 

NA WAF, DODOMA 


Serikali imesema huduma za afya ya akili zimeshajumuishwa kwenye vifurushi vya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), na hivyo wananchi wanaonufaika na bima wanaweza kupata matibabu hayo kwa mujibu wa mwongozo wa matibabu uliopo.


Akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Mhe. Jesca Msambatavangu, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa, huduma za afya ya akili, ushauri nasaha, pamoja na huduma za kibingwa kama vile utengamao, zote zimetajwa kama huduma muhimu kwenye Mwongozo wa Matibabu (Standard Treatment Guideline – STG) na zinagharamiwa na NHIF.


“Huduma hizi zinalipiwa kwa kuzingatia aina ya dawa na ngazi ya kituo cha huduma, kwa mujibu wa mwongozo wa matibabu wa Taifa,” amefafanua Naibu Waziri  Dkt. Mollel.


Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa huduma za afya ya akili zinapewa uzito sawa na huduma nyingine za msingi, na kuimarisha upatikanaji wake kupitia mifumo ya bima ya afya kwa wote.

HOSPITALI ZA BENJAMIN MKAPA, MLOGANZILA KUENDELEA KUTUMIKA KAMA VITUO VYA MAFUNZO UDOM NA MUHAS

 

NA WAF, DODOMA


Serikali imesema Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Mloganzila zitaendelea kuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya kwa madhumuni ya kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kuboresha ubora wa huduma sambamba na kutumika kama vituo vya mafunzo kwa wanafunzi wa vyuo vya Vikuu vya Dodoma na Muhimbili.


Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Thea Medard Ntara, Mei 07, 2025  kuhusu mpango wa kuzirudisha hospitali hizo chini ya vyuo husika, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema vyuo hivyo bado vinaendelea kuzitumia hospitali hizo kama sehemu ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa kada za afya.


“Vyuo vikuu vya Muhimbili na Dodoma vinaendelea kutumia Hospitali ya Mloganzila na Benjamin Mkapa kama hospitali za kufundishia, kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya katika kuhakikisha mazingira bora ya kitaaluma na huduma kwa wananchi,” amesema Dkt. Mollel.


Aidha, Dkt. Mollel amefafanua kuwa, usimamizi wa Wizara ya Afya umelenga kuimarisha mifumo ya huduma za afya huku ukihakikisha kuwa mahitaji ya vyuo vikuu vinavyotoa programu za afya yanaendelea kuzingatiwa.

SHULE 216 ZA SERIKALI ZATUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA-KAPINGA

 

NA MWANDISHI WETU

NAIBU Waziri Nishati,  Judith Kapinga amesema hadi kufikia mwezi Machi 2025 takribani Shule za Serikali 216 zimehamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo kati ya hizo, Sekondari 146 zinatumia gesi ya LPG.


Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Mei 07, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Liwale, Mhe. Zuberi Mohamedi Kuachauka aliyeuliza ni lini majiko yanayotumia gesi yataanza kutumika kote nchini.


“Serikali kupitia REA inaendelea kutoa ruzuku ya ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwa shule nyingine na  tarehe 20 Aprili, 2025, REA kupitia Wizara ya Nishati imepokea kibali kutoka TAMISEMI cha kufunga miundombinu ya huduma ya nishati safi ya kupikia katika shule 115 zikiwemo shule za Mikoa za sayansi za wasichana 16; shule za kitaifa za wavulana 7, shule za bweni za kawaida 66 na shule kongwe za sekondari 26”. Amesema Mhe. Kapinga


Amesisitiza kuwa Serikali kupitia REA na wadau mbalimbali itaendelea kufunga miundombinu ya nishati ya kupikia katika shule za sekondari kulingana na upatikanaji wa fedha. 


Mhe. Kapinga ameongeza kuwa Wizara ya Nishati kupitia Wakala wa Nishati Vijijini i(REA) inatekeleza miradi ya kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia Jeshi la polisi na Magereza katika Mikoa 24, jeshi la Zima Moto  pamoja na huduma za Wakimbizi.


Aidha, amesisitiza kuwa upo mkakati wa kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia katika Taasisi zilizo chini ya Wizara ya afya ikiwemo hospitali za Mikoa, za Wilaya na za kitaifa takribani 21.


Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Tunza Malapo aliyetaka kufahamu ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha shule, Zahanati na Vituo vya afya vipya vinajengwa vikiwa na mifumo ya nishati safi ya kupikia, Mhe. Kapinga amesema kupitia mkakati wa nishati safi ya kupikia ambao utekelezaji wake umeanza kutekelezwa, Serikali inaelekea kwenye mtazamo huo wa Shule, Zahanati na Vituo vya afya kujengwa sambamba na miundombinu ya nishati safi ya kupikia.

Tuesday, May 6, 2025

TANZANIA YAENDELEA KUSHIRIKIANA NA NCHI WASHIRIKA KUKABILIANA NA UJANGILI


Na, Mwandishi Wetu – Arusha 


Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama wa Mkataba wa Lusaka katika kukabiliana na biashara haramu ya Wanyamapori na mazao ya misitu inayovuka mipaka ya Nchi ili kuboresha uhifadhi, kuendeleza utalii na kukuza uchumi. 


Akifungua Mkutano wa 14 wa Kamati ya Wataalam wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba wa Lusaka ulioanza leo Mei 06, 2025 Jijini Arusha, Mkurugenzi wa Wanyamapori  Dkt. Alexander Lobora amesema Mkataba huo umekuwa na manufaa makubwa kwa Nchi Wanachama kwa kuunganisha nguvu za pamoja kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka. 

“Tumekuwa tukishirikiana na nchi nyingine kwa kupeana taarifa za kiintelijesia  za wahalifu pale ambapo wanatenda kosa na kukimbilia nchi nyingine, au kuwa na washirika wa uhalifu katika mataifa mengine na kuchukua hatua za kuwakamata na kuwarudisha katika nchi walikotenda uhalifu ili sheria iweze kuchukuwa mkondo wake.” Amesema Dkt. Lobora


Aidha Dkt. Lobora amesisitiza juu ya wananchi wanaojishughulisha na ujangili kuacha mara moja na  kujielekeza katika kazi halali za kujipatia kipato kwa kuwa utekezaji wa mkataba huo hautaruhusu wahalifu kujificha popote.


Awali, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambae pia ni  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Huduma za Wanyamapori Kenya Prof. Erustus Kanga ametoa rai kwa nchi za Afrika kushirikiana katika juhudi za kupambana na biashara haramu  za mazao wanyamapori na misitu ikiwemo uwindaji haramu wa wa wanyamapori adimu wakiwemo faru kwa ajili ya vipusa na ndovu kwa ajili ya meno yao. 

“Kupitia mkataba huu tungependa kuona Bara letu la Afrika hakuna mtu yeyote anayejihusisha na uwindaji haramu, wa Faru au Ndovu, atoe pembe Kenya ama atoe Tanzania na avuke mipaka ama, atoke Tanzania aende Zambia ama atoke Kenya aende kuziuza Kongo, hilo ndiyo jawabu letu kubwa kabisa.  Tunataka kuona rasilimali zetu zinalindwa kwa kukomesha biashara haramu za mazao ya wanyamapori na misitu ili tuweze kunufaika na rasilimali zetu za asili.” Amesema Prof. Kanga

Mkataba wa Lusaka ulianzishwa mwaka 1994 Jijini Lusaka Zambia na Tanzania ni miongoni mwa mataifa sita yaliyoanzisha Mkataba na kuridhia utekelezaji wake mwaka 1996. Katika Mkutano wa 14 wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba, Tanzania itakadhiwa kiti cha urais wa Baraza kwa kipindi cha miaka miwili kutoka Kenya